Je, Wajua? Hizi Ndizo Sababu Za Biashara Nyingi Kufa

Habari rafiki yangu,

Karibu tena katika makala nyingine inayolenga kukupatia maarifa ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Kutokana na hamasa, ukosefu wa ajira au hali ngumu ya maisha, vijana na watu wazima pia wameendelea kuzitafuta fursa na kuingia katika ujasiriamali au biashara kwa lengo la kujipatia kipato na kuboresha maisha yao.

Umakini unatakiwa katika uendeshaji wa biashara la sivyo itadorora hadi kufa

Hata hivyo, tafiti zinaonesha kuwa biashara nyingi zinazoanzishwa hufa ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake. Je unalijua hili? Fuatana na mimi ili uzifahamu sababu hizi, na ukizijua itakusaidia kujipanga ili usifikwe na dhahama hii. Kusudi langu hapa ni kwamba maarifa haya yatakusaidia kuchukua tahadhari mapema, na hii itakusaidia kuinusuru biashara yako iondokane na hatari ya kufa.

Wataalamu wanatuambia kuwa biashara nyingi hufa kutokana na matatizo yanayotokana, kwa kiasi kikubwa, na wafanyabiashara wenyewe. Maana yake hapa ni kwamba mchawi wa biashara huwa hatoki nje, bali yumo ndani ya mfanyabiashara mwenyewe. Ni sawa na msemo maarufu usemao, “kikulacho ki nguoni mwako.”

Zifuatazo ni baadhi ya sababu hizo ambazo mojamoja, au kwa pamoja, zinaweza kusababisha biashara yako kufa:

Moja, kutokuwa na elimu au uelewa mzuri wa biashara. Nimeandika huko nyuma kuhusu umuhimu wa elimu ya ujasiriamali. Nimeeleza kuwa elimu ya ujasiriamali inahitajika na ina umuhimu mkubwa, kwani ina msaada mkubwa katika kumpatia mjasiriamali umahiri katika kuanzisha, kuendesha, kuchambua na kutathmini mwenendo wa biashara yake, na kufanya marekebisho mapema ikibidi.

Nimesema kwamba elimu hii inamjengea mjasiriamali uwezo wa kujiamini, kuhoji na kutambua fursa na changamoto kwa uhakika. Elimu hii inamsaidia mfanyabiashara kufungua na kutanua akili yake ili ifikie uwezo wa juu wa kufikiri na kutafakari mambo.  Kwa hiyo nikahimiza kuwa kila mtu anapaswa kuitafuta kwa bidii.

Elimu au maarifa ya ujasiriamali yanapatikana kwa kujifunza kupitia mitandao, vitabu, majarida, blog, kuhudhuri semina na kupitia kwa wajasiriamali waliofanikiwa, au hata waliofeli.

Pili, kukosa umakini katika matumizi ya rasilimali na hasa fedha. Ukiwa mfanyabiashara unapaswa kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika matumizi ya rasilimali zako. Ukitumia fedha bila mpangilio mzuri zitapotea au utaziweka katika matumizi yasiyo ya lazima na hazitaweza kuzalisha tija katika biashara yako. Hii ni hasara tayari. Rasilimali nyingine ni muda, nyenzo za kutendea kazi, wafanyakazi n.k. Hivi vyote vinahitaji umakini wa hali ya juu katika mipangilio na matumizi yake.

Tatu, kukosekana kwa ubunifu. Nimeandika kupitia makala zangu umuhimu wa ubunifu katika uendeshaji wa biashara. Kuna ushindani mkubwa ziku hizi katika kila biashara unayopanga kufanya. Hivyo unapaswa kuja na vitu vya ki-bunifu kila siku ili uushinde ushindani huo. Jifunze kujitofautisha na kujiongeza ili ufanye vitu kwa ubora na umahiri wa juu.

Nne, kushindwa kulijua soko la bidhaa zako na kuitangaza biashara. Unapoanzisha biashara yoyote unapaswa kujua soko lako ni lipi; yaani nani atanunua bidhaa yako?. Hili linahitaji utafiti kidogo. Usipolijua soko utashindwa kupata wateja na biashara itayumba. Vivyo hivyo, ukishindwa kuitangaza biashara au bidhaa yako ni wazi haitajulikana.

Tano, kushindwa kutoa huduma nzuri kwa wateja. Kumbuka wateja ndio pesa katika biashara. Jiulize, bila mteja kuja, pesa itaingiaje katika droo yako ya dukani? Jifunze jinsi ya kuwavuta wateja na kuwabakiza. Usifanye mambo yatakayowafukuza wateja wako, hakikisha wanavutiwa na huduma zako na wanakusaidia kuitangaza kwa wenzao pia.

Sita, kukosa vipaumbele. Hili ni tatizo kwa wajasiriamali wengi. Wapo wanaotaka kufanya kila kitu kwa wakati mmoja. Yaani wangependa kuanzisha biashara zaidi ya moja kwa wakati mmoja. Ukifanya hivi ujue zitakwama zote! Kufanya hivi ni kukosa ‘focus’ yaani ni kupapasapapasa tu. Weka vipaumbele; yaani chagua uanze na ipi, kwa kuanzia – halafu angalia nini kifuatie baada ya hii kusimama chenyewe.

Saba, kushindwa kupambana na changamoto za biashara. Katika biashara kuna changamoto nyingi. Ndio maana nimekuwa nahimiza kujifunza ubunifu. Mbunifu ni mtu anayefikiri ki-udadisi kila siku. Kwa kufanya hivi ni wazi utavibaini vihatarishi au changamoto zinazonyemelea biashara yako na kuja na mbinu za kupambana nazo kabla hazijakufanya ukwame katika biashara yako.

Nane, uchaguzi mbaya wa eneo la biashara. Katika kusaka eneo la biashara unaweza kujikuta umepata eneo lililo mbali na wateja wako, au lisilo salama, au lililokatazwa kisheria. Hili likitokea kuna hatari ya kukosa wateja au kupata hasara, na kufanya biashara yako izorote hadi kufa.

Tisa, kushambuliwa na majanga ya asili kama mafuriko n.k. Hii ni sababu inayotokana na mazingira yaliyo nje ya mfanyabiashara, ingawa mfanyabiashara ana nafasi ya kuweza kufanya kitu mapema ili kuokoa biashara yake isiathirike. Kwa mfano, huwa kuna tahadhari zinazotolewa na watabiri wa hali ya hewa wakisema kutakuwa na mvua kubwa na vimbunga, hivyo watu wahame au wachukuwe tahadhari fulani. Usipochukua tahadhali ni wazi madhara yatakupata.

Ushauri wangu: Biashara nyingi hufa katika kipindi kifupi baada ya kuanzishwa kutokana na matatizo ambayo yanaweza kuzuilika; yaani yamo ndani ya uwezo wa mfanyabiashara mwenyewe. Kwa hiyo ni muhimu kila mfanyabiashara awe makini na mdadisi katika kuzibaini fursa na changamoto mbalimbali zinazojitokeza, na kufanya vitu sahihi, kila siku katika uendeshaji wa biashara.

Jinsi Hamu Ya Kujifunza Inavyomchochea Mjasiriamali Kufanya Ubunifu

Rafiki mpendwa,

Karibu tena katika mfululizo wa makala zangu zenye lengo la kuelimishana kuhusu masuala ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Katika makala hii nitazungumzia jinsi ambavyo mjasiriamali anavyoweza kujenga uwezo wa ubunifu kutokana na hamu au hamasa ya kujifunza aliyojijengea ndani yake. Matokeo ya kujifunza ni kupata elimu au maarifa na kuitumia elimu hiyo kufanya mabadiliko yenye tija.

Elimu, kwa maana pana, ni tendo au uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile wa mtu binafsi. Katika dhana ya kiufundi, elimu ni njia ambayo hutumiwa makusudi na jamii kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Ukipenda kutembelea maonesho ya biashara utajifunza mengi

Kujenga hamu au hamasa ya kujifunza ni moja ya njia muhimu za kuelimika na kuweza kufanya mabadiliko mbalimbali. Umuhimu wa kujifunza unaweza kuthibitishwa kupitia kwa Mjasiriamali na Mbunifu, Bi. Subira Mwaruka, ambaye ni mbunifu wa vikapu vya kupikia.

Kwa kawaida kikapu ni chombo kinachotumika hasa na kina mama wakienda sokoni au gengeni kununua chakula kwa matumizi ya familia. Je, umewahi kufikiria kuwa kikapu kinaweza kutumika kuivishia chakula? Huwezi kuamini, lakini Subira, akinukuliwa na gazeti moja, anasema kwamba kikapu maalumu alichobuni kina uwezo wa kuivisha hata maharage.

Yaani, unachemsha maharage kwenye moto wa kawaida, mfano gesi, kwa dakika tano hivi, halafu yakishachemka, unaipua na kuyafunika maharage yako ndani ya kikapu hiki, na baada ya kama masaa mawili, ukiyatoa maharage katika kikapu utakuta yameiva kabisa.

Anasema kuwa chakula kilichopikwa katika kikapu hiki, mfano wali, hakina ukoko, hakiungui na wala hakipotezi ladha yake.

Subira anasema, “kila penye nia pana njia, kwani jitihada zangu za kutamani kujifunza na kufanya vitu ki-utofauti, imenisaidia sana kuwa mbunifu.” Anadai pia kuwa hamu aliyonayo na jitihada za kuhudhuria maonesho yanayowakutanisha wajasiriamali kutoka nchi mbalimbali imemuwezesha kujifunza mengi na kuwa mdadisi.

“Kila ninapohudhuria maonesho, hulazimika kutafuta kitu kipya cha kujifunza, ambacho ni kigeni katika soko la Tanzania. Ukweli nina hamu ya kujifunza kitu kipya kila siku, hivyo mawazo ya ki-bunifu nayo huja kila siku, “ anadai Subira.

Subira, mbunifu wa teknolojia ya vikapu vya kupikia anasema kwamba hii ni teknolojia nzuri na rahisi ambapo kikapu, kilichotengenezwa kwa ukindu au malighafi nyingine, hufanyiwa utaalamu ambao hukifanya kiwe na uwezo wa kutunza joto la chakula muda mrefu, kiasi cha kuweza kuivisha chakula cha aina yeyote ile.

Anasema, “kuna material (malighafi) tunaiweka kwa utaalamu ndani ya kikapu, inayofanya kiweze kutunza joto kwa muda wote.” Anadai kwamba ujuzi huu aliupata baada ya kuhudhuria maonesho ya Wajasiriamali huko Kenya. Huko aliona vitu ambavyo wengine wanafanya. Aliona jinsi wanavyoongeza thamani ya bidhaa za kawaida zikawa bidhaa bora na zenye tija na mvuto zaidi kwa wateja.

Subira amepata faida kubwa baada ya kupata maarifa haya kupitia elimu. Yeye binafsi ameongeza thamani ya vikapu vyake na kuongeza mauzo kwa kiwango kikubwa.

Lakini pia, ubunifu wake umefanya matumizi ya vikapu vyake kuokoa matumizi ya nishati ya mkaa na kuni. Anasema ubunifu huu umempunguzia mama muda mwingi wa kukaa katika moto, na kumuepusha na magonjwa yatokanayo na moto au moshi.

Zaidi ya hayo, ameongeza kipato kwa kujiajiri katika kazi ya kutengeneza na kuuza vikapu, na pia anaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali na ubunifu kwa Wajasiriamali wengine waliopata hamasa ya kupata ujuzi huu.

Kwa hiyo, kuna somo kubwa la kujifunza kupitia kwa Bi. Subira. Kwanza, Mjasiriamali unapaswa kujitambua na kujitengeneza. Unapaswa kujenga hamu ya kutaka kujua mambo mbalimbali yanayolenga kuongeza thamani ya vitu, na kutatua changamoto zilizopo. Unapaswa kuwa na hamasa ya kujifunza vitu vipya, kila siku.

Pili, unapaswa kufungua milango yako yote ya fahamu ili iweze kuona, kusikia, kunusa na kuhisi vitu vyenye manufaa, na kuvifanyia kazi.

Ukijenga hamasa ya kujifunza na kuvuna maarifa, utapata uwezo wa udadisi utakaokufanya uanze kuona au kusikiliza vitu kwa mtazamo tofauti, mtazamo wa ki-dadisi, wenye lengo la kujifunza zaidi, kujenga taswira akilini, na kufanya vitu vitokee kiuhalisia. Na hii ndio hasa dhana ya ubunifu.

Nakukaribisha tena msomaji wangu katika mfululizo wa makala zangu za ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha, ili uendelee kupata maarifa na kufanya mabadiliko yako binafsi na jamii kwa ujumla.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com

 

Ubunifu Katika Mapenzi – Je, Wajasiriamali Tuna Cha Kujifunza Kwenye Hili?

Rafiki mpendwa,

Karibu tena katika mfululizo wa makala zangu zenye lengo la kuelimishana kuhusu masuala ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Nikiwa napitia makala mbalimbali katika gazeti moja la michezo nilikutana na makala moja iliyonivutia. Makala hii naweza kusema inahusu ‘mbinu za mchezo wa ndoa’. Hata hivyo, kichwa cha habari cha makala hiyo kilikuwa, ‘njia za ubunifu za kuyafanya mahusiano yako yasichoshe’.

Ubunifu katika mahusiano ya ki-mapenzi ni chachu ya kudumisha mapenzi yenu

Nilivutiwa na waudhui ya makala hiyo kwa kuwa yalisisitiza umuhimu wa watu kuwa wabunifu na kwamba wasiridhike kufanya vitu au mambo kwa mtindo uleule, kila siku. Mwandishi wa makala hiyo, nadhani amebobea katika utaalamu wa ‘mahaba’, lakini pia anajua umuhimu wa suala zima la ubunifu katika maisha ya binaadamu.

Maudhui ya makala ile yanatoa mafunzo mengi, sio tu kwa wanandoa – ili wadumishe ndoa zao na kujenga upendo endelevu, bali pia yanatoa mafunzo mengi kwa wajasiriamali.

Alianza kwa kuandika, “ili mahusiano ya ndoa yawe bora na yalete msisimko, ubunifu ni kitu muhimu sana. Bila kuwa mbunifu, makini na mwenye kujua jambo gani lifanyike, ulifanye vipi, na kwa wakati gani, basi mahusiano yako hayataweza kukupa kitu bora unachotamani kukipata.”

Aliongeza kwa kusema, “ili mwenzio asikuchoke katika mahusiano inabidi ujue kucheza na akili yake.” Hata hivyo, tathmini zinaonesha kuwa watu wengi walio katika mahusiano kwa zaidi ya miaka mitatu wanakabiliwa na tatizo la kuchokana.

Hili linachangiwa na wapenzi husika kutokuwa wajanja na wabunifu. Yaani, mambo yale ya jana na juzi wanataka wayafanye leo na kila siku, na matokeo yake ni kwamba mahusiano yao yanapoteza ladha na ule msisismko uliokuwepo zamani.

Mwandishi anasisitiza kuwa hata kama matendo yako ni mazuri kwa kiwango gani lakini kama unayafanya mambo kila siku kwa mtindo ule ule yatachosha tu. Akitoa mfano wa chakula unachokipenda sana anasema, “japo kinakupa msisimko kinywani mwako na utamu katika ulimi wako, lakini kama utakula kila siku kwa mtindo huohuo mmoja wa mapishi kitapoteza ile thamani iliyopo katika fikra zako.”

Kwa maelezo hayo, Wajasiriamali hapa tunapata mafunzo makubwa. Kupitia mfano huu utaona umuhimu wa kufikiri kwa kina tena mfululizo, ili kila siku uje na vitu vipya au ufanye vitu vilivyopo kwa mtindo tofauti. Hii itasaidia kuongeza thamani ya vitu hivyo katika hisia na mitazamo ya wateja wako.

Mwandishi hakuishia hapo, anasisitiza, “tambua mahusiano ya raha yanatakiwa yajengwe katika msingi wa ubunifu na ujanja. Kama huwezi kumfanya mwenzio ajihisi ana amani na raha kila siku, huwezi kuwa na udhibiti halisi juu yake – atakuwa na wewe ndani, mtalala kitanda kimoja, ndani ya shuka moja, ila ndani ya nafsi yake bado atakuwa anahangaika na kuweweseka juu ya nani ampe raha halisi. Hivyo ukitaka mahusiano yadumu, jifunze utundu, mfanyie mwenzio utundu fulani hivi, hadi apagawe.”

Hapa kuna mafunzo makubwa kwa wajasiriamali. Usione kwa kuwa watu wanaijua bidhaa au huduma yako na labda huja kuinunua, basi ukadhani wataifurahia bidhaa yako siku zote. La hasha! Huenda tayari wameshakinaishwa nayo, na labda tu hawajapata bidhaa mbadala mahala pengine. Sasa basi, ikitokea wakaipata, wataachana na bidhaa yako na huenda wasirudi tena.

Mwandishi anadai, “kupendana haitoshi, kulala pamoja haitoshi, kujifunika shuka moja haitoshi; nenda zaidi ya hapo umfanye mwenzio akuone kama kitabu kipya ama filamu mpya au safari ambayo hujawahi kusafiri. Mtilie utundu na chachandu!”

Lakini pia, tunaambiwa na wataalamu wa saikolojia kwamba kuna ushahidi kuwa wapenzi husalitiana huku wakiwa bado wanapendana, kisa? Kukosa ubunifu katika mahusiano!

Mjasiriamali pia una hatari kubwa ya ‘kusalitiwa’ na hata kukimbiwa na wateja wako kwa kuwa wateja mara zote wanapenda kupewa huduma au vitu vipya, vyenye radha na vionjo tofauti. Wanapenda ‘chachandu’. Wakigundua huna kipya – wewe kila siku mtindo wako ni uleule, bidhaa au huduma zako zina radha, rangi, au muundo ule ule kila siku, watachoka, watakinai, na mwisho ‘watasepa’!

Mwandishi anasema mapenzi ni sanaa, na daima hakuna sanaa bila ubunifu, utundu na ufundi. Kwa hiyo unapaswa kuwa mbunifu kwa kila jambo la kimapenzi ili mwenzio ajione yuko katika msitu wenye vitu vya kustaajabisha, kuvutia na kutia hamasa katika maisha yake.

Vivyo  hivyo kwa ujasiriamli, ambapo ujasiriamali ukifanywa kwa mtindo wa usanii – ubunifu hujitokeza; ambao utakufanya kila siku utengeneze fikra mpya kisha uje na vitu vipya, bidhaa au huduma, ili mteja wako ajione yuko katika msitu wa kustaajabisha na kutia hamasa kila siku.

Mteja huyu atajenga utii au ‘loyalty’ kwa bidhaa au biashara yako, na atahamasika kuwavuta wenzake kuzipenda na kuzinunua bidhaa au huduma zako, na mwisho wa yote ni kwamba biashara yako ‘itapaa’!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com