Mpendwa rafiki,
Karibu tena katika makala nyingine inayolenga kukupatia maarifa ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.
Mara zote tunapoanzisha biashara tunalenga kupata mafanikio; yaani tunatarajia kuwa baada ya kipindi fulani, cha kujituma na kupambana na changamoto nyingi, basi tuanze kuona matunda. Tunapenda tuone biashara zetu zikikua na kutupatia faida ya kutosha kuboresha maisha yetu.
Hata hivyo, katika uendeshaji wa biashara kuna wakati unaweza kugundua kuwa mambo hayaendi vizuri. Unaanza kuona idadi ya wateja inapungua, mauzo yanashuka, na faida pia inaenda chini. Unaanza kupatwa na mshangao na wasiwasi pia. Unaanza kujiuliza kulikoni?
Sasa, usipokuwa makini ni rahisi sana kutafuta majibu ya mkato. Hizi ni sababu rahisi ambazo hazizingatii uhalisia. Wafanyabiashara wengi tu, hasa wa nchi zetu za Kiafrika, wanaoishi vijijini na hata mijini, wanatawaliwa sana na imani za ki-shirikina. Jambo lolote lisilo la kawaida likitokea utasikia, ‘aaah, si bure bwana, lazima kuna mkono wa mtu hapa’!
Kinachofuata ni kuanza kumtafuta huyo mtu; yaani mchawi aliye nyuma ya Jambo hilo. Katika kufanya ufuatiliaji, mfanyabishara analazimika kuingia gharama kubwa ya fedha, muda, na rasilimali nyingine, ambazo kimsingi zinatoka katika biashara yake.
Ukifuatilia kwa u-makini utaona hakuna msaada wowote unaotolewa na waganga wa kienyeji wanaofuatwa ili wamtafute mchawi. Mfanyabishara atapewa madawa ‘kibao’, na masharti ‘lukuki’ ayatekeleze; lakini mwisho wake hakuna lolote linalobadilika.

Jambo kubwa ambalo wajasiriamali na wafanyabishara hawa wanasahau ni kwamba, mchawi mkubwa wa biashara zao ni wao wenyewe; yaani mfanyabiashara, yeye mwenyewe anaamua kujiroga, halafu akiyumba ki-biashara, hakumbuki; na ndipo huamua kukimbilia kwa waganga wa kienyeji ‘kupiga bao’.
Wafanyabiashara wengi wanajiroga kwa kushindwa kujua mambo muhimu, ya kawaida kabisa, ya uendeshaji wa biashara kitaalamu. Biashara ikiendeshwa kwa kufuata misingi yake na kuongezewa bidii na nidhamu, utaona ‘inachanja mbuga’, na wala masuala ya waganga hayatajitokeza.
Ni misingi tu inayotakiwa kufuatwa. Msingi wa kwanza mkubwa ni mjasiriamali kutafuta elimu ya ujasiriamali au biashara. Ukipata elimu hii na ukaizingatia utapata mbinu nyingi za uendeshaji wa biashara yako kitaalamu.
Kuna mambo mengine mengi yanayopatikana kupitia maarifa ya ujasiriamali. Kwa mfano je, biashara yako inahitajika? Je, eneo lako la biashara linaendana na aina ya biashara yako? Je, ulichunguza vizuri mahitaji ya wateja uliowalenga? Je. Ulichunguza vizuri washindani wako? n.k. Kama hukufanya hivi ulianza kujiroga mapema kabisa.
Swali jingine ni je, unatoa bidhaa bora zinazokidhi matakwa au mahitaji ya wateja wako? Je, bidhaa hizo zina ubora gani ukilinganisha na zile za washindani wako? Kama unauza bidhaa hafifu, ki-ujanjaujanja, wateja watagundua, na baada ya muda ‘watasepa’!
Soma pia: Jinsi Ya Kupima Kama Wazo Lako La Biashara Litaleta Tija
Huduma bora kwa wateja ni jambo muhimu sana iwapo unataka kubakiza na kuvutia zaidi wateja wako. Huduma zako zikiwa mbovu, hata kama zina ubora mkubwa, utashangaa kuona wateja wanakupita, na kwenda kwa washindani wako; halafu unalalamika umerogwa!
Kwa mfano, wapo watoa huduma kwa wateja, wakiwamo wamiliki wenyewe, hawana kauli nzuri wala uchangamfu kwa wateja. Wapo ambao hata neno ‘karibu’ tu, au ‘karibu tena’, hawana! Hapa unategemea nini?
Bei ya bidhaa ni moja kati ya mambo muhimu yanayogusa hisia za wateja. Angali bidhaa yako umeinunua au kuizalisha kwa gharama gani – halafu angalia uwezo wa wateja wako – halafu angalia pia bei za washindani wako zikoje, ili ujue bei gani ukiipanga itakupa faida bila kuwafukuza wateja wako. Usipozingatia hili, utasema umerogwa tu!
Fikiria pia, mteja amefika kwenye biashara yako, na umemwambia bei ya bidhaa. Mteja kwa kupungukiwa kidogo anakuomba umpunguzie, angalau kidogo; utasikia, “eeh bwana eeh, hiyo ndio bei, kama huna basi, we hujui gharama za bidhaa zimepanda?” Unachosahau hapa ni kwamba hauko peke yako unaeuza bidhaa hiyo; hivyo mteja ataondoka na hatarudi tena.
Tabia binafsi ya mmiliki wa biashara au mhudumu ni kigezo muhimu cha kuwavuta au kuwafukuza wateja kwenye biashara yake.
Kwa mfano, hivi utajisikiaje unapokutana na mmiliki wa biashara fulani, unamsalimia vizuri tu, lakini yeye anakujibu ki-mkato, tena kwa maringo, akiwa haoneshi hata umuhimu wako? Je, utakuwa na hamu ya kununua kitu kwake?
Lazima ujue kuna vichocheo vya ukuzaji biashara ambavyo havina gharama kabisa; kama kuwajali, kushirikiana na kuwa karibu na mambo au shughuli za kijamii za watu wanaoizunguka biashara yako.
Wasalimie watu kwa heshima, onesha unawajali, omba hata ushauri wao – huwezi kujua nani ana utaalamu gani utakaokufaa. Tabia hii inakujengea imani na ukaribu kwa jamii, na hatimaye inaijenga biashara yako.
Mwisho, nakuhimiza rafiki yangu ufuatilie makala zangu ili ujifunze mengi yahusuyo uendeshaji wa biashara na ujasiriamali kitaalamu – na hii itakuepusha na fikra za ki-shirikina. Ukweli hizi ni imani tu ambazo zimejengeka katika nafsi za baadhi ya wafanyabishara zinazowafanya washindwe kuuona ukweli unaotokana na upungufu wao binafsi.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.
Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com








