
Habari,
Wafanyakazi wengi hutumia pengine zaidi ya nusu ya maisha yao, wakiwa katika ajira. Kutokana na hili, wengi hujikuta katika mshikamano mkubwa sana na kazi zao, kiasi cha wengine kusahau hata mambo yao binafsi, au kwamba iko siku watastaafu. Na kwa kuwa huutumia muda mwingi sana katika majukumu ya ajira zao, wakati wa kustaafu ukiwadia mara nyingi huwaacha wakiwa katika mazingira magumu. Wengi wao huwa kama wameshtukizwa hivi; kitu ambacho kuwaachia hofu na taharuki.
Kwa hiyo, kuyafahamu mapema, baadhi ya mambo yaliyopo au yajayo inasaidia sana katika kufanya maandalizi ya kuyapokea mambo hayo, au athari zake; pale yatakapotokea. Kwa muktadha huu, kuna takwimu hapa ambazo pamoja na kwamba zinaihusu zaidi Marekani, lakini zinaweza kuwa na manufaa hata kwetu. Matumizi ya takwimu za wengine husaidia pia kuwachochea watafiti wetu kupata pa kuanzia ili kuja na takwimu zetu.
Kwa mujibu wa tafiti kadhaa, ni asilimia 58 tu ya Wamarekani ambao wamejijengea tabia ya kuweka akiba kwa ajili ya maisha baada ya kustaafu. Kwa maana hiyo, asilimia 42 ya Wamarekani hawana mpango huo. Na sababu kubwa wanayoitoa ni kwamba fedha (mshahara) hautoshi hata kwa matumizi ya muhimu, sembuse kuweka akiba. Hata hivyo, wapo wanaodai kwamba jambo hilo (kuweka akiba) halina umuhimu sana kwao. Na hawa ndio wale, ambao wakistaafu hutegemea zaidi kuanza maisha yao mapya kwa pensheni peke zao tu; wengi wao wakiwa hawajajiandaa vya kutosha kwa maisha hayo, na hivyo hujutia baadaye, jinsi uzee unavyozidi kukomaa.
Upo utafiti pia uliofanywa Marekani, unaoonesha kwamba, kwa wale ambao wanaweka akiba ni asilimia 10 tu, ambao huweka akiba inayozidi asilimia 15 ya mapato yao ya kila mwezi; kwa ajili ya maandalizi ya kustaafu. Hii ina maana kwamba asilimia 90 ya Wamarekani huweka akiba chini ya asilimia 15 ya mapato yao. Naomba hapa kutumia mfano wa gharama za Tanzania kufafanua hili.
Yaani katika kundi hili; ina maana wafanyakazi wanaopata shilingi 1,000,000/-,wengi wao (asilimia 90) huweka akiba isiyozidi shilingi 150,000/- kwa mwezi. Hapa ina maana kwamba, wapo wanaohifadhi mpaka shilingi 10,000/- au chini ya hapo, kwa mwezi. Na kwa mtazamo wao, hiki ni kiasi kisichokidhi haja, linapokuja suala muhimu la kustaafu. Kwa takwimu hii tunaweza kujifunza kitu; kwamba ili tuweze kujiandaa vizuri kwa maisha ya kustaafu, kwanza tujijengee tabia ya kuweka akiba, lakini pia akiba hiyo iwe kiasi cha kutosha kwa kufanikisha maandalizi hayo muhimu.
Utafiti mwingine unaonesha kuwa Wamarekani kati ya asilimia 60 na 70, wamepata maarifa na mbinu za kustaafu kupitia njia ya mdomo pekee. Hii ina maana kwamba asilimia kubwa ya Wamarekani wanategemea zaidi mazungumzo yasiyo rasmi au marafiki, wengi wao wakiwa sio wataalamu wa masuala hayo; kwa ajili ya kupata maarifa au taarifa hizo. Hii inatuonesha umuhimu wa kuandaa mafunzo maalum, yaliyo rasmi kwa ajili ya wastaafu, ambayo yatatolewa pia na watu waliobobea katika fani hii, ili wastaafu wafundishwe ukweli wa mambo na uhalisia wa maisha ya kustaafu.
Kuna utafiti pia, unaosema kwamba asilimia kubwa tu, ya vijana (millenials) wa Marekani, ambao wanaishi kwa madeni yanayofikia dola 30,000 kwa mwezi (nje ya kodi na michango mingine ya kisheria); ilhali kipato (mshahara) chao ni dola 55,000 kwa mwezi. Nikitumia uwiano huo, naomba nitoe mfano wa Mtanzania, anayepokea shilingi 1,000,000/- kwa mwezi. Ukitoa madeni, ukatoa kodi, halafu ukatoa michango mingine ya kisheria; kijana huyu atapokea kama asilimia 30 tu, ya mshahara wake; yaani shilingi 300,000/- kwa mwezi.
Kwa mujibu wa utafiti huu, mengi ya madeni haya ya vijana ni fedha zilizokopwa kwa ajili ya kununua magari, sofa na fenicha za nyumbani, matembezi (trips), kununua mavazi na ‘simu kali’, na matanuzi; ingawa wapo wachache waliokopa kwa ajili ya kujiendeleza kielimu, na ujenzi wa nyumba. Kwa hiyo, bila kujali fedha imekopwa kwa ajili gani, kilicho muhimu hapa ni kwamba, kiasi cha fedha kinachobaki ni kidogo sana kumudu maisha ya kawaida kwa mwezi. Kwa kiasi hiki, sio rahisi kujiwekea akiba, hasa kwa maandalizi ya kustaafu.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2020, nchini Marekani, kuhusu utayari wa wafanyakazi kustaafu; asilimia 73 ya wafanyakazi waliohojiwa walidai kwamba wakisikia suala la kustaafu hufadhaika. Kwa hiyo ni asilimia 27 tu ndio walioonesha kujiamini. Kuhusu suala hili hili, kuna utafiti ulioonesha kwamba asilimia takriban 60 ya Wamarekani waliohojiwa kuhusu suala la kustaafu, walisema suala hili huwakosesha usingizi, wanapolisikia.
Upo utafiti mwingine unaoonesha kwamba asilimia 70 ya Wamarekani waliohojiwa walisema kwamba wangependa kuwa na kitu cha kufanya (shughuli mbadala) baada ya kustaafu. Hii inaonesha kwamba, ukistaafu kinachobadilika ni aina ya kazi tu, lakini suala la kufanya kazi linabaki! Hata hivyo, asilimia 60 ya waliohojiwa walisema kwamba wakistaafu wangeanzisha aina ya shughuli iliyo tofauti na ile waliyokuwa wakifanya kabla, ambayo pia ni nyepesi.
Ukifuatilia takwimu hizi utaona kwamba maandalizi kwa ajili ya maisha ya kustaafu ni muhimu sana. Maandalizi yana nafasi kubwa ya kuwaondolea wafanyakazi hofu, wanaposikia suala la kustaafu. Hii ni hofu ya maisha nje ya ajira waliyoizoea. Wapo wengine wasio na maarifa juu ya mtindo gani wa maisha waishi sasa (kazini), ili maisha yao uzeeni yaendelee kunawiri. Kwa sababu hii ndio maana kuna haja kubwa kwa wafanyakazi kupatiwa maarifa kwa ajili ya kustaafu ili wajenge weledi na kujiamini, wakijiandaa kustaafu.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530