Habari rafiki.
Karibu tena katika mfululizo wa makala za ujasiriamali zinazolenga kukupatia maarifa yatakayokusaidia kubuni au kuboresha biashara kwa ajili ya kuboresha maisha yako. Nimesema katika makala zilizopita kuwa tafiti zinaonesha kuwa ni adadi ndogo sana ya Watanzania wana elimu hii muhimu na kwamba wakiipata itawasaidia kufungua bongo zao, watapata uthubutu na ujasiri wa kuingia katika tasnia hii.
Leo nitazungumzia mahusiano ya ubongo na uumbaji wa mawazo ya kijasiriamali. Katika hatua za uanzishaji wa biashara, jambo la kwanza kabisa ni kupata wazo la nini unataka kufanya.

Mawazo mbalimbali hutungwa ndani ya ubongo wa mwanadamu yakiwemo mawazo ya kibunifu kama kufungua biashara au kuanzisha stadi fulani, mfano uchoraji au uchongaji wa vinyago. Sayansi ya ubongo siyo rahisi sana, lakini kwa maelezo rahisi, yasiyo ya kisayansi sana, inaweza kueleweka. Vitu vinavyofanyika ndani ya ubongo hupangwa na kuratibiwa vizuri ili baadaye vijioneshe nje kama vitendo halisi.
Ndani ya ubongo kuna kitu kinaitwa akili. Akili, au uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo, kinatokana na michakato mbalimbali ndani ya ubongo. Kwa sehemu kubwa mwili wa binaadamu hujiendesha kwa kutumia akili au ufahamu. Huwezi kuishika akili, kama unavyofanya kwa ubongo. Bali, akili hujionesha kupitia mawazo, maneno na matendo ya binaadamu.
Mwandishi John F. Paul, katika kitabu kiitwacho ‘Weka Ufahamu Wako Huru’, anasema kuna sehemu tatu za akili ya mwanadamu na zina kazi tafauti. Kwa muktadha wa makala hii nitazungumzia na kuchambua sehemu mbili za mwanzo.
Sehemu ya kwanza ya akili inaweza kuitwa akili ya nje, ambayo hufanya kazi wakati mtu yuko macho na ana ufahamu, yaani hajalala. Sehemu hii hufanya kazi ya kufikiri na kupambanua mijadala ya ndani ya ubongo ambayo huwatokea binaadamu kila siku; na pia hufanya kazi ya kutambua vitu vinavyotokea kupitia milango ya fahamu kama kuona, kusikia na kunusa, na kuvipatia majibu; kwa mfano kutambua sura au sauti ya mtu. Sehemu hii huhifadhi vitu kwa muda mfupi sana kabla ya kuvihamishia sehemu ya pili.
Sehemu ya pili ya akili ni ufahamu wa ndani. Hii ina kazi kubwa kwa binaadamu. Ina kazi ya huhifadhi kumbukumbu zote. Mawazo awazayo mtu kwa muda mrefu, na maneno anayosema mara nyingi huhifadhiwa hapa. Sehemu hii pia hupokea na kuhifadhi kumbukumbu kutoka sehemu ya kwanza ya akili, kwa mfano, wakati fulani unaweza kuona au kusikia kitu, taarifa au maarifa fulani, halafu ukayaona ya kawaida tu wakati huo. Kumbukumbu hii huhifadhiwa katika akili ya pili.
Sasa, hutokea siku moja unapata tatizo au unawaza kufanya kitu, unawazaa – lakini hupati jawabu. Mara, umetulia kidogo, unaona kitu kama video kikipita katika akili yako, kinayaleta kama picha yale uliyoyaona au kuyasikia zamani. Yanakuja kama kitu halisi ambacho kimeambatana na maarifa ya utatuzi wa tatizo. Unapata jawabu la tatizo au unapata maarifa ya kibunifu.
Lakini kingine muhimu ni kwamba sehemu hii hupokea pia na kuhifadhi kumbukumbu zote zinazotoka katika ulimwengu wa roho na hufanya zieleweke bayana. Kumbukumbu hizi zinaweza kuitwa maono au ufunuo.
Hizi huingia katika akili zikitokea katika ulimwengu wa roho na huhifadhiwa hapa; yaani mtu umekaa mahala, na hasa ukiwa peke yako, au unatembea au umejilaza tu; na wakati mwingine umelala usingizi, na ghafla wazo kubwa linakujia kama ndoto fulani hivi; wazo la maana ambalo hujawahi kulifikiria, kulisoma au hata kulisikia mahala popote, linakuja tu na unaona lina maana na unaweza kulitumia kupata manufaa.
Sifa kubwa ya sehemu hii ni uwezo wa kuzitoa nje ya mwili kumbukumbu za mambo au mawazo yaliyohifadhiwa humo ili yawe kitu halisi au yajidhihirishe katika uhalisia au vitendo muda unapowadia.
Kwa hiyo, unapowaza au kutamka kwa muda mrefu kuhusu kitu fulani, akili huamini kuwa hicho ukiwazacho au kukitamkatamka ndicho unachokihitaji na kwa hiyo akili, kupitia nguvu ya uumbaji tuliyopewa na Mungu, itakihifadhi ili kitumike baadaye. Utendaji huu wa akili unashirikiana kwa kiwango kikubwa na mawazo na maneno yetu tunayosema kwa kurudiarudia na kwa msisitizo. Haya huhifadhiwa na akili ya ndani na huwa yanajidhihirisha kwa kutokea baadaye.
Kuna watu wanawaza na kujisemeasemea kuwa wanataka mafanikio makubwa ya kifedha, na wakifanikiwa watafanya mabadiliko makubwa kwao na kwa jamii zao. Haya ni maono. Watu hawa wana nafasi kubwa ya kutimiza ndoto zao. Ndio maana Mwandishi John F. Paul anatuhimiza tusitawaliwe na mawazo hasi; kwa mfano, “aah mimi sifai kwa lolote bwana, wala sidhani kama nitafanikiwa maishani”!
Anasema kuwa akili zetu hazikuumbwa ili kukaa na hasi, kwani unapokuwa mtu wa kuwaza au kusema hasi, kumbukumbu hizo zinahamishiwa sehemu ya pili ya akili na kuhifadhiwa, na baadaye kudhihirika au kutokea kiuhalisia. Anatuhimiza tuwaze au tuseme chanya. Mawazo au maneno chanya ni yale yaliyojaa imani, ujasiri na uhakika. Ni mawazo ya kutokubali kushindwa. Mfano, ukiwaza au kutamka mara kwa mara kuwa, “Niko imara katika nafsi, mwili na roho yangu, na nina uhakika wa kufanikisha jambo nililopanga kulifanya”, kumbukumbu hii huhifadhiwa akilini na mara nyingi hujidhihirisha baadaye.
Kuwaza chanya huzalisha matokeo chanya. Kwa wapenzi wa mpira wa miguu wanamfahamu sana mchezaji maarufu, mshambuliaji, Mohamed Salah, ambaye kwa sasa anachezea timu ya Liverpool, ya Uingereza. Salah alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mwaka wa ligi ya Uingereza (2018). Akizungumza na waandishi wa habari, wakati akikabidhiwa tuzo hiyo, aliulizwa kama aliwahi kuwa na fikra au wazo la kufanya vizuri kiasi hicho wakati akijiunga na timu hiyo.
Akijibu swali hilo Mo Salah alisema, “Ndiyo, jambo hilo kwa muda mrefu limekuwa linazunguka akilini mwangu. Nikiwa club ya Chelsea na baadaye Roma, sikuweza kutimiza ndoto zangu, kwani niliwekwa benchi muda mwingi. Hata hivyo wazo la kufanya vizuri pindi nikipata fursa lilizunguka ndani ya ubongo wangu siku zote. Kwa hiyo nilipopata fursa ya kujiunga Liverpool, na wakaniamini, niliona huo ndio hasa wakati wa kutimiza ndoto zangu, na kweli zilitimia kiuhalisia, na haya ndiyo matunda yenyewe.”
Kwa kumalizia napenda kuweka msisitizo kuwa ili upate wazo bora la kijasiriamali unapaswa kuanza kuwaza chanya. Unapaswa pia kujizoeza kuitumia vizuri milango yako ya fahamu ili uweze kutambua na kupambanua vitu vinavyotokea kupitia milango hii. Lakini pia unatakiwa ujenge imani ya uwepo wa ulimwengu wa roho, na kwa imani hii utashushiwa maono au ufunuo utakaokuonesha kitu cha kufanya na nguvu ya kukidhihirisha kitu hicho kiuhalisia.
Nakukaribisha tena usome makala ijayo katika mfululizo wa makala zangu za ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.
Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com


