
Habari rafiki,
Karibu tena katika mfululizo wa makala zangu zenye lengo la kuelimishana kuhusu masuala ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha. Napenda kuchukua fursa hii kukutakia heri ya mwaka mpya; mwaka wa 2022. Baada ya kukutakia heri hii, napenda kukukumbusha kwamba kuna kitu muhimu unapaswa kufanya, tena haraka, kama hujakifanya bado mwishoni mwa mwaka 2021. Kitu hicho ni kujipangia malengo utakayoyatekeleza mwaka huu, 2022.
Nimewahi kujadili katika moja ya makala zangu kuwa binaadamu wa kawaida huzalisha takriban mawazo 6,000 kila siku. Hii ni kwa mujibu wa tafiti kadhaa zilizowahi kufanyika. Na kwamba kila ukionacho hapa duniani, kilichoundwa, ni matokeo ya uwezo wa binaadamu kufikiri na hatimaye KUTENDA.
Kwa hiyo, kutoka katika mawazo yako mengi yanayopita ndani ya ubongo wako, huenda kuna wazo linatawala zaidi akili yako. Yaani kila ukilizungusha kichwani wazo hilo, na kulifanyia tathmini, unajiridhisha kuwa ni wazo litakalokupatia tija; hivyo kilicho muhimu baada ya hapo ni kuingia katika vitendo. Sasa, ili uweze kutenda kwa ufanisi, jambo mojawapo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa wazo lako ni kupanga malengo.
Malengo yanabebwa na mambo au kauli inayoelezea vitendo ambavyo vikifanyika kwa mpangilio fulani vitawezesha kufikia au kupata matokeo yaliyo katika ndoto au maono ya mtu. Malengo ndiyo mwongozo wa mahala unapotaka kufika. Baada ya kujua unataka kufanya nini, kupitia wazo lako bora ulilolichagua, mfano wazo la kufanya biashara fulani, au kuendesha mradi fulani; unapaswa sasa kulikatakata wazo lako na kuliweka katika malengo, ambayo ukiyatimiza, utakuwa umefanikisha ndoto yako.
Katika uandishi wa malengo, tunatangulia kuandika lengo kuu, halafu chini yake yanafuatia malengo saidizi. Malengo ni kiasi au kiwango cha mafanikio ambayo mjasiriamali anataka kuyapata ndani ya kipindi fulani. Malengo huandikwa katika mtindo wa kauli zinazoashiria matokeo yatakayopatikana kutokana na matendo yaliyopangwa kufanywa.
Wataalamu wa biashara wanasisitiza kuwa malengo, yanapoandikwa, yanapaswa kutimiza vigezo fulani. Yakitimiza vigezo hivyo yanapewa hadhi, kitaalamu, ya kuitwa malengo ‘SMART’. Tunaambiwa ili malengo yawe ‘SMART’ yanatakiwa: yawe na ‘uhalisia’, yaani yaeleze bayana nini hasa kinatakiwa kutimizwa; yaweze ‘kupimika’, yaani uweze kupima kama umetimiza lengo au la, kwa mfano uweze kusema, ‘lengo limekamilika kwa asilimia tisini ya matarajio’.
Vilevile, malengo SMART yanatakiwa pia yawe na ‘muda wa utekelezaji’, yaani uweze kujua kila lengo litakamilika lini; na yawe ‘yanawezekana kufikiwa’, yaani yaliyo ndani ya uwezo wako, na yasiyokatisha tamaa. Ki-ukweli wajasiriamali wengi, hasa wadogo, pengine hata wa kati, hawana uwezo wa kutimiza vigezo vya uandishi wa malengo ‘SMART’. Wanaojaribu kuandika wanaandika kile tu wanachotaka kifanyike, basi, na wanaingia moja kwa moja katika vitendo.
Kwa mfano, mjasiriamali mmoja, rafiki yangu, ambaye ana kipaji cha usanii wa maigizo, alipata wazo la kuanzisha kikundi cha sanaa za maigizo. Kwa kuwa anapenda kuandika, ameandika ndoto yake kuwa ni: “Kumiliki kikundi cha sanaa za maigizo na kukifanya kitoe sanaa zenye ubora wa juu katika ukanda wa Afrika ya Mashariki.”
Ameandika lengo kuu la biashara yake kama ifuatavyo: “Kutengeneza na kusambaza kazi za sanaa zenye ubora wa juu zitakazokidhi mahitaji ya wateja tarajiwa.” Kimsingi hii ndiyo dhima au ‘mission’ ya biashara yake.
Chini ya lengo hili kuu, ameorodhesha malengo madogomadogoambayo yakifanyiwa kazi yatawezesha kutimia au kufanikiwa kwa lengo kuu. Baadhi ya malengo hayo ni:
- Kufanya utafiti ili kukusanya taarifa za mahitaji ya soko la sanaa hii na aina ya maudhui yanayohitajika kwa sasa.
- Kubuni na kuandika miswada mizuri ya kazi hizo za sanaa.
- Kuwa na timu nzuri ya wasanii wenye vipaji na nidhamu ya kazi hii.
- Kuwa na timu ya wataalamu wa kutengeneza kazi mbalimbali zitakazotayarishwa.
- Kufanya tafiti za maeneo yatakayotumika kuchezea kazi hizo.
- Kusimamia utengenezaji wa kazi za sanaa zenye ubora.
- Kupata masoko mazuri ya kuuzia kazi hizi.
- Kufanya kikundi na kazi zake mbalimbali zifahamike kwa wateja
- Kupata mapato makubwa kutokana na kazi za kikundi.
Unaweza kuona kuwa malengo haya yameandikwa ki-kawaida sana, na kwa kweli hayako ‘SMART’. Hivyo anapaswa kuyafanya yawe ‘SMART’. Hata hivyo anastahili pongezi! Angalau anaonesha kujua anachotaka kufanya ili atimize lengo kuu. Hayo ya kitaalamu zaidi anaweza kuelekezwa tu na akaelewa.
Katika malengo, kuna malengo ya muda mrefu na mengine ya muda mfupi, na kila lengo linaloonekana ni kubwa linaweza kuvunjwavunjwa tena kupata malengo madogo ambayo ni rahisi kuyatia katika vitendo. Ni muhimu kuandika orodha ya malengo unayokusudia kupata matokeo yake, kwa sababu, kila lengo lina mpango wa utekelezaji, unaolenga kuonesha nini kitafanyika ili kufanikisha lengo husika na kitafanyika kwa kiwango gani, upi ni muda wa kuanza na kukamilika, mtu au watu gani watakaohusika kutekeleza, pamoja na bajeti ya utekelezaji.
Tunaambiwa na wataalamu kuwa ukishaweka malengo lazima pia uandike, kwa kila lengo, ni kwa namna gani utapima kama lengo lako limefanikiwa au hapana. Lazima uwe na kipimo cha mafanikio kitakachokuonesha hali halisi ya utendaji wako, kwa kujiuliza, je, unatimiza malengo au unakwama, kwa kiasi gani, na sababu zake ni nini hasa? Unaweza kujiuliza pia je, malengo yako labda yamekuwa makubwa sana, au tatizo ni changamoto zimezidi? Au labda ni uwezo wako wa kutenda ndio umekuwa mdogo? Hii inasaidia kujitathmini na kujipanga vizuri zaidi.
Ukishaweka malengo, una wajibu mkubwa wa kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wake, ukiongozwa na mpango wa utekelezaji. Ufuatiliaji ni shughuli inayofanyika mfululizo ikilenga kuona ni kwa kiwango gani yaliyopangwa yanatekelezwa. Lengo la ufuatiliaji ni pamoja na kutathmini endapo yaliyopangwa yanatekelezwa vizuri, kwa kuzingatia muda, bajeti na rasilimali zingine. Ufuatiliaji unaweza kufanywa kila siku, kila wiki, kila mwezi au baada ya miezi kadhaa, na unatusaidia kubaini pengo kati ya yaliyopangwa kufanyika na yaliyotekelezwa, na sababu zake pia.
Napenda kumalizia kwa kusema kwamba malengo ndiyo mwongozo wa mahala unapotaka kufika. Kupanga malengo ni jambo muhimu lisilopaswa kupuuzwa. Baada ya kujua unataka kufanya nini, kupitia wazo ulilolichagua, unapaswa kulipanga wazo lako katika malengo, ambayo ukiyatimiza, utakuwa umefanikisha ndoto yako. Na unapaswa kujitahidi kuyafanya malengo yako yawe SMART. Kwa hiyo kama una wazo tayari uliloingia nalo mwaka 2022, unapaswa sasa kuliwekea mpango ili liweze kutekelezeka kwa ufanisi.
Makala ijayo nitaelezea kuhusu mikakati katika biashara na umuhimu wake katika kufanikisha malengo. Naomba uungane na mimi kujadili pia. Heri ya mwaka mpya!!!!!
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com








