Rafiki mpendwa,
Karibu tena katika mfululizo wa makala zangu zenye lengo la kuelimishana kuhusu masuala ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.
Makala ya leo inahusu mbinu za uendeshaji biashara. Kuna wakati nilimsikia mfanyabiashara mmoja akitoa ushauri kwa jamaa yake. Alimwambia: “Mfanyabiashara mzuri ni yule anayefanya biashara nyingi kwa wakati mmoja. Yaani, unatakiwa usitegemee biashara moja peke yake; unatakiwa uwe na vyanzo vingi vya mapato kwa wakati mmoja.”
Aliendelea kwa kusema: “Ukiwa na biashara nyingi, na unazifanya kwa pamoja, zinasaidiana kuingiza pesa, lakini pia zinakufanya usitetereke; kwani moja ikidorora, nyingine inakukomboa. Ukitegemea chanzo kimoja tu, ujuwe ukianguka ndiyo basi tena, umekwisha!”
Mjasiriamali ukiyasikia maneno haya harakaharaka, utaona ni maneno mazito. Ni ushauri uliojaa busara na nia njema kabisa, ukilenga kukuletea manufaa na kukuepusha na hatari katika biashara. Na wapo watu wengi tu wenye mtazamo huu; wasomi wa biashara, na fani nyingine, na wasio wasomi pia. Utasikia wakisema: “Usiweke mayai yote kwenye kapu moja, likianguka yote yanavunjika.”
Labda kuna ukweli katika mtazamo huu – lakini kuna tafiti zinazoonesha kuwa kuna tatizo mahala fulani. Mwandishi mmoja anasema kwamba ni rahisi mtu kuanzisha biashara mpya kila baada ya muda fulani mfupi. Lakini swali la kujiuliza ni je, unapata mafanikio yaliyokusudiwa katika kila biashara? Mafanikio katika biashara ni pamoja na kumpatia mteja bidhaa au huduma bora; kuwapatia wadau mapato stahiki; kuwapatia wafanyakazi ujira bora; na kutengeneza faida ya kutosha.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Apple, Tim Cook aliwahi kusema: “Moja ya kanuni ambazo Steve Jobs alisisitiza katika Kampuni hii ni umuhimu wa kuwa focused, yaani kujikita katika kufanya kile unachoweza kufanya vizuri sana.” Kumbuka, Marehemu Steve Jobs ni mwanzilishi mwenza, na baadaye Mtendaji Mkuu wa Apple.
Kwa mujibu wa Tim Cook, Steve Jobs alisisitiza hili kwa kusema, “Ni rahisi kuongeza biashara zaidi, lakini ni vigumu kubakia focused.” Maana ya kuwa focused, kwa mujibu wa Jobs, ni kusema ‘hapana’ kwa mawazo mia kadhaa yanayozunguka kila mara ndani ya akili yako; hata baada ya kuchagua kwa umakini wazo moja zuri uliloamua kulifanya ki-vitendo.
Tunaambiwa kwamba, Steve Jobs hakujishughulisha na wingi wa vitu anavyofanya, kwa mfano, umezalisha au umeuza vipande vingapi vya bidhaa, hapana! Yeye alijishughulisha zaidi na kufanya ‘kitu fulani kilicho bora’, hata kama ni kimoja tu.
Wafanyabiashara wengi wakubwa wamejikita katika jambo moja, wakijitahidi kulifanya jambo hilo kwa ubora zaidi kila siku. Angalia wafanyabiashara hawa wakubwa: Henry Ford alijikita kutengeneza magari; Pablo Picasso alijikita katika sanaa ya uchoraji na rangi; Bill Gates alijikita kwenye uzalishaji wa software; na Mark Zucherberg amejizatiti katika Facebook.
Kitu cha kuzingatia hapa ni kwamba, hawa wamefanikiwa kwa viwango hivyo kwa sababu walikuwa focused. Walikuwa na hamu, motisha na mshawasha wa kupata kwanza hicho kimoja walichokuwa wanakipenda na kukimudu zaidi.
Tunaambiwa kuwa, wafanyabiashara wachache wakubwa unaowaona wanafanya biashara au wana Kampuni zaidi ya moja, mfano Mzee Reginald Mengi, Tanzania, hawakuanzisha biashara zote kwa pamoja. Walianza na moja, wakaipa uhai hadi ikaweza kusimama vizuri peke yake, ndipo ikaanzishwa nyingine.
Mfano mwingine ni Bw.Richard Branson. Tajiri huyu Mwingereza, kwa miaka kumi na tatu, aliifanya Kampuni ya Virgin ijishughulishe na muziki tu, Virgin Records, kabla ya kujitanua baadaye hadi kuanzisha Kampuni za usafirishaji na nyinginezo.
Ushauri unaotolewa hapa ni kwamba kufanya biashara nyingi kwa wakati mmoja inaweza kuonekana ni mbinu au ujanja wa kupunguza vihatarishi au risk ya kile kinachosemwa hapo juu kwamba, ‘Usiweke mayai yote kwenye kapu moja,…….’ Lakini upo ushahidi unaoonesha kuwa wafanyabiashara waliojaribu kufanya biashara nyingi kwa wakati mmoja, ama biashara zote zilidhoofika au zilikufa.
Tatizo kubwa katika hili ni kwamba mfanyabiashara anapoanza kufanya jambo moja na kabla hajaliwezesha kumpatia tija sahihi tayari amerukia jambo jingine – huyu anakosa maono na mwelekeo. Anakosa focus na hivyo anaanza kutangatanga asijuwe lipi alifanye, alifanye saa ngapi, na kwa kiwango gani.
Kikubwa zaidi ni kwamba rasilimali zinazohitajika kufanya haya zinaanza kugawanyika vipande vipande. Rasilimali hizo ni fedha, muda, akili, wafanyakazi, vifaa, majengo n.k.
Utakuta kila biashara mpya inayoanzishwa, kabla ya ile ya kwanza kukomaa, ina tabia ya kutaka kujitwalia rasilimali hizi na kujimilikisha yenyewe, na hivyo kuzinyima pumzi biashara zilizotangulia. Hapa, baada ya muda rasilimali zinakuwa kidogo kutosheleza mahitaji ya kila biashara, na hapo ndipo biashara zote zinakonda na kufa!
Mwandishi mmoja anasisitiza hili kwa kusema: “Angalia vitu kadhaa ambavyo vinamgusa mtu, au watu wanavipa umuhimu mkubwa, mfano mapenzi, kujali, umakini n.k. Jinsi unavyovitawanya vitu hivi kwa watu wengi zaidi ndivyo jinsi unavyofanya thamani yake ipungue.”
Kwa kumalizia, tunashauriwa kuwa focused, tusihangaike huku na kule wala kuondoa macho katika fursa iliyo wazi mbele yetu. Hivyo, jitahidi kuweka mkazo, macho, akili, nguvu na rasilimali zote katika fursa moja yenye uhakika wa kukupatia faida kubwa mpaka uikamate vizuri na kuyaona bayana matokeo yaliyokusudiwa.
Baada ya kufanikisha biashara moja vizuri, basi hapo unaweza kuanzisha nyingine, ukiwa tayari umeshakusanya rasilimali mpya za kutosha kuanzisha na kuendesha biashara mpya kwa tija, bila kuiathiri biashara yako ya mwanzo.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.
Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com









