Habari ndugu na rafiki,
Karibu tena katika mfululizo wa makala zangu zenye lengo la kuelimishana kuhusu masuala ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.
Nimeandika huko nyuma kwamba ukishapata wazo zuri la biashara kinachofuata ni kulitia wazo hilo katika vitendo. Sasa, mara nyingi katika hatua hii huwa kunatokea changamoto. Yaani katika utekelezaji kunatokea vikwazo au changamoto ambazo wakati fulani zinamtia mjasiriamali hisia za kukata tamaa.
Changamoto inayoongoza kutajwa ni kukosekana kwa ‘mtaji’, na hapa ukifuatilia kwa makini, kinachoongelewa kama mtaji sio kingine, ni pesa au mkopo.

Utasikia: “Nina ndoto yangu, na ninatamani kuanzisha biashara…lakini aah, sina mtaji bwana…na sijui nitaupata wapi!” Hii ni kauli inayotolewa na watu wengi na huenda umeshawahi kumsikia mtu wako wa karibu akisema, au wewe mwenyewe umewahi kulalamikia suala hili.
Ukweli ni kwamba, watu ambao wanataka kweli kuingia kwenye biashara, huwa wanaingia na hawakubali sababu yoyote iwarudishe nyuma. Hii inamaanisha kwamba wale wanaokubali sababu yoyote iwazuie, au wale wanaosema hawajaweza kuanzisha biashara kwa sababu ya kukosa mtaji, kwa maana ya pesa, ujuwe hawa hawajadhamiria ipasavyo kuingia kwenye biashara ila tu wanatafuta sababu rahisi ya kushindwa kuanza.
Kama kweli mtu umedhamiria, na upo tayari kuingia kwenye biashara, hakuna kinachoweza kukuzuia kuingia na kuanza. Kukosekana mtaji, hasa pesa, haijawahi kuwa sababu halisi, kwa sababu wapo watu wengi walioweza kuanzisha na kukuza biashara zao wakiwa hawana pesa kama kianzio.
Mtaji ni neno ambalo watu wengi hawalifahamu vizuri maana yake au wanajichanganya katika matumizi yake, na hasa wanapolihusisha neno hilo na dhana ya pesa. Kwa lugha rahisi, mtaji ni kitu au rasilimali yoyote ambayo mtu anaweza kuitumia ili imwezeshe kuanzisha biashara.
Kitu au rasilimali hii ndio ambayo itamfanya mtu yeyote, kwa kuzingatia hali na mazingira yake, aweze kuanzisha biashara na kuifanya biashara yake ikue. Dhana ya pesa kama mtaji mara nyingi inajitokeza kwa kuwa pesa hutumiwa kama njia ya haraka zaidi pale ambapo mtu anataka kuibadilisha kuwa kitu au rasilimali nyingine kwa njia ya kufanya manunuzi ya bidhaa au huduma.
Kuna ushahidi mwingi tu unaoonesha kwamba mtaji sio pesa tu, yaani mtaji ni zaidi ya pesa. Bosco John ni Mjasiriamali aishiye Dar-es-salaam. Bosco anasema, mtaji sio pesa tu, hivyo ukikosa pesa usije ukaanza kulialia, na kuona huwezi kufanya lolote.” Anasisitiza kwa kusema kwamba, uwe na ajira, usiwe na ajira, binaadamu unapaswa kujitahidi kuiangalia dunia kwa mtazamo tofauti, kwani kila mtu ana uwezo wa kufanya makubwa.
Bosco anatoa mfano akisema, “mimi baada ya kuona sina pesa, wala hakuna ndugu wala rafiki yeyote mwenye uwezo wa kunisaidia mtaji (pesa) wa kuanzishia biashara, nilijiuliza swali moja tu; je, nina nini mimi ambacho ni cha kwangu?”
Anadai kwamba aligundua ana uwezo mzuri wa kuongea kiingereza, kwa kuwa aliwahi kufanya kazi za utunzaji bustani kwenye familia ya wazungu fulani, ambao baadaye walirudi kwao, na yeye kulazimika kurudi kijijini kwa wazazi wake. Pesa kidogo aliyoachiwa na wazungu wale aliwapelekea wazazi wake ili wafanye ukarabati wa nyumba yao iliyokuwa na hali mbaya, na iliyobaki ilitumika kununulia chakula, ikaisha.
Kwa hiyo, anasema kwamba baada ya kumalizana na wazazi alirudi mjini, ambapo katika pitapita yake mjini, akiwaza nini cha kufanya, alipumzika karibu kabisa na kibanda cha wasanii na wabunifu wa uchongaji vinyago. Hapo alishuhudia wazungu, na watalii wengine, waliokuja pale kutaka kununua, na pia kupata maelezo kuhusu vinyago hivyo.
“Niligundua kuwa kati ya wale wabunifu wa vinyago hakuna aliyekuwa na uwezo wa kuwaelewa vizuri wale wazungu. Kwa hiyo niliwaza kwamba hapa naweza kufanya kitu. Walipoondoka wale wageni niliwafuata wale wabunifu, nikaongea nao, na kuwaomba niwasaidie kuongea na wageni mbalimbali wasiojua Kiswahili,” anasema Bosco.
Baada ya kukubaliwa, Bosco anadai kuwa alitumia vizuri sana uwezo wake wa lugha ya Kiingereza, kuongea, kutoa maelezo na kufafanua mambo mengi yahusuyo vinyago. Hili lilisababisha ongezeko kubwa la wateja, na mauzo ya vinyago pia yaliongezeka.
“Kwa kuwa wageni wale waliniamini na kuvutiwa na lugha na ucheshi wangu niliweza kuwashawishi wakanunua vinyago kwa bei ya juu kidogo, zaidi ya bei iliyopangwa na watengenezaji wa vinyago hivyo, kwa hiyo na mimi nikapata ‘dola’ kidogo ambazo wenyeji wangu waliridhia nichukue.” Bosco alidai.
Bosco anasisitiza, “ili ufanikiwe kimaisha usiwe mvivu wa kufikiri kwani uvivu wa kufikiri umewafanya Watanzania wengi kuonekana maskini, ilhali Taifa lina rasilimali nyingi. Tazama, mimi nimetumia uwezo wangu wa lugha na kuweza kutengeneza pesa, ambazo nimezitumia kuanzishia biashara niliyoipenda.”
Anashauri, “ifikie mahala elimu inayotolewa shuleni imjenge mtoto kuwa mdadisi, mgunduzi na mwenye uthubutu, badala ya kuwa tegemezi. Awe amefaulu au amefeli masomo ya shule, awe na pesa au hana, aweze kutumia uwezo wake wa kufikiri na kujiuliza ni kitu gani afanye kiweze kumuondoa kwenye umaskini na utegemezi.”
Ushauri wangu, hasa kwa vijana, jiulize una nini? Je, una kipaji au ujuzi wowote? Kwa mfano, kuimba, kuchora, uwezo wa kuongea, ujuzi wa kuchonga n.k. Hivi vyote mwanzoni siyo pesa, lakini ukiwa makini na mwenye uthubutu unaweza kuvigeuza vitu hivi kuwa biashara ambayo itakupatia kipato. Ukipata pesa unaweza sasa kuitumia kuimarisha kipaji chako au kufanya mradi mwingine wowote.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.
Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu: 0718219530








