
Habari,
Yupo mstaafu mmoja aliwahi kusema jambo fulani ambalo naona likidadavuliwa litasaidia kubadili namna wastaafu wanavyofikiri na wanavyofanya mambo yao, hasa ya kiuchumi, baaada ya kustaafu. Alisema, “nilipostaafu nililipwa pesa nzuri tu, mamilioni kadhaa. Lakini pia nilikuwa nimeshajenga na ninaendesha miradi midogomidogo; lakini cha kushangaza ndani ya mwaka mmoja mamilioni yangu yote yaliyeyuka na sikujua yameenda wapi.”
Aliongeza kwa kusema, “baada ya kugundua sina kitu mfukoni nilianza kutafakari…kwa nini? Nilianza kufanya utafiti mdogo, kuwafuatilia wastaafu wenzangu kadhaa, nikagundua siko peke yangu katika hali hii – na nilishangaa zaidi nilipowaona hata marafiki zangu waliosomea masuala ya fedha, nao ni matatizo tu. Fikiria mtu alikuwa na nafasi nzuri tu kazini halafu unamsikia akiomba hadi hela ya nauli; hili si jambo dogo!”
Naomba leo tujadili jambo hili, kwamba kwa nini watu wanaishiwa – tena muda mfupi sana baada ya kulipwa mafao yao ya kustaafu, pamoja na kwamba wengine tayari walishafungua miradi au biashara zao baada au hata kabla ya kustaafu, kwa lengo kwamba wajiingizie kipato endelevu kitakachochukua nafasi ya mshahara waliokuwa wakilipwa makazini kwao.
Kuna sababu kadhaa ambazo tunaweza kujadili hapa; kwamba huenda ndio sababu zinazofanya hali hii iwatokee wastaafu wengi. Zipo sababu zilizo nje ya uwezo wa wastaafu, lakini pia zipo sababu ambazo tunaweza kuziita za kujitakia, au uzembe. Naomba tuzijadili hapa:
Moja, matumizi mabaya ya fedha baada ya kustaafu. Katika hili Mtafiti mmoja anasema: “Asilimia 46 ya familia za wastaafu hutumia, kwa mwezi, kiasi kikubwa zaidi cha fedha, kuliko kilichotumika wakati mstaafu akiwa kazini.” Ukiyachunguza matumizi haya utakuta yanachochewa na kitu kiitwacho ‘show-off’ (kujionesha).
Wapo wastaafu ambao huwekeza fedha zao katika anasa au ulimbukeni mwingine wa maisha, kwa ujinga tu au kukosa nidhamu. Nawafahamu wastaafu waliowekeza katika ulevi, ufuska au ununuzi wa vitu vya anasa, kwa lengo la kujitutumua tu, au kuwakoga wabaya wao.
Ipo simulizi ya kweli inayomhusu afisa mmoja mstaafu wa taasisi moja ya serikali. Huyu alijipenda sana, na hakupenda kupitwa na kitu kizuri. Na hili liliweza kwenda alivyotaka kwa kuwa nafasi yake ilimwezesha, kupitia marupurupu aliyokuwa akipata, kwa hiyo alizoea maisha ya kuonekana mtu wa ‘matawi ya juu’. Alipostaafu aliendeleza mtindo ule ule wa maisha; na sasa alifanya hivyo kwa kukopa bila mpangilio. Alilipwa mafao miezi 11 baadaye na baada ya kulipa madeni yake yote alibakiwa na shilingi milioni tano tu benki. Kiasi hiki cha pesa hakikumtosha mstaafu huyu, si kwa matumizi yake tu, bali hata kuendeshea miradi, hivyo aliishia kufilisika.
Mbili, kutaka kubakiza hadhi aliyokuwa nayo kazini. Hili linafanana kidogo na hilo la kwanza hapo juu. Wakati hilo la kwanza linawalenga mahasimu; hili la pili linafanywa na mstaafu kuwaonesha waliobaki kazini kuwa kustaafu hakujabadilisha hadhi yake, na hivyo bado anaweza kuishi kwa staili yake ile ile ya zamani, bila kugundua kuwa kinachotoka kwa sasa ni kikubwa kuliko kinachoingia; kupitia miradi au kutoka katika akiba ya pensheni ya mkupuo au ya kila mwezi. Ndio maana utakuta mstaafu ghafla kipato kinakata, halafu anaanza kushangaa.
Tatu, kubeba majukumu yaliyopaswa kuwa yamekamilika. Watu wengi huanzisha familia wakishapata ajira. Baada ya muda kidogo majukumu yanayohusu watoto huanza. Moja ya jukumu linalowatesa wafanyakazi wengi ni gharama za kuwasomesha watoto wao. Na kwa wale wanaopenda, au waliojaliwa kuzaa watoto wengi, hili ni tatizo jingine. Suala la elimu ya watoto ni jambo muhimu sana, ingawa si kazi rahisi, na hasa linapokuja suala la gharama.
Ndio maana suala la uzazi wa mpango huingia. Mpango huu unahusu idadi ya watoto wanaopaswa kuzaliwa, na wazaliwe lini; ili jukumu la kusomesha lifanyike ndani ya kipindi cha ajira. Ukikosea katika hili utajikuta unaingia katika kustaafu na mzigo huu, na fedha hizi zitatokana na mapato ya miradi yako, ambayo pengine bado haijakomaa sawasawa, au zitatokana na pensheni yako. Sasa, hali ikiwa hivi huwezi kuepuka kuishiwa baada ya muda mfupi, na kubaki ukishangaa.
Nne, mafao ya pensheni kuchelewa kulipwa. Kiuhalisia suala hili lina mchango mkubwa kwa wastaafu wengi kuishiwa fedha muda mfupi baada ya kustaafu. Ingawa na wastaafu wenyewe wanastahili lawama fulani hapa. Ni ukweli ulio wazi kuwa wastaafu wengi, wakiwa kazini huwa hawana utamaduni wa kujiwekea akiba yoyote, kwa ajili ya maandalizi ya kustaafu. Wanachokipata kazini, mshahara na malipo mengine, humalizikia huko huko kazini.
Hivyo, wanapostaafu mshahara hukoma hapohapo, na hivyo mapato ya familia huwa yamekatika. Sasa mstaafu huyu ambaye ana familia ikimtegema huwa hana cha kufanya. Kwa kuwa mafao huchelewa, anachofanya ni kujipeleka kwa wakopeshaji ambao hukopesha kwa riba kubwa. Wastaafu huwa hawana jinsi bali kukopa; ingawa huwa wanajifariji kwa fikra kuwa fedha watakazolipwa mafao ni nyingi sana. Lakini wastaafu wengi wamelizwa na wakopeshaji hawa kwa kiwango cha baadhi yao kufilisika!
Anamtaja mstaafu mmoja (tumwite Jeijei) kwamba alishawishiwa kukopa shilingi milioni 6 kutoka kwa mkopeshaji mmoja tapeli. Pensheni ya mzee huyu ililipwa miezi kumi tokea alipokopa kiasi hicho cha fedha. Kawaida ya wakopeshaji hawa humtaka mkopaji awape kadi yake ya benki ya akaunti ya mshahara, ambamo mafao yakilipwa yatapitia.
Kwa hiyo mafao yalipolipwa, mkopeshaji alimpigia hesabu jeijei, iliyofikia shilingi milioni 27! Mafao aliyolipwa Jeijei yalikuwa shilingi milioni 49, hivyo mkopeshaji alimbakizia Jeijei shilingi milioni 22 na presha juu yake! Takukuru ndiyo iliyomnusuru Jeijei. Iliingilia kati baada ya kupata malalamiko kupitia watoto wa Jeijei, akaweza kurudishiwa fedha yake; na ndipo alipoanza tena kupumua kwa faraja!
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com









