Mambo haya huchangia wastaafu wengi kufilisika mapema

Mpango thabiti wa kustafu una nafasi kubwa ya kukujengea maarifa na tabia stahiki itakayokuepusha na majanga uzeeni

Habari,

Yupo mstaafu mmoja aliwahi kusema jambo fulani ambalo naona likidadavuliwa litasaidia kubadili namna wastaafu wanavyofikiri na wanavyofanya mambo yao, hasa ya kiuchumi, baaada ya kustaafu. Alisema, “nilipostaafu nililipwa pesa nzuri tu, mamilioni kadhaa. Lakini pia nilikuwa nimeshajenga na ninaendesha miradi midogomidogo; lakini cha kushangaza ndani ya mwaka mmoja mamilioni yangu yote yaliyeyuka na sikujua yameenda wapi.”

Aliongeza kwa kusema, “baada ya kugundua sina kitu mfukoni nilianza kutafakari…kwa nini? Nilianza kufanya utafiti mdogo, kuwafuatilia wastaafu wenzangu kadhaa, nikagundua siko peke yangu katika hali hii – na nilishangaa zaidi nilipowaona hata marafiki zangu waliosomea masuala ya fedha, nao ni matatizo tu. Fikiria mtu alikuwa na nafasi nzuri tu kazini halafu unamsikia akiomba hadi hela ya nauli; hili si jambo dogo!”

Naomba leo tujadili jambo hili, kwamba kwa nini watu wanaishiwa – tena muda mfupi sana baada ya kulipwa mafao yao ya kustaafu, pamoja na kwamba wengine tayari walishafungua miradi au biashara zao baada au hata kabla ya kustaafu, kwa lengo kwamba wajiingizie kipato endelevu kitakachochukua nafasi ya mshahara waliokuwa wakilipwa makazini kwao.

Kuna sababu kadhaa ambazo tunaweza kujadili hapa; kwamba huenda ndio sababu zinazofanya hali hii iwatokee wastaafu wengi.  Zipo sababu zilizo nje ya uwezo wa wastaafu, lakini pia zipo sababu ambazo tunaweza kuziita za kujitakia, au uzembe. Naomba tuzijadili hapa:

Moja, matumizi mabaya ya fedha baada ya kustaafu. Katika hili Mtafiti mmoja anasema: “Asilimia 46 ya familia za wastaafu hutumia, kwa mwezi, kiasi kikubwa zaidi cha fedha, kuliko kilichotumika wakati mstaafu akiwa kazini.” Ukiyachunguza matumizi haya utakuta yanachochewa na kitu kiitwacho ‘show-off’ (kujionesha).

Wapo wastaafu ambao huwekeza fedha zao katika anasa au ulimbukeni mwingine wa maisha, kwa ujinga tu au kukosa nidhamu. Nawafahamu wastaafu waliowekeza katika ulevi, ufuska au ununuzi wa vitu vya anasa, kwa lengo la kujitutumua tu, au kuwakoga wabaya wao.

Ipo simulizi ya kweli inayomhusu afisa mmoja mstaafu wa taasisi moja ya serikali. Huyu alijipenda sana, na hakupenda kupitwa na kitu kizuri. Na hili liliweza kwenda alivyotaka kwa kuwa nafasi yake ilimwezesha, kupitia marupurupu aliyokuwa akipata, kwa hiyo alizoea maisha ya kuonekana mtu wa ‘matawi ya juu’. Alipostaafu aliendeleza mtindo ule ule wa maisha; na sasa alifanya hivyo kwa kukopa bila mpangilio. Alilipwa mafao miezi 11 baadaye na baada ya kulipa madeni yake yote alibakiwa na shilingi milioni tano tu benki. Kiasi hiki cha pesa hakikumtosha mstaafu huyu, si kwa matumizi yake tu, bali hata kuendeshea miradi, hivyo aliishia kufilisika.

Mbili, kutaka kubakiza hadhi aliyokuwa nayo kazini. Hili linafanana kidogo na hilo la kwanza hapo juu. Wakati hilo la kwanza linawalenga mahasimu; hili la pili linafanywa na mstaafu kuwaonesha waliobaki kazini kuwa kustaafu hakujabadilisha hadhi yake, na hivyo bado anaweza kuishi kwa staili yake ile ile ya zamani, bila kugundua kuwa kinachotoka kwa sasa ni kikubwa kuliko kinachoingia; kupitia miradi au kutoka katika akiba ya pensheni ya mkupuo au ya kila mwezi. Ndio maana utakuta mstaafu ghafla kipato kinakata, halafu anaanza kushangaa.

Tatu, kubeba majukumu yaliyopaswa kuwa yamekamilika. Watu wengi huanzisha familia wakishapata ajira. Baada ya muda kidogo majukumu yanayohusu watoto huanza. Moja ya jukumu linalowatesa wafanyakazi wengi ni gharama za kuwasomesha watoto wao. Na kwa wale wanaopenda, au waliojaliwa kuzaa watoto wengi, hili ni tatizo jingine. Suala la elimu ya watoto ni jambo muhimu sana, ingawa si kazi rahisi, na hasa linapokuja suala la gharama.

Ndio maana suala la uzazi wa mpango huingia. Mpango huu unahusu idadi ya watoto wanaopaswa kuzaliwa, na wazaliwe lini; ili jukumu la kusomesha lifanyike ndani ya kipindi cha ajira. Ukikosea katika hili utajikuta unaingia katika kustaafu na mzigo huu, na fedha hizi zitatokana na mapato ya miradi yako, ambayo pengine bado haijakomaa sawasawa, au zitatokana na pensheni yako. Sasa, hali ikiwa hivi huwezi kuepuka kuishiwa baada ya muda mfupi, na kubaki ukishangaa.

Nne, mafao ya pensheni kuchelewa kulipwa. Kiuhalisia suala hili lina mchango mkubwa kwa wastaafu wengi kuishiwa fedha muda mfupi baada ya kustaafu. Ingawa na wastaafu wenyewe wanastahili lawama fulani hapa. Ni ukweli ulio wazi kuwa wastaafu wengi, wakiwa kazini huwa hawana utamaduni wa kujiwekea akiba yoyote, kwa ajili ya maandalizi ya kustaafu. Wanachokipata kazini, mshahara na malipo mengine, humalizikia huko huko kazini.

Hivyo, wanapostaafu mshahara hukoma hapohapo, na hivyo mapato ya familia huwa yamekatika. Sasa mstaafu huyu ambaye ana familia ikimtegema huwa hana cha kufanya. Kwa kuwa mafao huchelewa, anachofanya ni kujipeleka kwa wakopeshaji ambao hukopesha kwa riba kubwa. Wastaafu huwa hawana jinsi bali kukopa; ingawa huwa wanajifariji kwa fikra kuwa fedha watakazolipwa mafao ni nyingi sana. Lakini wastaafu wengi wamelizwa na wakopeshaji hawa kwa kiwango cha baadhi yao kufilisika!

Anamtaja mstaafu mmoja (tumwite Jeijei) kwamba alishawishiwa kukopa shilingi milioni 6 kutoka kwa mkopeshaji mmoja tapeli. Pensheni ya mzee huyu ililipwa miezi kumi tokea alipokopa kiasi hicho cha fedha. Kawaida ya wakopeshaji hawa humtaka mkopaji awape kadi yake ya benki ya akaunti ya mshahara, ambamo mafao yakilipwa yatapitia.

Kwa hiyo mafao yalipolipwa, mkopeshaji alimpigia hesabu jeijei, iliyofikia shilingi milioni 27! Mafao aliyolipwa Jeijei yalikuwa shilingi milioni 49, hivyo mkopeshaji alimbakizia Jeijei shilingi milioni 22 na presha juu yake! Takukuru ndiyo iliyomnusuru Jeijei. Iliingilia kati baada ya kupata malalamiko kupitia watoto wa Jeijei, akaweza kurudishiwa fedha yake; na ndipo alipoanza tena kupumua kwa faraja!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Haya Ndio Maarifa kuhusu Fedha Unayotakiwa Kumpatia Mwanao -2

Ukiweka ukaribu mapema, kati yako na mwanao, ni rahisi hata kumshirikisha katika masuala ya fedha akiwa bado mdogo ili akikua jambo hili lisiwe tena geni kwake.

Habari,

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii tumejadili stadi au mambo yanayohusu fedha ambayo mzazi unapaswa kujifunza; halafu na wewe umfundishe  mwanao. Kwa kumuelimisha mwanao, utakuwa umemwachia urithi mkubwa katika maisha yake. Mara nyingi stadi hizi huwa hazitolewi shuleni au hata chuoni; hivyo lengo la makala hii ni kuziba pengo hilo. Tumeshajadili stadi mbili, naomba tuendelee…

Tatu, mfundishe mwanao mipango ya fedha. Kuhusu masuala ya fedha, kuna kitu kiitwacho bajeti. Ukitaja dhana ya bajeti unaongelea, kwa lugha nyepesi, jinsi utakavyoingiza mapato yako na jinsi utakavyoyatumia kwa mambo yako mbalimbali. Sasa, wazazi welevu kuwaleta watoto karibu yao, wakati wakitengeneza bajeti zao. Wazazi wasio jielewa hujifungia chumbani; na kuwanyima watoto wao maarifa haya muhimu kwa maisha yao.

Wazazi werevu hukaa pamoja na watoto wao ili wangali wadogo; watoto wajue uhalisia wa mambo ya fedha. Watoto hufundishwa ili wajue mapato ya familia yanaingiaje. Hufundishwa wajue vyanzo mbalimbali vya mapato ya familia na michakato inayohusika katika kuingiza mapato hayo, ikiwa ni pamoja na changamoto zinazohusika; kulingana na umri wa mtoto husika.

Maarifa ya jinsi fedha zinavyopatikana huanza kumjenga mtoto kisaikolojia mapema; na kumjengea, taratibu, uwezo wa kujenga fikra za ki-jasiriamali na ki-ubunifu, ambazo atazihitaji sana hasa anapoelekea kuufikia umri wa kujitegemea; bila kujali ataanza maisha yake kwa kuajiriwa au kujiajiri.

Mtoto akishajua jinsi fedha zinavyopatikana, na michakato yake, inakuwa rahisi sana kumfundisha namna bora ya kufanya matumizi. Kuna matumizi mbalimbali hufanyika majumbani. Yapo matumizi ya lazima, ya kila siku, kama chakula na usafiri. Yapo yanayojitokeza kila mwezi kama bili za maji, umeme n.k. Yapo matumizi ya dharura kama magonjwa na vifo; na yapo pia matumizi ya mara moja moja, kama ununuzi wa nguo, vyombo vya nyumbani, ‘mitoko’ nakadhalika.

Mbali na matumizi hayo, ambayo yanaingia katika matumizi ya kawaida, ili maisha yaendelee; yapo tena matumizi kwa ajili ya mambo ya maendeleo; yaani mambo ambayo yakiwekewa fedha, yataziongeza fedha hizo kuwa nyingi zaidi. Matumizi ya fedha ya aina hii huitwa pia uwekezaji. Kwa maana kwamba, unawekeza kiasi fulani cha fedha ili kuzalisha fedha zaidi. Na hii ndio dhana ya ‘mapato’ kama ilivyoongelewa hapo juu.

Kwa hiyo kazi ya mzazi mwelevu ni kumfanya mwanae apate uhalisia huu ndani ya akili yake; akiwa bado mdogo. Mtoto huyu akiingia katika utu-uzima hatutarajii azubae-zubae mtaani. Huyu akiwa shuleni au chuoni, tunatarajia atakuwa mdadisi; na kwa kila anachofundishwa atakuwa anajaribu kukihusisha na maarifa ya fedha aliyokwishapatiwa nyumbani, hivyo hata akimaliza masomo, anakuwa mwepesi wa kuibadilisha elimu yake kuwa chanzo cha kujiingizia fedha.

Kwa upande wa pili; nimedokeza hapo juu kuhusu wazazi ambao ‘sio werevu’. Wazazi hawa wana usiri mkubwa linapokuja suala la mapato na matumizi ya fedha zao. Hawa ni wazazi wenye mtazamo hasi kuhusu fedha. Wazazi hawa hawapendi kuongelea, hasa kwa watoto wao, jinsi wanavyoingiza fedha zao, na hata wanavyopanga matumizi yao. Suala hili huonekana haliwahusu watoto; ni suala la wazazi peke yao – “watoto watajifunza wenyewe, wakikua”!   

Wazazi hawa, kwa kuwa wao wenyewe wana mtazamo hasi kuhusu fedha, hujikuta wakijiweka katika mazingira magumu ya kupata taarifa na maarifa kuhusu njia za kujiingizia mapato. Na hata wakiingiza mapato huathirika sana katika upande wa matumizi; kwa kuwa suala na kupanga bajeti ya mapato na matumizi huwa halijakaa ipasavyo katika fikra zao.

Na madhara ya tabia na mtazamo huu kuhusu fedha ni kwamba watoto nao hurithi tabia na mtazamo huu. ‘Ulemavu’ huu wa ki-akili na ki-fikra hujijenga vilivyo ndani za vichwa vya watoto hawa; na huendelea kuogelea humo hadi wanapofikia utu-uzima wao. Na hali hii kuwaathiri sana kiuchumi na kimaisha; wao pamoja na familia zao. Kibaya zaidi na wao huwarithisha watoto wao, na mnyororo huu huendelea bila ukomo!

Kwa hiyo, mzazi unahimizwa hapa – kujitathmini wewe na staili yako ya maisha kuhusu mbinu zako za uingizaji mapato; na namna unavyofanya matumizi ya fedha zako. Baada ya hapo una jukumu kubwa la kumuandaa mwanao kwa kumpatia maarifa sahihi kuhusu elimu hii – ili mtoto akifikia umri stahiki awe na mtazamo chanya kuhusu suala hili nyeti na aweze kulitia katika matendo ipasavyo, kwa manufaa yake, ya familia yake, na ya jamii nzima. Itaendelea makala ijayo….

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Haya Ndio Maarifa kuhusu Fedha Unayotakiwa Kumpatia Mwanao – 1

Pamoja na elimu ya kawaida ya darasani kuna umuhimu mkubwa mtoto apewe elimu ya msingi ya fedha toka akiwa mdogo; mfano uwekaji wa akiba

Habari,

Kuna stadi (skills) kadhaa ambazo mara nyingi huwa hazifundishwi shuleni au hata chuoni; ambazo zina maana sana katika maisha ya kila siku ya mtu. Moja ya stadi hizi ni ‘elimu ya msingi ya fedha’. Angalizo; usichanganye elimu ya usimamizi wa fedha (financial management), na elimu ya msingi ya fedha. Hiyo ya kwanza ndio watu hufundishwa zaidi shuleni. Hiyo ya pili; ‘vijana wenye bahati’ hufundishwa na wazazi wao nyumbani.

Nimesema vijana wenye bahati ndio huipata elimu hii, kwa maana kwamba wanaobahatika kuipata ni wachache, wenye wazazi waelewa, wanaoamua kwa makusudi kuwajengea watoto wao msingi imara kuhusu mbinu za kuingiza na kutoa fedha, ikiwa na lengo la kuwasaidia kuchochea maendeleo yao kiuchumu tokea wakiwa wadogo.

Lengo la makala hii ni kujadili mambo yanayohusu fedha ambayo mzazi akimuelimisha mwanae, atakuwa amemwachia urithi mkubwa katika maisha yake. Watoto wanaoyakosa maarifa haya wana nafasi kubwa ya kudumbukia na kudidimia katika umaskini ukubwani. Hivyo mzazi unatakiwa kuyajua maarifa haya, ili yakusaidie wewe mwenyewe; lakini zaidi umsaidie mwanao kujiweka vizuri.

Kwanza, mfundishe mwanao umuhimu wa fedha. Hii maana yake ni kwamba fedha ni kitu muhimu kwa maisha ya binaadamu, hivyo ni muhimu mwano akawa na maarifa au ufahamu wa jambo hili mapema. Hata hivyo, tafiti zinaonesha kuwa jambo hili hufanywa zaidi na watu waliofanikiwa kifedha (wenye ukwasi), kuliko wale wenye uwezo mdogo kifedha.

Watu wenye ukwasi mkubwa huwafundisha watoto wao umuhimu wa fedha kwa kuwa wanaamini kuwa fedha humpatia mtu uwezo wa kuchagua aina na staili ya maisha anayotaka kuishi. Pamoja na hayo, fedha humpatia mtu uhuru na uwezo wa kuamua na kuchagua aishi wapi, aende kutembelea wapi, anunue nini nakadhalika; lakini pia fedha inasemekana husaidia kumtoa mtu kwenye msongo wa mawazo. kwa hiyo ni muhimu sasa kila mzazi abebe jukumu hili kwa manufaa ya mwanae.

Mbili, mfundishe mwanao tofauti kati ya mali na madeni. Hii ni moja kati ya stadi muhimu ambazo ukimpatia mwanao utampa uwezo mkubwa wa kujijengea uhuru wa kifedha. Tukiongelea ‘mali’ tunamaanisha vile vitu vyenye uwezo wa kuingiza fedha katika akaunti yako; wakati ‘madeni’ ina maana ya vitu vinavyolazimisha fedha kutoka kwenye akaunti yako.

Kwa mfano, ukijenga au kununua nyumba na kuipangisha kwa mtu mwingine, nyumba hii ni mali, kwa sababu itakuingizia fedha kila mwezi kupitia kodi utakayolipwa na mpangaji. Lakini, ukiamua kununua nyumba, kwa ajili ya kuishi tu, hii nyumba inahesabika kama madeni, kwa sababu itakuwa inatoa fedha zako kila mwezi, kupitia ukarabati nakadhalika, wakati haiingizi mapato yoyote. Kwa hiyo watu wenye maarifa huwafundisha watoto wao kuwekeza zaidi katika vitu ambavyo ni mali kuliko vitu ambavyo ni madeni.

Kwa kufanya hivyo watoto waliolelewa kwa mtazamo huu huwekeza kwenye miradi au biashara zinazozalisha na kuwatengenezea mzunguko chanya wa fedha mfululizo; huku wakijiepusha na matumizi katika vitu vinavyotengeneza mzunguko hasi wa fedha, vinavyoitwa ‘madeni’.

Kwa mfano; chukua vijana wawili, wanaopokea mshahara wa shilingi milioni 1 kwa mwezi. Baada ya miezi kadhaa; kijana wa kwanza, baada ya kulipa bili zake mbalimbali anaanza kwa kuingia ‘shopping’. Huko ananunua vitu kama gari la kisasa la kutembelea, TV na friji za bei mbaya, na mavazi ya thamani. Kisha ananunua nyumba nzuri eneo lililochangamka. Halafu mara kwa mara anapenda kupata chakula katika migahawa ghali. Kwa staili hii ya maisha kijana huyu habakiwi na fedha zozote kama akiba.

Kijana wa pili; baada ya muda huohuo, naye anakuwa na mamilioni yake kadhaa chini ya umiliki wake. Tofauti na yule wa kwanza, yeye hanunui vitu vya thamani, wala hali chakula au vinywaji katika migahawa ghali. Anapanga nyumba nzuri lakini ya kawaida, maeneo yenye bei nafuu. Havai kwa kufuata mkumbo, na akitaka kuvaa huchagua brand zenye bei ya kawaida, zisizo na gharama kubwa. Kwa kuishi namna hii, kijana huyu anajikuta mwisho wa mwaka ana akiba ya shilingi 4,000,000/-.

Kwa kutumia akiba yake hii; kijana wa pili anaamua kuwekeza fedha hizi katika mradi fulani unaomwingizia shilingi 300,000/- kila mwezi; hivyo kwa mwaka anaingiza shilingi 3,600,000/-. Hizi ni fedha za ziada; juu ya mapato yake ya mshahara ya kila mwezi. Akibakiza staili yake ileile ya matumizi, mwaka unaofuata kijana huyu anaongeza mtaji wa biashara yake kufikia shilingi 7,600,000/- na faida yake kwa mwezi inaongezeka kufikia 600,000/-

Sasa, hebu tuwaangalie vijana hawa baada ya miaka kumi. Ukweli ni kwamba hadhi ya vijana hawa kiuchumi itakuwa tofauti kabisa! Ndio maana Mwandishi Robert Kyosaki ana msemo usemao, “wanaopenda kujionesha ‘wanazo’, hawaendi popote”; akiwa na maana kwamba wapo watu ambao hutumia fedha nyingi ili waonekane katika jamii kuwa ‘wanazo’; wakati ki-uhalisia ni maskini wa kutupwa!    

Fedha hizi wanazozitumia kufanya manunuzi ghali na matumizi ya kujionesha, wangeyatumia kama alivyofanya kijana wa pili, hakika maisha yao yangebadilika; hivyo kuwaweka katika ramani mpya ya watu wenye uchumi mkubwa na ubora wa maisha kwa maisha yao yote.

Hatua za kuchukua: mzazi una jukumu la kujitazama wewe mwenyewe na staili yako ya maisha kuhusu umuhimu na matumizi ya fedha. Baada ya hapo una jukumu kubwa la kumuandaa mwanao kwa kumpatia maarifa sahihi kuhusu elimu ya fedha ili akifikia umri stahiki awe na mtazamo chanya kuhusu suala hili nyeti.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Haya Ndio Makosa kuhusu Fedha Unayotakiwa Kuyaepuka! – 2

Ukifanya uwekezaji stahiki – pesa yako itamea na kukua kama mche huu – kila kukicha!

Habari,

Katika sehemu ya kwanza ya makala haya tumejadili mambo au makosa manne kuhusu fedha, ambayo watu huyafanya kwa kujua au kughafilika, wakaishia kupata matatizo, hasara au hata kufilisika. Hali hii ikitokea huwachanganya na kuwakatisha tamaa watu hawa. Tumejadili pia jinsi ya kushughulika na makosa haya, kwa kujiepusha au kuyakabili, yakitokea.

Hii ni sehemu ya pili ya makala haya ambapo tutajadili makosa mengine manne, tukianzia na kosa la tano kama ifuatavyo:

Yafuatayo ni makosa hayo, na tutayajadili hapa:

Tano, kuweka akiba bila kuwekeza. Kuna swali huwa linaulizwa, “je kipi bora zaidi kati ya kuweka akiba na kuwekeza?” Wapo wanaosema ‘akiba’, na wapo pia ambao wanasema kuwekeza ni bora zaidi.

Sasa, wataalamu wa biashara wanasema wapo watu waliohamasika na wakajenga tabia ya kuweka akiba, hadi wakawa na fedha nyingi. Lakini kwa kukosa maarifa, wameishia kukaa na mamilioni ya fedha, benki, kwa miaka mingi, bila kunufaika nayo.

Wanasema, kuziacha pesa zako nyingi, zikae benki miaka mingi, ni hasara! Kwanza kuna suala la fedha zako kupungua thamani kutokana na ‘inflation’, lakini pia riba za benki, kwa pesa zilizowekwa akiba ni ndogo sana, na faida yake ni ndogo, isiyo na tija yoyote. Hivyo, wakati unahimizwa kujijengea tabia ya kuweka akiba, unahamasishwa pia kujenga tabia ya kuwekeza.

Kwa hiyo, wakati unakuza akiba yako benki, unapaswa pia kuanza kuufikirisha ubongo, ili kuchakata fursa mbalimbali. Na ukishaona kitu cha kufanya (fursa), ni wakati sasa wa kufikiria kuziondoa fedha zilizoko benki (akiba), na kuziwekeza katika miradi au biashara unayoona itakupatia kipato endelevu.

Kwa kufanya hivi unapata faida mbili kwa pamoja. Moja, unatengeneza faida kwa mtaji wa akiba yako, na pili unajijengea tabia au hulka, na kukomaza maarifa ya kujiajiri (ujasiriamali), yanayohitajika sana hivi sasa. Kitu wasichojua watu ni kwamba, ukiweka fedha zako benki bila plani, utazitumia pia bila plani. Wengi huingiwa na tamaa na kujikuta wananunua vitu vya anasa, visivyo na tija yoyote kwa maisha yao.

Sita, Kukosa fungu la fedha ya tahadhari. Kumbuka maisha hayatabiriki, na wengi hatujui nini kitatokea kesho. Kuna wakati matatizo yanaingia kama mwizi, bila kutarajia! Kuna magonjwa, safari za dharura, gari au nyumba kuharibika, majanga nakadhalika. Yakitokea haya, unahitaji fedha kukabiliana nayo. Swali, je fedha hizo zipo?

Kwa hiyo, kama huna fedha za akiba ya majanga unafanya kosa kubwa! Utafiti uliofanyika Marekani unasema ni asilimia 40 tu ya Wamarekani ndio walio na uwezo wa kulipia hapohapo tatizo linalogharimu dola 400 (kama shilingi 900,000/= hivi). Asilimia 60 iliyobaki wakipata tatizo linalolingana na gharama hii, hulazimika kukopa, kwa riba kubwa! Sijui utafiti huu ukifanywa Tanzania hali itakuwaje!

Sasa, kinachosisitizwa hapa ni kwamba mikopo mingi hasa ya dharura huwekewa riba kubwa kiasi cha kuumiza. Wapo watu wamepoteza vitu vyao vya thamani (nyumba, gari n.k.) kupitia riba iliyolimbikizwa hadi ikawa haiwezekani kulipika. Hivyo, kujiepusha na tatizo hili unatakiwa kujenga utamaduni wa kujiwekea fungu la dharura.

Unachotakiwa kufanya ni kukata asilimia fulani kila mwezi kutoka katika mapato yako, na kuweka kiasi hiki katika akaunti maalum kwa ajili ya dharura. Hii ni akaunti utakayoitumia kuchukua fedha kwa matumizi ya dharura tu, na si vinginevyo.

 Saba, tabia ya kukopa kiholela. Tumejadili hapo juu jinsi ambavyo watu hulazimika kukopa ili kutatua matatizo yaliyokuja bila kutarajia (dharura). Hata hivyo, unatakiwa kuwa mwangalifu sana kuhusu tabia hii. Unapokopa kuna vitu viwili vinafanyika. Kwanza unapata fedha ili kutatua tatizo lako; lakini pili unauweka rehani uhusiano kati yako na mtu aliyekukopesha.

Katika kukopa kuna watu hukopa kwa ajili ya dharura na wengine hukopa kwa vitu visivyo na tija yoyote, na pengine kufanyia anasa tu; kama harusi, mahafali, ubarikio n.k! Kumbuka unapokopa fedha kwa ndugu, rafiki, au benki unaweka rehani uhusiano wenu, mbali na riba, gharama au usumbufu unaoweza kuupata utakaposhindwa kulipa kwa wakati.

Nawafahamu watu. Lilipofika suala la kuoa waliingia ‘madeni ya kufa mtu’; yaani walikopa kila mahala ili kuifanya harusi iache gumzo mjini. Sawa, kila mtu angependa kufanya sherehe kubwa kulingana na tukio la kihistoria linalokuja mbele yake. Lakini kinachogomba ni uwezo. Kama uwezo hauruhusu, unakopa ili iweje? Unaweza kuishusha shughuli yako ili ilingane na kiasi cha fedha ulichonacho.

Na kama bado unatamani shughuli yako iwe kubwa kwa kiasi cha ‘ndoto zako’, basi kubali kufanya subira. Na subira hii iendane na jitihada za kukusanya fedha taratibu kupitia mapato yako na msaada wa wadau, na kuiweka fedha hii katika akiba hadi ifikie kiwango kinacholingana na gharama inayohitajika. Usipofanya hivi, ukaamua kukopa, jiandae kwa majanga mbele ya safari, ikiwa ni pamoja na hatari ya hujishushia hadhi katika jamii!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Haya Ndio Makosa kuhusu Fedha Unayotakiwa Kuyaepuka! -1

Ujanja sio uwezo wa kutengeneza fedha tu; bali kuzidhibiti zisiyeyuke bila utaratibu ukabaki na maumivu!

Habari,

Wapo watu ambao hufikiri kwamba utajiri ni matokeo ya uwezo mkubwa wa mtu kutengeneza fedha, au kumiliki mali. Je, hii ni kweli? Wataalamu wa biashara wanaikataa hoja hii. Wanasema tatizo linalowasumbua watu wengi kuhusu suala la fedha ni uwezo mdogo walionao wa kuhifadhi au kutunza fedha au mali walizotengeneza kwa jasho jingi. Kwa sababu hii ni muhimu sana watu kujijengea maarifa kuhusu utengenezaji na uthabiti katika udhibiti wa fedha.

Kuna mambo kuhusu fedha ambavyo watu huyafanya kimakosa wakaishia kupata hasara au hata kufilisika. Hali hii ikitokea huwachanganya sana watu na  pengine kuwakatisha tamaa ya maisha. Hata hivyo, waswahili husema, ‘kufanya kosa sio kosa – kosa ni kurudia kosa’; hii ina maana kwamba kufanya makosa katika maisha ni jambo la kawaida, lakini kinachotakiwa baada ya hapo ni kuitumia fursa hiyo kujifunza, ili kosa hilo lisirudiwe.

Kitu kingine muhimu katika kujifunza ni kuangalia mambo ambayo yalifanywa na watu wengine, kwa utaratibu fulani, halafu wakapata hasara au matatizo. Kwa kuyajua mambo yaliyowasibu au kuwaangusha wengine, inakuwa rahisi kutengeneza mikakati ya kujiepusha na hasara au matatizo kama yalivyowatokea wengine.

Kwa hiyo kuhusu hili, kuna makosa yaliyowahi kufanywa na wengine, huko nyuma, kuhusu fedha, na wakapata matatizo. Sasa tusipojibidisha kuyajua makosa hayo, na kuweka mikakati ya kujiepusha nayo – kuna hatari ya kuyarudia, au kukosa mbinu ya jinsi ya kuyakabili, yakitokea. Na tukiacha yatokee, madhara yake ni makubwa kwa maisha yetu!

Yafuatayo ni baadhi ya makosa hayo, na tutayajadili hapa:

Moja, kushindwa kutengeneza mpango wa fedha. Kuwa na andiko linalohusu namna unavyoweza kupangilia mapato na matumizi ya fedha zako ni mwanzo mzuri wa safari yako ya mafanikio ya ki-fedha, na hiki kinatakiwa kuwa kipaumbele chako cha kwanza.

Mpango mzuri wa fedha unahusisha; malengo ya uzalishaji mapato, malengo ya uwekaji akiba, malengo ya uwekezaji, malengo ya matumizi mbalimbali (mfano ada za shule, matibabu nakadhalika).

Mbili, kutumia – zaidi ya uwezo wa mapato yako. Jambo hili huwapata zaidi vijana, hasa wanaongiza fedha kila mwezi kupitia mshahara; lakini hata wale walio katika biashara zao. Wapo vijana katika makundi haya, hupata tamaa ya kuishi maisha ya juu, ya kujionesha au kuwakoga watu, kwa ulimbukeni tu! Hawa hununua bidhaa au huduma za bei kubwa bila sababu. Utakuta kijana ananunua gari au simu ya bei mbaya, bila kujali gharama za manunuzi, uendeshaji au hata matumizi yake halisi ya chombo hicho.

Wapo ambao hununua mapambo ya mwilini na nyumbani, kama nguo za gharama, ‘fenicha kali’, au kupanga nyumba kubwa iliyo maeneo ya kifahari, bila sababu ya msingi. Wengine hupendelea ‘trip’ au mitoko, mfano kutembelea maeneo ghali. Na wengine hujijengea maisha ya kujirusha (anasa) na hujisahau wakajikuta wametumia kipato chao chote, hadi kuingia katika madeni.

Tatu, kufanya uwekezaji usio wa busara wala tija. Kufanya uwekezaji ni kuingiza fedha katika mradi au biashara, kwa lengo la kutengeneza faida. Sasa kuna tatizo kubwa pale unapoamua kuwekeza kizembe. Wapo watu ambao huamua kuwekeza katika miradi fulani kwa kufuata ushawishi wa marafiki au ndugu, bila wao binafsi kujiridhisha. Hivyo hujikuta wanaingiza fedha zao kwenye miradi inayonyonya fedha zao, badala ya kuwaingizia kipato.

Kwa hiyo, kabla hujafanya uwekezaji wowote ni vizuri ukafanya utafiti kwa kutosha, ili ujiridhishe. Ujue soko likoje na changamoto zake, ujue washindani wako, ujue wateja wako wakoje, na ni wengi kiasi gani; na taratibu nyingine za uendeshaji wa biashara. Usione rafiki yako anatengeneza fedha kupitia biashara au mradi fulani ukadhani ni rahisi; hapana!

Nne, kujiingiza katika taasisi za ‘tajirika haraka’. Kuna taasisi zilizo rasmi, na nyingine sio rasmi, ambazo kuwashawishi watu, na pengine kuwalaghai (utapeli), ili waingize fedha zao humo, kwa matarajio ya kujizolea ‘mihela’ mingi, baada ya muda mfupi. Mfano wa taasisi hizi ni Q-net, ambayo imejadiliwa sana, jinsi ‘ilivyowaingiza watu mjini’. Hii ni njia mojawapo kubwa ya kupoteza fedha zako. Kuna msemo unaosema, ‘pesa ya chap-chap hukaribisha matatizo chap-chap’!

Hapa ni suala la kutumia akili kidogo tu. Hebu fikiria mtu anakwambia uingize shilingi milioni 10 katika ‘pyramid scheme’, halafu baada ya miezi kadhaa tu uwe umepata milioni 10 kama faida, hii inaingia akilini kweli? Kumbuka wewe hiyo milioni 10 pengine umetumia zaidi ya miaka mitano kuitengeneza, leo mtu anakuambia unaweza kutengeneza fedha hiyo kwa miezi tu.

Kwa hiyo unapokuja ushawishi wa mtu, unaokutaka utumie fedha kiasi fulani ili uje kupata faida kubwa kupita kiasi, usiingie kichwa-kichwa. Fanya kazi ya ziada kupata ukweli wa jambo hili kwa kutafiti na kushirikisha watu, kabla hujaamua kingiza fedha zako, kwani wengi wamejikuta ‘pagumu’! Hii ni sehemu ya kwanza ya makala haya, ungana na mimi katika sehemu ya pili tujadili makosa mengine zaidi.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Hivi Ndivyo Pensheni Inavyowachanganya Akili Wastaaafu Wengi

Katika maisha ya ajira kuna wakati vijana hutamani ‘kujirusha’ na kuyafurahia maisha. Sawa! Lakini kuna kitu cha kuzingatia pia…kustaafu kunakuja!

Habari.

Pensheni ni neno linalotumika kuelezea malipo kutoka katika mfuko wa hifadhi ya jamii; ambayo mtumishi hulipwa anapostaafu. Kuna malipo ya pensheni ya mkupuo na yale ya kila mwezi – yanayolipwa hadi kifo cha mstaafu.

Kiwango cha pensheni anacholipwa mstaafu hutegemea vitu kadhaa kama: kipindi cha uchangiaji (miezi), wastani wa mishahara bora ya mwisho, na kikokotoo; ambavyo huingizwa katika kitu kiitwacho ‘kanuni ya pensheni’ kutegemeana na mfuko husika; ili kupata kiwango ambacho kitalipwa.  

Kwa hiyo, mfanyakazi hulipwa mafao yake ya pensheni anapostaafu kwa umri au kwa taratibu nyingine zilizoainishwa na sheria. Mafao haya; ya mkupuo na yale ya kila mwezi, kimsingi ndio huchukua nafasi ya malipo ambayo mfanyakazi alikuwa analipwa kila mwezi, akiwa kazini, ikiwa ni pamoja na marupurupu mengine; kulingana na sera na kanuni za mwajiri husika.

Sasa, ninachotaka kujadili hapa leo ni kwamba mafao ya pensheni ni malipo tunayoweza kuyaita ‘malipo maalum’. Ni maalum kwa maana kwamba yanatakiwa  ‘kubebwa’ kama anavyobebwa mtoto mchanga. Kuna ‘masharti’ kadhaa katika kumbeba mtoto mchanga. Yaani; ukikosea masharti hayo, utamuangusha au kumsababishia maumivu au majeraha. Sharti kubwa kabisa ni umakini!

Inafahamika wazi kuwa mafao ya pensheni ni malipo anayopewa mstaafu anapomaliza safari yake ya utumishi; akiwa anaingia katika kipindi cha kumalizia safari yake ya maisha hapa duniani – kipindi cha uzeee.

Umri wa uzee, baada ya kustaafu, nao una masharti yake; ambayo usipoyatimiza, maisha yako yanakuwa ya kusikitisha; na yaliyojaa mateso na majuto! Moja ya masharti hayo ni umakini katika matumizi ya mafao ya kustaafu.

Kuna mambo ya kuzingatia katika matumizi ya pensheni ambayo kila mstaafu anatakiwa kuyazingatia. Kwanza kabisa; fedha za pensheni sio nyingi kama zilivyo hisia za wastaafu wengi. Kwa kuziona kwa macho, au kuzitamka mdomoni, zinaonekana ni nyingi. Lakini ki-uhalisia si fedha nyingi – ingawa wingi au uchache wa kitu, kama fedha, unategemea sana akili, maandalizi na mipango ya mstaafu husika.

Wafanyakazi waliokuwa wakilipwa vizuri, mshahara na malipo ya ziada, tunasema hawa walizoea kuwa na fedha mfukoni. Kwa kuwa ‘wanazo’, wapo ambao maisha yao hughubikwa na matumizi ya ovyo; ikiwa ni pamoja na kutokuwa na presha ya kusaka maarifa ya kujiwekea akiba, na kujiingizia kipato kabla ya kustaafu. Hawa wakistaafu huyaona mafao yao ni fedha kidogo; kwa kuwa matumizi yao tayari yalikuwa makubwa; na wangependa yaendelee hivyo.  

Fikra hizi huwafanya wafanyakazi hawa kuogopa kustaafu – wanapokaribia umri huo; hadi wengine kushawishika hata kudanyanya umri, kitu ambacho hupunguza ufanisi wao ki-utendaji; kwani wengine huishia kusinzia tu wakiwa maofisini, na wengine hata kutembea au kuona huwa matatizo. Wapo wanaosema, “ni heri mateso wanayopata wakiwa kazini kuliko yatakayowapata wakistaafu”.   

Wastaafu hawa; pamoja na uzoefu wao wa kushika fedha nyingi, wakilipwa mafao yao, nao hupagawa na kupumbazika! Kwa ‘wingi’ ule unaoonekana kwenye makaratasi, mstaafu ‘hupigwa upofu’, asifikirie kama zitaisha; hivyo hujiingiza au kuendeleza matumizi ya ovyo; na mwisho wake unajulikana!

Kwa upande mwingine; mfanyakazi ambaye mapato yake kazini hayakumtosha ‘kutesa’; sasa huona fursa ya ‘kulipizia’ imeingia. Alikuwa anasikia tu ‘Casino’, sasa atataka aingie – na humo atakutana na ulevi, kamari, vibinti na kila uchafu. Na wahenga walisema “kila mwonja asali hachovyi mara moja”. Akija kustuka, zaidi ya robo tatu ya mafao yameondoka, yakimwachia uzee – ahangaike nao!

Ni jambo la kawaida katika familia za Ki-afrika, mfanyakazi kuwa na kundi kubwa la wategemezi; wengine ni watoto na wengine ni ndugu, upande wa mke au mume alioamua kuishi nao. Lengo kuu huwa ni ‘kuwavusha’ wote hawa; ili wajitegemee baadaye. Sasa, anaposhindwa kufanya hivyo akiwa bado kazini hulazimika kutumia mafao yake; ama kuwasomesha au kuwapa, kama mtaji, vijana wake.

Wakati ni wajibu wake kufanya hivyo; kimsingi anakuwa amechelewa – hadi kulazimika kutumia mafao kwa majukumu haya. Ifahamike kuwa pensheni sio fedha kwa ajili ya kuwagawia wategemezi. Kazi hii inatakiwa ifanyike kabla kabisa – kupitia akiba maalum. Pensheni ni fedha ya mstaafu kwa ajili ya kujiweka vizuri uzeeni; na hutakiwa kutumika kama ‘mtaji jazilizi’ kwa aliji ya miradi yake iliyoanzishwa akiwa bado kazini.

Ili kuepuka kuitumia pensheni yako kwa ajili ya matumizi ya wategemezi, ni vyema ufahamu mapema kuwa ukiajiriwa tu, ipo siku utastaafu. Na ukweli kabisa…kustaafu hakuji kama mwizi! Unajua utastaaafu…siku unapoweka saini katika mkataba wa ajira; kukubali ofa ya ajira hiyo. Kwa sababu hiyo unatakiwa kujiandaa mapema.

Kujiandaa mapema kunahusisha mambo mengi ikiwa na pamoja na mipango ya ndoa na familia; idadi ya watoto watakaozaliwa; na umuhimu wa watoto kuzaliwa mapema ili majukumu ya ‘kuwavusha’ hadi waweze kujitegemea yafanyike ndani ya kipindi cha ajira; na hii itaepusha mzigo wa kusomesha au kugawa mtaji baada ya kustaafu; kwa kutumia fedha za mafao.

Mambo mengine ya kujiandaa mapema ni pamoja na kujitafutia maarifa na taarifa mbalimbali kuhusu masuala ya miradi na biashara. Halafu; kujijengea nidhamu ya fedha na tabia ya kuweka akiba na kuwekeza, ndani ya ajira; ili kujijengea uzoefu na umahiri. Ni umahiri huu ambao utautumia utakapostaafu kuendeleza miradi/biashara zako, kwa kutumia pensheni yako kama ‘mtaji jazilizi’.  

Kwa hiyo, kujiandaa mapema, kwa kuweka akiba na kuwekeza, kunasaidia sana kumwingiza mfanyakazi katika maisha ya kustaafu kwa mguu mzuri. Kumbuka; kwa kawaida mafao ya kustaafu huwa hayalipwi hapo hapo, kuna kipindi kirefu cha kusubiri.

Katika kipindi hiki mstaaafu aliyejiwekea akiba, na ana miradi yake inafanya kazi, hatakuwa na presha; na mara akilipwa mafao yake…anachofanya ni kujaziliza tu pale palipopungua, na mambo mengine yanaendelea; yakimhakikishia furaha na amani tele ndani ya maisha ya uzeeni!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali ki-vitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Haya Ndio Madhara Ya Watoto Kulelewa Na ‘Single Mamaz’

Malezi ya watoto katika familia za ‘single mamaz’ yana changamoto nyingi; na yana athari kubwa kwa watoto husika

Habari,

Katika sehemu ya kwanza na ya pili  ya makala haya tumebainisha mambo yanayosababisha mtoto au watoto kulelewa na mama peke yake. Tumejadili  kwamba suala hili limeanza kujadiliwa kwa kina hivi sasa; kwa kuwa limeanza kuonekana ni tatizo; hasa la kuongezeka kwa tabia, na idadi, ya wanawake wanaopenda, kwa hiari yao, kuishi peke yao kama ‘single mothers’.

Akionekana kupingana na tabia hii, mwandishi Michelle Smith anasema kwamba tabia hii siyo ya kawaida; kwa kuwa serikali, taasisi za dini, na vyombo mbalimbali vya habari bado vinaitafsiri ‘familia’ kwamba ni ile yenye baba, mama na watoto, wanaoishi na kufurahia maisha pamoja. Na kwamba hali inayoonekana sasa, haikidhi matakwa ya tafsiri ya dhana halisia ya familia. Na kinachotia wasiwasi zaidi ni athari zinazowapata watoto katika familia hizo ‘mamboleo’.

Hata hivyo, katika makala iliyopita, waandishi kama Leah, Dr. Mauki, na T. Wright wameliongelea suala hili na kuonesha kuwa pamoja na athari zinazoweza kujitokeza katika malezi ya single mamaz, kuna manufaa pia; kwa mfano T. Wright anasema, mtoto akilelewa na mama yake tu, mara nyingi wawili hawa hujenga mshikamano mkubwa sana, huwa wana mapenzi ya dhati, na hufanikisha vitu vingi wanavyopanga kufanya pamoja.

Pamoja na madai ya waandishi hao, ni wazi kwamba uamuzi wa mama, kulea mtoto au watoto peke yake, si kazi rahisi; na ni dhahiri kuna athari; kama atafanya hivyo kwa kulazimishwa na mazingira, au kwa hiari yake. Zipo changamoto nyingi, ambazo husababisha athari kwa mzazi huyo; lakini hasa kwa mtoto au watoto anaowalea. Naomba sasa katika makala haya tujadili suala hili la athari.

Mama mmoja, Bi Aisha, akihojiwa na gazeti moja anasema, “bila kujali analelewa na mzazi mmoja au wawili, mtoto anatakiwa afundishwe maadili mema. Anatakiwa kufundishwa namna ya kuishi ndani ya familia, na ndani ya jamii yake. Anatakiwa pia apewe elimu na maarifa ili ajitambue, ajue wajibu wake, na awe raia mwema, mwenye adabu na heshima. Pamoja na hayo, mtoto huyu anapaswa pia kuyaona na kuyahisi mapenzi ya wazazi wake kwake. Sasa tujiulize je, mama peke yake anatosha kumpatia mtoto malezi haya?”

Katika hili, kuna akina dada wawili, Maureen na Sandra, waliolelewa na mama tu; wana mitazamo tofauti. Maureen, msanii wa muziki nchini Kenya, anaungana mkono na Bi. Aisha hapo juu. Anasema, “mtoto kuwa na maadili inategemea uwezo wa mama mwenyewe. Kwangu mimi, ‘my mom was a strong woman’. Alitulea ‘in a straight way’, na alitujengea nidhamu ya hali ya juu. Ndio maana mimi nimemudu vyema katika muziki, na sidhani kama ningepata zaidi ya haya, hata kama baba angekuwepo.”

Sandra, kwa upande wake anasema, “mimi nimepungukiwa makubwa kwa kupata malezi ya mama tu, ‘and I can see it clearly’. Nilikosa ‘guidance’, kwani mama hakumudu jambo hili. Mimi na wadogo zangu tulijikuta kukiingia katika magenge mabaya, na wala hakuwepo mtu aliyejali.”

Anasema, “tulikosa ‘father figure’ katika maisha yetu. Hatukuwahi kusikia ‘ngurumo’ ya baba ikituonya, kutupa maelekezo au kututia moyo kwa kila tulilokuwa tunakosea au kupatia. Hatukupata furaha wala mapenzi ya baba. Mama hakuwa na muda sana na sisi, ingawa pia hakumudu kutudhibiti wala kutuelimisha maisha. Akili na nguvu zake alizielekeza zaidi katika kukimbizana na pesa. ‘She was so busy‘, hivyo maendeleo yetu shuleni, na maadili yalishuka sana!”

Kupitia andiko lake moja, dada mmoja, Yusta anasema, “wapo watoto katika familia za ‘single mamaz’ huharibika kabisa ki-akili, kimatendo na kimaadili kutokana na kupendwa kupita kiasi na mama zao.”  Anasema, “wazazi hawa huwadekeza watoto wao kiasi cha kuwafanya wajinga. Lakini pia, hawawaambii wototo ukweli kuhusu maisha ili waweze kusimama kwa miguu yao; ama kwa kuwapenda sana, au kwa kuwaogopa!”

Anasema, “watoto waliolelewa na mzazi mmoja, na hasa mama peke yake, huharibika, wawe wa kiume au wa kike, kwa sababu ‘single mamaz’ wengi hujawa na hisia za kupungukiwa kupenda au kupendwa. Sasa, kwa kuwa yeye yuko peke yake, bila mume, hujijengea hisia mpya, za kupenda zaidi; na hisia hizo huhamishiwa kwa mtoto. Yaani anaamua ‘kumhonga’ mtoto mapenzi ambayo yalipaswa kuelekezwa kwa baba yake; na kwa kufanya hivyo anamharibu mtoto.”

Katika hili mtaalamu mmoja wa malezi, Vivian, anasema, “namjua ‘single mama’ mmoja aliyemdekeza mtoto wake wa kiume hadi akawa na tabia za kike. Utamsikia akimzungumzia mwanae kwa wenzake, ‘yaani ka-bebi boy kangu jamani…sijui kako salama huko Chuo? Na hivi hakajui hata kufua, yaani kanateseka kweli!’. Mama huyu, kwa jinsi alivyompenda mwanae, siku za nyuma, alifikia hatua ya kumpaka wanja, akijua huyo ni mtoto wa kiume!”

“Ukifuatilia ‘ka-bebi’ kanakozungumziwa hapa, ni kijana mtu mzima, anayetakiwa kujifunza kupambana na maisha ili akomae ki-akili. Sasa kijana huyu akija kuoa au kuajiriwa unadhani atakuwa na tija katika jamii hiyo? Huyu akili yake itabaki ki-mama-mama tu!” Ni hatari mama kumlea mtoto kwa kushindwa kumpa majukumu yake stahiki, na kumsimamia afanye – kwa kigezo cha kumuonea huruma. Mtoto huyu akizoea ‘spoon feeding’ anakuwa kituko!”

Vivian anasema kwamba kuharibika kwa mtoto kunatokana, kwa kiasi kikubwa, na malezi. “Malezi ndio kila kitu! Sasa mtoto aliyelelewa kwa kudekezwa namna hii hata akiwa mtu mzima hataacha kudeka-deka. Huyu akiajiriwa anakuwa mzigo kwa mwajiri na hata wenzake. Na akikosa ajira mara nyingi hukosa uwezo wa ubunifu, kujenga fikra au kuziona na kuzikamata fursa. Anakuwa tegemezi zaidi.” Anasema.

Zipo tafiti zinazoonesha kuwa watoto wengi wa ‘single mamaz’ huzaliwa na kulelewa katika mazingira yasiyo rafiki, na hivyo hupata malezi yenye upungufu. Watoto hawa; wengi huwa hawana nidhamu, hawafuatilii vizuri masomo (utoro), na wengine huingia mtaani, na hujihusisha na matumizi ya vilevi au uhalifu mwingine. Na wakiwa wasichana, huwa katika hatari kubwa ya kubeba mimba za utotoni. Kwa ujumla watoto hawa huishi kwa unyonge na upweke; na wengine hupatwa na sonona.  

Hata hivyo zipo tafiti pia zinazoonesha kuwa watoto waliojikuta wakilelewa na ‘single mamaz’ kwa sababu baba zao wamefariki au wamefungwa kwa sababu zinazoeleweka, hawapatwi sana na athari hizi; ambazo huonekana zaidi kwa watoto wa ‘single mamaz’ waliolazimika kuishi peke yao kwa sababu walipenda wenyewe, walipewa talaka au walizaa nje ya ndoa, kwa kupanga au kwa ‘bahati mbaya’.

Kwa hiyo, hizi ni baadhi tu ya athari zinazowakabili watoto wanaolelewa katika familia za ‘single mamaz’, ambazo takwimu zinatuambia (kwa mujibu wa mwandishi mmoja), kuwa takriban asilimia 30 ya watoto wote duniani wanalelewa katika ‘familia’ hizi. Sasa kwa kuwa hizi ni athari zinazomgusa mtoto, ni wazi kwamba zinaigusa na jamii nzima pia, kutokana na madhara yake; hivyo ni vizuri jambo hili likatazamwa kwa jicho maalum.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Ongezeko La Wanawake ‘Single Mamaz’: Tatizo Ni Nini? -2

Inasemekana mapenzi ya ‘single mothers’ na watoto wao huwa mazito, na wawili hawa huelewana sana!

Habari,

Kwa mujibu wa mtaalamu wa saikolojia, Dk Chris Mauki, takwimu za sasa ulimwenguni zinaonesha ongezeko kubwa la watoto wanaolelewa na kukuzwa na mzazi mmoja; tofauti na mila na tamaduni za miaka ya nyuma. Yaani kwamba malezi ya mzazi mmoja kwa sasa yanaonekana kuwa kitu cha kawaida!

Halafu; akinukuliwa na gazeti moja, mtaalamu wa sosholojia, Mbago Urio, anasema utamaduni wa watoto kulelewa na mzazi mmoja unazidi kushika kasi nchini Tanzania na nchi zingine. Wapo pia watu wa kawaida wanaonong’ona ‘vijiweni’ uwepo wa utamaduni huu, na kwamba suala hili linapaswa kutazamwa kwa jicho maalum; hasa na viongozi wetu wa ki-imani.

Tumeijadili mada hii katika sehemu ya kwanza ya makala hii ambapo tumebainisha mambo yanayosababisha mtoto kulelewa na mama peke yake. Tumeeleza pia uwepo wa tafiti zinazoonesha kuwa suala la malezi ya mzazi mmoja limeanza kujadiliwa kwa kina hivi sasa; kwa kuwa limeanza kuonekana ni tatizo linaloota mizizi taratibu; la kuongezeka kwa tabia, na idadi, ya wanawake wanaopenda, kwa hiari, kuishi peke yao kama ‘single mothers’. Sasa tuendelee na mjadala huu katika sehemu hii ya pili.

Siku za karibuni kumekuwa na wimbi la wanawake au ‘wadada’ kutaka kulea watoto bila msaada wa wanaume. Hivyo, kwa sababu moja au nyingine, ‘wadada’ hawa hufanya maamuzi ya kubeba ujauzito na kukataa kuendelea na mahusiano, ya mume na mke, na mhusika. 

Wapo ambao humficha mhusika (baba) wa mtoto kwamba huyo ni mwanae, na wengine huamua kubeba ujauzito wa mume wa mtu wakijua fika kuwa mhusika atakataa kuhusika na malezi kwa kujiepusha na mtafaruku unaoweza kumtokea katika ndoa yake.

Tabia hii ya ‘wadada’ kuamua kuishi, kuzaa na kulea peke yao haikuzoeleka ki-asili. Wataalamu wanadai kuwa pengine imesababishwa na mabadiliko ya majukumu – ambapo sasa wanawake nao wameingia katika ‘utafutaji’, tofauti na zamani ambapo jukumu lao la msingi lilikuwa ni usimamizi wa malezi, wakimsaidia baba (mtafutaji). “Wanawake watu wazima wenye vipato vikubwa wapo wengi katika kundi hili la wanaolea watoto peke yao”, anasema mtafiti mmoja wa mambo ya malezi.

Pamoja na hilo, dada mmoja aitwaye Saida anasema: “Katika zama hizi, ‘single mamaz’ watakuwa wengi sana…maana ‘wadada’ wengi wanapenda sana ‘maisha ya drama’, ingawa wengi hukwama mbele ya safari.” Drama inaelezewa kama dhana inayohusisha maigizo kama tamthiliya, filamu nakadhalika.

Wakihojiwa na mwandishi mmoja kuhusu kwa nini wameamua kwa hiari kuishi kama ‘single mamaz’, wanawake kadhaa walikuwa na mengi ya kusema; mradi kila mmoja alikuwa na kitu cha kuelezea hisia na msimamo wake.

Justinah anasema: “Wapo watu hudhani mtu kuishi peke yake maana yake ni kujiingiza kwenye upweke; hapana! Kuishi peke yako ni kujijengea uwezo. Mimi napata nguvu ya kujifanyia mambo yangu bila kulazimika kufuata matarajio au matakwa ya mtu mwingine. Maana yake ni kwamba napata nafasi ya kufuata kanuni au sheria zangu mwenyewe. Nikitaka kutoka, kulala, kuimba, kucheza au hata kulia; wakati wowote nafanya, bila kizuizi; napenda ‘freedom’ mimi!”

Leah anasema: “Ndiyo, ni mimi mwenyewe nimeamua kuishi maisha ya ‘single mama’, na huu ni uamuzi wangu ambao sitaki mtu aniulize maswali. Nina miaka 37 sasa, na sijaolewa na sitaki kuolewa, na sijawahi kuishi na mwenzi humu ndani; pamoja na kwamba tayari nina watoto. Mahusiano kwangu mimi ni mzigo, kwa sababu nyingi tu; lakini sababu kubwa ni kwamba mimi ni ‘single mama’ kwa hiari!”

“Nawajua ‘single mamaz’ waliongia humo kwa sababu za ki-mazingira; na wengine walichoka tu, wakaona kuishi na mtu ni kama utumwa fulani hivi; mimi niliamua mapema kabisa kuwa nitaishi kama single mama! Hata hivyo watoto wangu hawatofautiani ki-tabia na wale waliolelewa na wazazi wawili, kwa kuwa nilijipanga tokea zamani!” anasema Leah.

Kwa mujibu wa Dr. Mauki, yapo mambo mazuri ambayo mtu anaweza kujifunza kutokana na kuwa mzazi peke yake. Kwa mfano; mara nyingine mzazi anayelea na kukuza mtoto au watoto peke yake anaweza kugundua uwezo alionao ndani yake wa kukaa na watoto, ambao asingeweza kuufahamu kama wangekuwa wazazi wawili.

Anasema ‘Single mamaz’ wengi wamejikuta wana uwezo wa kujituma na kufanya mambo kwa bidii zaidi pasipo kuwa tegemezi, tofauti na wanapokuwa na mzazi mwingine. Anasema wengine wamejifunza kuwa furaha ya kweli haitokani au kuletwa na mtu mwingine, bali inachochewa na mtu mwenyewe kutokea ndani yake.

Mwanasaikolojia T. Wright anasema, “wakati fulani kuna manufaa makubwa mtoto akilelewa na mama yake tu. Mara nyingi wawili hawa hujenga mshikamano mkubwa. Utafiti mmoja unadai kuwa ‘bond’ inayoundwa kati ya mama na mtoto ni kubwa zaidi, ikilinganishwa na ile ya mtoto huyu akiwa na wazazi wake wote wawili. Sio hili tu; bali wawili hawa huwa wana mapenzi ya dhati, na hufanikisha vitu vingi wanavyopanga kufanya pamoja ili kufikia lengo fulani.”

Hata hivyo, pamoja na madai ya Leah, Dr. Mauki, na Wright hapo juu, ukweli ni kwamba uamuzi wa mama kulea mtoto au watoto peke yake si kazi rahisi kama inavyoweza kufikiriwa. Lakini pia; ni dhahiri kuna athari kwa mzazi mmoja kubeba jukumu hili; kama atafanya hivyo kwa kulazimishwa na mazingira, au kwa hiari yake. Kuna changamoto, ambazo husababisha athari nyingi kwa mzazi huyo…lakini hasa kwa mtoto au watoto anaowalea. Tutajadili suala hili, la athari, katika makala nyingine.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Ongezeko La Wanawake ‘Single Mamaz’: Tatizo Ni Nini? -1

Wakati fulani mama hujikuta amebanwa sana na majukumu ya kazi hivyo huhitaji msaada wa mwenzi wa kiume…upande wa malezi ya watoto

Habari

Akinukuliwa na gazeti moja, mtaalamu wa sosholojia, Mbago Urio, anasema utamaduni wa watoto kulelewa na mzazi mmoja unazidi kushika kasi nchini Tanzania na sehemu nyingine duniani.

Mtaalamu wa saikolojia, Dk Chris Mauki anasema takwimu za sasa ulimwenguni zinaonyesha ongezeko kubwa la watoto wanaolelewa na kukuzwa na mzazi mmoja; tofauti na mila na tamaduni za miaka ya nyuma. Yaani kwamba malezi ya mzazi mmoja kwa sasa yanaonekana kuwa kitu cha kawaida!

Upo utafiti unaoonesha kuwa waathirika wakubwa kwa jukumu la kulea watoto peke yao ni wanawake; ambao wanatengeneza asilimia 88 ya wazazi wanaolea watoto bila msaada wa wenzi wao wa jinsia ya kiume. Ukweli ni kwamba idadi ya familia zinazoishi na mzazi mmoja inaongezeka, hasa katika maeneo ya mijini.

Kwa mujibu wa machapisho kadhaa ya Umoja wa Mataifa; nchi za China, Iran, India, Indonesia, Israel, Jordan na Uturuki, zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaoelelwa na mzazi mmoja. Taarifa hizo zinaonyesha kuwa kwa wastani zaidi ya asimilia 10 ya watoto katika mataifa hayo, wanalelewa na mzazi mmoja, idadi ambayo ni theluthi moja ya familia za aina hii duniani kutoka katika nchi hizo. Nchini Afrika Kusini, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 40 ya watoto wanaishi na mama pekee; wakati ni asilimia 4 tu wanaoishi na baba pekee. Kenya inakadiriwa kuwa na asilimia 30, na Msumbiji asilimia 36.

Pamoja na kuwa ni mtindo unaoshamiri, wanasaikolojia wanasema hakuna mtoto anayetamani kukuzwa au kulelewa na mzazi mmoja, bali ni mazingira tu ambayo husababisha hali hii itokee; na kuna athari kubwa ambazo watoto waliolelewa na mzazi mmoja hukabiliana nazo mapema au baadaye sana; katika maisha yao. Tutazijadili athari hizi baadaye.

Hii ni sehemu ya kwanza ya makala haya yanayolenga kujadili mambo au mazingira yanayosababisha mtoto au watoto kulelewa na mzazi mmoja, na hasa mama peke yake; kitu ambacho kimezoeleka sasa kuitwa malezi ya ‘single mama’. Kwa mujibu wa tafiti, yapo baadhi ya mambo yanayosababisha hali ya mtoto kulelewa na mama tu; na mara nyingine hayaepukiki.

Kuna suala la kufariki kwa baba. Hii hutokea pale ambapo mzazi wa kiume wa mtoto au watoto akafariki, na mzazi aliyebaki akaamua kutofunga ndoa tena, au kuingia kwenye mahusiano  na mtu ambaye anaonesha kutokubali kubeba jukumu la kuwa baba kwa watoto hao. Wapo pia wanawake wanaotelekezwa, na hii hutokea pale ambapo mzazi wa kiume wa mtoto anapotelekeza familia, kwa kutokomea kusikojulikana au kupuuzia tu; na kuacha jukumu lote la malezi kwa mama wa mtoto. Dada mmoja aitwaye Francisca anasema: “mama wa mtoto hawezi kutelekeza familia, hasa watoto; ndio maana watoto wengi hulelewa na kina mama peke yao.”

Lipo suala la baba wa mtoto kukataa ujauzito aliousababisha; ambapo mwanaume anaweza kukataa ujauzito kwa sababu mbalimbali; kama kutokuwa tayari kubeba jukumu la malezi, kuwa na mahusiano mengine, kuhisi amesingiziwa ujauzito huo au kutotaka tu kuwa na mtoto na mwanamke husika.

Baba wa mtoto kufungwa jela ni moja ya sababu hizo, ambapo uamuzi wa mahakama kumtia hatiani baba wa mtoto kwa kosa fulani la jinai, unaweza kusababisha mzazi wa kike kubaki na jukumu la kulea watoto au mtoto peke yake. Lakini pia kuna sababu ya mama kubakwa na kutiwa mimba. Vitendo vya ubakaji hususani kwa mabinti wadogo husababisha watoto kulelewa na mama pekee aidha kwa sababu ya kutomjua mhusika au kuogopa kumtaja, au baada ya baba kuhukumiwa kwa kosa la ubakaji na kufungwa jela.

Pamoja na sababu hizo, kuna tafiti pia zinazoonesha kuwa suala la malezi ya mzazi mmoja limeanza kujadiliwa kwa kina hivi sasa; na limeanza kugusa hisia za watafiti na watunga sera; kwa kuwa limeanza kuonekana ni tatizo! Hii inatokana na kile kinachoonekana kama kuongezeka kwa tabia, na idadi, ya wanawake wanaopenda, kwa kuamua, kuishi peke yao kama ‘single mothers’. Hii ni sehemu ya kwanza ya mada hii. Ungana na mimi katika sehemu ya pili ili tujadili zaidi sababu za kuongezeka kwa tabia hii.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Jinsi Ya Kutumia ‘Utundu’ Katika Mapenzi Kuboresha Biashara yako

Kukosa ubunifu katika mapenzi, kuna mchango mkubwa katika ongezeko la migogoro ndani ya ndoa; sawasawa na jinsi kukosa ubunifu katika biashara, kunavyoweza kuzorotesha biashara yako…

Habari,

Nikiwa napitia makala mbalimbali katika gazeti moja la michezo nilikutana na makala moja iliyonivutia na kunitafakarisha sana. Ilikuwa inahusu njia za ki-bunifu, za kuyafanya mahusiano ya ki-mapenzi baina ya wawili wapendanao, yasichuje. Naweza kusema makala ile inahusu mbinu bora za ‘mchezo wa ndoa’.

Nilivutiwa na maudhui ya makala hiyo kwa kuwa ilisisitiza umuhimu wa watu kuwa wabunifu na kwamba wasiridhike kufanya vitu au mambo kwa mtindo uleule, kila siku; na wakategemea kupata matokeo tofauti. Mwandishi wa makala hiyo, nadhani amebobea katika utaalamu wa mahaba, lakini pia anajua umuhimu wa suala zima la ubunifu katika maisha ya binaadamu.

Maudhui ya makala yale yanatoa mafunzo mengi, sio tu kwa wanandoa – ili wadumishe ndoa zao na kujenga upendo endelevu; bali pia yanatoa mafunzo mengi kwa wajasiriamali na wafanyabishara sawia.

Mwandishi alianza kwa kuandika, “ili mahusiano yako ya ndoa yawe bora na yalete msisimko, UBUNIFU ni kitu muhimu sana. Bila kuwa mbunifu, makini na mwenye kujua jambo gani lifanyike, lifanyike vipi, na kwa wakati gani, basi mahusiano hayo hayataweza kukupa kitu bora unachotamani kukipata.”

Aliongeza kwa kusema, “ili mwenzio asikuchoke katika mahusiano inabidi ujue kucheza na akili yake.” Lakini pia, tathmini za kitaalamu zinaonesha kuwa watu wengi walio katika mahusiano kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo wanakabiliwa na tatizo la kuchokana.

Mwandishi mmoja aliandika kuhusu tabia inayooneshwa na baadhi ya watu, kutamani kununua kila kinachopita mbele yao. Akaiita tabia hii ‘uraibu wa kununua’. Alisema, “akili ya binaadamu imeumbwa kukinai, hivyo watu wenye uraibu wa kununua hufanya hivyo kwa sababu ya kukinai tu ”. Kukinai ni kama ugonjwa wa kukichoka kitu ulichonacho, hata kama ni kizuri, na kutamani kujiridhisha kwa kujimilikisha au kununua kitu kingine kipya!

Mazingira ya wanandoa kuchokana, yanachangiwa na wapenzi husika kutokuwa wajanja au wabunifu. Yaani, yale waliyoyafanya jana au juzi wanataka hayohayo wayafanye kila siku, na matokeo yake ni kwamba mahusiano yao hupoteza ule msisismko au ‘stimu’ iliyokuwepo zamani.

Mwandishi anasisitiza kuwa hata kama matendo yako ni mazuri kwa kiwango gani lakini kama unayafanya mambo kila siku kwa mtindo ule ule, lazima yatachosha tu! Akitoa mfano wa chakula unachokipenda sana anasema, “japo kinakupa msisimko kinywani mwako na utamu katika ulimi wako, lakini kama utakula kila siku chakula hicho hicho, kwa mtindo huohuo mmoja wa mapishi kitapoteza ile thamani iliyopo katika fikra zako.”

Kwa maelezo hayo, mjasiriamali hapa unapata mafunzo makubwa. Kupitia mfano huu utaona umuhimu wa kufikiri kwa kina tena mfululizo, ili kila siku uje na vitu vipya/tofauti, au ufanye vitu vilivyopo, kwa mtindo tofauti na ule uliozoeleka. Hii itasaidia kuongeza thamani ya vitu hivyo katika hisia na mitazamo ya wateja wako ikilinganishwa na vile ulivyowapa zamani, lakini pia ikilinganishwa na vile vya washindani.

Mwandishi hakuishia hapo, anasisitiza, “tambua mahusiano ya raha yanatakiwa yajengwe katika msingi wa ubunifu na ujanja. Kama kuwezi kumfanya mwenzio ajihisi ana amani na raha kila siku, huwezi kuwa na udhibiti halisi juu yake,”

“Hapa ina maana, atakuwa na wewe ndani, mtalala kitanda kimoja, ndani ya shuka moja. Mtagusana, na kila mmoja atahisi joto la mwenzake; ila ndani ya nafsi yake bado atakuwa anahangaika na kuweweseka juu ya nani ampe raha halisi anayoitarajia. Hivyo ukitaka mahusiano yadumu, jifunze utundu wa mapenzi! Mfanyie mwenzio vitu fulani hivi ‘amazing’ hadi apagawe!”, anasema.  

Hapa kuna mafunzo makubwa kwa mjasiriamali. Usione kwa kuwa watu wanaijua bidhaa au huduma yako, na labda huja kuinunua, basi ukadhani kwa kufanya hivyo wataifurahia bidhaa yako siku zote. La hasha! Huenda tayari wameshakinaishwa nayo, na labda tu hawajapata bidhaa mbadala mahala pengine. Sasa basi, ikitokea wakaipata, wataachana na bidhaa yako na huenda wasirudi tena.

Mwandishi anadai, “kupendana haitoshi, kulala pamoja haitoshi, kujifunika shuka moja haitoshi pia. Nenda hatua moja zaidi ya hapo umfanye mwenzio akuone kama kitabu kipya, ama filamu mpya, au safari ambayo hujawahi kuisafiri. Mtilie utundu na chachandu fulani ili aione dunia kwa mtazamo tofauti.”

Lakini pia, tunaambiwa na wataalamu wa saikolojia kwamba kuna ushahidi kuwa wapenzi husalitiana huku wakiwa bado wanapendana, kisa? Kukosa ubunifu katika mahusiano!

Mjasiriamali pia una hatari kubwa ya kukimbiwa (kusalitiwa) na wateja wako kwa kuwa wateja mara zote wanapenda kupewa huduma au vitu vipya, vyenye radha na vionjo tofauti. Wanapenda ‘chachandu’. Wakigundua huna kipya – wewe kila siku mtindo wako ni uleule, bidhaa au huduma zako zina radha, rangi, au muundo ule ule kila siku, watachoka, watakinai, na mwisho ‘watasepa’!

Mwandishi anasema mapenzi ni sanaa, na daima hakuna sanaa bila ubunifu ama ufundi. Kwa hiyo unapaswa kuwa mbunifu kwa kila jambo la kimapenzi ili mwenzio ajione yuko katika msitu wenye vitu vya kustaajabisha, kuvutia na kutia hamasa katika maisha yake.

Vivyo hivyo kwa ujasiriamali. Ujasiriamali ukifanywa kwa mtindo wa ‘usanii’ – ubunifu hujitokeza bayana; ambao utakufanya kila siku utengeneze fikra mpya, kisha uje na vitu vipya (bidhaa au huduma), ili mteja wako kila siku ajione yuko katika msitu wa kustaajabisha na kutia hamasa.

Mteja huyu atajenga utii au ‘loyalty’ kwa bidhaa au biashara yako, na atahamasika kuwavuta wenzake kuzipenda na kuzinunua bidhaa au huduma zako, na mwisho wa yote ni kwamba biashara yako ‘itapaa’!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com