Habari rafiki,
Karibu tena katika makala nyingine inayolenga kukupatia maarifa ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Ukiwa mjasiriamali au mfanyabiashara kuna gharama ambazo utakutana nazo, na hakuna biashara yoyote ambayo haihusishi gharama. Kwa hiyo ni muhimu sana kwa mfanyabiashara kuzifahamu gharama zinazohusiana na biashara zao.
Katika biashara kuna aina mbalimbali za gharama. Zipo zinazoonekana wazi; na zipo pia zilizojificha, ambazo ni vigumu kubainika kirahisi.
Mfano wa gharama zilizo wazi ni pamoja na gharama za bidhaa au malighafi, mishahara ya wafanyakazi, mashine na vifaa vya uzalishaji; na gharama za umeme, maji na usafiri. Gharama zilizojificha ni pamoja na riba, tozo (charges) na kamisheni za benki; gharama za miamala ya simu; na gharama ya bidhaa iliyoharibika.
Mfanyabiashara unapaswa kuzijua gharama hizi ili unapopiga hesabu za biashara yako uweze kujua kwa usahihi mchango wa gharama hizo katika faida au hasara utakayopata. Kumbuka faida au hasara katika biashara inapatikana kwa kutoa gharama kutoka kwenye mapato.
Katika biashara, kuna gharama zinazobadilika na zile zisizobadilika- kutegemeana na kiwango cha uzalishaji wa bidhaa au michakato ya uendeshaji wa biashara.
Kwa mfano, kama unazalisha sabuni za mche kiwandani kwako, ukizalisha miche 100 unaweza kuingia gharama ya jumla ya shilingi 20,000 (malighafi, umeme, maji n.k). Lakini ukizalisha miche 1000 gharama inapanda na kuwa shilingi 180,000. Huu ni mfano wa gharama zinazobadilika kutegemeana na ongezeko la uzalishaji.
Gharama zisizobadilika ni zile zinazobakia vilevile kila mwezi bila kujali kiasi cha biashara au uzalishaji uliofanyika. Kwa mfano, kodi ya pango, mishahara ya wafanyakazi, malipo ya bima n.k.
Baada ya kuzijua gharama za uendeshaji wa biashara, sasa tujikite katika kupanga mikakati ya kuzidhibiti au kuzipunguza.
Kumbuka, katika mazingira magumu ya biashara kila pesa ina thamani. Kwa hiyo mfanyabiashara unapaswa kuwa makini sana. Yaani, hata pesa ndogo kabisa iingiayo kama mauzo, au pesa kidogo inayotoka kama gharama; vina maana sana katika tathmini ya mafanikio ya biashara hiyo.
Kwa hiyo, ni wajibu wako kila baada ya muda fulani kupima gharama zilizotumika na kufanya tathmini. Kila mara jiulize je, gharama zangu ni sahihi na zenye ulazima? Je, kuna chochote cha kurekebisha ili kupunguza gharama hizi? Jibu utakalopata lifanyie kazi haraka.
Makala hii itakupatia njia nne kati ya kumi za kudhibiti au kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara; na makala ijayo itakupatia njia sita.
Moja, punguza gharama za manunuzi ya bidhaa. Hapa unashauriwa kutafiti kidogo na kisha kununua katika maduka au wagavi wenye bei nafuu, au wanaotoa punguzo (discount) ukinunua bidhaa nyingi.
Mbili, punguza gharama za usafirishaji wa bidhaa. Unashauriwa hapa kuwatumia wasafirishaji wenye bei nafuu. Tafuta usafiri unaolingana na ukubwa au uzito wa bidhaa zako, au changia usafiri na mwenzio mnaofanyia biashara sehemu moja.
Tatu, punguza gharama za uzalishaji. Hapa unashauriwa kukodi eneo au chumba cha biashara chenye unafuu kinacholingana na aina na ukubwa wa biashara yako. Malighafi ya uzalishaji itumike kwa uangalifu ili yote itumike, isije ikaharibika au kwisha muda wake.
Vilevile, malighafi iliyobaki, au bidhaa, zitunzwe vizuri zisiharibike na kuleta hasara. Unapaswa pia kusimamia vizuri wafanyakazi na rasilimali nyingine ili zitumike kwa kiwango cha juu katika uzalishaji au utoaji huduma.
Nne, punguza matumizi ya fedha. Ushauri hapa ni pamoja na kujiepusha na mikopo isio muhimu. Ukilazimika kukopa, angalia riba ni kiasi gani, na je biashara yako ina uwezo wa kumudu riba hiyo bila kuathiri mzunguko wa fedha?
Kama umeamua kukata bima ya biashara yako, chunguza gharama yake ili upate bima yenye tija lakini yenye unafuu.
Hatua ya kuchukua: mjasiriamali unapaswa kuwa makini sana katika kuzijua au kuzibaini gharama za biashara yako na kupanga mikakati ya kuzidhibiti au kuzipunguza kwani zinaathiri faida ya biashara yako. Makala ijayo tutamalizia njia zilizobaki.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.
Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com








