
Habari rafiki.
Nimeshaeleza kupitia makala zangu kadhaa, kuwa ubunifu ni uwezo wa kufikiri, kutafuta majibu na kutatua changamoto kwa namna ya kipekee; na kwamba ubunifu ni matokeo ya kuufikirisha ubongo ili kupata njia mpya na nzuri zaidi za kutatua changamoto au tatizo lililobainika. Nimeeleza pia kuwa ubunifu una nafasi kubwa katika ujasiriamali.
Ubunifu sio kitu rahisi ‘ki-vile’; yaani eti kila wakati uibuke na bidhaa mpya yenye utofauti, au huduma mpya, au mchakato mpya wa uzalishaji au utoaji huduma. La hasha! Hata hivyo, siyo kitu kigumu! Panahitajika maarifa tu. Yaani ujue mbinu ipi itakupatia mawazo mapya na ya maana ya kibunifu kuweza kukuletea tija katika biashara au shughuli yako.
Zifuatazo ni baadhi ya mbinu ambazo ukizitumia zitakusaidia kuongeza uwezo wako wa ubunifu:
Kwanza, Kukopi au kuiga mawazo ya wengine. Hii ni njia rahisi kabisa ya ubunifu. Hapa ni kwamba unaiga kitu ambacho wengine walishakifanya hapo kabla. Kuiga huku haina maana ya kukopi na ku-paste, hapana! Hapa ninamaanisha kwamba unachunguza kitu kizuri kilichofanyika mahala fulani, halafu unakiboresha kidogo, kisha unakizalisha na kukitumia kwako. Kuiga huku tunaita ‘kuiga kimkakati’, ambayo ni mbinu nzuri ya kufanya ubunifu.
Kwa mfano, Henry Ford, mwanzilishi wa Kampuni ya magari ya Ford, alitembelea kiwanda kimoja cha kusindika nyama, Marekani, akaona mtiririko wa utendaji kazi na mpangilio wa mashine na wafanyakazi katika mnyororo mmoja, mtindo unaoitwa ‘assembly line production system’. Akavutiwa na ubora, uharaka, na unafuu wa gharama za uzalishaji kwa kutumia mtindo huu.
Aliporudi kwake, akatumia maarifa hayo kwenye kiwanda chake cha magari, kisha akaongeza ujuzi wake kidogo; akafanikiwa kupunguza muda na gharama kwa kiwango kikubwa. Huu ni ubunifu wenye tija unaotokana na kuiga.
Pili, kuuliza wateja wako. Ukiweka utaratibu wa kuwauliza wateja wako kwamba wangependa bidhaa au huduma zako ziweje, utapata mawazo mengi sana, ambayo ukiyachuja, unaweza kuyatumia kuboresha bidhaa au huduma zako.
Kwa mfano, wateja wanaweza kuuliza au kutaka vitu, urembo au madoido fulani yawepo katika bidhaa yako. Au wakataka uweke vitu fulani vitakavyoifanya bidhaa yako iwe rahisi kutumia, au yenye mvuto zaidi; kwa mfano, mpangilio wa rangi, harufu au ulaini wa kitambaa au bidhaa husika.
Hapa unatakiwa usikilize maoni yao kwa umakini uone ni maoni yapi ukiyafanyia kazi unaweza kuongeza ubora wa bidhaa yako na ukaongeza mauzo zaidi.
Tatu, wachunguze wateja wako. Usiishie tu kuwauliza, wachunguze pia! Angalia wanatumiaje bidhaa zako, au ni vitu gani wanavibadilisha wakishanunua bidhaa yako. Fanyia kazi majibu ya uchunguzi wako.
Hivi ndivyo mmiliki wa Kampuni ya nguo ya Marekani, Levi Strauss, alivyofanya baada ya wateja wake wa Jeans kuwa wanazichana Jeans zao sehemu fulanifulani. Alipoona hilo, haraka sana akaanza kutengeneza Jeans zilizochanywa, na mauzo yake yakapaa!
Nne, fuatilia malalamiko na changamoto za wateja. Sio wateja wote wanalalamikia bidhaa au huduma unazowapatia. Hivyo ukipata wanaolalamika usiwachukie, shukuru, na wasikilize kwa makini. Sikiliza, pia fumbua macho, uone matatizo au changamoto wanazolalamikia. Hapa utapata pa kuanzia kufanya ubunifu, na ukiweza kufanikiwa kuondoa changamoto hizo utaongeza imani ya wateja wako, wataona jinsi unavyowajali, na mauzo yatapanda sana.
Tano, unganisha au changanya bidhaa. Kuchanganya bidhaa moja na nyingine ni mbinu ya kuja na bidhaa mpya na yenye matumizi bora zaidi. Kwa mfano, simu za mwanzo za mkononi hazikuwa na kamera wala radio.
Hivyo, wabunifu katika Makampuni ya simu waliwaza na kuona uwezekano wa kuzalisha bidhaa moja yenye nyongeza ya vitu hivyo, ndipo wakaunganisha vitu hivyo na kuja na simu yenye kamera na radio. Na sasa vitu vingi zaidi vimeongezwa.
Ubunifu mwingine ni wa kuunganisha redio, cassete, mp3 au flash player, kupata bidhaa moja yenye upana zaidi wa matumizi. Uvumbuzi huu umewawezesha kuongeza thamani ya bidhaa hizo na kuongeza mauzo pia.
Sita, punguza vitu kwenye bidhaa zako. Katika hili, jiulize, ni vitu gani ukiviondoa kwenye bidhaa, mchakato au njia za usambazaji wa bidhaa yako, itafanya bidhaa hiyo ipate ubora zaidi. Kwa mfano, Amazon waliamua kuondoa uuzaji wa vitabu kwa kutumia maduka halisi ya kuuza vitabu. Wakabakiza uuzaji vitabu kwa mtandao, online retailing.
Mfano mwingine ni uamuzi wa kuondoa mwamba wa mbele, au kiti cha kubebea mizigo, kwenye baiskeli. Kumbuka wasichana wengi, hasa warembo wa mjini, hawapendi baiskeli zenye mwamba au zenye kiti cha nyuma,wakitaka kuendesha baiskeli. Kwa kuviondoa vitu hivi utajikuta unaongeza mauzo yako kwa kiwango cha juu.
Saba, angalia washindani wako. Waangalie kwa umakini washindani wako. Unaona wanafanya nini? Kipi kipya wanachokuja nacho? Una kitu cha kujifunza? Unaweza kuiga kimkakati? Unaweza kuboresha ukaja na kitu kipya na bora zaidi? Basi fanya hivyo.
Nane, geuza bidhaa za kizamani kuwa za kileo. Angalia huduma, mchakato au bidhaa iliyokuwa inatumika zamani, ambayo inaonekana imepitwa na wakati, kisha angalia jinsi unavyoweza kukirudisha kitu hicho au fasheni hiyo ya zamani, kwa kuifanyia mabadiliko fulani, ikawa bidhaa ya kileo na itakayowapa vionjo vipya watumiaji wa kileo.
Kwa mfano, ‘Dungarees dress’ ni vazi lililokuwa likivaliwa katika mazingira ya shamba au gereji, lakini wabunifu wamelichukua, wakalifanyia ukarabati kidogo, wakalitangaza kupitia kwa wasichana warembo, na sasa linapendwa na linavaliwa na warembo karibu kila mahala.
Kwa kumalizia, ubunifu ni chachu kubwa ya ujasiriamali na hivyo ili kuongeza tija katika bidhaa au huduma zako huna budi kuwa na maarifa na mbinu. Yaani ujue mbinu ipi itakupatia mawazo mapya na ya maana ya kibunifu kuweza kukufanya utengeneze bidhaa au utoe huduma bora zaidi itakayokuletea tija katika biashara au shughuli yako.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com








