Zijue Stadi Muhimu Za Maisha Kwa Kijana…(1)

Habari rafiki,

Ujana unaelezewa kama kipindi cha maisha ya mtu kati ya utoto na utu uzima, ingawa umri ambao mtu anahesabiwa kuwa ni kijana unatofautiana duniani kote.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, mtu anakuwa kijana akiwa na umri kati ya miaka 15 na 24. Na kwa mujibu wa Alternative Homes for Youth, umri wa kijana ni kati ya miaka 13 na 19.

Kwa muktadha wa makala hii nitajadili stadi muhimu ambazo kijana wa kiume na kike anatakiwa kuwa nazo anapokuwa katika umri wa miaka 13 hadi 19. Kwa kiingereza kijana huyu anaitwa teenager.

Kama wewe ni kijana uliye katika umri huu, kuna mambo au stadi ambazo unapaswa kuzifahamu ili upate maarifa sahihi juu ya maisha yako na uweze kuwajibika kikamilifu.

Kijana anahitaji stadi muhimu kama kupanda na kutunza miti na maua katika mazingira ya nyumbani

Na kama wewe ni mzazi basi ujuwe una wajibu wa kuhakikisha kijana wako anapata stadi hizi ili zimsaidie kuwa kijana bora, anayejitambua na anayeweza kuwa tegemeo kwa jamii na Taifa.

Maisha yanakwenda mbio sana na siku hazigandi. Kijana utashangaa, kabla hujakaa sawa, tayari unajikuta wewe ni mtu mzima. Sasa, kama hukujiandaa vyema, ukapata stadi muhimu, utajikuta unaonekana kituko.

Kwa upande wa mzazi, usije kushangaa kumwaona kijana wako anaishi maisha ya ovyo, yasiyo na mpangilio wala maadili; yaani anakuwa na tabia zinazoudhi na zisizompatia heshima katika jamii anamoishi.

Sasa, kama unataka kumsaidia mwanao asipatwe na fedheha katika maisha yake, wala asikutie aibu wewe mzazi wake, basi msaidie kupata stadi hizi.

Katika makala hii nitajadili stadi tano kama ifuatavyo:

Moja, usafi binafsi na utanashati. Nimejadili huko nyuma kuwa mtoto anaanza kufundishwa suala la usafi kabla hajatimiza miaka 10.

Mtoto anapofikisha umri wa ujana bado mzazi unapaswa kutia msisistizo ili kijana aweze kufanya usafi mwenyewe pasipo kusimamiwa. Hivyo msisitize kijana wako kuwa mtanashati.

Kwa kijana wa kiume na kike; vitu kama kuoga, kufua, kupiga pasi, kukunja nguo na kuzipanga kabatini, kunyoa au kuchana nywele n.k, ni vya lazima.

Kwa wasichana kuna masuala kama kusuka na yale yanayohusu usafi wakati wa hedhi, kwake yeye binafsi na kwa mazingira.

Pili, usafi na uboreshaji wa mazingira. Kijana wako anatakiwa kujua kufanya usafi na kuboresha mazingira ya ndani na nje ya nyumba.

Ajue kukwatua majani kando ya nyumba; kuzoa taka na kuzihifadhi sehemu sahihi; usafi wa chumba, choo na jiko; na kuondoa vikolokolo vilivyozagaa bila utaratibu nje na ndani ya nyumba.

Tatu, elimu ya afya binafsi na huduma ya kwanza. Kuwa na uwezo wa kujali afya yake binafsi na ya wenzake ni kitu cha msingi kwa kijana.

Elimu ya lishe bora, yaani ale chakula gani na kwa utaratibu gani; maarifa ya kuepuka magonjwa; na jinsi ya kutibu magonjwa madogomadogo kama mafua, homa na michubuko ni vitu muhimu kufahamu.

Maarifa ya kutoa huduma ya kwanza; kama kusafisha kidonda, kufunga bandeji na kumsaidia mtu aliyeungua kawaida na moto ni muhimu pia. Ajue pia kuwa tatizo likizidi uwezo wake atafute msaada wa daktari.

Nne, maarifa ya jamii na tabia njema. Usisubiri hadi kijana wako apewe majina ya ajabu-ajabu kutokana na tabia zake. Mfundishe mwanao tabia na maadili mema.

Mfundishe heshima na unyenyekevu kwa watu wote. Mfundishe kusalimia kila mtu kulingana na umri wake. Mpe maarifa ya kumkaribisha mgeni na kumhoji ili apate taarifa muhimu.

Msaidie kijana wako ajue kuishi vizuri na watu wote, na ajue kujenga urafiki bora. Ajue pia kutoa mawazo yake na kuheshimu mawazo ya wengine, na kujiepusha na lugha chafu kama matusi, kejeli na umbeya.

Tano, maarifa ya kupangilia mambo yake. Mtu akizoea kufanya mambo bila mpangilio hupoteza muda na rasilimali nyingine bila sababu.

Mfundishe kijana wako kuwa na mpangilio wa kazi na vitu vyake. Ajue ratiba ya kufanya kazi zake; yaani nini kifanyike, wakati gani, na kwa utaratibu gani.

Ajue kuweka kila kitu mahala pake, yaani vitu vinavyofanana vikae sehemu moja. Mpangilio mzuri unapendezesha mazingira, unafanya kila kitu kujulikane kilipo, unaondoa msongo wa mawazo na kufanya vitu vifanyike kwa wakati.

Hatua ya kuchukua leo. Malezi kwa kijana wako ni wajibu wako mzazi. Lakini pia ni wajibu wa kijana mwenyewe kujitambua mapema na kuchukua hatua ya kujifunza stadi muhimu za maisha.

Ukitimiza wajibu wako mapema na ukamfanya kijana wako kuwajibika utamtengeneza kuwa mtu bora katika jamii.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Jinsi Ya Kushughulika Na Wateja Waliokasirika

Habari rafiki,

Binaadamu kukasirika au kupatwa na hasira ni kitu cha kawaida. Na sio binaadamu tu, hata wanyama na wadudu hukasirika pia. Hivyo hasira, au mhemko ni hali isiyoepukika inayotokana na hisia hasi juu ya kitu au jambo.

Wataalamu wa saikolojia wanasema binaadamu ndiye kiumbe ambaye hupatwa na hasira mara kwa mara kuliko viumbe wengine na hasira yake huchukua muda mrefu hadi kuisha.

Siyo jambo la ajabu kuona wateja wamekasirika kwa kiwango cha kuogopesha

Katika uendeshaji wa biashara, wateja ndiyo pesa yenyewe. Biashara ikikosa wateja ni wazi itayumba.

Sasa, tunapoongelea suala la wateja tunazungumza kuhusu binaadamu – na binaadamu ana tabia ya kukasirika.

Kuna sababu nyingi za kukasirika. Zipo zilizo halali na zile ambazo si halali – lakini zote ni hasira.

Kwa mfano kuna wateja wanaokasirika wakijibiwa vibaya, na wapo wanaokasirika wasipopewa huduma haraka. Wapo pia wanaokasirika wanapogundua hawasikilizwi au wanapuuzwa.

Hata hivyo, wapo pia wateja ambao hukasirishwa na sababu ndogondogo zisizo na msingi. Mara nyingi watu hawa huwa wana msongo wa mawazo na huhitaji kitu kidogo sana ‘kumgusa’ ili hasira yake ipande.

Sasa, jinsi wewe mfanyabiashara unavyoweza kushughulika na hali hizi ndivyo jinsi unavyotengeneza mazingira ya kuwabakisha au ‘kuwafukuza’ wateja wako, na pengine wasirudi tena.

Mbinu zifuatazo zitakusaidia kushughulika na changamoto za wateja waliopandwa na hasira.

Moja, tulia na jizuie kupandwa na jazba. Ukishagundua kuwa mteja amepandwa na hasira – tulia kabisa! Usijaribu kumjibu haraka. Kila binaadamu ana jazba – jizuie na jazba kwa kuwa mtulivu.

Pili, usifikirie kuwa mteja ana ugomvi na wewe. Mteja anapopatwa na ghadhabu akiwa katika biashara yako huwa hana ugomvi na wewe.

Hasira zake hutokana na kutokuridhika na huduma yako mbovu. Hivyo usianze kujifikiria wewe, fikiria nini biashara yako haikumfanyia mteja wako.

Tatu, tumia kipaji chako cha kusikiliza. Kitu cha kwanza kabisa anachohitaji mteja aliyekasirika ni kutiwa matumaini. Anahitaji kuliwazwa – na ili kufanya hili ni lazima uwe fundi wa kusikiliza.

Kumsikiliza mteja kwa umakini hushusha hasira za mteja haraka, hasa anapogundua unamjali na unajitahidi kumwelewa.

Kumsikiliza mtu ni pamoja na kutumia kwa usahihi lugha ya mwili. Simama wima, mwangalie mteja usoni wakati anaorodhesha malalamiko yake, na usikunje mikono kwa staili itakayoonesha unamdharau.

Nne, onesha kusikitishwa na yaliyomsibu mteja. Kila wakati jiweke katika nafasi ya mteja. Akishashusha hasira muoneshe kuwa jambo alilofanyiwa halikuwa zuri na hakupaswa kufanyiwa hivyo.

Tano, omba msamaha wa dhati. Usiishie kusikitishwa tu na yaliyotokea, nenda hatua moja zaidi kwa kumuomba msamaha wa dhati. Usijali sana kama ulikosea kweli au la, wewe muombe msamaha!

Tambua bado unamhitaji mteja huyu au rafiki zake pia, hivyo usiache kufanya mambo yatakayoboresha uhusiano wenu.

Sentensi moja tu inatosha, mfano: “Nimegundua hukufurahishwa na majibu uliyopewa na mhudumu wa malazi, naomba nafasi ili nilifanyie kazi hili – samahani kwa usumbufu!”

Sita, tafuta ufumbuzi wa tatizo la mteja. Tayari sasa umeshaelewa kitu ambacho kimemkasirisha mteja wako na tayari umeshamudu kumtuliza. Kilichobaki sasa ni kutatua tatizo lake.

Ni vizuri kutatua tatizo la mteja kwa kumshirikisha ikibidi. Muulize jinsi ambavyo angependa jambo lake lifanyiwe kazi. Kwa kiasi kikubwa, hivyo ndivyo mteja anavyotarajia ahudumiwe.

Saba, tafuta faraja baada ya mteja kuondoka. Mteja akipatwa na hasira na wewe ukahusika kumtuliza na kutatua tatizo lake, kuna wakati anakuacha na maumivu pia.

Unabaki na msongo wa mawazo kutokana na maneno, ukali na ghadhabu zake. Kuna wakati anakuacha ukiwa unaumwa kichwa kabisa.

Ikitokea hivi, kabla hujaendelea kumhudumia mteja mwingine, pumzisha akili kidogo. Tafuta sehemu au mtu atakayekuchangamsha au kukutania hadi ukacheka. Hii ni tiba ya msongo wa mawazo.

Ukisharudi katika hali ya kawaida unaweza sasa kuendelea na huduma kwa wateja wengine.

Hatua ya kuchukua: kwa kuwa biashara ni wateja, jitahidi sana kuwa karibu nao ili kujua vitu vinavyowakwaza ili ushughulike navyo mapema kabla hawajapatwa na hasira. Wakikasirika fuata maelekezo hapo juu kuokoa jahazi.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Jinsi Kufeli Kunavyoweza Kuchochea Mafanikio Yako…(2)

Habari rafiki

Vikwazo, changamoto na matatizo ni vitu visivyoepukika katika safari ya kutafuta mafanikio. Ukiweza kulielewa hili mapema unajiweka katika nafasi nzuri ya kumudu misukosuko ya ujasiriamali.

Vitu ambavyo mara nyingi watu huviona juu ya uso wa dunia, kuhusu mtu, ni matokeo, au mafanikio yake – lakini kuna vitu vingi wasivyoweza kuviona, kwa mfano; vikwazo, mateso, maumivu, machozi, n.k. ambavyo mtu huyu kapitia.

Kuna nyakati za maumivu, kuchanganyikiwa na mateso katika safari ya mafanikio

Kama hujawahi kupatwa na masaibu haya katika maisha yako, na wala haufikirii kuwa yatakupata siku moja, basi ni bora uachane na kitu kiitwacho ujasiriamali – hutauweza.

Ujasiriamali ni uthubutu na ujasiri alionao mtu katika jitihada zake za kujitafutia riziri au kipato. Katika safari hiyo watu hukabiliwa na changamoto nyingi – ikiwa ni pamoja na kufeli kutimiza malengo yao.  

Hata hivyo tunahimizwa tusiogope kufeli kwani wakati fulani kufeli kuna maana.

Hii ni sehemu ya pili ya mada hii inayohusu umuhimu wa kufeli katika safari ya kusaka mafanikio.

Katika sehemu ya kwanza nilijadili sababu nne kwa nini tunahimizwa tusiogope kufeli. Leo nitajadili sababu nyingine tano, kama ifuatavyo:

Tano, kufeli kunasaidia kujenga kinga dhidi ya woga. Mwandishi Paulo Coelho de Souza anasema, “kuna kitu kimoja tu kinachosababisha ndoto za watu zisitimie. Kitu hicho ni woga wa kufeli.”

Woga wa kufeli hufunga milango ya ufaulu. Kama unaogopa kufeli huwezi kujaribu. Woga wa kufeli ni kikwazo cha mafanikio. Ukiwa tayari kufeli unajitengenezea kinga dhidi ya woga – na hivyo huwezi kuogopa kujaribu.

Sita, kufeli kunakomaza tabia za kijasiriamali. Mwanariadha Wilma Rodolph aliwahi kusema, “kupata ushindi ni jambo kubwa – na hili halina ubishi. Hata hivyo, kama unataka kushinda medali ya Olympic unapaswa kujifunza kushindwa.”

Ukweli ni kwamba hakuna mtu ambaye hajawahi kufeli. Lililo muhimu ni kwamba, kama unaweza kumudu kuinuka, baada ya ‘kupiga mweleka’, na ukaendelea mbele, hadi ukapata ushindi, basi wewe ni shujaa; na huu ndio ujasiriamali wenyewe!

Saba, kufeli kunanogesha mafanikio. Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Sir. Winston Churchil anasema, “mafanikio ni matokeo ya kuanguka na kuinuka, mara nyingi, bila kupoteza hamasa.”

Ushindi unakuwa mtamu zaidi unapotanguliwa na kufeli au msoto. Unapokumbuka mateso uliyopitia kabla ya kushinda unapata faraja, na ushindi huu unakuwa na thamani kubwa.

Nane, kufeli kunaongeza thamani yako mbele za watu. Watu hawapati heshima kwa kufanya vizuri tu. Kuna heshima zinazotokana na kufeli. Jinsi ulivyofeli, mara kadhaa, lakini ukainuka, ukasonga mbele –  hili ni somo!

Kuna hamasa binafsi unayopata kwa kufeli baada ya jitihada. Kufeli kukitokana na jitihada za makusudi za kupata kitu kuna watu wataona, na hawa watakupa heshima; na thamani yako itapanda.

Tisa, kufeli kunakujenga kuwa mnyenyekevu. Kuna manufaa makubwa pale mtu anapoanguka, mara nyingi, halafu akainuka. Hali nii inamjengea unyenyekevu.

Mjasiriamali ambaye hajapitia misukosuko ya kufeli, mara nyingi hujenga kiburi na majivuno. Kiburi hiki kinatokana na ujinga unaosababishwa na kupata mafanikio kiurahisi, bila kuyasotea.

Ukweli, mtu huyu ni rahisi sana kupiga mweleka mbaya siku akikutana na misukosuko mikubwa mbele ya safari. Huyu hatakuwa na ukakamavu, ujasiri wala uvumilivu unaopatikana kupitia kufeli.

Mtu huyu ni rahisi sana kukata tamaa na kumwaga manyanga chini. Hivyo rafiki yakupasa kujifunza kufeli kama hatua ya kujipatia mafanikio. Usizoee ushindi wa mteremko – huu utakulemaza!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Jinsi Kufeli Kunavyoweza Kuchochea Mafanikio Yako…(1)

Habari rafiki

Ukifuatilia sana utagundua kuwa tunaishi katika jamii inayoabudu mafanikio. Kifupi, mafanikio ni hali anayokuwa nayo  mtu  anapoweza kusogea kutoka hatua moja kwenda nyingine katika jitihada za kutimiza malengo yake ya maisha.

Usipende kushangilia kufaulu tu. Hata kufeli wakati fulani kuna manufaa

Kwa mfano, mtu aliyekuwa anateseka na familia yake kwenye nyumba ya kupanga – akiweza kujenga nyumba yake na kuamia humo, hivyo kuepukana na adha za kupanga, huyu tunasema amepata mafanikio kimaisha.

Kinyume na mafanikio ni kufeli, pale mtu anaposhindwa kutimiza jambo alilopanga kulifanya. Kwa kawaida watu huchukia kufeli – na hii huwafanya baadhi yao kuogopa kufanya vitu au shughuli fulani.

Watu hawa huogopa kufanya vitu kwa kuwa wana hofu ya kufeli, na wanaogopa kuwa wakifeli watapata maumivu.

Binaadamu kimaumbile ni kiumbe anayeogopa na hujitahidi sana kujiepusha na mazingira yatakayomletea maumivu. Na kwa sababu hiyo binaadamu hupenda kuikimbilia faraja; yaani maisha yasiyo na karaha.

Kwa hiyo tunaogopa kufeli kwa kuwa tunahusisha kufeli na maumivu na hivyo tunajitahidi kufanya mambo kwa jinsi ambayo itatuepusha na kufeli, ili tusiziumize nafsi zetu.

Hata hivyo wataalamu wa saikolojia wana mtazamo tofauti. Wataalamu hawa wanahamasisha watu wasiogope kufeli. Wanasema kufeli kuna maana, na sio kitu cha kuogopa. Wanatoa sababu zifuatazo; na leo nitajadili sababu nne:

Moja, kufeli ni njia muhimu ya kujifunza. Watu wanaofeli mara nyingi, hawa hujifunza zaidi. Kufeli kunaibua maarifa mapya na kuifanya akili kufanya kazi kwa bidii kubwa.

Ndiyo maana baadhi ya wawekezaji wakubwa, wenye pesa nyingi, huwakubali na kuwapa mitaji wajasiriamali wachanga, wenye mawazo mazuri, lakini waliowahi kufanya biashara, wakaishia kufeli.

Kwa mujibu wa matajiri hawa, Mjasiriamali ambaye hajawahi kufeli – hajajaribiwa! Huyu hana uzoefu wa misukosuko ya ki-biashara na hivyo hana uwezo kwa kupambana na matatizo na kutafuta njia za kuyashinda.

Mjasiriamali aliyewahi kufanya jambo – halafu akafeli huyu amepata maarifa ya ziada. Anajua changamoto sio kwa kusimuliwa bali kwa kukutana  nazo uso kwa uso. Huyu ni mjuzi tayari, na akisukumwa kidogo tu anapiga hatua!

Pili, kufeli kunasababisha kasoro kugunduliwa. Kufeli kunatoa ishara kuwa kitu fulani hakijakaa sawa….yaani kuna upungufu. Kufeli kunaweka wazi vitu vinavyotakiwa kufanyiwa marekebisho ili vifanye kazi sawasawa.

Kufeli kunabainisha mapengo uliyonayo wewe binafsi, mikakati yako, mifumo yako ya utendaji na watu wanaokusaidia kufanya shughuli yako. kuujua udhaifu na kubuni mbinu za kuboresha ni hatua nzuri kuelekea  mafanikio.

Tatu, kufeli mapema kunatoa fursa ya kupunguza kasi kidogo. Kuna wakati, katika kufanya shughuli fulani unapaswa kupunguza kasi kidogo, ukavuta pumzi. Ni pale unapogundua kuwa kitu unachokifanya kina walakini fulani.

Kupunguza kasi au kusimama kwa muda kunakupatia fursa ya kufanya tathmini ili kujua endapo panahitajika msaada, maarifa au rasilimali zaidi ili kufanya shughuli iendelee.

Katika kipindi hiki unapata pia fursa ya kujipima kama bado una motisha au hamu ya kuendelea kufanya jambo hilo.

Ukikosa fursa ya kufanya tathmini unaweza kujikuta unaingia harasa kwa kupoteza bila sababu pesa, muda, nguvu na rasilimali nyingine kwa kufanya mradi usio na tija.

Nne, kufeli kunaweza kuwa ishara ya kupiga hatua. Siyo rahisi kupata kitu kikubwa au manufaa kama unajificha katika joho la faraja au mazingira yasiyo na changamoto.

Mara nyingi changamoto zinapozidi ndipo milango ya mafanikio hufunguka. Yaani kufeli kunawasha moto wa mafanikio. Mtaalamu mmoja anasema kufeli kwa kiwango kikubwa mara nyingi huambatana na mafanikio makubwa.

Hatua ya kuchukua: kufeli ni njia au hatua muhimu katika safari ya mafanikio. Katika safari hii ambayo imepambwa na changamoto nyingi ukifeli usianze kubabaika bali elewa kuwa unapitia katika hatua ya kujifunza na kukomaa – hivyo shikilia na utayaona mafanikio.

Katika sehemu ya pili ya mada hii nitajadili mbinu tano zilizobakia.

Soma pia: Ukishaiona Fursa, Acha Kusitasita – Anza Mara Moja!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Jinsi Ya Kujinasua Na Watu Wanaokukatisha Tamaa

Habari rafiki,

Katika makala hii nilijadili jinsi watu wanavyojitahidi kufikiri ili kupata mawazo mbalimbali ambayo yanaweza kubadilishwa kuwa fursa zitakazowaingizia kipato na kubadili maisha yao.

Ukikutana na kelele za kukatisha tamaa tulia – usibabaike – zisikilize hisia zako

Nilijadili pia kuwa katika jitihada za kuanza kuyatia mawazo katika matendo kuna wakati watu wanakutana na  mawazo pingamizi au hasi kutoka kwa marafiki, ndugu na hata wazazi wao.

Kama mjasiriamali, unatakiwa kuwa tayari kukabiliana na kila aina ya ushawishi na kujitahidi kuushinda au kupunguza athari zake – kabla haujaathiri maamuzi yako ya msingi.

Yaani umeota ndoto ya mafanikio. Una wazo ambalo ukiinama ukiinuka unaona kabisa linakupeleka katika mafanikio kimaisha. Unafanya utafiti wako – unathibitisha ubora na uwezekano wa kufanyika; lakini ukilitoa wazo hilo kwa wengine, unakutana na kimbembe.

Utasikia, “mmm, biashara hiyo – wala usithubutu! Unamjua Abduli – yule jirani yangu – alijaribu biashara hiyo, yaliyompata hatakaa asahau, sikushauri kufanya biashara hiyo!”

Maoni ya aina hii hutokea sana pale unapowashirikisha wazo lako watu wako wa karibu. Wapo wachache watakaokuunga mkono – lakini wapo watakaokukatisha tamaa, na usishangae hawa wakawa wale wa karibu zaidi na wewe.

Somo muhimu hapa ni kwamba lazima ujue kuwa kila mara unapoamua kuanzisha mradi au biashara tegemea kukutana na wapinzani. Hawa ni watu wenye mtazamo hasi kwa kila kitu kinachoingia katika akili zao, hivyo unapaswa kuwajua.

Ukiwachunguza, utaona baadhi yao kama wanakutakia mema hivi au wanakuepusha na balaa wanayoiona mbele yako. Jihadhari na watu hawa!

Tatizo ni kwamba ukikosa uangalifu na ujanja watakuondoa kwenye reli. Wataiondoa hamasa yote uliyojikusanyia ulipopata wazo lako. Kumbuka dunia imejaa watu hawa, wanaotilia shaka kila kitu. Unachopaswa kufanya ni kuwa na msimamo.

Sasa, leo nimekuja na sababu na mbinu ambazo zinaweza kukusaidia kuwa na msimamo na msukumo wa kusonga mbele, pamoja na ‘presha’ za watu hawa, kama ifuatavyo:

Moja, zisikilize hisia zako. Kuna kitu umetokea kukipenda. Ni wazo linalozunguka kichwani mwako kutokana na mapenzi uliyonayo ya kufanya jambo fulani.

Jitahidi kuheshimu hisia zako. Ukifanya hivi utajiepusha na kuyumbishwa-yumbishwa. Weka msimamo – songa mbele!

Mbili, pengine hawajakuelewa tu. Wakati fulani unaweza kuumia rohoni unapogundua watu wa karibu na wewe wakikukatisha tamaa au kukutisha usifanye ndoto yako. Ukichunguza unakuta kumbe hawajakuelewa tu.

Pengine una wazo jipya la kibunifu – na wao hawana taarifa au maarifa ya kutosha nalo, kwa hiyo watalipinga kwa ujinga wao, ni kitu kipya – hawakijui vizuri.

Hawa waelimishe huku ukisonga mbele; au wapuuze – watakukwamisha bure!

Tatu, pengine wana wivu tu. Wakati fulani watu hawakuungi mkono kwa sababu ya husuda waliyonayo juu ya mafanikio yako. Wachunguze; ukigundua ni wivu tu, wanakupinga ili wakuvute shati, uanguke, ili ufanane nao, achana nao. Wewe piga kazi.

Nne, wapo wanaoishi kwa mazoea. Watu wengi tu wamezoea kuona vitu vikifanyika kwa utaratibu waliouzoea. Hawana kipya wao – hawana ubunifu.

Hawa wangependa kuona unafanya mambo yaliyozoeleka; yaliyowahi kufanyika yakafanikiwa – basi. Ni waoga wa vitu vipya. Hawa ni wa kupuuza. Achana nao endelea na ndoto zako.

Tano, iambie nafsi yako kila kitu kinawezekana. Siyo rahisi kutabiri mambo yote kwa uhakika. Duniani kuna kufanikiwa na kufeli pia, ndiyo kanuni ya maisha.

Hivyo usije kufanya vipingamizi kutoka kwa wengine viwe ndio ukweli wenyewe, vikasababisha utetereke na kurudi nyuma – hapana! Tambua kila kitu kinawezakana ukithubutu na ukatia nia.

Sita, huwezi kumridhisha kila mtu. Hii nayo ni kanuni ya asili ya maisha. Hata ufanye nini huwezi kumridhisha kila mtu. Lakini pia huwezi kumridhisha mtu mmoja wakati wote.

Kwa hiyo ukilenga kufanya hivyo utakwama na utachanganyikiwa bure. Weka msimamo wako kwa kile unachokiamini – tia nguvu – kifanye.

Saba, ungana na washauri wenye mawazo chanya. Unapowaza kuingia katika biashara fulani tafuta wataalamu au washauri wa fani hiyo. Hawa, hata wakikuambia biashara yako ina changamoto – hawaishii hapo.

Watakuonesha pia njia za kupambana na changamoto hizo na kuzishinda ili wazo lako liweze kufanyika. Hawa wana mtazamo chanya, watakwambia, “njia hii ina miiba – lakini ili safari iendelee tafuta buti, vaa, songa mbele!”

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Je, Umeota Ndoto Ya Kufanya kitu? Acha Kelele Basi!

Habari rafiki,

Kila mtu huota ndoto. Kuna ndoto za usiku na ndoto za mchana. Ndoto ni mfululizo wa mawazo, picha au hisia ambazo hutokea akilini kupitia nguvu za asili.

Ndoto hushuka kama maono kutoka ulimwengu wa roho

Kwa kiasi kikubwa ndoto hutokea mtu akiwa usingizini na akiamka huweza kukumbuka alichoota, lakini wakati mwingine hawezi kukumbuka. Baadhi ya ndoto za usiku, zikikumbukwa, zinaweza kusababisha ubunifu.

Kwa kawaida ndoto za usingizini huwa ziko nje ya udhibiti wa mtu – isipokuwa pale unapoota ukiwa unajitambua, au ndoto za mchana.

Kwa mujibu wa maandiko, Mungu hujifunua kwa mtu kupitia maono na hunena na mtu huyo kupitia baadhi ya ndoto hizi.

Yaani mtu umetulia mahala, mchana; ghafla wazo la maana linakuja kama ndoto fulani hivi; wazo ambalo hujawahi kulisikia, kuliwaza wala kulisoma mahala popote – linakuja tu na unaona lina uwezo wa kukupa mafanikio.

Kwa maana hiyo Mungu huongea na watu wake kupitia ndoto na maono. Kupitia ndoto Mungu huwa anakuonesha kitu cha kufanya au anakufunulia maarifa kwa njia asilia.

Sasa, unapopata ndoto, ukafunuliwa maono ya kitu cha maana cha kufanya, usipende kupiga makelele!

Binaadamu tumezungukwa na watu wa kila aina wenye mitazamo inayotofautiana. Wapo watu wenye roho nzuri na nia njema nasi, lakini pia wapo watu wenye kijicho, choyo na husda; wasiopenda mafanikio ya wenzao.

Wataalamu ya biblia wanasema kosa kubwa alilofanya Yusufu ni kuwaambia ndugu zake ndoto alizoota, zilizoashiria kuwa baadaye angekuwa bosi wao.

Biblia inasema kuwa Yusufu aliota ndoto…kisha akawasimulia ndugu zake…nao kwa husda, wakazidi kumchukia.

Ukichunguza, Yusufu alifanya hivyo kwa nia njema kabisa kuwashirikisha ndugu zake maono toka kwa Mungu, lakini hakuna aliyependezwa na hilo – walimchukia!

Kwa hiyo, ukipenda kupiga kelele, kumwambia kila mtu ndoto zako – jiandae kufeli. Utakutana na maadui ambao hukuwahi kuwafikiria kuwa maadui zako. Jiandae kukatishwa tamaa au hata kutishwa.

Unapokuwa na ndoto kaa kimya, hiyo ni ndoto yako, siyo ya mtu mwingine. Ni wewe uliyepata wazo la kitu cha kufanya.

Mara chache sana unaweza kumchagua mtu, unayemwamini, ambaye ana uwezo wa kutoa msaada katika kuliendeleza wazo lako; na sio kila mtu.

Cha kuzingatia ni kwamba kuna muda unapaswa kuwa kimya ili ndoto yako ianze kutia kasi. Huu ni muda wa kupangilia mambo yako, kuyatia katika reli na kuanzisha mwendo.

Pangilia maudhui ya ndoto yako vizuri. Fanya utafiti au tathmini ya kimyakimya – bila kuweka wazi undani wa ndoto au wazo lako, kisha anza.  

Ukipenda kusemasema utakutana na watu wasio na nia njema. Hawa watakutoa katika reli. Wapo watakaokuona hamnazo na wapo wa kukutisha wakikwambia huwezi kufanya kitu kama hicho; na kweli utaishia njiani.

Mwandishi Stephen Hough anasema, “ukimya ni udongo muhimu unaoweza kuotesha wazo lolote.’

Kama una wazo la kuanzisha biashara fulani, huna sababu ya kupiga kelele ili kila mtu ajue – ‘inahusu?’ Wewe fanya utafiti kimyakimya, kusanya taarifa, halafu anza.

Kama kitajitokeza kitu hukifahamu vizuri uliza kitu hicho ili uweze kuboresha uanzishaji na uendeshaji wa biashara yako – kisha endeleza utendaji.

Kukosa ukimya kulikaribia kumfanya Yusufu auliwe na ndugu zake hivyo jihadhari na hili. Fanya kazi kwa bidii ndani ya ukimya, yaache mafanikio ndio yapige kelele.

Kwa wapenzi wa muziki, watakumbuka baadhi ya maneno ya muziki wa zamani (zilipendwa) uliopigwa na Dar Jazz Band, yasemayo, “we mtoto wacha kupiga mayowe, waache watu waone wenyewe.”

Hatua ya kuchukua: Ukishapata ndoto yako ukaona inakwenda kukupatia kitu cha maana, unapaswa kuifanyia kazi haraka kwa kuitia katika vitendo. Lakini kitu cha muhimu ni kujiepusha na kelele.

Fanya mambo yako kimyakimya kwa umakini mkubwa kuhakikisha wazo lako linafikia malengo. Usipende kumshirikisha kila mtu kwa kuwa binaadamu tunatofautiana sana. Wapo wasio na nia njema. Jiepushe nao!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Jinsi Ya Kukinoa na Kukiendeleza Kipaji cha Mwanao… (2)

Habari rafiki,

Hii ni sehemu ya pili ya mada inayohusu mbinu ambazo mzazi anapaswa kuzifuata katika kumsaidia mwanae kukinoa kipaji chake. Hii ni baada ya mzazi kugundua kuwa mwanae ana kipaji fulani.

Katika sehemu ya kwanza nilijadili mbinu sita. Naomba sasa tuendelee pamoja ili tumalizie mbinu zilizobakia kama ifuatavyo:

Saba, Mhimize ajiunge na vikundi maalum. Mzazi unapaswa kumsaidia mwanao kujiunga na timu, jumuia au klabu za wenye vipaji kama yeye.

Kipaji cha mtoto kinakua haraka akiwa ndani ya timu

Kama yeye ni mcheza mpira mtafutie timu nzuri, yenye vifaa na wataalam. Kumbuka kwa kucheza ndani ya timu anapata fursa ya kupata maarifa mapya yanayotokana na kufanya mazoezi pamoja.

Atakutana na wenzake wenye vitu fulani ambavyo yeye hana. Atajifunza nidhamu ya utendaji, ushirikiano na matumizi bora ya muda na rasilimali nyingine.

Kwa mfano, kama mwanao ana kipaji cha ufundi magari, msaidie kuingia katika gereji ili ajifunze kupitia ushirikiano na vipaji vya wenzake.

Thomas Ulimwengu, Mtanzania anayecheza soka la kulipwa Algeria, alikuza kipaji chake baada ya kujiunga na Tanzania Soccer Academy, iliyokuwa chini ya TFF.

Afisa Maendeleo wa TFF, Jemedari Said aliwahi kusema, “kufanya vizuri kwa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ni matokeo ya jitihada za makusudi za kuviendeleza vipaji vya vijana kupitia vituo maalum.”

Nane, mtafutie mwanao kocha mahiri. Ni muhimu kipaji cha mwanao kinolewe na mwalimu mbobezi. Kama anapenda riadha mtafutie mwalimu mbobezi katika riadha.

Usisite kuingia gharama kwa kumlipia ili apate mtu wa kumsimamia, kumwongoza na kumtia hamasa ya kujifunza kwa bidiii. Kumbuka kila kitu kizuri kina gharama. Kubali kubeba mzigo huu, lakini baadaye utafaidika.

Tisa, mhimize mwanao aambatane na marafiki wazuri. Hata kama hawana kipaji kama yeye, msaidie mwanao kuwa na marafiki bora.

Hawa ni wale marafiki watakaoweza kumtia moyo, kumhimiza asiwe mvivu, kumfariji akikutana na changamoto na kumhamasisha katika safari yake ya kunoa kipaji.

Ni vizuri achague marafiki wenye maono na busara, wasio na choyo wala husda na ambao hawatamsababishia maumivu ya moyo kwa kumkatisha tamaa.

Mchezaji maarufu wa kimataifa Christiano Ronaldo amewahi kumtaja kijana mwenzake Alberto Fantrau kuwa nyuma ya mafanikio yake ya soka.

Anasema, mafanikio yangu yamechangiwa sana na rafiki yangu huyu. Tukiwa tunacheza pamoja katika timu ya vijana… ni yeye, kwa makusudi, aliyenipa pasi iliyonifanya kufunga bao lililonifanya kuchaguliwa kujiunga na Academy ya Sporting Lisbon.”

“Ukweli Fantrau alikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufunga bao hilo, na angechaguliwa yeye, lakini aliamini mimi ni bora zaidi kuliko yeye, hivyo alitaka mimi ndiyo nifunge bao hilo na nijiunge na academy….huu ni zaidi ya urafiki.” Alisema Ronaldo.

Kumi, mhimize mwanao awe mnyenyekevu. Nimewahi kusikia  kiongozi wa timu kubwa ya soka akilalamikia baadhi ya wachezaji kuwa na kiburi kwa makocha – wakidai kocha hana kipya cha kuwafundisha….kwani amewakuta na vipaji vyao tayari.

Tabia hii ni mbaya sana kwani inaua vipaji. Ni kweli wewe una kipaji lakini kama hutaki kuelekezwa na kukosolewa hutajifunza, na hutapiga hatua yoyote. ‘Mastaa’ kama Messi wanawasikiliza walimu – sembuse wewe?

Mhimize mwanao awe msikivu, mnyeyekevu na mdadisi. Kujifanya kujua hakumsaiii bali kutamuangamiza kwani atanyimwa ushirikiano na kuishia njiani katika safari yake muhimu.

Hatua ya kuchukua: mzazi bado nakuhimiza kumwongoza mwanao katika  kukiendeleza kipaji chake. Msaidie kumwonesha njia sahihi na jinsi ya kupita ili hatimaye kipaji chake kijidhihirishe na kimsaidie kujikomboa kiuchumi.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Jinsi Ya Kukinoa Na Kukiendeleza Kipaji Cha Mwanao… (1)

Habari rafiki,

Nafurahi kukukaribisha tena mzazi mwenzangu, au mzazi mtarajiwa, ili tuendelee kujifunza stadi za maisha hususan kwa ajili ya vijana wetu; ingawa hata wewe mtu mzima utafaidika pia.

Makala iliyopita niliongelea jinsi ya kutambua kipaji cha mwanao. Katika makala hii nitakupatia mbinu za kukinoa kipaji cha mwanao ili kukifanya kikue na hatimaye kionekane bayana.

Mtoto mwenye kipaji ni sawa na mche mzuri wa mchungwa. Ukiulea vyema utafaidi matunda yake.

Mzazi ukishachunguza na kugundua kuwa mwanao ana kipaji fulani una wajibu wa kukikuza kipaji hicho. Zifuatazo ni mbinu sita ambazo nitazijadili leo.

Kwanza, mpe mwanao nafasi na uhuru wa kutenda. Mzazi mruhusu na msaidie mwanao kutia kipaji chake katika vitendo. Ukikosa ushirikiano utaua kipaji chake kwa uzembe tu.

Nimeshamshuhudia mzazi mmoja akimchapa mwanae kila siku aliporudi kutoka shule akiwa amechafuka sana, na hasa shati lake jeupe.

Nilimsikia akimgombeza, “mimi siyo boi wako kukusugulia shati lako unalochafua kwa michezo yako ya kipumbavu; leo mwisho, ukirudi hivi kesho utakoma.”

Ukweli ni kwamba mtoto huyu alikuwa anasifika kwa uwezo wa mpira wa miguu na alikuwa tegemeo katika shule yake.

Uwanja wao wa mpira haukuwa na nyasi, hivyo ilikuwa lazima nguo zichafuke, lakini mama yake hakujishughulisha kuelewa hadi siku moja alipomuona mwanae katika TV akipongezwa kwa kuisaidia timu yake kushinda mashindano ya mashule.

Pili, Mhimize mwanao kufanyia mazoezi kipaji. Baada ya kugundua kipaji cha mwanao mzazi una wajibu wa kumtia shime ili asizembee kufanyia mazoezi kipaji chake.

Kwa mfano mtoto mwenye kipaji cha uimbaji atajenga uwezo wake zaidi kwa kufanya mazoezi ya sauti na pumzi. Mtoto mwenye kipaji cha uchoraji yafaa asaidiwe ili apate muda na vifaa vya kumwezesha kufanya mazoezi yake

Tatu, Mhimize ajitume na aweke bidii. Hata kama mwanao ana kipaji, akiwa mvivu hataweza kukuza kipaji chake.

Ni wajibu wako mzazi kumpa hamasa ili atie bidii na nguvu za kutosha katika  kuboresha kipaji chake. Kwa mfano, mwanariadha anayeshinda sio yule mwenye kipaji tu bali anayetia bidii kufanya mazoezi ya nguvu.

Hata mwanasoka ni hivyo hivyo. Mbwana Samatta ni mfano wa wachezaji soka wenye kipaji, aliyefanikiwa kwa kujituma.

Alipoulizwa siri ya kutwaa tuzo ya ufungaji bora katika Ligi ya Mabingwa Afrika, akiwa TP Mazembe, mwaka 2015, Samatta alisema, “bidii, kujituma na uvumilivu ndiyo siri kuu ya ushindi wangu.”

Nne, Msaidie mwanao kupata elimu stahiki. Kipaji peke yake bila maarifa ni kazi bure. Bila elimu ya kutosha katika fani aliyojaliwa, mtoto anakosa umahiri na uendelevu. Wasanii maarufu wa zamani, Bambo na Kingwendu, ni mfano mzuri katika hili.

Elimu inampatia mwanao mbinu za zamani na za kisasa za kufanya jambo lake kwa ubora na urahisi zaidi na kumkutanisha na wataalam wanaoweza kumsoma na kujua anahitaji msaada gani ili kumkuza.

Pamoja na kwamba elimu ni gharama mzazi usijali, bali msaidie mwanao. Msaidie ahudhurie semina na masomo mbalimbali vyuoni.

Mhimize asome magazeti, vitabu, na majarida yahusuyo kipaji chake. Mhimize pia kuangalia TV na mitandao ya kijamii inayoongelea fani yake.

Tano, Muunganishe mwanao na ‘role models’. Wapo watu ambao ni mifano ya kuigwa katika fani mbalimbali. Kujifunza kutoka kwa watu hawa ni mkakati muhimu.

Kwa mfano, kama mwanao ni mwigizaji, muunganishe na muigizaji mwenye mafanikio aliye karibu nanyi ili kijana ajifunze kutoka kwake.

Hii itamsaidia kujua alivyoanza, changamoto alizopitia na siri za mafanikio yake. Akijifunza kwa waliofanikiwa ataepuka kurudia makosa yaliyofanywa na watangulizi.

Sita, mhimize mwanao asiangalie udhaifu wake. Inawezekana mwanao ana kipaji lakini pia ana upungufu fulani katika maumbile yake.

Wapo watoto, kwa mfano, wana kipaji cha kuimba lakini wana ulemavu wa miguu. Mzazi mtie hamasa mwanao kwamba ulemavu hauzuii kuonesha kipaji chake.

Msaidie ajiamini na akifanyie mazoezi kipaji chake. Mwambie wapo wasanii wengi ni walemavu wa viungo lakini wana mafanikio makubwa kuliko wenye viungo vilivyokamilika.

Hatua ya kuchukua: mzazi una jukumu la kumsaidia mwanao kukinoa na kukiendeleza kipaji chake kwa kumwonesha njia sahihi za kupita. Ukizembea na kumwacha peke yake utakuwa humtendei haki.

Makala ijayo itajadili sehemu ya pili ya mada hii kwa kukupatia mbinu zilizobakia.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Jinsi Ya Kutambua Kipaji cha Mwanao

Habari rafiki,

Katika makala hii nilieleza maana ya kipaji, kisha nikaeleza nafasi ya mzazi katika kukuza na kuendeleza kipaji cha mwanae.

Maana yake ni kwamba, kipaji kikikaa tu ndani ya mtu bila kumletea manufaa kiuchumi, kinakosa maana.

Makala hii inapiga hatua moja zaidi kwa kukupatia mbinu za kutambua kipaji cha mwanao. Hii ni hatua muhimu kwani ndio inajenga msingi mkuu wa mchakato mzima wa kuongeza thamani ya mwanao.

Ukiwa na mawasiliano na ushirikiano mzuri na walimu utabaini mapema kipaji cha mwanao

Vipaji hujidhihirisha kupitia uwezo asilia wa kufikiri, kubuni, kusanifu na kuvumbua vitu. Vipaji pia huonekana katika uwezo wa mhusika kutumia kwa umahiri viungo vya mwili kwa mfano kucheza, kuchora au kuimba n.k.

Tunajua wapo watoto wenye vipaji majumbani mwetu lakini kwa bahati mbaya wazazi na hata watoto wenyewe hawajui kama wana vipaji hivyo.

Wote ni mashuhuda kuwa kuna watoto ambao vipaji vyao vimegunduliwa na watu wa mbali kabisa – na wakati fulani baada ya muda mrefu kupita.

Kipaji ni kama sukari iliyomiminwa ndani ya kikombe cha chai – ikatuama chini. Sukari hii isipokorogwa hautapata ladha ya chai yako.

Kipaji ni tunu kutoka kwa Mungu, hivyo kikitambulika na kutumika ipasavyo tunasema kipaji hiki kimeleta tija. Kipaji kisipogundulika kikaishia kukaa tu ndani ya mtu kinakosa tija, hivyo kumnyima mhusika fursa za kiuchumi.

Sasa utajuaje kuwa mwanao ana kipaji ndani yake? Twende pamoja….

Kwanza, ana shauku ya kuendelea kufanya vitu bila kuchoka. Mtoto mwenye kipaji hufanya vitu kwa umahiri na upekee pasipo kuchoka wala kukata tamaa.

Kwa mfano, kama ana kipaji cha kuimba kila wakati utamsikia akirudia-rudia nyimbo za waimbaji maarufu. Hupenda kuongelea maisha ya waimbaji na jinsi anavyowahusudu. Hupenda kujiunga na vikundi vya uimbaji, kama kwaya, na hupenda kusikiliza vipindi vya muziki.

Pili, hufanya vitu kwa urahisi bila kutumia nguvu nyingi. Mzazi angalia jambo ambalo mwanao anapenda kulifanya – na hulifanya vizuri bila jitihada kubwa sana.

Kwa mfano, mtoto anarudi toka shule na kukwambia kuwa mwalimu wao amewapa kazi ya kuunda sanamu ya ndege ya abiria na kesho wanatakiwa kuonesha darasani.

Akisha kukwambia, unaona tayari anakusanya maboksi na vifaa vingine na tayari keshaanza kukatakata na kuunganisha vipande – na baada ya muda mfupi tayari umbo la ndege linaonekana wazi.

Kama anafanya hivi mara kwa mara, hii ni ishara kuwa mwanao ana kipaji cha ubunifu, ufundi au usanifu wa vitu.

Tatu, ana uwezo wa kuiga vitu kwa waliofanikiwa. Uwezo wa kuigiza na kufanya vitu kama wanavyofanya watu waliofanikiwa ni moja ya dalili kuwa mwanao ana kipaji.

Wasanii kama Steve Nyerere ni mfano katika hili. Utashangaa mwanao kila anachofanya mtu fulani maarufu na yeye anafanya hivyo hivyo tena bila shida yoyote. Huyu ana kipaji hicho.

Mchoraji wa katuni, Masoud Kipanya aliwahi kuulizwa alianza vipi kuchora hadi akawa mahiri na maarufu kiasi hicho. Alijibu, “nilianza kwa kuiga tu katuni za ndani na nje…yaani ukiona wengine wanafanya kitu; ukakihusudu na kuanza kukifuatilia – hicho ndio kipaji chako.”

Nne, angalia michezo/vitu anavyopenda kuliko vingine. Ukiwachunguza, watoto hucheza michezo mingi kwa wakati mmoja. Wataruka kamba, watakimbia, wataimba, watacheza ngoma, wataigiza, watachora n.k.

Sasa, chunguza mwanao anapendelea kushiriki zaidi katika eneo lipi. Chunguza furaha anayoonesha anapofanya jambo hilo. Sikiliza wenzake wanasifia au wanasema nini kuhusu mwanao.

Angalia vitu gani wenzake wakishindwa, kutenda au kuamua, wanamfuata yeye. Je wenzake wanamfuata kuomba ushauri au mwongozo? Katika jambo gani? Vitu hivi ni ishara kuwa mwanao ana kipaji hicho.

Tano, angalia vitu vikubwa anavyofanya bila kujali malipo.  Wapo watu wanaofanya vitu kwa msukumo tu kutoka ndani. Yaani hujikuta tu wanataka kufanya vitu fulani, wala hawawazii malipo yoyote.

Angalia kama mwanao ana sifa hii. Furaha ya mtu huyu ni yale mafanikio anayopata kwa kufanya kitu kizuri kinachowavutia au kuwafaa watu wengine. Ukiona mwanao anajituma sana kufanya jambo bila kuwazia malipo, hii ni dalili ana kipaji hicho.

Sita, angalia kitu cha kipekee anachofanya kwa uwezo asilia. Wapo watu wanaofanya mambo ya kipekee kwa sababu ya elimu au kisomo walichopata. Angalia vitu anavyofanya mwanao ikilinganishwa na elimu yake.

Ukigundua anafanya kitu kisicho cha kawaida, kwa ufanisi na mara kwa mara, na elimu ndogo aliyonayo, basi ujue hiki ni kipaji chake.

Saba, muulize anataka kuwa nani. Mara nyingi watoto jinsi wanavyokua huwa wanabadilika-badilika katika mitazamo yao. Utasikia leo, “nataka kuwa dokta.” Baada ya mwaka mmoja utasikia, “napenda utangazaji.” Na kadhalika.

Mfuatilie polepole jinsi anavyokua na kuelimika, baada ya muda utaona kitu kinachotawala hisia zake zaidi – na utaona anakiigiza au kukisema kwa kurudiarudia, kwa msisitizo. Ukiona hivi, hiki ni kipaji chake.

Hatua ya kuchukua: mzazi una jukumu la kumsaidia mwanao kutambua kipaji chake. Hili likifanyika mapema lina maana zaidi kwa kuwa linakupa fursa ya kujua hatua gani zaidi upige ili kuongeza thamani ya mwanao.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Ukitoa Msaada Huu Hakika Utakumbukwa Daima

Habari rafiki,

Kila mtu, bila kujali ana nini, hujikuta wakati fulani anahitaji msaada kutoka kwa rafiki, jirani au ndugu zake.

Msaada unaweza kuelezewa kama kitu anachotoa mtu au taasisi ili kutimiza haja fulani au kutatua tatizo la mtu au taasisi yenye uhitaji.

Wakati wa dharura au maafa misaada kama hii ni ya lazima

Sasa, tukiongelea suala la uhitaji, je ni wakati gani tunaweza kusema taasisi au mtu ana uhitaji ili apewe msaada? Je, ni wakati wowote tu? Je, ni wakati wa maafa au majanga? Au ni wakati gani?

Na kama utagundua, baada ya tathmini, kuwa ndugu, rafiki, au taasisi inahitaji msaada, je ni msaada gani utampatia? Je, ni pesa? Je, ni vifaa? Je, ni ushauri – au ni nini?

Kabla hujatoa maoni yako kwa maswali haya nakuomba ufuatilie hadithi hii fupi kutoka katika kitabu cha dini.

Hapo zamani za kale, katika kijiji kimoja, waliishi vijana wawili, Rahim na Rahman. Kila siku asubuhi vijana hawa waliondoka na mashoka yao kwenda msituni, jirani na kijiji chao, kuchanja kuni kwa ajili ya kuuza.

Inapofika mchana, baada ya kukata kuni za kutosha, vijana hawa walikuwa na tabia ya kukaa kando ya mto ili kula chakula walichofungashiwa asubuhi.

Baada ya mlo walizibeba kuni zao kuelekea sokoni kwa ajili ya kuziuza kabla ya kuanza safari ya kurudi nyumbani jioni.

Sasa, siku moja baada ya kukata kuni zao, waliketi kwa ajili ya mlo wa mchana. Kuinua macho, Rahim akamwona kijana mmoja aliyedhoofika, mchafu na mwenye mavazi duni, ingawa alionekana hana tatizo la kiafya.

Kijana huyu alitokea porini kuja upande wao na alipokaribia macho yake yote yalilenga bakuli lenye chakula. Alionekana ana njaa sana, na bila kupoteza muda alipeleka ombi la chakula ili akidhi njaa yake.

Rahim, huruma ilimshika na haraka aliuendea mkoba wa chakula akatoa kipande kimoja ili ampatie ‘ombaomba’ yule maskini.

Kabla Rahim hajampatia kipande kile, Rahman aliudaka mkono wake na kuuvuta, kisha akamwambia yule ombaomba, “hatuna chakula cha kutosha sisi.”

“Angalia, tunajituma kufanya kazi kutwa nzima, tumekaa hapa tupate mlo wetu halafu tutakwenda sokoni kuuza kuni; hivyo hatuna chakula cha kukupa wewe – lakini kama uko tayari nitakusaidia kitu.”

Rahman alimwonesha shoka na kumwambia, “nitakuazima shoka langu, nami nitakufundisha kukata kuni, kisha nitakufundisha jinsi ya kuuza kuni sokoni.”

Akamwambia kuwa akishauza kuni atapata pesa kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine, na kwamba hatakuwa ombaomba tena na heshima yake itarudi.

Baada ya kuelewa somo, kwa shingo upande, ombaomba aliungana na Rahman, wakaenda msituni. Kijana akafundishwa kukata kuni na kuzifunga vizuri kwa ajili ya kuzipeleka sokoni.

Walipofika sokoni Rahman alimfundisha maskini yule mbinu za kuuza na kumwacha aendelee na mauzo. Ulipita muda mwingi bila kijana yule kuuza chochote hadi akapata hasira na kukata tamaa.

Alianza kuwaza, “yaani hawa vijana bora wangekuwa wakarimu – wangenipa chakula chao – ningekula nikashiba nakuachana nao, kuliko kuteseka namna hii hapa.”

Akiwa katika mawazo haya, ghafla likatokea gari likapiga breki karibu naye. Akashuka mzee mmoja aliyenunua kuni zake zote, akaziweka katika gari lake na kumkabidhi bunda la noti.

Akiwa haamini macho yake, alipokea pesa zile kwa furaha na haraka akamkimbilia Rahman kumwonesha alichopata.

Rahman alimpongeza kisha akampeleka kwenye duka la mashoka. Kijana alinunua shoka moja na kumshukuru Rahman kwa kumfundisha kazi na mbinu za kuuza.

Kwa vile alikuwa na njaa alinunua chakula cha kushiba, akala na kupumzika tayari kwa kazi ya kukata kuni kesho yake

Alipoondoka, Rahman alimgeukia Rahim na kumwambia, “angalia, tungempa chakula ombaomba yule angekula haraka, angeshiba na kurudi tena msituni kulala. Kesho angekuja tena kutuomba na angeendelea hivyo kila siku.”

“Kwa kumpatia ujuzi wa kukata kuni na kuuza, na kwa kumsaidia kupata shoka lake, tumempa vitu ambavyo vitampa chakula na mahitaji mengine siku zote – na sasa hatakuwa na njaa tena.”

Hatua ya kuchukua: msomaji unashauriwa kuzingatia msemo usemao “usimpe mtu samaki – bali mpe ndoana na mfundishe jinsi ya kuvua samaki.”

Hivyo… ndugu, rafiki au jirani akiwa na uhitaji unatakiwa kuwa makini ili umsaidie kitu ambacho kitampa suluhisho la kudumu la tatizo lake. Misaada mingine inalemaza akili kuliko kutatua matatizo. Je, nini maoni yako kwenye hili?

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Mobile: 0718219530