Nini Nafasi Ya Nidhamu Kufanikisha Biashara au Kazi?

Habari rafiki,

Sababu kubwa inayofanya watu wachelewe kufanya – waahirishe kufanya – au wasifanye kabisa kazi au majukumu waliyopanga au kupangiwa kufanya ni moja tu…ukosefu wa nidhamu!

Hili huonekana wazi katika kazi mbalimbali za kuajiriwa, ambapo, mwajiriwa asipotimiza wajibu wake kabisa au akichelewa kufanya kazi yake kwa ubora au muda uliopangwa, anaadhibiwa kwa mujibu wa taratibu za kinidhamu.

Kwa hiyo kumbe nidhamu ni jambo muhimu sana katika kufanikisha utendaji wa kazi yoyote.

Shule ni moja ya taasisi zinazomjenga mtoto kuwa na maadili na nidhamu binafsi

Kifupi, nidhamu ni ile nguvu ya ndani iliyojengeka kwa mtu inayomsukuma mtu huyo kufanya mambo kwa wakati, umakini, ujuzi na usahihi wa hali ya juu ili kufikia kusudio fulani.

Yaani nidhamu ni kitu kinachotoa msukumo au uwezo binafsi unaomwezesha mtu kuinuka na kufanya kitu au kazi anayopaswa kufanya – na aifanye bila kujali anajisikia kufanya au la.

Nidhamu inaelezewa pia kama ile hali ya mtu kuwa na utii, heshima, unyenyekevu na umakini katika kufuata kanuni, sheria na miongozo mbalimbali ili kuyafikia malengo tarajiwa.

Kwa sababu hiyo, ndio maana mtu mwenye kiburi na dharau; ambaye hafuati sheria na kanuni; na anayefanya mambo ya aibu mbele za watu, husemwa kuwa hana nidhamu. Nidhamu humfanya mtu aheshimike na aonekane wa kipekee tofauti na wengine.

Watu wengi hupenda kupata matokeo mazuri katika kazi, biashara, masomo, ndoa na mambo ya kijamii. Hata hivyo, tatizo linalowakabili wengi, wakashindwa kupata matokeo hayo, ni kushindwa kuwekeza katika kujenga nidhamu binafsi.

Hebu mfikirie mtu anayeamka mwenyewe saa kumi alfajiri akikatiza usingizi wake – akitoka nje usiku wenye baridi kali au mvua ikinyesha – ili akafanye kazi au jukumu alilojipangia au kupangiwa kufanya.

Huyu, sio kwamba anafanya hivyo kwa sababu anajisikia sana kufanya kazi hiyo; au sio kwa vile ni muhimu sana kazi hiyo kufanyika; au siyo kwa sababu asipofanya kazi hiyo atamuudhi mtu fulani – hapana.

Kwa sababu… wapo watu ambao hukaidi au kuchelewa kufanya kazi zao muhimu au kazi walizopangiwa kufanya na viongozi wao kwa sababu hawajisikii tu; na wakati mwingine wako tayari hata kuadhibiwa kwa kosa hilo.

Kwa hiyo, kitu kinachomfanya mtu ainuke na kujituma kufanya kazi au kutimiza wajibu bila kujali mazingira yanayomzunguka ni nidhamu binafsi aliyojijengea yeye mwenyewe.

Utakuta mtu huyu kabla ya kulala usiku, anajipa ‘ahadi’ ya dhati kabisa kuwa ni lazima aamke alfajiri sana, bila kujali mazingira, na aanze kufanya kazi aliyojipangia au kupangiwa kufanya.

Ile ahadi anayojipa mtu – kwamba ni lazima ainuke ili afanye kitu fulani bila kujali hali – ndiyo nidhamu yenyewe – na ndiyo msukumo au kichocheo kinachomwezesha kuinuka na kufanya.

Nidhamu ni chumvi au kirutubisho kinachounganisha malengo mazuri aliyojiwekea mtu na bidii anayoweka katika kutekeleza au kuyafikia malengo hayo.

Nidhamu ni nguvu au msukumo unaokuwezesha kuwa na uthibiti wa mambo au maamuzi yako mwenyewe pasipo kulazimishwa na nguvu ya mazingira yanayokuzunguka.

Nidhamu hujenga nguvu ya mwili na akili, na hali ya kujiamini, na humfanya mtu ajipambanue miongoni mwa wengi kama mtu aliyekamilika na kukomaa.

Kwa hiyo, hatua ya kuchukua leo ili uweze kufanikisha kazi au biashara yako ni lazima ujenge nidhamu binafsi. Ni nidhamu ndiyo itakupa msukumo wa kutenda kwa wakati, umakini, ujuzi na usahihi wa hali ya juu ili kuyatimiza malengo yako.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Mobile: 0718219530

Utafiti Kupita Kiasi Huzorotesha Utekelezaji

Habari rafiki,

Karibu tena katika mfululizo wa makala zangu zenye lengo la kuelimishana kuhusu masuala ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Katika makala hii nitazungumzia tathmini ya wazo la biashara na yatokanayo na tathmini hiyo; na nitaongozwa na msemo wa kiswahili usemao, “ukimchunguza sana bata huwezi kumla.”

Nimeandika huko nyuma kuwa unapopata wazo la biashara unakuwa umeliunda wazo hilo kichwani, na unaona jinsi unavyoweza kulitia wazo hilo katika vitendo, na jinsi unavyoweza kufanikiwa kupata matokeo.

Hata hivyo wataalamu wa biashara wanashauri kwamba mjasiriamali apatapo wazo au mawazo kadhaa ya biashara yanayomtia hamasa, anapaswa kujiridhisha kwanza kabla ya kuanza utekelezaji kivitendo.

Yaani mjasiriamali anatakiwa kufanya utafiti ili kukusanya taarifa muhimu zitakazompatia uelewa wa kutosha wa biashara na mazingira yake.

Akijiridhisha kwamba tayari amepata taarifa hizo na kuzielewa – basi anaweza kuanzisha vitendo.

Ukweli ni kwamba kufanya utafiti ni hatua muhimu katika kuifanikisha biashara. Utafiti huzalisha taarifa na takwimu ambazo humpatia mjasiriamali nguvu na ujasiri wa kuanza utekelezaji.

Ukifika kituoni usiendekeze mno uchunguzi wa mabasi…utaishia kuachwa!

Hata hivyo, utafiti au uchunguzi unaofanyika ukizidi kiasi unakwamisha uwezekano wa wazo zuri kutiwa katika matendo. Kwa mujibu wa Mwanasaikolojia Barry Schwartz, utafiti haupaswi kwenda ndani sana kwani utakwamisha utekelezaji.

Kuchukua muda mrefu katika hatua ya kufikiri, kukusanya na kuchambua taarifa kuna madhara ya kuchelewesha au kukwamisha kabisa utekelezaji. Na kitu chochote kinachosababisha hatua stahiki isichukuliwe ni adui wa mafanikio yako.

Maana yake ni kwamba mjasiriamali anakuwa na nia nzuri tu ya kupata taarifa nyingi na muhimu kuhusu uwezekano wa biashara husika kufanikiwa ili akifanya maamuzi – yawe bora zaidi.

Hata hivyo, kinachojitokeza ni kwamba jinsi anavyokusanya taarifa nyingi zaidi ndivyo anavyotengeneza ugumu katika kutoa maamuzi ya utekelezaji. Ni ukweli pia kuwa taarifa nyingine humtia mhusika woga au kumkatisha tamaa.

Sasa, kama kufanya utafiti mwingi huzorotesha utekelezaji – kumbe jambo hili linapaswa kuangaliwa kwa tahadhari. Hii ina maana kuwa pamoja na umuhimu wa utafiti ipo haja ya kuufanya utafiti huu kwa kiasi tu ili kuacha nafasi ya kufanyika kwa haraka maamuzi ya utekelezaji.

Ndiyo maana mtaalamu mmoja wa ujasiriamali anasema kwamba kitu cha msingi na muhimu kabisa baada tu ya kupata wazo – ni uamuzi wa kuanza utekelezaji mara moja.

Anasema, “fanya utafiti kiasi ili kupata ushahidi fulani kuwa wazo lako ni la maana na lina mashiko. Ukishapata ushahidi huu basi anza utekelezaji, tena usisitesite.

Hili linatiwa nguvu na kaulimbiu ya kampuni ya viatu vya michezo, Nike, inayosema ‘just – do – it! Yaani; ‘usichelewe, anza kufanya’. Maana yake ni kwamba kama una wazo zuri na kila linavyozunguka kichwani mwako linakupa ushawishi ulifanye – basi anza kulifanya haraka.

Wataalamu wa saikolojia wanasema kuwa ukianza mapema kulitia wazo lako katika vitendo, akili na mwili vinapata msukumo wa ziada wa kuendelea kulifanya jambo hilo.

Vilevile kwa kuanza mapema kulitia wazo lako katika vitendo unapata nafasi nzuri ya kujipima ili kuthibitisha kama unalipenda wazo hilo na unalifurahia; lakini pia unaendelea kujifunza huku ukiendeleza utendaji.

Kimsingi wazo hilo ni la kwako na huenda umechukua muda mrefu kabisa kulifikiria na kulitafakari kabla ya kuamua kuwa ni wazo la maana ambalo unapaswa kulitia katika vitendo.

Ushauri kwa wajasiriamali ni kwamba ni jambo zuri na la maana kufanya utafiti wa wazo lako kabla ya kulitia katika utekelezaji. Hata hivyo utafiti huu usiwe wa kina mno kiasi cha kukukatisha tamaa au kuchelewesha utekelezaji.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com

Je Kufeli Ni Dalili Ya Udhaifu?

Habari rafiki

Kinachowakabili watu wengi, wakashindwa kuanza au kuendeleza kitu walichokianzisha, ni woga. Na kwa kweli – ni woga wa kufeli!

Ndiyo, watu wengi wanaogopa kuanza wakihofia watafeli, na kikubwa, wanaogopa gharama za kufeli. Ukifuatilia utagundua kuwa tunaishi katika jamii inayoabudu mafanikio. Na kwa hiyo kufeli kunachukuliwa kama udhaifu hivi.

Ukweli ni kwamba tunafanya makosa makubwa; yaani tunachukulia kufeli kama alama ya udhaifu au upungufu, wakati kiuhalisia kufeli ni hatua muhimu katika kujenga ufahamu au ujuzi wa mtu.

Mwandishi Robert Kyosaki amewahi kuandika kuwa tunajifunza kwa kiwango kikubwa kuhusu sisi binafsi au yale tunayofanya – tunapofeli; na anasisitiza kuwa tusiogope kufeli kwani kufeli ni sehemu muhimu katika mchakato wa mafanikio.

Kufeli ni hatua muhimu katika safari ya mafanikio -hivyo usiiogope

Kwa kawaida, kufeli sio kitu kinachoshabikiwa sana, na mara chache sana kukuta matukio ya kufeli yakirekodiwa na kutunzwa katika vitabu vya kumbukumbu. Kumbukumbu nyingi zimejaa historia za waliofanya vizuri. Hata hivyo, kufeli ni chombo muhimu katika kumpatia mtu mafanikio.

Na ni umuhimu huu ambao unayafanya makampuni mengi siku hizi kupenda kuajiri watu  wenye historia ya kufaulu na kufeli pia. Makampuni haya yanaona kuwa ili kutengeneza njia ya haraka ya mafanikio ni muhimu kujenga mtazamo chanya juu ya dhana ya kufeli.

Makampuni kama General Electric na Virgin Atlantic yanaamini katika uthubutu, na kwamba kufeli ni moja ya matokeo ya tabia ya kuthubutu kutenda jambo. Viongozi wa juu katika makampuni haya hawana tabia ya  kulalamika ikitokea wao au wafanyakazi wa chini wakafeli kufanya kitu fulani.

Badala ya kulialia, wao huangalia ni kwa namna gani wanavyoweza kugeuza kufeli huko kuwa kitu chenye tija. Na njia iliyo rahisi kuleta mafanikio ni kujenga mtazamo chanya juu ya dhana ya kufeli.

Ukweli wa mambo ni kwamba ukitaka ‘kutoboa’, yaani kufikia uwezo wako wa juu, au kufanya yasiyofikiriwa au yasiyowezekana – hutakiwi kuogopa kufeli. Unatakiwa uwe na uwezo wa kubadili makosa yako ili kuyafanya yatumike kama ngazi ya kuyafikia mafanikio.

Kufeli ni kitu kizuri, na hasa dhana hii inapotumika kama ngazi ya kuyafikia mafanikio. Mfano mzuri unatoka kwa Thomas Edison, aliyevumbua balbu ya umeme. Inasemekana Edison alifanya majaribio yapatayo 1000 kabla ya kumudu kuunda balbu.

Alipoulizwa alijisikiaje kufeli mara 1000 nzima – Edison alisema, “ukweli sikufeli mara 1000, bali nilipitia hatua 1000 kabla ya kuvumbua balbu.” Tofauti na Edson, watu wengi huogopa au hujiepusha sana na uwezekano wa kufeli – wanapofanya vitu.

Mtu mwenye roho ya uthubutu haogopi kujaribu wala hana woga wa kufeli kwa kuwa ana uwezo wa kuvumilia kufeli. Mtu huyu analitazama suala la kufeli kwa jicho chanya. Na ikitokea akafeli hapungukiwi na nguvu, bali anapata motisha na ujasiri zaidi. Hii inamsaidia kujifunza na kujua amekosea wapi na kwa nini.

Ukijiuliza kwa nini umefeli, unaanza kuifungua milango ya mafanikio. Udadisi huu unazaa uwezo wa kufikiri ili kutafuta majawabu na mwisho wake ni kufanikiwa.

Unahimizwa usijali umefeli mara ngapi, cha msingi ni kwamba kila unapofeli unapata somo la kujifunza kupitia uzoefu na hivyo unapata maarifa zaidi na uwezo wa kusonga mbele. Kufeli kunakufanya uujue uwezo au udhaifu wako na kukufanya uchukue hatua stahiki.

Wakati fulani kufeli kunakupa ufahamu na kukuonesha kitu ambacho hujakiweka sawa au uzembe uliofanyika katika jitihada zako za kuyafikia malengo. Na kwa hiyo siri ya mafanikio yako ni kuwa makini  kuhakikisha malengo yako yanafikiwa.

Somo tunalojifunza hapa, kama wajasiriamali, ni kwamba kufeli au kushindwa kufanya kitu fulani ni fursa ya kujifunza. Kufeli ni mwalimu muhimu – hivyo kama unataka kufanikiwa katika shughuli yako yoyote usiogope kufeli.

Hata hivyo sio vizuri pia kuingia kichwakichwa katika kufanya jambo eti kwa kuwa huogopi kufeli – hapana! Kwa kila unachotaka kufanya unapaswa kujiandaa vizuri ili hata ukifeli unapata urahisi wa kujifunza na kubaini mahala ulipokosea. Hii inakusaidia kujipanga upya, kukusanya nguvu, na kusonga mbele.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Jinsi Faraja Inavyoweza Kuwa Sumu Ya Mafanikio Yako

Habari rafiki,

Faraja ni neno la Kiswahili lenye maana ya utulivu wa moyo. Mtu akiwa katika mazingira ambayo hayampi maumivu au shida – anajihisi kuwa na faraja – yaani, anakuwa ‘comfortable’.

Kwa kawaida, binaadamu anapenda na anafurahi anapoishi katika mazingira yanayompa faraja. Ukweli hakuna mtu anayependa kupata shida au kuishi kwa maumivu au mateso. Na mtu akijikuta katika mazingira yanayompa mateso anajiona ana mkosi au balaa, na angependa kuepukana na hali hiyo haraka.

Ukitaka mafanikio jifunze kuzikabili changamoto kwa kukubali kuishi kwenye discomfort zone

Sasa, kinyume na fikra za wengi, Mwanafalsafa mmoja anatuhimiza tusishabikie sana maisha ya faraja. Anatuhimiza tujenge uwezo wa kusaka, kutafuta au kupokea mazingira ya maumivu au mateso, ili kupata mafanikio. Anatuhimiza tuzikabili changamoto.

Bill Eckstrom, ni mwanzilishi wa Taasisi ya Ecsell ya nchini Marekani na ni mfanyabiashara maarufu. Bill anasimulia mkasa uliompata katika maisha yake ya kazi ya kuajiriwa.

Yeye alikuwa Mtendaji Mkuu katika Kampuni moja binafsi. Alikuwa analipwa vizuri sana na alipewa marupurupu mengi. Kwa kweli alifurahia maisha kwa kuwa nafasi yake ilimwezesha kuishi maisha ya faraja, yasiyo na shida wala maumivu.

Kutokana na faraja aliyoipata akiwa katika nafasi hii kubwa, hakuwahi kufikiria kujihusisha na kitu chochote, cha kwake binafsi, kinachoweza kumpatia kipato akiwa kazini au hata wakati atakapomaliza utumishi wake katika kampuni hiyo.

Hebu tujiulize, hivi fikra hiyo ingetoka wapi? Mtu anayepata kila kitu, ikiwa ni pamoja na heshima anayopewa na kila mfanyakazi na hata wateja huko nje ya Kampuni, ana presha gani?

Ki-ukweli, aliona Mungu kamjalia kumpatia neema hii, hivyo hakuwa na haja ya kusumbuka – aliipumzisha akili yake, isibugudhiwe na mambo mengine, isipokuwa majukumu ya kazi yake, basi!

Lakini, Waswahili wanasema Mungu si Athumani! Siku moja ameingia kazini kwake vizuri tu asubuhi kama kawaida. Amefanya kazi hadi mchana alipoondoka kwa ajili ya chakula cha mchana. Aliporudi tu, alikuta wito maalumu katika ofisi ya Rais wa Kampuni.

Alipoingia ofisi ya Rais, alikaribishwa na maneno machache sana yaliyoambatana na barua fupi iliyomtaarifu kuwa kuanzia siku hiyo, hataendelea kuwa mtumishi katika Kampuni hiyo.

“Nilichanganyikiwa nisijue la kufanya, na sijasahau jinsi maneno ya Rais wangu yalivyokata pumzi yangu,” anasema. Anadai kuwa alipewa sababu, ambazo ingawa hakukubaliana nazo, hakuwa na njia nyingine bali kukubaliana na uamuzi huo.

Anasema, “nikiwa mnyonge na niliyechanganyikiwa, niliondoka ofisini jioni ile na nilipofika nyumbani nilijifungia ndani kwa masaa manne, nikitafakari, nikiwa siamini kilichotokea.”

Hata hivyo, Bill anasema, alikuja kubaini baadaye kuwa tukio lile lilikuwa tukio muhimu sana katika maisha yake. Ni tukio lililomuondoa ‘kwa nguvu’ kutoka katika faraja, na kumdondosha juu ya jukwaa la maumivu au shida.

Alijikuta katika mazingira ya kutokuwa na kazi wala kipato, na alianza kukabiliana na msoto uliomfanya aone jinsi upande wa pili wa faraja; upande wa discomfort, ulivyo. “Hata hivyo sikukata tamaa wala kubweteka,” anasema. “Nilituliza akili na kuanza kujenga fikra bunifu ndani ya ubongo wangu.”

Anasema baadaye aligundua kuwa ni msoto alioupata; yaani mateso ya kuondoka katika mazingira ya faraja ndiyo yaliyobadilisha maisha yake. Na ndipo akabaini kuwa, kumbe faraja ikizidi inadumaza akili za watu.

Msoto ulimfanya Bill kupata wazo la kuanzisha Kampuni yake binafsi. Na ni msoto uliomfanya ‘aione’ milango ambayo mwanzioni alikuwa haioni. Ni msoto pia uliomfanya apate nguvu na ujasiri wa ‘kuifungua’ milango hiyo – vitu ambavyo hakuwa navyo zamani.

Baada ya muda si mrefu, Bill alianza kuendesha biashara yake mwenyewe na kila mtu alishangazwa na mafanikio na kasi ya ukuaji wake. Kutokana na mafanikio haya, Bill anatoa ushauri kuwa ili binaadamu apate kukua, anapaswa, kila wakati, kujiondoa kutoka katika faraja.

Ni faraja – ambayo hudumaza akili, na ambayo humwondolea mtu uwezo wa kufikiri na kutenda. Faraja humfanya mtu awe kama kuku wa kisasa, asiyeweza hata kusogelea chakula alichowekewa umbali wa futi mbili.

Fundisho tulipatalo hapa ni kwamba watu hupata shida wanapoondoshwa katika faraja. Lakini kikubwa ni kwamba hali hii ikitokea unafanya nini? Bill anasema, “ni jinsi unavyoipokea hali hii ndivyo ambavyo utatengeneza njia yako ya mafanikio” Tukimuiga Bill, hakika mafanikio yatakuwa upande wetu.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Je, Uko Tayari Kuwa Mtumwa Wa Mawazo ya Wengine?

Habari rafiki,

Katika utafutaji wa maisha watu hujitahidi kufikiri ili kupata mawazo mbalimbali ambayo yanaweza kubadilishwa kuwa fursa zitakazowaingizia kipato na kubadili maisha yao.

Katika mchakato wa kubadili mawazo kuwa fursa ya kibiashara watu hufanya uchunguzi au utafiti ili kuona uwezekano wa mawazo yao kuwa bidhaa ya kuwaingizia kipato.

Vilevile, katika mchakato wa utafiti ni wazi kuwa utahitaji kupata mawazo ya watu wengine. Na wakati mwingine kabla hata hujaomba ushauri au maoni ya wengine, tayari wapo ambao wameshafika kutoa maoni yao, mengine chanya na mengine hasi.

Watu wengi huguswa au hujali maoni yanayotolewa na watu wengine kusifia au kukosoa kile wanachokusudia kufanya. Hili ni jambo zuri, kwani ubora wa kitu au kazi fulani unaweza kuchangiwa pakubwa na mawazo ya wengine.

Katika jitihada za kupambana na maisha utakutana na mawazo pingamizi – jitahidi yasikuondoe katika reli

Hata hivyo, wapo watu ambao mawazo ya wengine huwaondoa kwenye malengo yao na huwakwamisha. Na hapa ndipo linapokuja suala la mtu kuwa focused, yaani kujikita katika kitu ambacho umepanga kukifanya hadi ukifikishe mwisho.

Kiubinadamu tu, watu huathiriwa sana na mawazo au mitazamo ya watu wengine. Hii ni mitazamo ya watu walio karibu nao ambao wengine wana ushawishi mkubwa juu yao. Watu kama wazazi, marafiki, majirani na washirika wa kibiashara huathiri sana maamuzi.

Kwa mfano, kila unachofikiria au kupanga kufanya unakutana na mawazo pingamizi au hasi kutoka kwa marafiki na hata wazazi. Watakwambia, kwa mfano, “aah, mradi wa kuku kipindi hiki..? achana nao, sasa hivi kuku wanashambuliwa na magonjwa kibao, utakata mtaji wako.”

Au kwa mfano, una kipaji cha kuimba na unamshirikisha rafiki yako. Utasikia, “mmh, kuimba? Utaweza rafiki yangu? Sidhani. Kwa jinsi ninavyoifahamu sauti yako siyo rahisi ukampata hata huyo ‘producer’ wa kukurekodi.”

Kwa kauli hizi, kama una roho nyepepi ni lazima utakata tamaa na utaogopa kuchukua hatua ya kuendelea na wazo lako. Watu wanaokwambia haya kwa mtazamo wao wanaona wanakusaidia ili usipoteze muda na rasilimali zako bure, ingawa wapo pia ambao ki-ukweli hawakutakii mema.

Sasa, nikwambie, ukiwa mtu wa kuingiwa na hofu au kusikiliza sana watu wengine wanasema nini juu yako au juu ya kitu unachotaka kufanya, hakika utakuwa mtumwa. Labda kama wewe mwenyewe umeamua – lakini kitendo cha kukubali kuwa mtumwa wa mawazo ya wengine ni ujinga.

Hupaswi kujali sana watu wanasema au kufikiri nini juu yako. Unachotakiwa kufanya hapa ni kujitambua. Jitambue wewe ni nani na una uwezo gani. Jitahidi kujua unataka kwenda wapi na kuwa mtu wa aina gani – na amini  katika uwezo ulionao wa kukufikisha huko.

Kilicho muhimu, hasa kwa mjasiriamali ni kujipima na kujua uwezo ulionao wa kuhimili  ‘ushawishi’ kutoka kwa watu wengine, yaani uwezo wa kukubali kukosolewa, kupingwa na kupokea mawazo hasi.

Kama mjasiriamali unatakiwa kuwa tayari kukabiliana na kila aina ya ushawishi na kujitahidi kuushinda au kupunguza athari zake – kabla haujaathiri maamuzi yako ya msingi. Unapaswa kujua uchukue ushauri kiasi gani kutoka kwa wateja, marafiki, wafanyakazi, ndugu na hata wapita njia.

Wapuuze kabisa watu wanaokwambia kuwa wazo lako ni baya au halifai. Na hawa wako wengi tu. Wanaweza kuwa sahihi, lakini hili ni wazo lako wewe, na huenda umelitafakari kwa muda mrefu na kulifanyia utafiti. Kinachotakiwa ni kulitia wazo lako katika vitendo na kusonga mbele.

Jifunze kusema kimoyomoyo, “sipendi hayo ‘makelele’ yenu – na sitaki yaniondoe katika uamuzi au mipangilio ya miasha yangu.”

Wapo watu  ambao wanachokiweza zaidi katika maisha yao ni kukosoa, kutoa mawazo hasi, kuponda na kukatisha tamaa wenzao. Ingia kwenye mitandao ya kijamii uone jinsi watu wanavyochangia mada au maoni ya wenzao, ndio utajua ninachosema hapa.

Sasa, kama wewe una kipaji chako; una kitu unakiweza na unataka kukifanya kwa ajili yako au jamii yako, tengeneza au fanya kitu hicho na wapatie watu. Huenda sio wote watakipenda sasa, lakini wapo watakaokipenda, na wengine baadaye.

Msanii maarufu wa sanaa za uchoraji, And Warhol, anasema, “tengeneza kazi ya sanaa, halafu, wakati watu wanafikiria kama wataipenda au la – tengeneza kazi nyingine – na nyingine tena.”

Hatua ya kuchukua hapa ni kwamba, kama mjasiriamali unatakiwa kujiamini na kuamini kile unachotaka kufanya. Elewa kuna wakosoaji wengi. Usiwe mwepesi kushawishika na kupelekwa nje ya kile unachoamini na ulichopanga kufanya. Jitahidi kuwa focused!

Soma pia: Jinsi Ya Kukabiliana Na Hisia Ya Kukata Tamaa

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

 

Tukimuiga Huyu – Mafanikio Hayatachelewa

Habari rafiki,

Makala ya leo itazungumzia kitu muhimu sana katika jitihada za kujikwamua katika maisha kupitia ujasiriamali. Kitu hicho ni uthubutu na kuchangamkia fursa.

Utakumbuka, tarehe 9 mwezi Mei mwaka huu (2019) ilikuwa ni siku muhimu katika historia ya nchi yetu, ambapo tulishuhudia mfanyabishara maarufu, Mzee Reginald Mengi, akizikwa kijijini kwao Kisereni, Machame.

Tukitumia vizuri bongo zetu tutapata mahala pa kuanzia kuyafikia  mafanikio

Umuhimu wa siku ile ulitokana na sifa alizokuwa nazo mzee huyu hasa katika kujitoa na kuwasaidia watu wenye shida mbalimbali, na hasa walemavu. Mengi ametuachia urithi katika mambo mengi ikiwa ni pamoja na udadisi, ujasiri na uwezo wa kuthubutu katika jitihada za kujinasua kutoka katika umaskini.

Kutokana na sifa hizi, watu wengi ndani na nje ya Tanzania walivutiwa na mawazo na matendo yake, na hata alipofariki, shughuli ya maziko ilikuwa kubwa, na watu kwa maelfu walihudhuria kutoa heshima zao za mwisho.

Wakati wa mazishi, huko Machame, wapo watu walikwenda huko kwa lengo moja tu la kumuaga mtu waliyempenda, basi! Lakini wapo watu wenye hulka ya ujasiriamali ambao nao walikwenda.

Watu hawa, pamoja na upendo waliokuwa nao, na hamu ya kutoa heshima zao kwake, lakini waliona kitu cha ziada katika msiba huu. Waliona fursa ya biashara; yaani, kama alivyokuwa Reginald Mengi, walipata wazo kuwa hata msiba ni fursa ya biashara.

Mjasiriamali unapaswa kuwa na maono na uwezo wa kufikiri haraka, kutengeneza wazo, kulichuja – ili kuona kama wazo hilo linaweza kuzaa fursa ya kupata pesa. Hili hata Mzee Mengi alilisisitiza sana.

Sasa, katika hili, yupo mjasiriamali mmoja raia wa Uganda, Molakya Godfrey, aliyetengeneza pesa nyingi kupitia msiba huu – pale alipoungana na waombolezaji wengine huko kijijini Kisereni.

Molakya alisikia na kuona taarifa za kifo cha Mzee Mengi kupitia Facebook. Aliona aina ya mapokezi aliyopewa kuanzia uwanja wa ndege, jinsi watu walivyojipanga barabarani na baadaye siku ya kuagwa, jijini Dar-es-salaam, kabla ya kupelekwa kijijini kwao.

Molakya aligundua kuwa Mzee huyu ni kipenzi cha watu wengi ndani na nje ya Tanzania, na hivyo alipata wazo kuwa kuna kitu anaweza kufanya kutengeneza pesa kupitia msiba huu. Wakati wengine waliwaza msiba tu, yeye alienda zaidi ya hapo, aliona kuna fursa pia.

Molakya aliamua kuichangamkia fursa hii bila ajizi. Hivyo alikuna kichwa na kugundua bidhaa ambazo aliamini akizitengeneza zitaendana na shughuli ya msiba na vilevile zitavuta hisia za waombolezaji, na hivyo zitapata soko.

Alitengeneza bidhaa kadha wa kadha, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kubebea funguo (key holders) na beji za kuvaa shingoni zenye ujumbe na michoro ya kuvutia iliyopambwa na picha ya marehemu Mengi. Alitengeneza pia picha mbalimbali za Reginald Mengi akiwa katika matukio fulani, na zingine akiwa na familia yake.

Anasema, “nikiwa Mganda nimeona niichangamkie fursa hii, kupitia kwa mtu anayependwa na Watanzania wengi kujitengenezea kipato kwa ajili ya maisha yangu.”

“Na ninafanya hivi nikiwa nayaenzi maisha yake ambayo yaliongozwa na falsafa ya kuzitafuta, kuziona na kuzichangamkia fursa, kama yeye mwenyewe alivyoamini na kufanya.” Alisema Molakya.

Ki ukweli, wazo lake lilizaa matunda kwani wananchi na wageni waliokuwa wamejipanga katika mistari kutoa salamu zao za mwisho kwa marehemu walizichangamkia sana bidhaa hizo, kwani kila mmoja alitamani kuondoka katika msiba huo akiwa na kumbukumbu muhimu ya tukio hilo.

Katika hili Molakya anatupa somo muhimu sana. Sifa kuu ya mjasiriamali, kama alivyokuwa Mzee Mengi, ni uwezo wa kufumbua macho na masikio – kuona na kusikia, ili kugundua fursa zilizojificha na kuzikamata – na mwisho kuzibadili fursa hizo kuwa kitu halisi chenye thamani.

Tumuige Molakya kwa yale aliyofanya katika msiba huu ambapo pamoja na kushiriki kikamilifu kama muombolezaji, lakini pia alitumia fursa hiyo kujitengenezea kipato kwa ajili ya kuboresha maisha yake.

Hivyo, kama alivyofanikiwa Molakya, kila mtu anaweza kufanikiwa, na hivi ndivyo nguvu ya kuthubutu inavyowea kuleta matokeo bora na mazuri katika maisha yetu.

Soma pia: Ukiwa Na Macho Ya Namna Hii, Utatengeneza Fursa Nyingi za Biashara

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Hivi Ndivyo Shule Zinavyoua Ubunifu Wa Watoto

Habari rafiki,

Hebu chungulia nje ya nyumba yako na wachunguze kwa umakini watoto wadogo, wanapokuwa wakicheza na wenzao au hata wakiwa peke yao. Unaona nini?

Ukweli ni kwamba wanapokuwa wadogo, watoto ni wadadisi sana na wana hamu ya kukifahamu kila kitu kwa kina. Watoto hudadisi mambo mapya na hupenda sana kuuliza maswali.

Kutokana na tabia yao hii, wataalamu wa tabia za watoto wanaweka wazi kwamba watoto, katika umri mdogo, wana uwezo mkubwa wa ubunifu; ingawa wanadai kuwa uwezo huu huendelea kupungua jinsi wanavyokuwa, na wanapofikia umri wa utu uzima, uwezo wao hushuka kufikia kiwango kidogo.

Walimu wana wajibu wa kuwajengea watoto ujasiri na hamasa ya kuthubutu – na kufanya mambo kinyume na mazoea

Sasa, ili tuweze kujua kwa nini uwezo huu hupungua ni vyema tukafuatilia makuzi ya watoto hawa. Je watoto wanalelewa katika utaratibu gani? Je wakiwa shule wanafundishwa nini na kwa njia gani? Je hayo wanayofundishwa yanawasaidia kujenga au kukuza uwezo wao wa kufikiri?

Maswali haya yanatupeleka katika kuudodosa mfumo wetu wa elimu kwa mtazamo wa jumla, hasa nchini Tanzania. Katika mfumo wetu, mwalimu ndiye mjuzi wa mambo. Mwanafunzi kazi yake ni kusikiliza na kufuata maelekezo ya mwalimu.

Nakumbuka kama miaka thelathini iliyopita, katika shule moja ya msingi, kulikuwa na wanafunzi wawili waliokuwa na kipaji cha uchoraji. Walipenda kuchora na walichora picha za kuvutia zilizofanana na picha halisi.

Kitu cha kusikitisha ni kwamba hakuna mwalimu aliyeonesha kuwapa moyo wala kuwaunga mkono ili kuendeleza kipaji chao.

Ukweli waliwakatisha tamaa watoto hawa. Mwalimu mmoja, aliyeungwa mkono na wenzake, alisikika akisema, “yaani nyie kazi yenu ni ‘mapicha’ tu. Kwa kuwa mmekalia kuchora basi mjue mtaishia pabaya! Mnapaswa kusoma kwa bidii masomo mnayofundishwa darasani, mapicha yenu hayatawasaidia kitu.”

Hata hivyo katika miaka ya karibuni masomo ya kibunifu kama ushonaji na uchoraji yanafundishwa katika baadhi ya shule. Pamoja na uamuzi huu bado mfumo au methodolojia ya ufundishaji haiwezeshi kukuza uwezo wa mtoto kufikiri na kubuni.

Utakuta, darasani, katika kipindi cha uchoraji mtoto anafundishwa, kwa mfano, kuchora picha ya umbo la pembetatu. Kisha anaambiwa apake rangi ndani. Sasa, ikitokea mtoto akapitiliza rangi hadi nje ya mstari basi mwalimu atakuja juu, “acha uzembe wewe, nilikwambia upake rangi ndani tu kwa nini umevuka mstari?”

Hivi ni baadhi ya vitu vinavyowapunguzia watoto uwezo. Wanaanza kuwa waoga na tegemezi; na uwezo wao wa kuvitazama vitu kwa jicho tofauti unapondwapondwa.

Katika shule zetu, watoto wanazoeshwa kufanya vitu kama walivyoelekezwa na mwalimu, na wanaaminishwa kuwa huo ndio uwezo, yaani hiyo ndiyo akili. Mtoto mwenye uwezo wa kukariri kila kitu kama mwalimu alivyoandika ubaoni, huyo ana akili!

Mtoto mwenye uwezo wa kukumbuka vitu vichache alivyofundishwa lakini akajaribu kuongeza vitu vingine, kwa mtazamo wake, huyu ni mjinga, yaani hana akili. Na ukweli, huyu anapata alama ndogo na kuishia kufeli.

Darasani, watoto wanafundishwa kukaa kimya na kutulia. Wanahimizwa kusikiliza zaidi kuliko kuongea, hivyo fursa ya kuuliza maswali inakuja kwa nadra.

Mfumo wetu wa elimu huchagua aina ya masomo ambayo kila mtoto anapaswa kuyasoma. Watoto wanatakiwa kusoma masomo yanayofanana na kusisitizwa kuyaweka kichwani na kuyarudiarudia kwa ajili ya mtihani.

Wakishafundishwa, baadaye mwalimu huwapa watoto mtihani ulio na maswali sawa kwa wote ambapo kwa kila swali linaloulizwa kuna jibu moja tu lililochaguliwa na mwalimu kuwa ndilo jibu sahihi. Ukijibu nje ya hapo wewe huna uwezo, ni ‘kilaza’.

Shuleni – mwalimu anapowapa watoto, kwa mfano, ‘assignment’ ya kuandika insha, utakuta amewapatia maelekezo yote ili wao wafuate staili anayoitaka yeye. Mwalimu atawapatia kichwa cha habari, muundo (outline) wa insha, na muhtasari wa maudhui pia, na kuwahimiza watoto kuandika kama alivyoelekeza.

Kwa kufanya hivi, watoto wanajenga utegemezi mkubwa kwa mwalimu, hivyo hawawezi kufikiri na kuandika kwa mtazamo na staili yao. Hili ni jambo ambalo huua ubunifu.

Darasani, watoto wanafundishwa kuwa kukosea ni udhaifu, hivyo wajitahidi kumsikiliza vyema mwalimu na kukariri alichowafundisha, na mtihani ukija wajibu bila kukosea.

Kiuhalisia, kuwakataza watoto kukosea ni kuwanyima fursa ya kujifunza kutokana na makosa.

Na kwa hali hiyo, vipaji vya watoto huanza kufa taratibu, na watoto huanza kutengenezwa kuwa watu wanaofanana kitabia, kiujuzi na kifikra, kitu ambacho huzidi kudidimiza uwezo wao wa ubunifu kila siku.

Kwa kweli, elimu inatakiwa iwezeshe ukuaji wa fikra na vipaji vya watoto. Elimu inapaswa kuwaongezea watoto uthubutu na hamasa ya kujaribu vitu vipya – na hiki ndicho hasa kiini cha ubunifu.

Ninachosisitiza hapa ni kwamba shule zetu pamoja na walimu, wanapaswa kuwa makini katika malezi na makuzi ya mtoto awapo shule. Wanatakiwa  kumjengea mtoto mazingira ya kujifunza ambayo hayataua uwezo wake wa kufikiri na kubuni.

Haya ni mazingira ya kumfanya mtoto awe na ujasiri na hamasa ya kufikiri, na ajenge mazoea ya kujiamini na kuyaamini mawazo yake. Mazingira yakiwa hivi, uwezo wa mtoto kufanya ubunifu utazidi kukua kwa jinsi anavyokua.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Hivi Ndivyo Wazazi Wanavyoua Ubunifu Wa Watoto

Habari rafiki,

Tafiti  za kitaalamu kuhusu ubunifu zinaonesha kwamba watoto, katika umri mdogo, wana uwezo mkubwa wa ubunifu. Hata hivyo, kwa mujibu wa tafiti hizo, jinsi mtoto anavyozidi kukua kuelekea utu uzima, uwezo wake wa ubunifu unapungua siku hadi siku; na anapofikia utu  uzima uwezo huo hushuka kufikia kiwango kidogo kabisa.

Hebu wachunguze watoto; wanapokuwa wadogo ni wadadisi sana kuhusu kila kitu wanachoona – wakiwa na hamu ya kukifahamu kitu hicho kwa kina. Watoto hudadisi mambo mapya na kuuliza maswali mengi.

Kupitia makala hii, niliandika sababu zinazofanya watoto kuwa wabunifu zaidi katika umri mdogo ikiwa ni pamoja na kwamba akiwa mdogo, mtoto anaamini kila kitu kinawezekena na kinaweza kufanyika.

Sasa, tujiulize, kwa nini mtoto anavyozidi kuwa mkubwa uwezo wake wa ubunifu unashuka? Swali hili ni muhimu sana kwa kuwa jibu lake litatusaidia kuingilia kati na kuweka mikakati ya kubadili hali hii, hivyo kufanya ubunifu wa mtoto uendelee kwa kiwango hicho hicho, au zaidi, hadi katika utu uzima wake.

Kwa mujibu wa watafiti zifuatazo ni baadhi ya sababu kubwa za kuua ubunifu wa watoto wetu na kuwafanya wakifikia utu uzima wasiwe na mchango wa maana katika uundwaji wa vitu vipya. Makala hii itajikita katika sababu zinazotokana na tabia za baadhi ya wazazi.

Mzazi usimdhibiti mno mtoto wako, kwa mfano kumkataza mtoto kushiriki michezo unadumaza ujasiri na uwezo wake wa kufikiri

Kwa kuanzia naomba niseme kuwa, ubunifu wa mtoto huanza kuuawa nyumbani, chini ya usimamizi wa wazazi wake. Baadhi ya wazazi huwapokonya kabisa uhuru watoto wao, wakidhani wanawasaidia. Wakiwa na lengo la kuwaepusha na  matatizo, wazazi hawa huwawekea watoto wao udhibiti wa hali ya juu.

Yaani kila anachotaka kufanya mtoto, utasikia mzazi akiingilia kati, kwa mfano, “aah, we Abasi, acha kuchazea hiyo redio utaharibu!” Au kwa mfano, utasikia, “we James, acha kuchezea hivyo vyuma, vitakuumiza!” Au utasikia, “aaah we mtoto, nilikukataza kuchezea udongo, sasa ngoja nikuchape hadi ukome!”

Ukimchunguza mzazi huyu utagundua kuwa anachotaka ni kuona mtoto wake anafanya kila kitu kwa maelekezo na miongozo yake, basi! Hii si sawa. Ukifanya hivi unamnyima mtoto uhuru; na uhuru ukiondoka, akili ya mtoto inakuwa tegemezi na dumavu, na ikiwa hivi uwezo wake wa ubunifu unadumaa.

Huko huko nyumbani, ubunifu wa mtoto huuawa kwa mzazi kumnyima mtoto fursa ya kukutana na kuzikabili changamoto. Utakuta baadhi ya wazazi wanajisikia vibaya wanapoona mtoto wao anakabiliwa na changamoto au shida, kwa hiyo utaona mzazi anampa mtoto kila kitu anachotaka, na akikwama kidogo tu – kufanya kitu kigumu – tayari mzazi keshaingilia kati kumsaidia.

Kisaikolojia changamoto zinahitajika katika makuzi ya mtoto kwani zinamjengea hamasa na uwezo wa kuuhangaisha ubongo wake kufikiri  na hatimaye kuibua ubunifu. Hivyo usimlee mtoto kama yai, bali mpe nafasi kukutana na changamoto ili aweze kutafuta majibu kwa kuufikirisha ubongo wake.

Jingine, baadhi ya wazazi, utakuta wanajisikia furaha wanapowanunulia watoto wao vitu vya kuchezea kama magari, mipira ya kuchezea, midoli n.k. Ni kweli watoto wanapenda kuchezea vifaa hivi, na wanafurahi. Lakini kuna tatizo hapa. Kumpatia mtoto vitu ambavyo viko tayari ni kudumaza akili yake na kuifanya isiweze kuibua kitu kipya.

Ili kumsaidia mtoto, usimletee kitu kilichokamilika bali mletee malighafi ambazo atazitumia kuunda kitu chake mwenyewe. Mchunguze mtoto – je, ana hamu ya kutengeneza kitu gani? Kama ni gari, kwa mfano, mletee maboksi, gundi, mbao, n.k, halafu mwache atengeneze kitu anachotaka yeye mwenyewe. Kwa kufanya hivi unamsaidia mtoto kutumia na kukuza uwezo wake bunifu.

Kitu kingine kinachoua ubunifu ni kumnyima mtoto fursa ya kufikiri tofauti na wewe au tofauti na mazoea, au hata kukupinga. Kumbuka watoto wana uwezo wa kuitazama dunia kwa jicho tofauti. Kwa hiyo ukiona mtoto anafikiri au kutoa maelezo yanayotofautiana na wewe msikilize, kwani huo ndio mtazamo wake.

Kwa kufanya hivi utamjengea ujasiri wa kufikiri nje ya mazoea, na hiki ni kitu kizuri katika kukuza ubunifu. Ukimlazimisha afuate mtazamo wako anaweza – lakini moyoni mwake atakuwa na kinyongo, na hivyo atapoteza ujasiri na hamasa ya kufikiri na kujenga mawazo bunifu.

Kwa hiyo, ninachosisitiza hapa ni kwamba kama wewe ni mzazi, jitahidi uwe makini katika malezi na makuzi ya mtoto wako. Kama nilivyofafanua hapo juu, jifunze kumjengea mtoto mazingira ambayo hayataua uwezo wake wa kufikiri na kubuni vitu.

Ukiweza kumfanya mtoto awe na ujasiri na hamasa ya kufikiri nje ya mazoea utamfanya mtoto ajiamini na kuyaamini mawazo yake, na hivyo uwezo wake wa ubunifu alioanza nao akiwa mdogo utazidi kuongezeka na akifikia umri wa utu uzima atafanya maajabu katika ubunifu.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Ukiwasikiliza Hawa Utajenga Uwezo Mkubwa Wa Ubunifu

Habari rafiki,

Nimeeleza katika makala yangu iliyopita kuwa katika mazingira ya sasa, ya kazi na biashara, ambayo ushindani uko juu, kitu pekee kinachoweza kumsaidia mfanyabiashara binafsi au taasisi, kupambana na ushindani, ni uwekezaji katika ubunifu.

Nikasema kwamba ili ubunifu uweze kufanyika ni lazima kuwepo na fursa ya kuyafanya mawazo bunifu kuingia, na kupokelewa, katika taasisi au biashara husika.

Ukijenga utamaduni wa kuwasikiliza wateja wako utapata taarifa na maarifa mengi

Wapo watu ndani au nje ya taasisi ambao wana uwezo mkubwa wa kuitumia milango yao ya fahamu au fikra bunifu (imaginations) kubaini matatizo au changamoto katika jamii au taasisi. Watu hawa wamejaliwa pia uwezo wa kuja na mawazo au mbinu za kutatua changamoto hizo.

Sasa, mtu anayekuja na wazo lake kwa lengo la kusaidia au kusababisha kuundwa kwa kitu kipya au kuboresha kitu au mchakato fulani, huyu anahitaji kitu kimoja tu – kusikilizwa!

Ili mtu aweze kusikilizwa katika taasisi au sehemu ya biashara ni lazima wahusika, hasa viongozi, katika sehemu hizi wawe na utamaduni wa kusikiliza; yaani wasipende kuongea sana na kutoa maelekezo tu, hapana!

Mtu akiwa na wazo lake zuri, akalileta kwa wenzake ili walipime kuona kama linaweza kuzaa ubunifu – akigundua wenzake wanajali – anapata faraja kubwa, na uwezo wake wa kufikiri kiubunifu unaongezeka.

Kwa muktadha wa ubunifu, kuna makundi matano ya watu wenye mawazo bunifu ambao wakipewa nafasi ya kusikilizwa wana uwezo mkubwa wa kuisaidia taasisi au biashara kukuza ubunifu.

Makundi haya ni kama ifuatavyo:

Moja, wateja wako. Hawa ni wadau wakuu wa biashara yako. Watakwambia ni kitu gani kinahitajika, na kiweje, ili kiweze kuridhisha nafsi zao. Watakwambia hisia na vionjo vyao na kukupa maoni ili uunde bidhaa inayogusa nyoyo zao. Wanachohitaji ni kusikilizwa tu.

Mbili, wafanyakazi wako. Katika biashara nyingi kuna watu wapo kwa ajili ya kumsaidia mmiliki wa biashara katika utendaji wa kila siku. Hawa wanaona na kusikia mengi kuhusu biashara husika.

Wanazijua vizuri changamoto za vitendea kazi, michakato ya utendaji, malighaji, na bidhaa; na hata wateja na tabia zao. Wanajua kipi kinaenda vizuri na kipi kinadorora. Ukiwapa nafasi ya kusikilizwa utapata mengi yatakayosaidia kupata vitu vipya au kuboresha.

Tatu, washirika. Washirika katika biashara ni watu tunaokubaliana nao kuendesha biashara pamoja kwa maelewano fulani. Hawa, hata kama hawahusiki na utendaji wa kila siku, wana nafasi ya kukosoa au kutoa maoni yao. Wakisikilizwa wana mchango mkubwa katika kukuza ubunifu.

Nne, washindani. Kumbuka washindani sio maadui. Fuatilia wanachofanya au wanachosema kuhusu biashara zao au biashara yako. Tega masikio upate taarifa, teknolojia au maarifa yatakayokuwezesha kuja na mikakati ya kuboresha ubunifu wako.

Tano, wapiti njia. Mchakato wa ubunifu unakutaka uwe na uwezo wa kuwasiliana na watu wote katika jamii inayokuzunguka. Usibague umsikilize nani – wasikilize wadau wote, hata wapiti njia, bila kujali hali zao.

Huwezi kujua ni nani atakupatia wazo au neno ambalo ukilifanyia kazi utaibuka na ubunifu utakaokuongezea tija katika biashara yako.

Hivyo, kama utafanikiwa kujenga mfumo imara ndani ya taasisi au biashara yako, wa kuwasikiliza watu waliomo katika makundi haya utashangaa jinsi utakavyopata, kila siku, mawazo mengi bunifu na biashara yako itapiga hatua kubwa.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

 

Ukipenda Kusikiliza Utakuza Fikra Bunifu

Habari rafiki,

Katika mazingira ya sasa, ya kazi na biashara, ambayo ushindani uko juu, kitu pekee kinachoweza kumsaidia mfanyabiashara binafsi au taasisi, kupambana na ushindani, ni uwekezaji katika ubunifu.

Ukifanya uchunguzi utagundua kuwa biashara zenye mafanikio makubwa zina mikakati ya kukuza na kuboresha ubunifu, na kuufanya kuwa sehemu muhimu ya utendaji wao wa kila siku. Hawa wana mifumo ya kuwezesha ubunifu kufanyika.

Hata hivyo, uwepo wa mifumo ni jambo moja, lakini uwezo wa kuitumia mifumo kuchochea ubunifu ni suala jingine. Kitu kinachokosekana kwa wajasiriamali na taasisi nyingi ni msukumo wa kupiga ile kiki ya kwanza ya kuanzisha mchakato wa ubunifu.

Kwa kawaida mchakato wa ubunifu huanzia katika ujenzi wa mazingira, ndani ya taasisi, ya kupatikana kwa mtiririko wa mawazo bunifu. Pasipo mawazo bunifu kuingia, na kupokelewa, katika taasisi au biashara, ni vigumu ubunifu kufanyika.

39127701_507
Sio katika biashara tu, popote, ukipenda kusikiliza utapata mengi, na utakuza ubunifu pia

Kuna vyanzo na njia nyingi za kuingiza mawazo bunifu katika taasisi. Njia inayotumiwa zaidi ni ile ya mazungumzo ya mdomo.

Yaani mtu anakuja na wazo lake na kutaka wenzake wamsikilize kisha wapime kama lina nguvu ya kusababisha kuundwa kitu kipya. Anachokihitaji mtu huyu ni kitu kimoja tu – kusikilizwa!

Sasa, kuna watu, na hata viongozi, katika sehemu za kazi au biashara ambao ‘kipaji’ chao kikubwa ni kuongea na kutoa maelekezo, basi. Hawa kazi yao ni kutoa taratibu, maelekezo, miongozo na kanuni mbalimbali ili watu wengine watekeleze.

Ukiwachunguza hawa utagundua kuwa hawana muda wala uwezo wa kusikiliza, na mara nyingi hudhani kila wanachosema wao kina mantiki, na hupenda kifanyiwe kazi kama kilivyo. Hawaoni kama wapo wengine wenye uwezo kama au kuwazidi wao.

Watu hawa ni kikwazo katika suala la ubunifu. Wasichokijua ni kwamba binaadamu huwezi kujifunza chochote kama kazi yako ni kuongea tu. Wanaojifunza ni wale wenye uwezo wa kusikiliza zaidi na kuongea kidogo.

Mwanafalsafa mmoja anasema Mungu hakuwa mjinga kuumba masikio mawili na mdomo mmoja, akiwa na maana kwamba Mungu mwenyewe alitaka watu wasikilize zaidi kuliko kuongea. Hivyo watu ‘smart’ hupenda kusikiliza zaidi ili waweze kuelewa na kutoa maamuzi yenye tija.

Kwa asili, binaadamu hupenda kusikilizwa na hupenda pia mawazo yake yaheshimiwe na kufanyiwa kazi. Hili humpatia mtu motisha kubwa. Binaadamu hapendi kukosolewa kwa utaratibu utakaomfanya aonekane hana maana.

Wapo watu ninaowafahamu, wengine ni viongozi, ambao kabla hata hujamaliza kusema ulichokusudia, yeye tayari keshadakia na kudai tayari ameshaelewa unachotaka kusema, na tayari anaanza kutoa majibu. Hii si sawa, kwani mara nyingi utakuta walikuwa hawajaelewa.

Tunaposhindwa kuwapa watu fursa ya kusikilizwa tunadumaza mahusiano yetu na wao, na zaidi tunawaondolea hamasa ya kujenga mawazo bunifu vichwani mwao na ujasiri wa kuyaweka hadharani.

Kwa muktadha wa ubunifu, suala la kusikiliza lina umuhimu wa kipekee. Hebu fikiria, hivi usiposikiliza mawazo ya watu wengine utapata wapi uwezo wa kuunda kitu kipya?

Hatua ya kuchukua leo ni kwa kila mjasiriamali na mfanyabiashara kujenga utamaduni wa kusikiliza. Usipende kuongea sana ukadhani unajua kila kitu. Kuna watu wamejaliwa maarifa na busara nyingi ambao hawapendi kuongea.

Hivyo, jifunze kuwafanya watu hawa waongee ili upate maarifa na busara zao na uzitumie katika kuboresha kazi au biashara yako. Ili waongee ni lazima wawe na uhakika kuwa una uwezo na utayari wa kuwasikiliza. Ukiliweza hili utashangazwa na mtiririko wa mawazo bunifu utakayopata kila siku.

Soma pia: Usijihangaishe Sana Na Jina – Fanya Ubunifu!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530