
Kimsingi, ni wajibu wa mzazi kumsaidia mtoto au kijana wake kuwa na taarifa au kukuza maarifa muhimu katika maisha yake. Na hili laweza kufanyika kupitia Stadi za Maisha. Haya ni maarifa ambayo yakitumika na kusimamiwa vizuri humjenga mtoto/kijana kuwa na mtazamo chanya kuhusu maisha yake binafsi na maisha yake ndani ya jamii.
Stadi za Maisha ni moja ya masomo muhimu sana kwa mtoto/kijana kwani humpatia maarifa kuhusu anavyoweza kukabiliana na changamoto za maisha, na kupata uwezo wa kuziona fursa, na kuzikamata. Stadi hizi hujumuisha mbinu zinazoweza kumsaidia kuyafanya maisha yake yawe na uelekeo ulio sahihi, kujitambua, kuwa na nidhamu, na kufanya vitu sahihi, mahala sahihi na wakati sahihi.
Nimesema huu ni wajibu wa mzazi, kimsingi. Sasa, wapo wazazi waliokosa umakini wakajikuta wanazodolewa na watoto wao wenyewe, halafu wanaanza kulalamika; pale watoto wao wanapoanza kujitambua, kupata akili za ki-utu uzima, na kuanza kuhoji mambo. Watoto hawa hugundua kuwa udhaifu au upungufu wao katika maadili, kumbe umesababishwa na uzembe wa wazazi wao walioshindwa kutimiza wajibu.
Kiukweli wapo wazazi wanaojitahidi kuwalea watoto au vijana wao kimaadili lakini watoto hushindwa kuzingatia maelekezo, wakawa wakaidi, na kuishia kuharibika. Hii ni habari nyingine… inayopaswa kushughulikiwa ki-upekee. Lakini wapo pia wazazi, ambao kwa uzembe tu, huwafanya watoto wao wakose maarifa muhimu kwa maisha yao. Sasa, watoto wakijitambua, na wakagundua hili, mzazi hawezi kukwepa kuzodolewa!
Hapo zamani kidogo, katika jamii za kiafrika kulikuwa na mila zilizohakikisha mtoto kabla ya kuingia katika umri wa kiutu uzima anapata maarifa au stadi ambazo zinalenga kumfanya awe mwanajamii anayejielewa, kujitambua na kuwajibika. Kulikuwa na ‘shule maalum’ za malezi ya vijana, kupitia matamasha ya jando na unyago. Cha kusikitisha, mila hizi zinazidi kumomonyoka kutokana na kasi ya ‘maendeleo’ ya utandawazi.
Hivi sasa, kutokana na sababu kadhaa, baadhi ya wazazi hawapati nafasi, au hawajali, au labda hawamudu, kuwapatia watoto wao stadi hizi, na sasa baadhi ya vijana wameanza kulalamikia kuikosa haki yao hii. Wanawalaumu wazazi wao kwa uzembe au kushindwa kuwajibika.
Katika hili, kijana mmoja Alexis, anasema, “wazazi wangu walishindwa kunifundisha stadi muhimu za maisha, na sasa nimegundua kwa kuzikosa stadi hizo utotoni, naona nimepungukiwa vitu muhimu sana katika maisha yangu. Nilipowauliza kwa nini hawakujali kunipa maarifa hayo, walijibu kwamba hata wao hawakuwahi kufundishwa na wazazi wao. Nilisikitika!”
Kijana mwingine Gavin anasema, “najua wapo wazazi wanaowafundisha watoto/vijana wao stadi za maisha…lakini najua pia kuwa wapo ambao hawana muda huo kwa kuwa hata wao hawakuwahi kufundishwa, au hata kama walifundishwa…wao hawana uwezo wa kuwafundisha watoto wao, na hili ni tatizo! Hata hivyo, najua pia kuna watoto ambao ni wakaidi, hawataki kujifunza,…pamoja na jitihada za wazazi wao”
Akitoa maoni katika mdahalo mmoja, kijana Bitter anasema, “nimekuzwa na wazazi ambao msisitizo wao mkubwa ulikuwa kusoma kwa bidii ili nifaulu masomo yangu vizuri, na waliniambia kila mara, ‘elimu ndio kila kitu’! Kwa kuzingatia maelekezo yao, nimekuja kugundua kuna maarifa muhimu sana, nje ya darasa, sikuweza kuyapata, mfano ujenzi wa fikra tunduizi, uthubutu, ujasiri, uchambuzi, kutoa maamuzi, na uwezo wa kujitegemea.
Akionesha madhara mengine ya kunyimwa stadi hizi, Kijana Bitter anasema, “kuna kitu muhimu ambacho nimekuja kugundua hivi karibuni, ambacho kimenisononesha sana. Nimegundua sikupewa hata stadi zinazonigusa moja kwa moja; kama kufanya usafi, kuoga, kupika, kufua, na hata kupiga mswaki. Sikuwahi kufikiria kitu hiki zamani, kwamba vitu hivi kumbe huwa vinafundishwa na wazazi majumbani, inasikitisha!”
Kijana mwingine anasikitika kwa kusema, “jinsi ninavyokuwa mtu mzima na kuanza kutambua mambo ndivyo ninavyobaini kuwa wazazi wangu hawakuwajibika ipasavyo kwangu. Ukweli, hawakunipa zana au ‘silaha’ kwa ajili ya kuyajenga na kuyalinda maisha yangu. Kuna mambo nahangaika kuyafanya mwenyewe hivi sasa, ingawa ukweli napata wakati mgumu, na wazazi wangu hawana namna ya kunisaidia, wameshachelewa!”
Sasa, ukifuatilia maoni haya utakubaliana na mimi kuwa baadhi ya watoto wanaofika katika umri wa kiutu uzima wakiwa hawana stadi muhimu za maisha, hawakutaka kuwa hivyo. Walijikuta hivyo ukubwani na baadaye kugundua kuwa kumbe wazazi wao kuna kitu hawakuwafanyia. Hata hivyo vijana hawa hawapaswi kukata tamaa; na kuacha kufanya jambo. Wanapaswa kujiongeza.
Mchangiaji mmoja katika mjadala kuhusu suala hili anasema, “nawasikitikia na kuwapa pole vijana wote waliokosa stadi muhimu za maisha, kwa kuwa wazazi wao walishindwa kuwajibika. Hata hivyo, pamoja na wazazi kukunyima stadi hizi, angalau wape shukrani, kwani walikulea ukawa na afya njema, na pengine kuhakikisha umepata elimu nzuri ya darasani.”
“Kwa kuwa sasa wewe ni mtu mzima, na sasa unajitambua, na unatambua nafasi yako katika jamii, unapaswa kuchukua hatua haraka! Acha kulalamika na badala yake anza kujifunza mwenyewe vitu vyote ulivyovikosa utotoni. Hili linawezekana, na wapo waliobadili maisha yao kabisa hadi watu wakawashangaa!”
Anasema, “ni kweli kama mtoto, ulipaswa kupendwa, kupewa malezi bora, kufundishwa maadili n.k. Lakini kama hukupata bahati hii utotoni, usianze kulia-lia. Kubali hili limeshatokea, kilichobaki ni kufanya kitu. Cha kuzingatia ni kwamba stadi yoyote unayoihitaji sasa, ambayo hukuipata utotoni, jiwekee mpango na mkakati wa kuipata. Na hata wale waliopatiwa stadi hizi, bado kuna haja ya kujifunza zaidi ili kujenga umahiri.”
Hatua ya kuchukua: wakati kijana unaweza kuungwa mkono, na kusikitikiwa na kila mtu, pale utakapoonesha kusononeshwa na matokeo ya wazazi wako kushindwa kuwajibika na kukupatia maarifa muhimu kwa ajili ya maisha yako, kwa upande mwingine unapaswa kukumbuka msemo huu, ‘yaliyopita si ndwele, tugange yajayo’!
Ukishalijua hili, una wajibu sasa wa kulibeba jukumu hili wewe mwenyewe. Unapaswa kutafuta njia mbalimbali za kukupatia maarifa na stadi zote ulizozikosa. Uzuri, tayari sasa unajua unahitaji nini katika maisha yako, au unataka kuwa nani, na unataka kukuza vipaji gani, hivyo chukua hatua!
Wakati fulani inabidi tuwasamehe wazazi wetu kwa kushindwa kuwajibika. Wazazi wengine walijaribu kufanya walichoweza, kulingana na jinsi wao wenyewe walivyolelewa, habati mbaya hawakufikia viwango stahiki. Pamoja na hayo, ujumbe muhimu kwao ni kwamba wanapaswa kuujua ukweli huu, na kujifunza kwamba walishindwa kutimiza wajibu.
Mzazi anapaswa kujua kuwa suala sio kuzaa na kumleta mtoto duniani – hapana. Kilicho muhimu ni kuhakikisha kuwa mtoto, mapema kabisa, anasimamiwa ipasavyo ili aweze kuwa na maarifa na taarifa zote muhimu kumfanya awe kijana anayejitambua, kufanya mambo kwa usahihi na kuyamudu vyema mazingira yake. Asipofanya jukumu lake hili ajue atalaumiwa, ataaibika na atazodolewa!
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530








