Habari rafiki,
Kila mtu, bila kujali ana nini, hujikuta wakati fulani anahitaji msaada kutoka kwa rafiki, jirani au ndugu zake.
Msaada unaweza kuelezewa kama kitu anachotoa mtu au taasisi ili kutimiza haja fulani au kutatua tatizo la mtu au taasisi yenye uhitaji.

Sasa, tukiongelea suala la uhitaji, je ni wakati gani tunaweza kusema taasisi au mtu ana uhitaji ili apewe msaada? Je, ni wakati wowote tu? Je, ni wakati wa maafa au majanga? Au ni wakati gani?
Na kama utagundua, baada ya tathmini, kuwa ndugu, rafiki, au taasisi inahitaji msaada, je ni msaada gani utampatia? Je, ni pesa? Je, ni vifaa? Je, ni ushauri – au ni nini?
Kabla hujatoa maoni yako kwa maswali haya nakuomba ufuatilie hadithi hii fupi kutoka katika kitabu cha dini.
Hapo zamani za kale, katika kijiji kimoja, waliishi vijana wawili, Rahim na Rahman. Kila siku asubuhi vijana hawa waliondoka na mashoka yao kwenda msituni, jirani na kijiji chao, kuchanja kuni kwa ajili ya kuuza.
Inapofika mchana, baada ya kukata kuni za kutosha, vijana hawa walikuwa na tabia ya kukaa kando ya mto ili kula chakula walichofungashiwa asubuhi.
Baada ya mlo walizibeba kuni zao kuelekea sokoni kwa ajili ya kuziuza kabla ya kuanza safari ya kurudi nyumbani jioni.
Sasa, siku moja baada ya kukata kuni zao, waliketi kwa ajili ya mlo wa mchana. Kuinua macho, Rahim akamwona kijana mmoja aliyedhoofika, mchafu na mwenye mavazi duni, ingawa alionekana hana tatizo la kiafya.
Kijana huyu alitokea porini kuja upande wao na alipokaribia macho yake yote yalilenga bakuli lenye chakula. Alionekana ana njaa sana, na bila kupoteza muda alipeleka ombi la chakula ili akidhi njaa yake.
Rahim, huruma ilimshika na haraka aliuendea mkoba wa chakula akatoa kipande kimoja ili ampatie ‘ombaomba’ yule maskini.
Kabla Rahim hajampatia kipande kile, Rahman aliudaka mkono wake na kuuvuta, kisha akamwambia yule ombaomba, “hatuna chakula cha kutosha sisi.”
“Angalia, tunajituma kufanya kazi kutwa nzima, tumekaa hapa tupate mlo wetu halafu tutakwenda sokoni kuuza kuni; hivyo hatuna chakula cha kukupa wewe – lakini kama uko tayari nitakusaidia kitu.”
Rahman alimwonesha shoka na kumwambia, “nitakuazima shoka langu, nami nitakufundisha kukata kuni, kisha nitakufundisha jinsi ya kuuza kuni sokoni.”
Akamwambia kuwa akishauza kuni atapata pesa kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine, na kwamba hatakuwa ombaomba tena na heshima yake itarudi.
Baada ya kuelewa somo, kwa shingo upande, ombaomba aliungana na Rahman, wakaenda msituni. Kijana akafundishwa kukata kuni na kuzifunga vizuri kwa ajili ya kuzipeleka sokoni.
Walipofika sokoni Rahman alimfundisha maskini yule mbinu za kuuza na kumwacha aendelee na mauzo. Ulipita muda mwingi bila kijana yule kuuza chochote hadi akapata hasira na kukata tamaa.
Alianza kuwaza, “yaani hawa vijana bora wangekuwa wakarimu – wangenipa chakula chao – ningekula nikashiba nakuachana nao, kuliko kuteseka namna hii hapa.”
Akiwa katika mawazo haya, ghafla likatokea gari likapiga breki karibu naye. Akashuka mzee mmoja aliyenunua kuni zake zote, akaziweka katika gari lake na kumkabidhi bunda la noti.
Akiwa haamini macho yake, alipokea pesa zile kwa furaha na haraka akamkimbilia Rahman kumwonesha alichopata.
Rahman alimpongeza kisha akampeleka kwenye duka la mashoka. Kijana alinunua shoka moja na kumshukuru Rahman kwa kumfundisha kazi na mbinu za kuuza.
Kwa vile alikuwa na njaa alinunua chakula cha kushiba, akala na kupumzika tayari kwa kazi ya kukata kuni kesho yake
Alipoondoka, Rahman alimgeukia Rahim na kumwambia, “angalia, tungempa chakula ombaomba yule angekula haraka, angeshiba na kurudi tena msituni kulala. Kesho angekuja tena kutuomba na angeendelea hivyo kila siku.”
“Kwa kumpatia ujuzi wa kukata kuni na kuuza, na kwa kumsaidia kupata shoka lake, tumempa vitu ambavyo vitampa chakula na mahitaji mengine siku zote – na sasa hatakuwa na njaa tena.”
Hatua ya kuchukua: msomaji unashauriwa kuzingatia msemo usemao “usimpe mtu samaki – bali mpe ndoana na mfundishe jinsi ya kuvua samaki.”
Hivyo… ndugu, rafiki au jirani akiwa na uhitaji unatakiwa kuwa makini ili umsaidie kitu ambacho kitampa suluhisho la kudumu la tatizo lake. Misaada mingine inalemaza akili kuliko kutatua matatizo. Je, nini maoni yako kwenye hili?
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.
Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Mobile: 0718219530










