Habari rafiki,
Karibu tena katika makala nyingine inayolenga kukupatia maarifa ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.
Biashara yoyote unayofikiria kuanzisha tarajia kukutana na ushindani, sasa au hata baadaye. Huwezi kulikwepa hili, ni suala la kawaida.
Je ukikutana na ushindani – tayari unaacha kufanya biashara? Hapana! Biashara ni akili na mipango. Ikitokea hali hii usikonde, unapaswa kuishughulisha akili yako. Inakupasa kupanga kufanya kitu tofauti.

Kuna mbinu za kiubunifu ambazo mjasiriamali akizitumia anaweza kuibuka na bidhaa au huduma ambazo ni za kipekee zinazoweza kumfanya ajipambanue miongoni mwa washindani.
Moja ya mbinu za kibunifu za kupambana na ushindani katika soko ni kutengeneza ushirikiano wa kibiashara kati ya makampuni au biashara zinazofanya shughuli tofauti-tofauti.
Ushirikiano huu utatengeneza nguvu moja kubwa ambayo itawasaidia wote kujiweka juu ya upinzani uliopo.
Kampuni za Mastercard, BancABC na Vodacom ni mfano mzuri wa makampuni yaliyojipambanua katika kujali suala la ubunifu kupitia ushirikiano, na kulitekeleza jambo hili kivitendo.
Mastercard ni kampuni iliyojikita katika teknolojia ya kuwezesha malipo ya kimataifa. BancABC inajishughulisha na utoaji wa huduma za kifedha, na Vodacom ni kampuni ya mawasiliano ya simu za mkononi.
Suala ya ununuzi wa bidhaa hasa za kimataifa, kwa njia ya mtandao, nchini Tanzania halikuwa suala la kawaida; lilikuwa linatazamwa na wengi kama ndoto hivi, yaani haikuwa rahisi.
Ushirikino baina ya Makampuni haya matatu, yenye utaalamu na rasilimali tofauti, umefanikisha utengenezaji wa kadi ya kwanza iitwayo M-Pesa Virtual Card, inayowezesha manunuzi ya mtandaoni.
Kwa mujibu wa msemaji wa Vodacom, huduma ya M-Pesa kutoka Vodacom imeendelea kuwezesha upatikanaji wa uhakika wa huduma za kifedha. Hata hivyo imekuwa ni ngumu pale linapokuja suala la kulipia manunuzi mitandaoni, hasa kupitia tovuti za kimataifa.
Uzinduzi wa Virtual Card, mwaka 2018, kupitia M-Pesa ni ubunifu ulioleta mapinduzi makubwa katika manunuzi ya mtandaoni. Hili limewezesha kuondokana na kikwazo cha kulazimika kuwa na akaunti ya benki; na pia hatari ya kulazimika kuweka taarifa za kibenki, za mteja, mtandaoni.
Ubunifu wa kadi hii umelenga kuwawezesha wateja wa M-Pesa kufanya malipo kwenye tovuti za hapa nyumbani, na zile za kimataifa, bila kuhitaji kuwa na akaunti ya benki au kadi ya mkopo (credit card).
Kupitia ubunifu huu, mteja anaweza kutengeneza Virtual Card na kuijaza pesa kupitia mfumo wa M-Pesa, na ikawa tayari kwa matumizi. Hii inamaanisha kuwa sasa watu wengi zaidi wataweza kufanya malipo bila kuhitaji kuwa na pesa taslimu.
Sasa swali, je wewe mjasiriamali unayefanya shughuli yako yoyote ya kijiingizia kipato, una cha kujifunza kupitia ubunifu huu? Ukweli kipo cha kujifunza.
Wakati fulani huwa tunaambiwa kwamba kidole kimoja hakivunji chawa. Kwa hiyo wajasiriamali wanapaswa kuongozwa na mawazo chanya kila wakati. Wanatakiwa kuangalia pande zote ili waweze kuona nini kinafanyika, wapi, na kinafanywa na nani.
Uamuzi wa kuunda ushirikiano wa kibiashara ili kufanya uboreshaji wa bidhaa au huduma ni uamuzi unaotokana na uwepo wa watu wanaofikiri kwa mtazamo chanya, ndani ya Kampuni.
Hili linafanyika pale mjasiriamali mmoja mwenye ujuzi au bidhaa fulani anakaa na mjasiriamali mwingine mwenye ujuzi au bidhaa nyingine, na kufanya mjadala wenye lengo la kuunda bidhaa mpya itakayoongeza thamani ya bidhaa au huduma ya kila mshirika.
Ubunifu wa aina hii una nafasi kubwa ya kuwawezesha washirika kuunda bidhaa mpya inayoweza kuliteka soko vizuri na haraka zaidi, na kila mmoja akanufaika ipasavyo.
Hatua ya kuchukua; kama yalivyofanya makampuni haya matatu, mjasiriamali unapaswa kujifunza kutazama huku na kule ili uweze kuona ni kampuni au biashara gani unaweza kuhitaji kuomba ushirikiano nayo utakaowezesha wewe na yeye kunufaika kibiashara.
Ushirikiano wa makampuni katika masuala kama ya teknolojia, malipo, huduma za fedha n.k ni moja kati ya mikakati muhimu inayolenga kuongeza tija kwa makampuni husika, lakini pia kwa wateja wao.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com








