Je, Twaweza Kujifunza Ubunifu Kutoka Kwa Watoto?

Habari rafiki,

Matokeo ya utafiti  wa wataalamu wa ubunifu Beth Jarman na George Land yanaonyesha kwamba hadi kufikia umri wa miaka mitano, asilimia 98 ya watoto wana uwezo mkubwa wa ubunifu. Wanapokuwa watu wazima idadi hiyo hushuka kufikia asilimia 2 tu.

Fikra bunifu, udadisi, focus na uhuru binafsi – huchochea watoto kufanya ubunifu

Wakiongozwa na udadisi na uthubutu, watoto huweza kutengeneza vitu mbalimbali kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira yao. Mtoto atajenga nyumba kwa kutumia miti, mbao au udongo; au atatengeneza vifaa vya jikoni kwa kutumia makopo au vifuu vya nazi; au atatengeneza mpira kwa kutumia makaratasi na vipande vya nguo.

Wakati anafanya ubunifu huu hebu mchunguze mtoto. Utakuta mtoto yuko ‘focused’ – yaani akili na viungo vyake vyote vimezama katika kuhakikisha anapata ufanisi mkubwa wa kile anachotengeneza, na mara nyingi huibuka na kitu fulani kipya.

Sasa, tafiti zinatuambia kuwa asilimia kubwa ya watoto ni wabunifu zaidi ya watu wazima; na ukifuatilia hili utakuta kuna sababu zake. Zifuatazo ni baadhi ya sababu hizo:

Akiwa mdogo, mtoto anaamini kila kitu kinawezekena na kinaweza kufanyika; yaani kila tatizo au changamoto ina utatuzi.

Watoto wengi ni wadadisi na wanatamani kupata majibu kwa kila wakionacho na ndio maana wanakuwa wabunifu. Kinachochochea ubunifu wao ni uwezo wao wa kuuliza maswali, ‘kwa nini’, na  ‘nini kitatokea?’ Kwa mfano, kwa nini nikishika moto naungua? Au, hivi nini kitatokea nikichanganya sukari na chumvi?

Mwanzo maswali haya wanajiuliza wao wenyewe, na wasipopata majibu huwa wanayasogeza kwa watu wazima.

Kwa mfano mtoto mdogo aitwaye Richie Stachowshi alimuuliza baba yake, “hivi baba kwa nini watu hawawezi kuongea na kusikilizana wakiwa ndani ya maji?”

Hili ni swali fikirishi sana, na bahati nzuri baba yake alilipa uzito mkubwa. Utafutaji wa majibu kwa swali hili umewezesha kugunduliwa kwa kifaa cha kuongelea ndani ya maji bila kuhitaji watu au vifaa vya majini kuunganishwa kwa waya.

Watoto hufanya mambo yao kwa uhuru na hawaogopi kujaribu . Watoto wako huru kufanya chochote wanachohitaji na wala hawabanwi na hisia za kuwepo kwa vikwazo.

Ukweli watoto hawafikirii kuwa vitendo vyao vinaweza kuwaudhi au kuwaletea madhara wengine. Kila wanachokifanya wanafanya kwa nia njema kabisa. Akili yao inawaelekeza kuwa wao hawana uadui wala mgogoro na yeyote, hivyo hawana hatia kwa lolote wanalofikiria kufanya.

Watoto wanafanya vitu wakiwa hawabanwi na uwajibikaji kwa mtu yoyote na hivyo hawana hofu kwamba wanaweza kufanya makosa na wakawajibishwa. Vilevile, watoto hawana mawazo ya kufeli, wala hawajali matokeo ya kufeli. Wao kinachoingia katika anga zao wanaanza kukifanya. Kwamba watafaulu au watafeli – hilo kwao sio suala.

Kwa upande mwingine, watoto hawako ‘busy’ na majukumu ya kila siku ya utafutaji wa maisha au uwajibikaji, na kwa sababu hiyo wanapofikiria kufanya kitu wanapata nafasi nzuri ya kutuliza akili na kufanya vitu kwa umakini.

Katika ubunifu watoto wanaongozwa na ‘imaginations’ au fikra bunifu, hivyo wana uwezo wa kuunda picha ndani ya nafsi zao ya kitu wanachokitaka hata kama hawajawahi kukiona au hata kukisikia.

Asili ya watoto ni kujaribu. Na wakijaribu kufanya kitu kipya kwa kutumia njia fulani halafu wakiona hawapati matokeo, hujaribu njia tofauti hadi wapate walichokusudia.

Watoto wanakuwa wabunifu kwa kuwa muda mwingi wanafanya kazi za sanaa kwa vitendo. Watoto wanapenda kuchora, kupaka rangi, kufinyanga, kupika, kulea watoto n.k. Hivyo, kuchezeachezea sana kazi za sanaa huwapatia watoto uwezo mkubwa wa kujenga fikra bunifu.

Kazi za sanaa anazofanya mtoto zinavikomaza  viungo vyake kama ubongo, macho na mikono, na kuvifanya viweze kushirikiana na kutegemeana katika kuumba; na hapo ndipo ubunifu unapojitokeza.

Mtafiti Suzan Engel anasema watoto wa miaka mitatu wanaelewa tofauti kati ya kitu halisi na kitu cha kufikirika au kuigiza. Ukichunguza hili utakubaliana naye.

Utaona, watoto wakiwa katika maigizo au michezo yao, suala la uhalisia sio muhimu sana – cha muhimu kwao ni kufanya kile hisia zao zinawatuma – basi! Kwa mfano, mtoto mmoja kujifanya punda na mwingine kujifanya mwenye punda, na hivyo kumpanda mwenzake mgongoni na kumswaga – hili kwao ni kitu cha msingi kuliko kufikiria uhalisia.

Kutokana na hili mwanasayansi Einstein anasisitiza kuwa kujenga fikra bunifu au ‘imaginations’ ni muhimu zaidi kuliko kuwa na ufahamu unaotokana na elimu au kujifunza. Ni hisia za ndani anazojenga mtu – ambazo hutoa msukumo katika ubunifu.

Hatua ya kuchukua ni kwamba sisi wajasiriamali, kama tunataka kuwa wabunifu ni lazima tuanze kufikiri na kutenda kama watoto. Watoto wana uthubutu na hamasa kubwa ya kutengenezea kazi za sanaa.

Tukitumia mitazamo na mbinu fulani wanazozitumia watoto tunaweza kujenga uwezo mkubwa wa ubunifu utakaotusaidia kuongeza thamani na tija katika kazi au biashara zetu.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Jinsi Hisia Za Wateja Zinavyochochea Ubunifu

Habari rafiki,

Nimeeleza katika moja ya makala zangu kuwa katika sayansi au sanaa ya ubunifu kuna aina mbili za mikakati ya ubunifu. Aina ya kwanza ni ubunifu unaotokana na hisia au fikra za mbunifu mwenyewe. Yaani kutokana na uwepo wa teknolojia fulani  mbunifu anapata wazo la kuunda bidhaa au kitu anachodhani kitakuwa na manufaa kwa mtumiaji.

Wateja wana nafasi kubwa ya kuchochea ubunifu – tusikilize hisia zao

Mkakati wa pili ni ubunifu unaosukumwa na mahitaji au hisia za wateja. Yaani, kutokana na taarifa zinazoonesha kuwa wateja wana mahitaji ya bidhaa fulani, basi mbunifu anaanza kuuhangaisha ubongo wake ili apate teknolojia itakayomuwezesha kutengeneza bidhaa hiyo.

Hata hivyo, mkakati  wa kwanza wa ubunifu umekuwa ukikosolewa kwa maelezo kwamba unapoamua kuingiza bidhaa sokoni, kabla ya kupata au kujua hisia za wateja kwa bidhaa hiyo, unajiweka katika hatari, kwani  unakuwa huna uhakika kwamba bidhaa hiyo inaweza kukubalika na walaji.

Kwa hiyo, mjasiriamali anayetaka kupiga hatua katika zama hizi ni yule atakayewekeza ubunifu katika kuziteka saikolojia, hisia, mitazamo na mitindo ya kimaisha ya wateja wake.

Kwa mfano, ni ukweli kuwa wanawake wengi wanapenda kuonekana nadhifu na wanaovutia machoni pa watu wengine kwa kuvaa nguo nzuri na kujiremba kwa mapambo, vipodozi na vito vya thamani.

Sasa, kwa kuzingatia kuwa suala la urembo limepewa kipaumbele kiasi hiki, wajasiriamali makini wameiona fursa hii na kubaini kuwa ikitumiwa vizuri itawainua kiuchumi. Hivyo, kupitia hili wameongeza uwezo wao wa kufikiri na kufanya ubunifu na pia kuongeza kasi ya kuzalisha bidhaa hizi kuendana na mahitaji ya wateja.

Mjasiriamali Raniyah Rashid, mkazi wa Iringa, anatupa somo katika suala la kukuza ubunifu kwa kuzingatia mahitaji au hisia za wateja. Raniyah anamilki duka la bidhaa za urembo zinazoundwa na yeye mwenyewe.

Mwanzoni hata yeye alianza kutengeneza bidhaa za shanga, vitenge na ngozi kwa kuongozwa na hisia zake tu, na ujuzi alionao. Ingawa aliweza kupata wanunuzi, lakini alijifunza kitu na akaamua kukifanyia kazi.

Aligundua kuwa wateja walikuwa na vionjo fulani ambavyo wangependa viwepo katika bidhaa zake. Wateja wake, hasa watalii, waliulizia bidhaa ambazo alikuwa hana pale, lakini pia walitoa maoni yao juu ya aina na mpangilio wa rangi, michoro na mapambo kwenye bidhaa alizokuwa akitengeneza.

Alipozijua hisia hizi za wateja, Raniyah hakulaza damu, kwani aliona hii ni fursa ya kipekee. Anasema, “niliwasikiliza kwa umakini na kuunda taswira kichwani ya vitu vyote walivyohitaji. Niliporudi nyumbani nilitulia na kuanza kufanya ubunifu wa bidhaa hizo.”

Anasema, “pamoja na kipaji cha ubunifu nilichonacho, kwa kuwa sikufundishwa na mtu, nilichofanya ni kupitapita kwenye maduka yanayouza bidhaa kama zangu kufanya uchunguzi na udadisi wa mitindo, mapambo na nakshi zinazobebwa na bidhaa hizo. Baada ya hapo nilitengeneza bidhaa zangu kwa kuunganisha kipaji changu na maarifa niliyoyapata kwa kujifunza.”

Raniyah anabainisha kuwa japo kwa mara ya kwanza bidhaa inaweza isiwe na ubora au mvuto mkubwa, lakini anaporudia mara ya pili bidhaa yake huwa na ubora na mvuto wa hali ya juu na wateja wake wamekuwa wakizisifia sana, na mauzo yake yamekuwa yakiongezeka.

Kiuhalisia, wateja wanapoulizia bidhaa za aina fulani na kuonesha nia ya kuzinunua, hili peke yake, kwa mtu makini, ni kichocheo cha jitihada za kufikiri, kutafuta taarifa na maarifa, na mwisho kuibua ubunifu wenye tija.

Mwisho Raniyah anasema, “kadri ninavyowasikiliza wateja, maoni yao, malalamiko yao na kadhalika, ndivyo kadri ninayoongeza muda na uwezo wa kufikiri vitu vya kubuni ili kukidhi haja na mahitaji ya wateja wangu. Kwa kufanya hivi nimekuwa nikija na ubunifu wa hali ya juu wa bidhaa zangu, na wateja wanazidi kuridhika na hata kuwaleta rafiki zao.”

Soma pia: Jinsi Vifungashio Vinavyoongeza Thamani Ya Bidhaa Yako

Katika hili napenda kuwahimiza wajasiriamali kufumbua macho na masikio ili kuona na kusikiliza. Sikiliza kwa umakini ili uzijue hisia za wateja wako. Ukijua wanataka nini jipange kuwapatia wanachotaka – na kwa kufanya hivyo utaongeza uwezo wako wa ubunifu na pia idadi ya wateja wako itaongezeka.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu: 0718219530

Tukiwaiga Hawa Tutapiga Hatua Kubwa Kiuchumi

Habari rafiki,

Kuiga kitu au tabia njema ni moja ya sifa nzuri kwa binaadamu. Kuiga kimkakati kunaleta maendeleo. Siyo kwa watu binafsi tu, bali hata taasisi kubwa za kiserikali na kibiashara huwa zinaiga mambo mazuri kwa lengo la kupata manufaa au mafanikio fulani.

Mtu aliyefanikiwa kiuchumi ana uwezo wa kuyamudu vizuri maisha yake kwa sababu ni rahisi zaidi kwake kukabiliana na changamoto za maisha, lakini pia inakuwa rahisi kwake kuzidaka fursa zinazojitokeza.

Watu wengi waliokuja kufanikiwa kiuchumi walianza hivi – wakatia juhudi na nidhamu

Sasa, mafanikio ya kiuchumi hayaji hivi hivi tu, yanajengwa. Ili ufanikiwe kiuchumi huna budi kuwa na tabia fulani ambazo zinachochea mafanikio unayoyataka. Kuna jamii ambazo ukiziangalia kwa umakini utagundua zina mila na tamaduni za kujenga tabia za mafanikio.

Jamii hizi zinatupatia jukwaa la kujifunza au kuiga mila na tamaduni hizi nzuri ili kila atakayeguswa nazo aweze kuzitumia kwa lengo la kujikwamua kiuchumi. Jamii hizi zimefanikiwa kujenga tamaduni au tabia za kijasiriamali zilizojikita ndani ya mila na desturi za makabila yao.

Hizi ni mila zinazowapa mafundisho na miongozo vijana, tangia wakiwa wadogo, kuwa baada ya muda fulani ni lazima waondoke nyumbani – waende ‘duniani’ – wakaanze kutafuta maisha yao; yaani waanze kujitegemea.

Katika Tanzania jamii zinazosemekana kuongoza katika mila na utamaduni huu ni Wachaga na Wakinga. Inasemekana Wachaga ndio wanaongoza nchini katika uchakarikaji unaohusisha shughuli za kibiashara na ujasiriamali.

Hawa utawakuta kila mkoa na hata vijijini ndani wapo wakiendeleza uchakarikaji, wakiwa wanaendesha biashara kuanzia ndogo kabisa hadi makampuni. Utakuta wakiendesha maduka, mabaa, mabucha ya nyama n.k. Utawakuta pia wakifanya shughuli za kiufundi kama ufundi saa, viatu, gereji na hata baiskeli.

Kwa hiyo kijana wa Kichaga akiondoka nyumbani anaondoka akijua kuwa anakwenda kutafuta! Wapo wachache wanaopewa mitaji kidogo na wazazi wao, kwa maana ya pesa. Lakini wengi wanaondoka nyumbani wakiwa hawana pesa.

Vijana hawa wanaondoka nyumbani na kitu kimoja tu – hamu au hamasa ya mafanikio. Hawa, wakifika ugenini wanafumbua macho na masikio ili wasikie na kuona. Kisha wanaufungua ubongo ili uweze kuwasaidia kuchakata taarifa wazipatazo na kuzibadilisha kuwa vitendo.

Wanatumia walichonacho mkononi kuanzisha michakariko. Kama kijana ana kipaji anatumia kipaji chake. Kama ana nguvu za kufanya kazi, anaanza na hizo, na kuzibadilisha kuwa pesa. Kama ana ujuzi fulani basi anautumia ujuzi huo kuzalisha pesa.

Kwa kuwa wamelelewa kuwa na hamu ya kupata mafanikio, kuna vitu ambavyo hawavifanyii masihara. Hivi ni vichocheo muhimu kwa mafanikio katika utafutaji. Vitu hivi ni uthubutu, ujasiri, bidii na nidhamu ya kazi na matumizi ya pesa.

Mafanikio wanayoyapata Wachaga kutokana na kujituma kuna wakati yanahusishwa na ujambazi. Baadhi ya watu wanasema, “aah si bure, hawa watu ni wezi bwana!” Ukweli, hizi ni kauli za wavivu wa kufikiri!

Jamii ya Wakinga nao huwalea watoto wao kuwa na uvumilivu hasa katika kufanya kazi ngumu. Hawa mara nyingi wana uwezo mkubwa wa kilimo. Wanajituma katika kilimo wakiwa na malengo ya kukitumia kilimo kama ngazi ya kupandia ili kupata mtaji wa biashara.

Na wakishaanza biashara Wakinga wana nidhamu na umakini sana katika kuendesha biashara zao. Kutokana na kujituma, bidii, nidhamu ya kazi na ya fedha, Wakinga hupiga hatua haraka sana kiasi ambacho watu huhusisha utajiri wao na masuala ya kishirikina, kitu ambacho sio kweli.

Somo tunalopata hapa ni kwamba kuna haja ya kujifunza kutoka kwa jamii hizi mbili. Kama kuna watu wanafanya mambo kwa utaratibu fulani mzuri na wanapata mafanikio, kwa nini sisi wengine tusiige?

Tunapaswa na sisi wengine tuanze utamaduni wa kuwaandaa watoto wetu ki-saikolojia kuwa wanatakiwa, baada ya muda fulani wajitegemee, kwa hiyo wajiandae kuondoka nyumbani na kwenda mbali kutafuta. Wakiwa na mawazo haya toka wadogo wataanza mapema kuchemsha bongo, na matokeo yake wataweza kuziona fursa mbalimbali mapema na kuzikamata.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Huyu Ndiye Mbunifu Aliyeleta Balaa Kubwa Duniani

  • Habari rafiki,

Kupitia makala zangu nimeandika kuwa ubunifu ni uwezo wa mtu kuanzisha au kuvumbua kitu chochote kipya, chenye utofauti na ubora zaidi, ambacho kina thamani au kinaongeza thamani ya kitu kilichopo, kwa manufaa ya mtu mwenyewe, wateja na ya jamii kwa ujumla.

Wakati mwingi uvumbuzi wa silaha kali kama hizi huleta madhara makubwa kwa jamii

Makala hii itajikita katika kujadili matokeo ya ubunifu au ugunduzi kwa mhusika mwenyewe na kwa jamii inayomzunguka. Naomba kwanza nianze kwa kuongelea vitu viwili muhimu katika kufanikisha ubunifu na ugunduzi. Hivi ni kipaji na elimu.

Kuna watu waliofanya ubunifu na ugunduzi wa hali ya juu kupitia vipaji walivyozaliwa navyo. Yaani wamezaliwa wakiwa na uwezo wa kuyaangalia mazingira yao kwa jicho la kidadisi linalowawezesha kung’amua yaliyojificha na kisha wakabuni kitu kipya.

Wapo waliofanya ubunifu kupita elimu au kujifunza, shuleni au vyuoni. Hawa, hata kama mwanzoni walionekana hawana vipaji, lakini walipopata elimu rasmi, elimu hiyo iliibua uwezo mkubwa wa ubunifu.

Mwandishi mmoja anasema, “elimu ndio mama wa mapinduzi yote ulimwenguni, na mafanikio katika maisha yameegemezwa katika hili.” Tangu zamani wasomi wametoa mchango mkubwa katika utatuzi wa mambo magumu na migogoro iliyozikabili jamii – kwa urahisi kabisa kwa kutumia mantiki au logic.

Kwa hiyo elimu inampatia mtu maarifa na ujuzi ambavyo vikitumika vizuri vinaleta manufaa kwa mtu na jamii nzima. Utaona kuwa ubunifu na ugunduzi mwingi wa vitu kama ndege na mashine  ni matokeo ya maarifa au ujuzi uliotokana na elimu – lakini pia uwepo wa ‘nia njema’.

Hata hivyo kuna wakati maarifa na ujuzi vilivyotokana na elimu havikuwa na nia njema. Vilikuwa na nia ovu. Mwanafalsafa Mgiriki, plato, aliwahi kusema kuwa, “maarifa ya mwanadamu, ili yalete tija kwa jamii, yanapaswa kutumika kwa njia nyoofu yenye kuleta ustawi bora wa maisha ya watu.”

Hivyo, kama maarifa na elimu vikitumika kuzalisha maafa, ukandamizaji au dhuruma kwa jamii, elimu hiyo inakuwa haina maana, yaani ni ujinga. Mwanafalsafa mmoja aliuita huu kuwa ni ‘ujinga ulioboreshwa’. Na hapa ndipo linapoingia suala la Mwanafizikia msomi Robert Oppenheimer.

Msomi huyu, aliyekuwa Profesa wa Fizikia, Chuo Kikuuu cha California, alipata umaarufu kama ‘Baba wa Bomu la Atomic’. Akiwa na wenzake, yeye ndiye alikuwa mkuu wa maabara maalum iliyotengeneza bomu hatari la atomic, katika kipindi cha maandalizi ya vita kuu ya pili ya dunia, mwaka 1945.

Bomu walilovumbua lililodondoshwa na ndege ya kivita ya Marekani katika miji ya Horoshima na Nagasaki, Japan, na kuangamiza watu, vitu, na miundombinu yote iliyokuwepo. Inakadiriwa watu wapatao 200,000 walikufa na wengine wengi kupata vilema vya maisha.

Taaluma, ujuzi na maarifa ya Oppenheimer, badala ya kuleta neema, yalileta maafa na msiba mkubwa kwa wengine. Maarifa yaliyodhaniwa yangeboresha maisha na kuleta furaha kwa watu yaligeuka kuwa balaa.

Kitu cha kujifunza hapa ni kwamba, wewe kama mbunifu, msanii au mjasiriamali unapaswa kujitahidi kufanya ubunifu kila siku ili uboreshe bidhaa na huduma zako. Tumia elimu, maarifa na vipaji vyako kuibua ubunifu na uvumbuzi wenye tija.

Lakini cha muhimu ni kwamba, usije na ubunifu usioleta tija na manufaa kwa jamii kwa kuwa hauna maana – na huu unapaswa kupingwa na kulaaniwa kila sehemu, kama ilivyokuwa kwa Oppenheimer.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

 

Jinsi Ya ‘Kuwaiba’ Wateja Wa Washindani Wako

  • Habari rafiki,

Mara nyingi biashara yoyote utakayofikiria kuifanya utakuta tayari kuna watu wengine wanaifanya. Hawa wanaitwa washindani wako. Hawa utakuta tayari wana wateja wao, na wengine ni wa muda mrefu kabisa.

Kwa hiyo unapoanzisha biashara yako ujue hutakuja na wateja wako. Ni wateja walewale wa washindani wako ndio utahitaji waje kuwa wateja wako.

Ukijua wateja wanavutiwa na vionjo gani – na ukawapatia, hutakuwa na hofu ya ushindani – na utawajengea utiifu kwako

Katika biashara mteja ndiyo pesa. Hii ina maana kwamba usipokuwa na wateja walio tayari kununua bidhaa yako, hutauza chochote na hivyo hutapata mapato.

Unaweza ukawa na bidhaa bora, zenye mvuto na zinazohitajika na wateja lakini kama wateja hawakuja kuzinunua ni bure. Utakaa sokoni au dukani kutwa nzima, na mwisho utarudi nyumbani mikono mitupu.

Kwa hiyo ili uwapate wateja unapaswa kuwa na mikakati maalum ya kuwavuta na kuwabakiza wateja kwako.

Kabla na baada tu ya kuanza biashara unatakiwa kufanya uchunguzi wa soko la bidhaa yako. Pamoja na maeneo mengine, unapaswa kuwajua vizuri washindani wako.

Jiulize je, washindani wapo kiasi gani katika eneo lako, na wana wateja kiasi gani? Je, wateja wao wanaridhika na bidhaa au huduma za washindani wako?  Je, bidhaa zako zikoje na zina utofauti gani na zile za washindani wako? Je una mbinu gani za kuweza kuwavuta wateja hawa kwako?

Fanya utafiti kujua ni vitu gani ambavyo wateja wanapenda au hawapendi kuhusu bidhaa au huduma za washindani wako, na ukipata jibu jiulize kama unaweza kufanya tofauti na wao. Unaweza kupata taarifa hizi kupitia kwa wateja wao.

Kuna taarifa ambazo unaweza pia kuzipata kupitia kwa wateja wako wachache ambao umeweza kuwapata. Waulize kama wanaridhika na bidhaa au huduma zako. Lakini pia waulize, kwa umakini na tahadhari, kuwa kabla ya wewe kuja walikuwa wananunua wapi, huduma ilikuwaje, na kama sasa huduma yako inakidhi haja zao.

Sikiliza kwa umakini hoja, maoni na malalamiko yao na ubaini ni vitu gani wanavyolalamikia. Je, ni bidhaa au huduma gani hawaipati au wanaipata kwa utaratibu wa hovyo? Je, ni kitu gani wangependa kibadilishwe au kisiwepo kabisa?

Ukiweza kuhudhuria mikutano, semina au jumuia zinazohusiana na biashara au bidhaa zako, utasikia mengi. Mengine ni tetesi tu. Kwa mfano unaweza kujua habari za washindani wako au watu waliokuwa wakifanya biashara kama yako. Utasikia na kujua mahusiano yao na wateja yakoje au yalikuwaje.

Baada ya kuwajua vizuri wasindani wako, mazuri na mabaya yao, unapaswa sasa kuweka mikakati yako ya kuwavuta wateja wao na kuwabakiza kwako. Yaani unatengeneza wateja watiifu kwako.

Mbinu ya kwanza muhimu ni kujitangaza. Angalia njia iliyo bora na rahisi kwako kuwafikishia ujumbe wateja ili wajue aina na ubora wa bidhaa na huduma zako. Kisha endelea kuwasikiliza na kuwajali muda wote. Zisome hisia zao na uwe mnyenyekevu na mwenye lugha ya kuvutia, isiyo na maringo wala majivuno.

Jenga ukaribu kati yako na wateja ambao wanarudi kwako mara kwa mara, na ukiweza angalia ni zawadi gani, hata ndogo tu, unayoweza kuwapatia, au hata punguzo la bei.

Waoneshe wateja kuwa wewe ni tofauti na washindani wako. Usiishie tu kusema, kwa mfano, “furaha ya wateja wetu ndiyo fahari yetu.” Nenda katika vitendo ili wateja waone. Usipoonesha vitendo kauli hii haina maana.

Kama washindani wako walizoea kufungua biashara zao saa mbili asubuhi, wewe fungua saa moja. Kama walizoea kufunga saa kumi na mbili, wewe funga saa moja usiku. Kama hawakufungua kabisa jumapili au sikukuu, wewe fungua angalau masaa matatu, na wazoeshe wateja hivyo.

Kwa hiyo, ‘kuwaiba’ wateja kutoka kwa washindani wako na kuwabakisha kwako ni matokeo ya bidhaa na huduma bora unazowapatia, tofauti na washindani wako; na mikakati stahiki. Unapaswa kuboresha kila kitu na kila siku, kwani ukirudi nyuma tu ujue watakukimbia pia.

Soma pia: Jinsi ubunifu unavyoweza kuboresha huduma kwa wateja

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Mahitaji Ya Wateja Na Hamu Ya Kujitofautisha Huzaa Ubunifu

Habari rafiki,

Leo, kwa muktadha wa ubunifu, napenda kumjadili mmoja wa wanamuziki nchini Tanzania, maarufu kama Rayvan. Kwa wapenzi wa muziki hili ni jina kubwa Tanzania, kwa hiyo katika ufuatiliaji wangu wa kazi za ubunifu nimepata kitu kutoka kwake ambacho nimeona nikushirikishe. Hata hivyo naomba uvute subira kidogo.

Msanii Rayvan akiwa na mwenzake Diamond. Ubunifu ni moja ya siri ya mafanikio yao

Katika sayansi au sanaa ya ubunifu kuna aina mbili za mikakati ya ubunifu. Aina ya kwanza ni ubunifu unaotokana na msukumo wa teknolojia iliyogunduliwa. Yaani mbunifu anapata wazo la kuunda bidhaa au kitu anachodhani kitakuwa na manufaa, halafu anatafiti na kupata teknolojia inayomwezesha kuunda bidhaa hiyo.

Kwa kuongozwa na uwezo wa kibunifu alionao, ukisaidiwa na teknolojia iliyopo, mbunifu anatengeneza bidhaa hiyo na kuiingiza sokoni, kwa watu wanaodhaniwa kuwa walaji au wateja. Hapa ubunifu unatokana na matokeo ya tafiti  zinazokuja na mapendekezo ya bidhaa ambazo zinadhaniwa zinaweza kutatua matatizo au changamoto katika jamii.

Kwa mfano, kutokana na matokeo ya tafiti walizofanya, hatimaye mwaka 2012 Samsung waliibuka na teknolojia iliyozaa ubunifu wa  simu ya kupangusa (touch screen technology). Kuna ubishi katika hili, lakini inasemekana kuwa Samsung ndiyo kampuni ya kwanza kuunda simu ya kupangusa, kupitia simu yao ya Samsung Galaxy.

Njia au mkakati huu wa ubunifu unakosolewa kwa maelezo kwamba unapoamua kuingiza bidhaa sokoni, kabla ya kupata au kujua hisia za wateja kwa bidhaa hiyo, unajiweka katika hatari iitwayo pata-potea, kwani  bidhaa hiyo inaweza isikubalike na walaji, na mbunifu akaingia hasara kubwa.

Kwa mfano, mwaka 1997, Honda, baada ya tafiti zao za kiteknolojia, walibuni na kutengeneza  gari lao la kwanza la kutumia umeme (electric vehicle). Ubunifu huu ulilenga kupunguza utegemezi wa matumizi ya mafuta, lakini  majaribio kwa wateja hayakuzaa matunda. Wateja waliiponda teknolojia hiyo kwa kusema gari  hilo lilikuwa zito sana na lenye gharama kubwa.

Mkakati wa pili ni ubunifu unaosukumwa na mahitaji au hisia za wateja. Yaani, kutokana na tafiti zinazoonesha kuwa wateja wana mahitaji ya bidhaa fulani, na ‘wanasumbua’, basi wabunifu wanaanza kukuna vichwa ili wapate teknolojia itakayowawezesha kutengeneza bidhaa hiyo.

Kwa mfano, miaka 20 iliyopita, utafiti wa soko uliofanywa na makampuni ya bidhaa za kielektroniki ulibaini uwepo wa mahitaji ya kamera ambayo ingeweza kupiga picha ambazo zitaonesha picha hapohapo, bila kusubiri kusafisha studio, na kuzifanyia uhariri (editing) picha hizo.

Hivyo mahitaji haya yaliwalazimisha wabunifu kufanya tafiti. Tafiti hizi zilizaa matunda ambapo ulipatika ubunifu wa kamera ya kidigitali, ndogo, nyepesi na rahisi kubeba. Huu ni mkakati wa ubunifu unaopigiwa upatu kwa kuwa unabeba vionjo vya mlaji.

Kwa muktadha huu, naomba sasa nimrudie mwanamuziki Rayvan. Kwa mujibu wa mwandishi mmoja, Rayvan anajipambanua kama msanii anayefanya muziki wake kwa kuvutwa na mahitaji au hisia za mashabiki wake.

Kwa mfano anasema, “najua mashabiki wangu wa muziki wanapenda burudani, na wala sio kelele za kile kinachoitwa muziki. Kwa hiyo, ndio maana kila ninapoandika wimbo kwanza nafikiria kwa kina mashairi ambayo ni rahisi kusikilizwa, na yanayotoa burudani, badala ya kelele.”

Anasema anaogopa sana kuwasikilizisha mashabiki zake kelele badala ya burudani. Akionekana kukosoa mkakati wa ubunifu ‘unaosukumwa na teknolojia’, Rayvan anasema, “si rahisi kufanya kitu unachowaza kukifanya wewe, kisha ukatarajia kipendwe na mtu mwingine ambaye hakuwepo wakati unakitayarisha.

Kwa hiyo, ili ujitofautishe na wengine ni lazima ujue unaowapelekea kazi yako wanataka vionjo au ladha gani, ndipo ufikirie kupata kazi yenye vionjo hivyo, ambavyo wakivisikia watakuelewa na kuburudika.

“Natunga mashairi yanayosikika ambayo shabiki au mpenzi akiyasikia anaguswa kihisia, na inakuwa rahisi kwake kuimba pamoja na mimi, na hapo ndipo nakuwa nimeziteka hisia zake,” anasema.

Kutunga wimbo unaoteka hisia za mashabiki sio ‘kazi ya kitoto’, yaani huna budi kuzijua hisia zao kwanza ili uje na ubunifu utakaofanya wimbo wako ukubalike inavyostahiki.

Hili linahitaji nidhamu ya hali ya juu na uwezo wa kusikilia mawazo ya mashabiki na miongozo ya viongozi. Napenda kupata maoni au mawazo ya viongozi na wadau mbalimbali, na nisipopata najiona nimepungukiwa kitu muhimu.

Hapa Rayvan anatoa somo kubwa kwa wabunifu, wasanii na wajasiriamali kwa ujumla, kwamba kabla ya kuja na bidhaa yoyote ni vizuri kuchunguza mahitaji ya wateja ambao ndio walaji. Ukijua wanataka nini na kwa vipi, utakuja na bidhaa ambayo wataipokea kwa mikono miwili.

Soma pia: Maswali Haya Yatakupatia Msukumo Katika Kufanya Ubunifu

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com

 

Haya Ndiyo Manufaa Ya Kuanza Utekelezaji Haraka!

Habari rafiki,

Kuna methali ya Kiswahili inayosema, “maji ukiyavulia nguo huna budi kuyaoga.” Maana ya methali hii, kwa muktadha wa ujasiriamali, ni kwamba ukishapata wazo, ukalifanyia utafiti na kuona linaibua fursa ya kibiashara, hutakiwi kuanza kujizungushazungusha.

Unachotakiwa ni kuanza utekelezaji mara moja. Nimeandika huko nyuma kuwa baada ya kuridhika kuwa wazo lako lina tija unaweza kuamua kuanza utekelezaji. Lakini, kuamua peke yake hakutoshi. Wapo walioamua – lakini hawakufanya kitu!

Sasa ninachosisitiza hapa ni kule kujenga ujasiri wa kuanza mara moja. Yaani ukishajiridhisha tu, basi anza utekelezaji. Usianze kusubiri hadi kila rasilimali itimie. Kuna baadhi ya vitu unaweza usiwe navyo mwanzoni, lakini ukishaanza utashangaa vinaanza kujitokeza.

Hapa ndipo umuhimu wa kuanza kidogokidogo unapoleta maana. Anza kidogo-kidogo, na kwa kufanya hivyo unajenga hamasa binafsi, ndani yako, ya kufanikiwa. Uthubutu na hamasa unayoijenga ina tabia ya kusababisha milango iliyoonekana migumu, kuanza kufunguka yenyewe.

Ukishajitupa majini utagundua kumbe hauko peke yako – wapo watu wanakuona – pokea mikono yao!

Yaani unapoanza tu utashangaa kuona unaanza kupata marafiki ambao hukutarajia kuwa na uhusiano nao. Wengine ni watu wanaofanya biashara kama yako, wanakuja wenyewe tu; na bila hiyana wanakupa miongozo mbalimbali. Hii inatokea, na ukiwa makini utanufaika.

Ukiwa mnyenyekevu, utaona unaanza kupata taarifa au maarifa kutoka kwa watu waliowahi kufanya biashara hiyo huko nyuma. Watakujulisha wateja wako wapi, tabia zao, na nini ufanye au usifanye, ili kuweza kuliteka soko.

Utaanza kujua kwa undani taratibu za kisheria zinazohusiana na biashara yako na nini ufanye au usifanye ili usiingie kwenye mitafaruku na serikali, taasisi au jamii inayokuzunguka.

Kupitia wateja au majirani zako, unapata fursa ya kuanza kuwajua vizuri washindani wako wa kibiashara, wana uwezo gani na wanatumia mbinu gani kunasa wateja na kupambana na changamoto zinazojitokeza.

Utaanza kuwajua zaidi wagavi (suppliers) wa bidhaa zako, na usishangae kuona wengine wanakuja wenyewe tu kuanzisha uhusiano na kujua mahitaji yako ya bidhaa, ili ukihitaji wakuletee.

Kama unafanya biashara ya kuzalisha bidhaa, unaanza kupata taarifa za mashine, malighafi na vipuri bora, rahisi na vya bei nafuu, kwa ajili ya kuzalisha bidhaa yako.

Utashangaa unapoanza tu hata kama hukujua utapata wapi wafanyakazi wenye sifa, unaanza kupata taarifa za wafanyakazi wanaoweza kukusaidia kuendesha biashara. Inabaki kazi yako tu kuwachunguza na pengine kuchagua.

Unaanza kupata taarifa za kina kuhusu eneo lako la biashara, changamoto zake, na jinsi unavyoweza kuzitatua. Watu usiotarajia wanakuletea taarifa hizi, wanakuachia wewe uamuzi wa nini cha kufanya.

Unaanza kujua kwa usahihi bei za malighafi au bidhaa, na wapi zinapatikana kwa wingi, ubora zaidi na unafuu wa bei.

Mwanzo ni mgumu. Huwezi kuanza biashara kwa kuwa na wateja wengi mara moja. Lakini ukishaanza tu unaanza kujenga mtandao wako. Kwa hiyo, jinsi unavyokua ndivyo mtandao unavyokuwa mkubwa, mradi tu ujuwe mbinu za kuujenga na kuukuza.

Unaanza kujua udhaifu ulionao au walionao wasaidiazi wako. Udhaifu huu utaujua kupitia kwa wateja, washindani na hata wagavi wa bidhaa. Unaanza pia kugundua vihatarishi vya biashara yako na changamoto zilizomo.

Kwa hiyo, unapoanza kufanya biashara kwa vitendo ujue kuna watu wanakufuatilia hata kama wewe mwenyewe huna habari. Wapo wenye nia nzuri na nia mbaya. Umakini unatakiwa katika hili. Ukiwa mjanja utapata watu watakaokusaidia, kwa mfano vyanzo vya mtaji n.k.

Mwisho, mjasiriamali hapa unahimizwa kujenga uthubutu. Yaani ukishapata wazo, ukaridhika kuwa ni wazo zuri, hiyo ni fursa tayari! Hivyo kinachofuata ni kuanza haraka. Ukishaanza tu utashangaa kuona mambo yanajitokeza bila hata kutarajia, ambayo yanaipalilia njia yako kuelekea mafanikio. Tumia akili yako vizuri kuchuja kila kitu na kufanya kilicho sahihi.

Soma pia: Ukishaiona Fursa, Acha Kusitasita – Anza Mara Moja!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com

Je, Twaweza Kujifunza Ubunifu Kupitia Wasanii Wa Filamu?

Habari rafiki,

Karibu tena katika makala nyingine inayolenga kukupatia maarifa ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Nianze makala hii kwa kusema kwamba ubunifu ni matokeo ya kuufikirisha ubongo ili kupata kitu kipya,  njia mpya na nzuri zaidi ya kuleta mabadiliko, au kutatua changamoto au tatizo linaloikabili biashara, kazi au jamii.

Ubunifu ni silaha kubwa kwa wasanii wa filamu – kama wanataka kukonga zaidi nyoyo za wapenzi wao

Leo naomba niwaongelee, kwa muktadha wa ubunifu, wasanii maarufu wa Tanzania – ambao wanafanya sanaa za maigizo au filamu. Hawa ni Jacob Steven (JB), Riyama Ally na Single Mtambalike (Richie). Hawa wamejizolea sifa nyingi kwa uigizaji bora wa filamu.

Pamoja na uwezo wa kuigiza, wanasifika pia kwa uwezo wa kuufikirisha ubongo na hatimaye kuja na kazi za sanaa zenye ubunifu mkubwa, zinazokonga nyoyo za wapenzi wa filamu.

Wakitoa maoni yao katika gazeti moja, wanasema kwamba uigizaji wenye ubunifu ni jambo muhimu sana. Wanasema, kuwa na wazo kichwani ni jambo moja, lakini kulitia wazo katika uhalisia, na kwa namna ya kipekee, ndio suala gumu; na ukweli linawashinda wengi – watayarishaji na waigizaji pia.

Akitoa maoni yake, JB anasema kwamba njia moja kuu ya kutia vitu vipya katika tasnia ya uigizaji, ambavyo vitaonesha ubunifu wa wasanii, ni kuwapa nafasi wenye uwezo, utashi, ubunifu na vipaji asilia.

Anadai kwamba kuna tatizo kwa watunzi wa kazi za filamu kupendelea kutaka waigizaji wenye majina tayari kwa sababu za ki-biashara. Lakini ukweli ni kwamba watayarishaji wengi hupenda kupata waigizaji wenye vipaji, uwezo, utashi, ubunifu, na nidhamu – hata kama hawana majina.

Kwa maoni ya Riyama Ally, ubunifu wanaofanya unachochewa na uchungu walionao, kwa kazi za sanaa. Anasema, “inauma sana kuona kazi unayoifanya na kuiheshimu inaelekea mahala ambapo huenda ikapotea. Ukweli, ni uchungu huu ndio unatufanya tujifunze kufikiri ki-ubunifu, ili tupate kazi bora zaidi.”

Kwa mujibu wa mwigizaji Richie, kuna vichecheo viwili vinavyowasaidia kuibuka na mawazo ya kibunifu katika sanaa zao. Kichoceo cha kwanza ni dhamira ya kutowaangusha wapenzi, wadau au washirika wao.

Anasema, “tunajituma na kuongeza ubunifu katika kazi ya uigijazi ili wapenzi wetu wasituchoke. Na sio wapenzi tu, bali hata wamiliki wa visimbuzi (decorders), kwani hakuna mmiliki wa kisimbuzi ambaye atakubali kisimbuzi chake kioneshe pumba.”

Kichocheo kingine, kwa mujibu wa Richie, ni hamu ya kujifunza zaidi. Hapa anasisitiza kuwa wasanii, ili waweze kufanya sanaa zenye ubunifu wanapaswa kupenda kujifunza. Wapende kusoma vitabu vya watunzi mahiri, majarida na kuangalia kazi za wengine kiudadisi.

Richie anashauri wasanii wazitumie simu zao kujifunza na kutafiti kazi za wasanii waliotangulia, ili kujua wanafanya nini kizuri. Hii itawasaidia kupata uelewa mpana na kupata mawazo mapya ya kibunifu. Kusoma vitabu na kuangalia waliotangulia wamefanya nini, inaongeza uwezo wa ubunifu.

Anasema wapo wasanii wa filamu wanaoonekana kukua kila siku, huku wengine wakiporomoka. Wasanii wanaokua ni wale wenye ubunifu, wanaojifunza kila siku, na wanaokuja na vitu vya kipekee na vyenye utofauti. Hawa ni wasanii wenye upeo na akili mpya.

Kupitia makala hii, wewe mjasiriamali, msanii, mchoraji, n.k, unayekusudia kuongeza kipato kupitia katika shughuli unayoifanya, unapaswa kufahamu umuhimu na mbinu za ubunifu, kama walivyotufafanulia wasanii hawa.

Ni kupitia ubunifu ndio utaweza kuongeza ubora na thamani ya bidhaa, sanaa au huduma yoyote unaoitoa. Na ongezeko hilo la thamani ndilo litakalokuhakikishia ongezeko la mapato na mafanikio makubwa katika shughuli yako.

Soma pia: Jinsi Wasanii Wanavyofanya Ubunifu – Somo Kwa Wajasiriamali

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Je, ‘Kubeti’ Ni Ishara ya Vijana Kukosa Ubunifu?

Habari rafiki,

Karibu tena katika makala nyingine inayolenga kukupatia maarifa ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Makala ya leo itaongelea tabia ambayo imezoeleka hivi sasa, hasa kwa vijana, ingawa kuna wazee kadhaa pia wanashiriki. Hii ni tabia ya kusaka pesa kwa njia ya kubahatisha, maarufu kama kubeti.

Kubeti kunapoteza muda na nguvukazi kubwa ikishinda kutwa nzima kwenye vibanda hivi

Hivi sasa, ukikutana na vijana wa Kitanzania watatu au zaidi wakiongea, hasa wapenzi wa soka, si ajabu ukasikia lugha ya, “eeh bwana eeh, jana nimetandika mkeka ukachanika.” Yaani ameweka dau fulani katika kamari ya kubashiri ushindi wa timu fulani lakini ameliwa.

Wapo wanaodai kuwa kubeti ni njia ya kutafuta mtaji wa biashara, kama mchangiaji mmoja wa Jamii Forum alivyoandika kuwa, “kuna jamaa yangu ana kibanda cha chips Morogoro, na aliniambia kuwa mtaji wa kuanzisha biashara hiyo, shilingi laki tatu, ulitokana na kubeti.”

Jinsi siku zinavyokwenda kumekuwa na ongezeko la vijana wanaopenda kushiriki michezo ya kubahatisha, na kuna ongezeko pia la matangazo ya kuhamasisha watu kushiriki bahati nasibu hizi ili kutajirika haraka.

Pamoja na kwamba tabia hii kwa vijana wengi inaweza kuonekana kama fursa ya kujipatia mtaji au utajiri wa haraka, lakini inapaswa kuhojiwa.

Kubeti ni kamari, yaani ni kucheza bahati nasibu, ambayo ina kupata na kukosa. Kwa hiyo vijana wanaojihusisha na zoezi hili wanahangaikia maisha ya bahati nasibu, na ukweli ni wachache wanaofanikiwa.

Sasa tujiulize, je ndio kusema vijana wetu wamefilisika kimawazo kwa kiwango hicho kwamba wamekosa mbinu za ki-bunifu za kuwapatia kipato hadi wapoteze pesa zao, hata kama ni ndogo; na muda wao mwingi kwa kucheza kamari kutwa?

Hii inaonesha kuwa kama Taifa, nchi yetu imeshindwa kuwapatia vijana wetu maarifa ya ujasiriamali na ubunifu, na hivyo wamekosa mbinu za kujipatia ajira kupitia uthubutu, ujasiri na ubunifu – kwa kutumia rasilimali nyingi zinazotuzunguka.

Kwa kukosa maarifa haya, vijana wameamua kutumia muda wao mwingi kubahatisha kupata fedha za harakaharaka kupitia kubeti. Tatizo ni kwamba, kuna ukweli, wanaobahatika kupata ni wachache, lakini wanaoshiriki na kushinda mitandaoni wakibeti ni wengi – na hivyo nguvukazi inayopotea kila siku bila kuleta tija kwa Taifa ni kubwa.

Nguvukazi inayotumika katika mitandao ya kijamii, kubeti, ingetumika katika kilimo, ufugaji au biashara, Taifa na vijana hawa wangepiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Ongezeko la matangazo ya kuhamasisha kubeti yameongeza ushiriki wa vijana

Hasara wanayopata vijana hawa ni pamoja na fedha wanayotoa, au dau, fedha ya kununua bando la internet, na muda wa kucheza. Hasara nyingine mbaya zaidi ni kudumaa kwa ubongo na kushuka kwa uwezo wa kufikiri na kudadisi – ili kuibua mawazo bunifu.

Hatua ya kuchukua kwa serikali na waelimishaji binafsi, kama jukwaa la Mbunifu Blog, ni kuzidi kutoa elimu ya ujasiriamali inayowalenga vijana hawa. Elimu hii itawawezesha kuona, kusikia na hata kunusa vitu vilivyomo ndani ya mazingira yetu, na kufanya udadisi.

Udadisi huu ndio utawawezesha vijana kutengeneza mawazo ya kibunifu ambayo yatazaa fursa za biashara au shughuli yoyote halali ya kuzalisha kipato – badala ya kushinda kwenye vibanda vya kamari kubahatisha.

Kijana, ukiwa na elimu ya ujasiriamali unapata uwezo wa kuitazama dunia au mazingira unayoishi kwa ‘jicho maalumu’ lenye uwezo wa kuviona vyanzo mbalimbali vya fursa. Lakini pia unajenga hamasa na uthubutu wa ‘kuinyakua’ fursa unayoiona na kuibadilisha kuwa kitu halisi kivitendo.

Soma pia: Jinsi Wasanii Wanavyofanya Ubunifu – Somo Kwa Wajasiriamali

Kwa hiyo, kijana unahimizwa kujifunza ujasiriamali na kuacha kufikiria kutajirika kwa njia za mkato kama kubeti. Elimu hii itakupanua akili na kukupatia uwanja mpana na uwezo wa kuziona fursa, na kuzitumia ili kujinasua na umaskini. Hivyo jiunge na Mbunifu Blog upate maarifa haya.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Jinsi Ya Kupunguza Gharama Za Biashara Yako…(2)

Habari rafiki,

Makala iliyopita ilikuwa ni sehemu ya kwanza ya mada hii. Kama utakumbuka, nilizungumzia gharama za uendeshaji wa biashara – na nikasema kuna gharama za aina nyingi ambazo mfanyabiashara unapaswa kuzifahamu ili unapopiga hesabu za biashara yako uweze kujua kwa usahihi mchango wa gharama hizo katika faida au hasara utakayopata.

Chunguza biashara yako uone ni gharama zipi unaweza kuzipunguza – fanya hivyo!

Nikasema tena kuwa baada ya kuzijua gharama za uendeshaji wa biashara yako, kinachofuata ni kupanga mikakati ya kuzidhibiti au kuzipunguza. Hii inatokana na ukweli kwamba mfanyabiashara haupaswi kuidharau pesa yoyote inayoingia au kutoka katika biashara yako. Kwani kila pesa ina maana!

Kwa hiyo, nilihimiza kuwa ni wajibu wako kila baada ya muda fulani kupima gharama zilizotumika na kufanya tathmini kujua kama gharama zako ni sahihi na zenye ulazima, na kama kuna chochote cha kurekebisha, kifanyike ili kupunguza gharama hizi.

Katika makala iliyopita nilikupatia njia nne za kudhibiti au kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara. Sasa makala hii itakupatia njia sita zaidi kama ifuatavyo:

Tano, punguza gharama za matangazo. Utakumbuka kuwa moja ya mikakati ya biashara ni matangazo. Hata hivyo usikurupuke katika hili.

Kama ni lazima utangaze kwa malipo, tafuta chombo cha gharama nafuu zaidi; kwa mfano, kipi ni rahisi zaidi kati ya vipeperushi, gazeti, radio, TV au mitandao ya kijamii? Kama unaweza kujichanganya na watu, au networking, je, unaweza kutumia njia ya mdomo na ikalipa? Chunguza, chukua hatua.

Sita, fanya kazi kwa muda uliopangwa, yaani usipoteze muda bila sababu. Muda uliopotea hovyo ni gharama iliyojificha, au ni pesa iliyopotea. Panga muda wa kuanza kazi, kupumzika na kumaliza, kwa kila mmoja. Punguza vitu vinavyoiba muda wa kazi, mfano kupiga soga au stori.

Saba, punguza wigo wa utoaji huduma. Wakati fulani mfanyabiashara anakuwa ameatamia vitu au tenda nyingi peke yake hadi zinamwelemea. Ikitokea hivi matokeo yake ni kutoa huduma duni, zisizo za haraka na wakati fulani gharama zake zinakuwa kubwa. Inashuriwa kugawa kazi au tenda hizi kwa wenzio ili kupunguza gharama za uendeshaji.

Nane, boresha matumizi ya nafasi ofisini, katika karakana au kiwandani. Kama umepanga ofisi, tumia nafasi kwa umakini, na kama inawezekana rudisha nafasi isiyotumika kwa mwenyewe. Tunza vifaa, mafaili, fenicha na bidhaa kwa umakini ili nafasi itumike kwa kiwango cha juu. Tumia nafasi au chumba kimoja kwa matumizi zaidi ya moja.

Tisa, ajiri wafanyakazi kulingana na mahitaji halisi na kwa kuzingatia mchango wa kila mmoja ukilinganisha na gharama zao. Usiajiri mfanyakazi mwenye elimu au ujuzi mkubwa bila sababu kwani unaweza kulazimika kumlipa zaidi.

Ajiri mtu mmoja mwenye ujuzi na uwezo wa kufanya kazi mbili au tatu (multi-tasking). Mfano dereva mwenye ujuzi wa ufundi wa mashine au magari n.k. Wasaidie wafanyakazi kuwa na afya bora, kwani afya duni ni hasara kiutendaji.

Kumi, punguza gharama kwa kujali vitu vinavyoonekana vidogovidogo. Kumbuka msemo wa ‘bandubandu humaliza gogo’ .

Kwa mfano, jenga tabia ya kutumia taa zinazotumia umeme kidogo, energy servers, lakini pia taa au feni zisiwashwe bila sababu. Ikibidi tumia karatasi pande zote mbili. Tumia usafiri wa umma, badala ya gari la ofisi kwa kila safari. Dhibiti matumizi ya maji yasipotee bure.

Ndugu yangu, hizi ni baadhi tu ya njia za kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara, ziko nyingi; hivyo ichunguze biashara yako uone gharama zinazojitokeza, kisha ziorodheshe na uzifanyie tathmini stahiki.

Hatua ya kuchukua: mjasiriamali unapaswa kuwa makini sana katika kuzijua au kuzibaini gharama za biashara yako na kupanga mikakati ya kuzidhibiti au kuzipunguza kwani zina athari kubwa kwa faida ya biashara yako.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com