Je, Mzazi Una Nafasi Gani Katika Kukuza Kipaji cha Mwanao?

Habari rafiki,

Karibu tena katika makala hii tujifunze stadi za maisha. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) stadi za maisha ni elimu yenye lengo la kujenga tabia njema ya mtu na kumpa uwezo wa kubaini fursa na matatizo yake – na kujua mbinu za kushughulika nayo.

Lengo la stadi za maisha ni kukuza na kuendeleza stadi zinazohitajika katika maisha ya kila siku, mfano kufanya maamuzi.

Makala ya leo itajikita katika kitu kiitwacho ‘kipaji cha mtoto’ na nafasi ya mzazi katika kushughulika nacho.

Mchunguze mtoto – anapenda kujifunza nini? Huenda ndio kipaji chake – msaidie kukikuza

Mhubiri mmoja amewahi kusema kuwa Mungu alipomuumba mtu aliweka vipaji ndani yake. Kipaji ni uwezo asilia alionao mtu unaomwezesha kutenda mambo yenye matokeo makubwa kwa kutumia nguvu au rasilimali kidogo.

Kinachompa mtu huyu nguvu ya kuendelea kufanya ni ile motisha iliyomo ndani mwake.

Moja ya changamoto zinazowakabili wazazi kuhusu suala la vipaji ni kutokujua kama mtoto wake ana kipaji. Changamoto nyingine ni kushindwa kukinoa kipaji kilichogundulika na kukitumia kiuchumi kutengeneza pesa.

Mwandishi mmoja anasema kuwa kutokujua kipaji alichonacho mtu ni chanzo kimojawapo cha umaskini. Kwa hiyo ni jambo muhimu katika familia au jamii kuwa na utaratibu wa kuvibaini na kuviendeleza vipaji vya vijana wetu.

Nchi zilizoendelea kama Marekani zimepiga hatua kubwa katika hili ambapo katika nchi hizi, vijana huendelezwa katika fani au stadi wanazozipenda. Kwa kufanya hivi vipaji vyao hukuzwa kirahisi hadi kufikia uwezo wa juu.

Watu mashuhuri na wabunifu kama Steve Jobs, mwanzilishi wa Apple, na Mark Zuckerberg, mwanzilishi wa Facebook – ni mifano hai ya watu waliofanikiwa kiubunifu na kimaisha kupitia vipaji vyao – vilivyoendelezwa.

Tatizo tulilonalo katika nchi yetu, Tanzania, ni ushiriki mdogo wa wazazi kwenye maendeleo ya watoto wao walio na vipaji; yaani kushindwa kuvibaini, kuvikuza na kuvibadilisha kuwa pesa.

Tunao watoto wengi tu wenye vipaji, lakini ni wazazi wangapi  wanaojishughulisha kujua mtoto wake anapendelea nini kama ishara ya kipaji alicho nacho?

Na katika eneo la taaluma je, ni wazazi wangapi wanaofuatilia kujua mtoto wake anamudu au hamudu zaidi masomo gani ili ajipange kutoa ushauri au msaada?

Mzazi kuwa na taarifa hizi ni jambo muhimu kwani zinakusaidia kujua ni kwa namna gani umsaidie mwanao, kwa kushirikiana na walimu, ili kumpatia mtoto uelekeo ulio sahihi katika maisha yake.

Ikigundulika kuwa mtoto wako ni mzuri upande wa kipaji fulani, mfano kuchora, mzazi na mwalimu mna wajibu wa kumsaidia mtoto huyu kukinoa kipaji hiki – badala ya kulazimisha mtoto asome taaluma asiyoipenda.

Kuna tabia inayofanywa na wazazi wengi tu ya kumlazimisha mtoto kusomea fani ambayo ni chaguo la mzazi. Wapo wazazi eti kwa kuwa yeye amesomea fani ya uhandisi, kwa mfano, basi atashinikiza mtoto wake asome sana hisabati, ili naye aje asomee uhandisi.

Huenda mtoto huyu ana kipaji cha uigizaji, uandishi vitabu au ubunifu mitindo, na mwenyewe anakipenda kipaji chake; kitendo cha mzazi kumlazimisha kufanya kitu asichokipenda kina madhara makubwa.

Mtoto aliyelazimishiwa fani asiyoitaka anaweza kufaulu na hatimaye akaajiriwa katika kazi hiyo. Lakini atakapokuwa ndani ya ajira hiyo ufanisi wake utakuwa wa kiwango cha chini.

Huyu atafanya kazi kinyonge, na atakosa ubunifu kwa sababu kazi aifanyayo haina msukumo kutoka ndani.

Na ikitokea mtoto huyu akakosa kuajiriwa haitakuwa rahisi kwake kujiajiri mwenyewe kwa sababu ya kukosa hamasa na ubunifu kupitia fani aliyolazimishwa kuisomea.

Kijana mwenye kipaji halafu akasaidiwa kukikuza na kukinoa, huyu hawezi kukosa ajira. Kwa upande mmoja anaweza kuwavutia watu, kwa kipaji chake, na wakaamua kumwajiri katika kampuni zao.

Kwa upande mwingine mtoto mwenye kipaji ana uwezo mkubwa wa kukitumia kipaji chake kujiajiri yeye mwenyewe – akajipatia kipato na kupiga hatua kubwa kimaendeleo.

Mfano mzuri wa hili ni mchoraji mahiri wa katuni, Masoud Kipanya.

Hatua ya kuchukua: mzazi usilazimishe mwanao aelekee upande wako kitaaluma wala kiujuzi. Msaidie kukijua kipaji chake, kisha msaidie kukinoa na kukibadilisha kuwa pesa.  

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Zijue Stadi Muhimu Kwa Mwanao Hadi Umri Wa Miaka 10… (4)

Habari rafiki,

Pole na majukumu ya kazi. Karibu tena katika mada hii muhimu, ikiwa inalenga kukukumbusha wewe mzazi ili uwe na mipango na mikakati ya kumpatia stadi za maisha mwanao.

Stadi hizi zina lengo la kuwasaidia vijana wetu kujijenga kimwili na kifikra kwa ajili ya kukabiliana vyema na maisha; likiwemo suala la uwezo binafsi wa kujitafutia ajira.

Kabla hajafikia umri huu – mtoto anapaswa awe anajitambua na kujisimamia, na hili ni jukumu la wazazi na walimu

Suala hili linatiwa uzito na kauli ya Dr. Vicensia Shule (soma sehemu ya tatu ya makala hii); aliposema kwamba kijana kujiajiri ni matokeo ya ujuzi na uwezo wake wa kujitambua, kujitegemea, kuthubutu na kufanya kazi bila kusimamiwa.

Hii ni sehemu ya nne na ya mwisho ya mada hii ya stadi zinazomhusu mtoto wa umri wa kufikia miaka kumi.

Huu ni muendelezo wa maeneo au mambo ambayo mtoto anapaswa kusaidiwa kuyajua ili akue akiwa na maarifa muhimu kwa maisha yake na ya jamii nzima. Katika sehemu ya pili ya mada hii tuliishia eneo la tano, sasa tuendelee…

Sita, elimu ya kupanga bajeti na kuisimamia. Hakikisha mtoto anajua mapema maana na jinsi ya kupanga bajeti.

Mwambie aseme mahitaji yake ya wiki nzima na gharama zake. Mpatie mtoto pesa kiasi fulani kila mwanzo wa wiki, na mhimize azitunze yeye na ahakikishe zinafika mwisho wa wiki.

Kama zitabaki kidogo, kila wiki, mhimize azitunze kama akiba ambayo baada ya mwezi mmoja atasema ametunza kiasi gani, na kiasi hicho akipangie matumizi yenye faida yanayomhusu yeye. Hapa atajifunza kutumia kwa umakini na pia uwekaji wa akiba.

Saba, elimu ya matumizi ya fedha kifamilia. Hii ni elimu ya fedha ambayo mtoto anapaswa kuianzia utotoni.

Mtoto ajue kuwa kila manunuzi yanapofanyika yanafuata bajeti iliyopangwa. Kwa mfano aambiwe kuwa leo hatukununua maziwa, anayoyapenda sana, kwa sababu bidhaa hiyo haikuwemo kwenye bajeti ya manunuzi.

Afundishwe kujua kuwa bidhaa huwa zinatofautiana bei. Kwa mfano; tumenunua sukari kutoka duka X badala ya duka Y kwa sababu duka X linauza kwa bei nafuu zaidi kwa sukari ileile.

Mzazi zoea kumhusisha mtoto kununua baadhi ya bidhaa. Mpatie pesa anunue, hasa bidhaa zinazomhusu moja kwa moja. Dukani mwambie mtoto aulize bei ya bidhaa hiyo na aoneshe bidhaa iliyo na bei nafuu zaidi, kisha mshauri anunue hiyo – na sababu ya kufanya hivyo.

Nane, elimu ya maadili na tabia njema. Ili kijana awe na tabia njema katika utu uzima wake ni jukumu la wazazi kumtengeneza tokea utoto wake. Mtoto anatakiwa afunzwe namna ya kusalimu watu wa rika mbalimbali.

Mtoto afunzwe namna ya kuongea na watu wazima, namna ya kuitikia akiitwa, namna ya kutoa majibu akiulizwa, na mambo yote yanayomjenga mtoto kuwa na maadili mema. Mtoto akikua hivi, hata akifikia utu uzima, atamheshimu kila mtu; na tabia hii itampa heshima na imani kubwa katika jamii.

Tisa, elimu ya kufanya maamuzi. Kila siku tukiwa watu wazima tunafanya maamuzi.  Tabia hii inapaswa kuanzia utotoni vinginevyo mtoto atakosa umahiri wa kufanya maamuzi sahihi ukubwani.

Anza kumsaidia mwanao kidogokidogo, kwa kumtaka achague kimoja kati ya vitu vingi; kwa mfano vyakula tofauti, nguo tofauti, vitabu tofauti n.k; na aseme kwa nini amechagua hicho kimoja.

Baadaye mshirikishe katika kufanya maamuzi makubwa zaidi. Hakikisha anafahamu kuainisha faida na hasara ya kila chaguo au uamuzi anaofanya, ikiwa ni pamoja na kujua umuhimu wa kutoa maamuzi kwa wakati sahihi.

Kumi, kuongoza ibada na kufanya maombi nyumbani. Ni muhimu mtoto alelewe katika maadili ya kumjua na kumcha Muumba wetu. Kwa hiyo mapema, aanze kuzoea kusali na kuomba kwa mujibu wa imani yenu.

Hatua ya kuchukua leo: mzazi una jukumu la kuhakikisha kijana wako anajifunza maarifa haya muhimu. Hakikisha unamsimamia na kuwa karibu naye kila siku ili kutoa mrejesho pale anapofanya vizuri au kukosea.

Kwa kufanya hivi utakuwa umemsaidia mwanao kukua kiakili na kimwili na kuwa raia mwema na tegemeo kwako na kwa Taifa.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Zijue Stadi Muhimu Kwa Mwanao Hadi Umri Wa Miaka 10… (3)

Habari rafiki,

Pole na majukumu ya ujenzi wa Taifa. Karibu tena katika mwendelezo wa mada hii muhimu ya stadi za maisha, ikiwa inalenga zaidi watoto wetu.

Hii ni sehemu ya tatu ya mada hii ya stadi zinazomhusu mtoto wa umri wa kufikia miaka kumi.

Uwezo wa kijana kujiajiri, kuajiriwa na kuwa makini kazini ni matokeo ya malezi bora ya wazazi

Nikiwa katika maandalizi ya mada hii napata bahati ya kumsikia kupitia redio, Mhadhiri wa fani ya Sanaa za Ubunifu, Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam, Mwl. Vicensia Shule, akiongelea suala la vijana wa Kitanzania kukosa ujuzi wa kujiajiri. Ni mada iliyonivutia sana, na nimeona nikushirikishe pia.

Pamoja na mambo mengine Mhadhiri huyu anasema, “malezi yakiwa ya hovyo utotoni, tabia mbaya zinazojengeka hujitokeza kwa uwazi watoto wanapofikia utu uzima.”

Anaongeza kwa kusema, “kijana kujiajiri ni matokeo ya ujuzi na uwezo wake kujitambua, kujitegemea, kuthubutu na kufanya kazi bila kusimamiwa. Ujuzi huu unakosekana kwa vijana wengi kwa sababu wazazi wameshindwa kutimiza wajibu wao wa malezi.”

Anasema, “kujiajiri sio suala la mtaji tu. Ni suala la ujuzi. Vijana wanatakiwa wawe na maarifa ya kujiajiari, ambayo ni pamoja na kujisimamia na kujituma. Ni wajibu wa wazazi kuwafundisha watoto tabia hizi. Hata hivyo, ni wazazi wachache wanafanya hili.”

Akifafanua hili, Mwl. Vicensia anasema kwamba kutokana na uzembe wa wazazi, vijana wengi, hata wanaohitimu elimu za juu, wanakosa maarifa ya kujiajiri au hata kutafuta kazi.

“Huko majumbani, zipo familia zimeajiri wasaidizi, wanaitwa ‘wadada wa kazi’, ambao wengine wanafanya kazi kama watumwa. Katika familia hizi mtoto anafanyiwa kazi zote, hadi kuogeshwa, pengine hadi anafikia umri wa kubalehe, hii ni hatari sana.”

“Kijana aliyelelewa hivi hawezi kujitegemea. Huyu amedekezwa kimwili na kiakili. Nina mifano mingi ya vijana ninaowafundisha Chuo Kikuu ambao hawawezi kufua, kupiga pasi, kujipikia, na hata kuoga…ukweli wapo wanaonuka!”, anasisiza Mwl. Vicensia.

Anasema kama mtoto alizoea kufanyiwa kazi zote; kufuliwa, kufanyiwa usafi wa chumba chake, kupikiwa n.k, mtoto huyu, hata akipata elimu ya Chuo Kikuu, hawezi kujiajiri kwa kuanzisha biashara; na hata akiajiriwa hawezi kujituma kazini (atakuwa goigoi tu); kwa kuwa hakuzoea kuwajibika nyumbani.

Mwalimu Vicensia anasema ujuzi wa kujiajiri unaanzia nyumbani, pale mzazi anapoanza kumpatia mtoto maarifa ya kujitambua na kuwajibika.

Mzazi hapaswi kumdekeza mtoto kwa sababu tu nyumbani kuna ‘mdada wa kazi’. Anapaswa kumzoesha mtoto kazi zote muhimu zinazogusa maisha yake ya kila siku. Mtoto akijengewa maarifa haya akili yake inakomaa na anaanza kuwaza ki-utu-uzima. Huyu anaweza kujitegemea. 

Hatua ya kuchukua leo: kama anavyosisitiza Mwl. Vicensia, mzazi una jukumu la kuhakikisha kijana wako anapata maarifa haya. Usije ukadhani mwanao bado mdogo kuyajua haya – utajikuta umechelewa.

Jenga mifumo nyumbani kwako ya kuwafanya watoto wako wawe na ujuzi na maarifa muhimu yatakayowafanya wajitambue na kujenga uthubutu.

Maarifa haya, baadaye, yatawapa uwezo wa kujiajiri, kujisimamia, kuwa na nidhamu, na kuwaza kimkakati kwa ajili ya kujenga maisha yao.

Tukutane katika sehemu ya nne ya makala hii ambapo nitafafanua maeneo mengine muhimu ambayo mwanao anatakiwa kuyajua mapema.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Zijue Stadi Muhimu Kwa Mwanao Hadi Umri Wa Miaka 10… (2)

Habari rafiki,

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii nimeeleza kwa ujumla kuwa stadi za maisha hujumuisha maarifa, ujuzi na mbinu zinazosaidia kuyafanya maisha yetu ya kila siku yawe na uelekeo ulio sahihi.

Stadi hizi zinatupa uwezo wa kujitambua, kuwa na nidhamu na kufanya vitu sahihi, kwa usahihi, vikifanywa mahala sahihi na kwa wakati sahihi.

Mzazi una wajibu mkubwa kumsaidia mwanao kujifunza stadi za maisha

Makala hii inatoa mada inayomlenga zaidi mtoto, kuanzia anapoanza kuelewa mambo hadi kufikia umri wa miaka kumi (10). Na hii ni sehemu ya pili katika mada hii.

Ukweli ni kwamba kuna vitu vingi muhimu ambavyo mtoto anapaswa kuvijua lakini kinachojitokeza ni kwamba wazazi wengi wanazembea katika kutimiza wajibu wao.

Sasa tunakwenda kuyajadili maeneo na vitu ambavyo mtoto anapaswa kusaidiwa kuvijua ili akue akiwa na maarifa haya muhimu kwa maisha yake na ya jamii.

Kwanza, mfundishe kupanga ratiba ya siku. Mzazi unapaswa, mapema, kumfanya mwanao kuyajua majukumu yake na kuthamini matumizi ya muda. Anza kwa kumfundisha kupanga na kuheshimu ratiba yake.

Kwa mfano, mtoto ajue anapaswa kuamka saa ngapi na azoeshwe kuamka saa hiyo. Ajue akiamka atafanya usafi kwa ujumla wake, kisha ataenda shule. Akitoka shule atasaidia kazi za nyumbani na halafu atafanya home work.

Akimaliza atakuwa huru kwa muda fulani ambapo anaweza kucheza au kuangalia TV. Baada ya hapo anatakiwa ajiandae kwa masomo ya kesho shuleni. Ukifika muda anaopaswa kulala mtoto ahimizwe kwenda kulala.

Ratiba, ikipangwa vizuri, na ikifuatwa, inamjengea mtoto nidhamu ya hali ya juu ambapo anayajua majukumu yake na muda wa kufanya, na hili linamkuza mtoto kiakili na kimwili.

Pili, usafi wa chumba na kitanda chake. Siku mpya huanzia asubuhi pale tunapoamka. Mtoto anatakiwa kujua jinsi na umuhimu wa kuweka chumba na kitanda chake nadhifu kabla ya kuondoka.

Hili linawashinda wengi wakiwemo watu wazima, na ukichunguza utagundua kuwa hawakupewa maarifa haya wakiwa wadogo. Wazazi waliwafanyia kila kitu kwa kudhani hawawezi. Majuto ni mjukuu.

Tatu, Kuoga, kufua na kusafisha choo, bafu na mazingira. Usafi wa mwili kwa mtoto huanza mara tu anapozaliwa. Mzazi ndiye anayefanya kazi hii. Sasa wazazi wengine hujisahau na kuendelea kumfanyia usafi mtoto hadi umri usiostahili.

Wapo watoto ambao hadi wanaenda Sekondari au Chuo hawawezi kufua nguo zao. Hii ni hatari. Mzazi unapoanza kufua, mwite mwanao akae karibu yako, aone. Baadae anza kumshirikisha taratibu hadi aweze mwenyewe.

Mfundishe mtoto hadi aelewe kuoga nwenyewe, kusafisha bafu na choo alichotumia, pamoja na usafi wa mazingira ya nyumba nzima. Kwa kufanya hivi mtoto anaanza kuujua vizuri mwili wake na mazingira yake.

Nne, kutayarisha chakula rahisi na kuosha vyombo. Ni busara, wakati unatayarisha chakula kumwita mwanao aje ashuhudie chakula kikitayarishwa. Anza na vitu kama chai, uji n.k, na jinsi anavyokua endelea kwa vyakula vingine. Mfundishe kuchambua mboga, kukatakata viungo n.k.

Kitu cha kuzingatia ni suala la usalama wake na wa nyumba, kwa mfano vitu kama moto na vitu vyenye ncha kali kama visu.

Tano, kujipa huduma ya kwanza kwa ajali ndogo. Mzazi huwezi kuwepo nyumbani muda wote. Mtoto akiwa nyumbani anaweza kujikata, kuumwa na mdudu n.k. Mfundishe mtoto kushughulika na dharura hizi.

Kwa mfano, mtoto akijikata mfundishe kutokubabaika. Asiogope damu. Mfundishe jinsi ya kuchukua kitambaa safi na kubana eneo alilojikata kuzuia damu, kisha alifunge jeraha kwa bandeji.

Mwambie hii ni huduma ya kwanza, na kama tatizo ni kubwa basi ajue anapaswa kwenda hospitali. Hili alifanye kwake na kwa watoto wenzake pia.

Sita, kuweka sawa mambo madogomadogo ya nyumbani. Mfundishe mtoto kupiga pasi, kupiga kiwi viatu, kushona kifungo cha shati kilicholegea n.k. Mtoto akishindwa haya madogo anakosa umakini na hata makubwa yatampa taabu baadaye.

Hatua ya kuchukua leo: mzazi, kuyasimamia maarifa haya, ni jukumu lako la msingi. Usipojali na ukadhani mtoto bado mdogo kuyajua haya utajikuta umechelewa na madhara yake ni makubwa.

Tukutane katika sehemu ya tatu ya makala hii ambapo nitamalizia maeneo mengine muhimu kwa mwanao kuyajua mapema.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Zijue Stadi Muhimu Kwa Mwanao – Hadi Umri Wa Miaka 10… (1)

Stadi za maisha ni moja ya masomo muhimu sana kwa watoto na vijana kwani huwapa maarifa mbalimbali kuhusu namna wanavyoweza kukabiliana na changamoto za maisha.

Ni wajibu wa mzazi kumsaidia mtoto kujenga maarifa muhimu katika maisha yake

Kwa ujumla, stadi za maisha hujumuisha maarifa, ujuzi na mbinu zinazoweza kusaidia kuyafanya maisha yetu ya kila siku yawe na uelekeo ulio sahihi. Zinatupatia uwezo wa kujitambua, kuwa na nidhamu na kufanya vitu sahihi, mahala sahihi na wakati sahihi.

Maarifa haya yakitumika na kusimamiwa vizuri humjenga mtu kuwa na mtazamo chanya kuhusu maisha yake binafsi na maisha yake ndani ya jamii.  

Kumbuka maisha yana changamoto nyingi, hivyo ni jambo muhimu sana kuwajengea watu uwezo ili waweze kuzishinda changamoto hizo na kusonga mbele kwa urahisi.

Makala hii inamlenga zaidi mtoto, kuanzia anapoanza kuelewa mambo hadi kufikia umri wa miaka kumi (10). Hii ni sehemu ya kwanza katika mada hii.

Wataalamu wa masuala ya watoto wanatuambia kuwa watoto, katika umri mdogo, ni wadadisi sana. Udadisi wao una lengo la kutafuta ukweli wa yale wanayoyaona na kuyasikia.

Watoto wana hamu ya kufahamu vitu kwa undani na ndio maana huuliza maswali mengi. Hili linawafanya watoto wengi wawe na uwezo mkubwa wa ubunifu katika umri mdogo, na huwazidi hata watu wazima katika hili.

Ki ukweli watoto wana uwezo mkubwa wa kuelewa mambo kuliko tunavyofikira.

Sasa, cha ajabu, na kinyume na ukweli hapo juu, ni kwamba kuna stadi muhimu kabisa za maisha ambazo watoto wanapaswa kuzijua – lakini kwa bahati mbaya – hawajizui!

Kwa mfano, si ajabu kumuona mtoto wa miaka mitano akiwasha simu janja (smart phone), kutafuta mahali ilipo ‘game’, na kuanza kucheza. Lakini mwambie mtoto huyu awashe jiko la mafuta achemshe chai yake,…hawezi!

Ukweli kuna vitu vingi muhimu ambavyo mtoto anapaswa kuvijua lakini kinachojitokeza ni kwamba wazazi wamezembea katika kutimiza wajibu wao.

Baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwadekeza watoto wao au kudhani hawawezi kufanya vitu fulani wao wenyewe…yaani wanahisi kuwa watoto bado hawajakomaa kimwili na kiakili pia.

Wakiwa na mtazamo huu, baadhi ya wazazi wamezoea kuwafanyia watoto kila kitu. Wapo wanaoogopa kuwa watoto wakifanya vitu fulani wenyewe wanaweza kuumia au kuviharibu vitu hivyo au vifaa vitumikavyo kutengenezea vitu hivyo.

Kimsingi watoto wanapaswa kusaidiwa katika kuanza kukua na kuwajibika. Hili linapaswa kufanywa mapema na mfululizo ili watoto wajenge uwezo na mazoea.

Kumfundisha mtoto stadi za maisha, kwa utaratibu mzuri, kunampa mtoto huyu uwezo wa kuanza kujitambua mapema, kuwajibika na kujenga uwezo wa kiuongozi – kwa kuanza kujiongoza yeye mwenyewe, na baadaye kuwaongoza wenzake.

Kwa muhtadha huu stadi za maisha ni muhimu sana kwa watoto. Na kwa watoto wenye umri wa kufikia miaka kumi, wazazi wana wajibu mkubwa kuwasaidia watoto hawa kupata stadi hizi na kuzitumia ipasavyo.

Hatua ya kuchukua leo: kama wewe ni mzazi na hukuwa na wazo wala mpango wa makusudi wa kumsaidia mtoto wako kuwa na maarifa haya, lichukue suala hili kwa uzito wake. Tengeneza mpango maalumu kwa ajili ya mtoto wako na anza kumweka karibu na wewe ili ajue kwamba una mpango maalum na yeye.

Kisha, usikose kuwa na mimi katika makala inayofuata ili uweze kuyajua maeneo ambayo unatakiwa umsaidie mwanao mwenye umri huo ili awe na uwezo nayo na aanze mapema kujenga nidhamu na uwajibikaji.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kupata Wagavi Bora Wa Bidhaa Zako

Rafiki mpendwa,

Unapofanya biashara yoyote, iwe ya kununua na kuuza, au ya kuzalisha mali na kuuza, ni lazima utafanya zoezi la ununuzi.

Ununuzi una taratibu na kanuni zake ambazo unapaswa kuzifuata ili kila unachopanga kununua kiweze kuwa na manufaa na kiongeze tija kwenye biashara unayoifanya.

Moja kati ya kanuni hizi ni kutafiti na kujua wauzaji au wagavi sahihi wa bidhaa au malighafi unayoihitaji na unayotaka kuinunua. Kumbuka sio kila muuzaji wa bidhaa ana sifa za kukupatia bidhaa unazohitaji.

Mfanyabiashara makini huchagua mgavi sahihi kati ya wengi wakiopo sokoni

Makala hii inakwenda kutoa ufafanuzi wa jinsi unavyoweza kupata wagavi wazuri kwa ajili ya biashara yako na jinsi ya kujenga uhusiano na ushirikiano nao.

Kwanza, chagua wauzaji bidhaa wanaoweza kukupatia huduma itakayotimiza mahitaji au matarajio yako. Kwa mfano, kama biashara yako ni ya bidhaa inayotoka kwa kasi, unahitaji mgavi mwenye uwezo wa kufanya hili.

Yaani hapa suala la gharama halitakuwa muhimu sana kwa kuwa suala kubwa kwako ni kupata bidhaa kwa muda unaotakiwa na kwa haraka.

Pili, jenga uhusiano mzuri na wagavi wako. Yaani, kwa mfano, kama unafanya biashara ya uzalishaji bidhaa, tengeneza ratiba ya uzalishaji kwa jinsi unavyoufanya, kisha wapatie ili waoanishe na ratiba yao ya uzalishaji wa malighafi unazozihitaji.

Tatu,wapatie mapema taarifa ya mahitaji yako ili wapate nafasi ya kufanya maandalizi yao na kukupatia bidhaa au malighafi kwa muda stahiki.

Nne, jaribu kukadiria mauzo yako ili ujue muda sahihi wa kutoa oda ya bidhaa yako.

Tano, kama unapewa bidhaa kwa mkopo, lipa bili zako mapema kwani kuchelewa kulipa kutazorotesha mahusiano.

Sita, tumia teknolojia kwa mawasiliano. Siku hizi teknolojia imekuwa kubwa na mawasiliano yamerahisishwa. Mawasiliano ya kisasa yatasaidia kufikisha taarifa za manunuzi haraka au pia kupata taarifa za bidhaa kwa wakati.

Saba, pata majibu sahihi ya maswali haya:

  • Je, bei unayopewa na anayekuuzia bidhaa ni nzuri kiasi gani?
  • Je, mgavi anakubali kukupunguzia bei au kukupa masharti nafuu?
  • Je, mgavi wako anakupa taarifa ya bidhaa au huduma mpya zilizoingia sokoni zinazoweza kuboresha biashara yako?
  • Je, mgavi wako anafanya mambo yake kwa wakati au muda sahihi?
  • Je, bidhaa zinafikishwa kwako zikiwa katika hali nzuri, mfano hazijavunjika?
  • Je, mgavi wako anaonesha uharaka au kujali kiasi gani unapoagiza bidhaa?
  • Je, mgavi wako anakupa maelezo ya matumizi sahihi ya bidhaa anayokuuzia?
  • Je, mgavi anakupa huduma za ziada baada ya manunuzi? Kwa mfano, kukusafirishia?

Nane, mtembelee muuzaji wako wa bidhaa uzungumze naye ana kwa ana kuhusu anavyofanya biashara yake; na chunguza thamani anayoipa biashara yako. Hii itakupa mwanga kujua kama atakufaa au hapana.

Tisa, ukiweza tafuta kujua mpango wake wa muda mrefu wa bidhaa anazouza ili ukisie athari za mpango huo kwa bidhaa au huduma anazokupatia. Kwa mfano, kama anakusudia kubadilisha biashara huenda ukakosa kupata bidhaa ulizokuwa ukinunua kwake.

Kumi, msaidie mgavi wako kwa kufanya haya:

  • Elewa unataka kununua bidhaa gani
  • Agiza bidhaa kwa wakati sahihi
  • Kuwa makini kuhusu aina ya bidhaa unayoagiza, usikosee maelekezo unayompatia
  • Eleza namna utakavyofanya malipo yako

Nihitimishe kwa kukuhimiza wewe mjasiriamali kuwa makini sana katika suala na ununuzi. Jitahidi kufanya uchunguzi wa kutosha ili upate muuzaji wa bidhaa atakayekupatia bidhaa bora na kwa wakati –  kisha jenga uhusiano mzuri naye.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Ukijenga Nidhamu Katika Maeneo Haya – ‘Utatoboa’

Habari rafiki,

Nimeeleza katika makala iliyopita kuwa nidhamu ni ile nguvu iliyojengeka ndani ya mtu inayomsukuma mtu huyo kufanya mambo kwa wakati, umakini, ujuzi na usahihi wa hali ya juu ili kufikia malengo fulani.

Mwanariadha maarufu, Haile Gabrselassie, aliwahi kusema, “kama umedhamiria kufanya kitu…ili uitimize dhamira yako…unatakiwa kuweka nidhamu na bidii ya kazi.” Kwa hiyo, kumbe nidhamu ni suala muhimu.

Ukitaka kujenga nidhamu binafsi – ongea na nafsi yako – na ielekeze unakotaka kufika – kisha ifuate

Katika makala hii nitatoa ufafanuzi wa tabia 8 ambazo ukizifanyia kazi utajijengea nidhamu ya hali ya juu na hakika maisha yako yatabadilika kwa kiwango kikubwa.

Moja, kuweka malengo imara. Uamuzi wa kujiwekea malengo katika maisha ni kiashiria kikubwa cha nidhamu binafsi. Yaani unataka kufanya mambo yako kwa mpangilio, umakini na usahihi, ukijua unataka kupata matokeo gani.

Ukipanga malengo na kujiwekea mpango wa utekelezaji, unakuwa umejiwekea dira na mwelekeo unaokufanya uone uendako.

Unashauriwa ujiwekee malengo ya mwaka, mwezi, juma hadi siku na uhakikishe malengo yako SMART, kama nilivyosisitiza katika makala hii.

Mbili, kufanya kazi kwa bidii. Jinsi unavyoweka juhudi na maarifa katika kila shughuli unajipambanua kwa nidhamu ya utendaji. Kwa kufanya hivi unatuma meseji murua juu ya umuhimu wa kazi.

Kuna misemo kama, “kazi ni kipimo cha utu…,” au “kazi ni uhai…” Hivyo nidhamu katika kazi ni jambo lisilohitaji mjadala kwa sababu linabeba mafanikio yako.

Tatu, nidhamu ya matumizi. Kila mtu anayejishughulisha anapata mapato kwa ajili ya kuendesha maisha. Kinacholeta tofauti huwa ni nidhamu ya matumizi.

Mtu mwenye nidhamu ya matumizi hubaki na ziada ambayo huihifadhi kwa ajili ya dharura na uwekezaji wa baadaye.

Ziada hii huhifadhiwa kama akiba. Akiba inatokana na utashi binafsi wa kujinyima leo ili kuijenga kesho njema. Hivyo ukijenga nidhamu ya matumizi, ukajizoeza kuweka akiba hakika utapiga hatua.

Nne, nidhamu ya kujifunza na kujiendeleza. Dunia tuliyomo kwa sasa ni dunia ya taarifa na maarifa. Mabadiliko yanakuja kwa kasi sana na ili uweze kunufaika na mbadiliko haya unapaswa kujifunza kila siku. Hili linahitaji nidhamu ya juu – kujituma, kuelimika na kuyatumia maarifa kupiga hatua.

Tano, nidhamu ya matumizi ya muda. Muda ni rasilimali muhimu sana kwa maendeleo. Muda ni mtaji…muda ni mali…muda ni pesa! Nidhamu ya muda inakutaka kuwa mahala sahihi, ukifanya kitu sahihi kwa wakati sahihi.

Yaani unatakiwa usiwe mtumwa wa muda na badala yake…uutawale. Hivyo, unapaswa kila dakika inayopita kujua umeifanyia nini cha maana.

Unatakiwa ujue ni muda gani wa kufanya kazi, kupumzika, kufikiri, kupanga, kusikiliza, mazoezi, burudani n.k. Ukishindwa kuwa na nidhamu katika hili ujue mafanikio utayasikia tu.

Sita, nidhamu ya ulaji. Tunapokula chakula tunapata nguvu za kimwili na kiakili kutuwezesha kufikiri vizuri na kufanya kazi. Mafanikio yako katika utafutaji wa mali yanategemea sana afya yako.

Nidhamu hapa ni katika matumizi ya chakula; yaani ule nini, saa ngapi na kwa kiasi gani. Ulaji usiofaa unahusishwa na magonjwa kama shinikizo la damu, kuongezeka uzito, kisukari na upungufu wa nguvu za mwili na akili.

Saba, nidhamu ya mazoezi. Mazoezi ya mwili ni suala lenye mahusiano makubwa na afya ya mwili. Nidhamu katika kufanya mazoezi siyo kitu cha kufanyia mzaha.

Ukweli suala hili linawashinda wengi. Wapo wasiofanya mazoezi kwa uvivu tu…wapo wanaodai hawana muda…wapo wanaosema hawana vifaa au maeneo ya kufanyia mazoezi n.k.

Sababu hizi zote hazina msingi, kinachohitajika ni nidhamu tu na kujituma kwa kuwa suala hili ni nyeti.

Mazoezi yana faida kubwa kama kuondoa msongo wa mawazo, kuweka sawa mzunguko wa damu mwilini, kuongeza oksijeni katika seli, kupunguza uzito wa mwili, na kuimarisha kinga ya mwili kupambana na magonjwa.

Hivyo jenga tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara. Anza taratibu, kidogokidogo kila siku na endelea hivyo siku zote, utaona matokeo yake.

Nane, nidhamu katika kumcha Mungu. Biblia inatuambia kuwa kumcha Mungu ndio mwanzo wa maarifa. Tunahimizwa kumcha Mungu na kumtumikia yeye…kuambatana naye…kumpenda yeye na kuapa kwa jina lake.

Nidhamu katika uchaji wa Mungu inatuelekeza kumtii muumba wetu na kufuata maagizo yake, kila siku, ili tuwe kama alivyotukusudia. Mafanikio yetu ni matunda ya nidhamu kwa muumba wetu.

Hatua ya kuchukua leo ni kuanza na kuendelea kujenga nidhamu binafsi. Tunaambiwa kuwa watu waliofanikiwa maishani wamefikishwa hapo na nidhamu katika mambo hayo juu, na mengine pia.

Walijifunza kujenga nidhamu katika kila walifanyalo na hii ikawasaidia sana kutimiza ndoto zao. Tuwaige watu hawa nasi tutafanikiwa.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Mobile: 0718219530

Vitu Hivi Hukwamisha Ubunifu Katika Biashara

Habari rafiki,

Dunia ya kibiashara hivi sasa imetawaliwa na mazingira ya ushindani wa kiwango cha juu, na kitu kinachoweza kumsaidia mjasiriamali binafsi au taasisi, kufanikiwa, ni uwekezaji katika ubunifu.

Taasisi ya DOT Tanzania inauelezea ubunifu kama uundwaji wa bidhaa au modeli mpya; bidhaa au huduma iliyoboreshwa; au bidhaa, huduma au modeli ya biashara iliyokuwepo lakini inaingizwa kwenye soko jipya kwa mara ya kwanza.

Ubunifu katika taasisi ni zao la umoja na mshikamano unaosimamiwa na viongozi wenye maono

Sasa, ili ubunifu uweze kufanyika katika taasisi au biashara, yanatakiwa yawepo mazingira yanayochochea ubunifu kufanyika.

Wapo watu ndani ya taasisi za kibiashara wenye mawazo mazuri kabisa ya kibunifu. Kwa bahati mbaya, viongozi wao wanakosa uelewa, mikakati au utashi wa kuyapokea mawazo bunifu na kuyafanyia kazi, na hiki ndicho kiini cha kudumaa kwa biashara nyingi kiubunifu.

Vipo vizuizi vingi ambavyo huwekwa mbele ya watu wenye mawazo bunifu vinavyowakatisha tamaa wasiweze kuyatoa mawazo yao yenye lengo la kuboresha.

Makala hii inakuletea sababu au vikwazo vinane vinavyokwamisha ubunifu katika maeneo ya kazi au biashara.

Moja, wasimamizi wa kazi kukosa maono na mbinu. Ili ubunifu uweze kufanyika, watu wenye mawazo bunifu wanatakiwa waelimishwe dira na lengo kuu la taasisi husika ili walete mawazo yanayolenga katika kufanikisha haya.

Hili ni jukumu la msimamizi wa biashara au taasisi. Huyu anapaswa kuwa na maono na mbinu, na uwezo wa kuwapatia wafanyakazi mwongozo na hamasa itakayowawezesha kufanya ubunifu ndani ya taasisi.

Mbili, watu hawana muda wa kujaribu vitu vipya. Zipo taasisi, ukizichungulia  utakuta kila mtu yuko ‘bize’ anakimbizana na malengo yake ya siku. Watu hawana muda wa kufikiri wala kujaribu kufanya kitu kipya. Sasa, viongozi wakishindwa kuliondoa hili hakuna ubunifu utakaofanyika.

Tatu, viongozi ni wazito kutoa maamuzi. Wapo viongozi katika taasisi ambao wametawaliwa na kigugumizi katika kuamua. Hawa huwa na tahadhari kubwa kwa kila kitu. Wanaogopa kuharibu mambo!

Kampuni ikiongozwa na watu wa aina hii hudumaa kwa kuwa kila mtu anakuwa mwoga, na utamaduni wa kulaumiana unatamalaki, na hivyo hakuna mtu anayethubutu kuleta mawazo bunifu au kitu kipya.

Nne, taasisi kuwa na mlolongo mrefu kutoa maamuzi. Hili ni tatizo – yaani, hata pale ambapo wazo limepokelewa na kuonekana lina tija ya kuzaa bidhaa bunifu – tatizo jingine linajitokeza.

Pendekezo la kulitia wazo zuri katika vitendo hupitishwa katika meza nyingi ili lipate idhini. Mchakato huu huchukua muda mrefu na huchelewesha utekelezaji. Ni vigumu ubunifu kupiga hatua katika mazingira haya.

Tano, ushirikiano hafifu baina ya idara. Taasisi nyingi zina udhaifu mkubwa katika mawasiliano na ushirikiano ki-idara. Yaani watu wa idara moja hawajishughulishi kujua kinachofanyika katika idara nyingine ili watoe msaada, taarifa, ushauri au rasilimali zitakazowezesha kazi kufanyika kwa wakati au ubora.

Kwa mfano, utakuta watu wa idara ya uzalishaji hawajishughulishi kujua nini kinaendelea katika idara ya masoko au mauzo. Huu ni udhaifu unaozorotesha hata suala la ubunifu – kwani kila idara inawaza ya kwao tu.

Sita, ubunifu wa wafanyakazi haupimwi. Ni muhimu katika kazi kila lengo analopewa mfanyakazi liwe na kipimo cha ufanisi. Kwa hiyo inapaswa pia pawepo utaratibu wa kupima uwezo wa wafanyakazi kufanya ubunifu unaoendana na malengo yao ya kazi.

Kipimo hiki kikiwepo huchochea mawazo bunifu kwa kuwa kinatoa msukumo kwa kila mtu kuonesha uwezo wake. Kipimo hiki kikikosekana kinaondoa hamasa, na hivyo watu hawaoni kama suala hili lina maana yoyote.

Saba, kukosekana kwa motisha. Taasisi ikilipa kipaumbele suala la ubunifu inapaswa kutoa motisha au bakshishi kwa watu ambao mawazo yao yanaongeza tija.

Motisha ikikosekana watu wanakosa msukumo na kuanza kuitazama taasisi kama chombo chenye ubinafsi, kinachoangalia maslahi yake tu.

Nane, hakuna bajeti ya kufanikisha ubunifu. Ukweli hakuna ubunifu utakaofanyika kama hakuna watu, muda na pesa. Hivyo kama taasisi itashindwa kufanya uwezeshaji huu ni wazi ubunifu utakwama.

Hatua ya kuchukua: Maeneo ya kazi na biashara, bila kujali ukubwa, yanapaswa kuondoa vihunzi katika ubunifu kama ilivyoainishwa hapo juu. Hili likifanyika, kasi ya ubunifu itakuwa kubwa na biashara zitapiga hatua kubwa za mafanikio.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Tabia Hizi Huwachukiza Sana Wateja – (2)

Habari rafiki yangu,

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii nimetoa ufafanuzi wa tabia tatu ambazo hazipendwi na ambazo huwaudhi wateja.

Hizi ni baadhi ya tabia ambazo zikiwepo katika biashara yako wateja huchukizwa nazo kiasi ambacho wapo tayari kuachana nayo na kutafuta huduma hiyo mahala pengine.

Mteja huchukia sana anapowekwa katika mstari au kwenye benchi muda mrefu bila huduma

Kumbuka tunapoongelea kitu kinachoitwa biashara kimsingi tunaongelea mteja – kwa kuwa hakuna biashara pasipokuwa na mteja, na mteja ndiyo pesa yenyewe.

Sasa, tabia yoyote inayofanywa na mtoa huduma ambayo itampatia mteja hisia hasi juu ya biashara husika, basi tabia hiyo haifai na inaweza kusababisha mteja kuichukia biashara hiyo na hata kuachana nayo.

Katika makala hii nitachambua tabia sita nilizobakiza, nikianzia na ya nne – kama ifuatavyo:

Nne, kutoa huduma ya upendeleo. Zipo biashara kadhaa, hasa mabaa na migahawa au mahoteli, ambapo wahudumu hutoa huduma kwa upendeleo. Kuna tabia ya baadhi ya wateja, na hasa wenye uwezo mkubwa wa pesa, wanapopewa huduma nzuri huwapa wahudumu chenji iliyobaki au bakshishi.

Kutokana na hili, baadhi ya wahudumu, nafsi zao huwa tayari zimetekwa na wateja hawa kiasi cha kupoteza uadilifu wa kazi. Nimewahi kushuhudia, mara nyingi tu, mhudumu akimruka mteja ambaye hamjui, au yule ambaye hana tabia ya kutoa ofa – baada ya kumwona ‘mteja wake’ aliyezoea kumpa bakshishi.

Tabia hii sio tu inaudhi bali pia inadhalilisha na siyo ya kistaarabu. Hakuna kitu anachokichukia mteja kama kuonekana hana thamani, kwa hiyo akiondoka hutamwona tena.

Tano, kubadilika-badilika kwa bidhaa au huduma. Wateja hupenda bidhaa au huduma inayoeleweka na kutabirika. Hawapendi leo huduma ni nzuri lakini kesho huduma mbovu. Au leo bidhaa ina ubora lakini kesho unakutana na  bidhaa duni kabisa.

Mteja anapenda kujua kwa uhakika kuwa siku yoyote akija katika biashara yako atakuta bidhaa bora, au atakutana na utaratibu fulani maalum wa namna huduma inavyotolewa. Akigundua kuwa huduma au taratibu zako hazileweki-eleweki, leo hivi – kesho vile, mteja anakosa amani na anaweza kuhama.

Sita, ushawishi uliopitiliza kumtaka mteja kununua. Kwa kawaida mtoa huduma mzuri anapaswa kuwa na uwezo wa kumshawishi mteja kununua bidhaa au huduma. Hata hivyo, wapo wateja mbao ushawishi ukizidi, huchukuliwa kama shuruti.

Mteja akishawishiwa mno anaanza kuhisi kama analazimishwa kununua, na hivyo anaanza hata kutilia mashaka ubora wa bidhaa hiyo. Tabia hii huwaudhi wateja hawa na wengine huikimbia biashara hiyo.

Saba, bei isiyoendana na hali halisi. Hapa haidhuru ni bei kubwa sana au ndogo sana – inategemeana na bidhaa au huduma husika. Sasa, kama unauza bidhaa ya kawaida kwa bei kubwa, tofauti na wengine, wateja wanaweza kukukimbia.

Vilevile, kama unauza bidhaa yenye thamani kwa bei inayoonekana ya chini sana, wateja wanaanza kupata wasiwasi na thamani iliyomo ndani ya bidhaa hiyo; na hasa bidhaa kama chakula, dawa na hata vifaa vya ki-elektroniki.

Nane, huduma hafifu baada ya mteja kununua. Wapo watoa huduma ni wazuri sana kabla mteja hajanunua. Hapa mteja ni mfalme. Akishanunua tu ufalme wake unaisha na tayari anakosa maana.

Akishanunua bidhaa, mteja huyu hasaidiwi kuifunga, kuibeba wala kuipakia katika chombo cha usafiri. Aidha mteja hapewi maelekezo ya matumizi ya bidhaa, namna ya kuisafirisha kwa usalama na hata jinsi ya kuihifadhi.

Wateja wanachukia sana biashara zenye urafiki wa msimu zinazomjali mteja kwa lengo la kumvuta tu; pasipo kumjali wakati wote.

Tisa, mazingira machafu na yasiyo salama. Suala la usafi au usalama katika biashara ni jambo muhimu sana. Jambo hili lina mashiko zaidi hasa unapoongelea bidhaa za vyakula na vinywaji. Mteja hayuko tayari kurudi anapogundua kuwa bidhaa yako haimhakikishii usalama na afya yake.

Ushauri kwa Wajasiriamali: hizi ni baadhi ya tabia mbaya ambazo wateja hawazipendi. Kwa hiyo, kama unataka kupiga hatua katika mazingira ya ushindani wa biashara jiepushe na tabia hizi.

Kumbuka ni rahisi kumpata mteja mpya lakini ukimuudhi ujue hatarudi na atapeleka sifa hiyo mbaya kwa rafiki zake, na hao utawakosa pia.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com

Tabia Hizi Huwachukiza Sana Wateja – (1)

Habari rafiki yangu,

Tunapoongelea kitu kinachoitwa biashara kimsingi tunaongelea mteja – kwa kuwa hakuna biashara pasipokuwa na mteja. Kifupi mteja ndiyo pesa kwa sababu biashara ikikosa mteja haitakuwa na mapato – na kwa hiyo haitazalisha faida – na mwisho wake itakufa!

Biashara zinazofanikiwa ni zile zenye uwezo wa kuwavuta wateja na kuwabakiza katika himaya ya biashara kwa sababu ni wateja ambao huifanya biashara iinuke na kuendelea kukua.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wafanyabiashara hawajui, wanajisahau au wanapuuzia umuhimu wa wateja. Hawa ni wale wanaoendesha biashara zao kwa mazoea na kushindwa kuwapatia wateja wao huduma bora.

Wateja wanapenda mtu anayewasikiliza na kuwajali

Huduma bora kwa mteja inaweza kuelezewa kama zile hisia chanya anazojenga mteja ndani yake – zinazobebwa na namna mteja alivyoridhishwa na bidhaa au huduma aliyopewa na mtoa huduma wake.

Sasa, kama wewe ni mfanyabiashara, unapaswa kujua vitu au tabia ambazo wateja hawazipendi au wanachukizwa nazo wanapokuja katika biashara yako. Ukiweza kuzijua tabia hizi unatakiwa kuchukua hatua haraka ili kuepusha biashara, bidhaa, huduma na watoa huduma wako kupoteza mvuto mbele ya wateja.

Zifuatazo ni  tabia ambazo hazipendwi na ambazo huwaudhi wateja, na zikiwepo wateja wapo tayari kuachana na biashara yako na kutafuta huduma hiyo mahala kwingine. Katika makala hii nitachambua tabia tatu, halafu katika makala ijayo nitachambua zilizobakia.

Moja, hakuna tabasamu, karibu wala kwa heri. Hii ni tabia inayoonekana kwa watoa huduma wengi. Yaani mteja anaingia katika duka, kwa mfano –  lakini mhudumu anakuwa kama hajamwona. Utakuta yuko bize na simu yake anaongea au ku-chat. Akiwa amesitisha kwa muda ku-chat, utasikia, ‘enhe ulikuwa unasemaje?

Ukweli wateja hawapendi mhudumu mwenye dharau, anayenunanuna na asiye na tabasamu. Mhudumu mwenye maringo, mkaidi, mkali na asiyechangamka hugeuka kuwa kitisho kwa mteja.

Mteja anapoingia katika biashara yako akaona hachangamkiwi wala hakaribishwi vizuri anakosa amani ya roho. Akigundua anaweza kupata vitu hivi mahala pengine, hakika hutamwona tena mteja huyu.

Mbili, watoa huduma wasiojali wala kusikiliza. Tabia hii hutokea mara nyingi pia, hata katika biashara kubwa. Unaingia katika baa, hoteli au duka – unakaa hadi robo saa, hakuna mhudumu anayekuja kukuuliza unahitaji nini. Lakini unawaona wanaongea na kupitapita tu bila kujali.

Au pengine umeagiza juisi, kwa mfano, lakini mhudumu anakuletea soda na hata kabla hajathibitisha tayari keshaifungua hiyo soda na kuimimina katika glasi. Ukilalamikia kitendo hicho unashangaa mhudumu, badala ya kuomba radhi, anakunja uso, wakati ni yeye aliyekosa usikivu.

Ukweli tabia hii inaudhi sana – ni tabia ya dharau kwa mteja inayomfanya mteja ajiulize kama kuna sababu ya wewe kuanzisha biashara halafu unawapuuza namna hii watu wanaokuletea pesa.

Ni kweli kwamba wakati mwingine watoa huduma wanakuwa wametingwa na wingi wa wateja. Hata hivyo ni wajibu wa msimamizi kuhakikisha anakuwa na mawasiliano na wateja ili wajue kuwa hawajapuuzwa – na jitihada zinafanywa ili nao wapate huduma.

Tatu, wahudumu kupiga soga na kuteta. Ukiingia katika maeneo ya biashara fulani utashangaa. Unaweza kuwa na bahati – ukakaribishwa na kuambiwa usubiri. Lakini baada ya hapo utashangaa wahudumu wawili au watatu wamekusanyika katika pembe moja ya chumba – wanamteta mtu – wanacheka na kugongeana mikono.

Yaani wameshasahau kama kuna mteja anahitaji huduma na ana haraka zake. Ukisikiliza vizuri unagundua kuwa wanayemteta ni mteja aliyeondoka punde hivi. Wanajadili mambo yake!

Ukweli tabia hii inaudhi sana. Hata kama wanaloongea linamhusu mteja mwingine; lakini anayetetwa ni mteja kama wengine. Hujui ukitoka, kama na wewe hutaishia kusemwa kama mteja aliyetangulia.

Ushauri kwa Wajasiriamali: huduma bora kwa mteja ni jambo lisiloepukika kama unataka kupiga hatua na kama unataka kuushinda ushindani wa biashara.

Unapaswa kujiepusha na tabia zote zinazoweza kumuudhi mteja kwani ni rahisi kumpata mteja lakini ukimpoteza unaweza usimpate tena na hii ni hatari kwa mustakabari wa biashara yako. Makala ijayo nitamalizia tabia zilizobakia.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com