
Katika hali ya kawaida kijana anapoanza kujitegemea, baada ya muda fulani angependa kuwa na mwenza (mke/mume). Sasa, wataalam wa Saikolojia wanasema vijana wengi huingia katika mahusiano, hadi ndoa, kwa kusikiliza zaidi hisia tu! Ni hisia zinazochochewa na mvuto wa nje, kwa msichana/mvulana, unaoitwa ‘romantic love’.
Wanasema ‘romantic love’ huzaa mshikamano mkubwa sana mwanzo, lakini baada ya muda, vile vitu vilivyokuwa sababu ya ‘stimu’ huanza kuonekana vya kawaida; na hapo ndipo mshikamano huanza kulegea. Wawili hawa huanza kugundua kuwa kuna mambo mengi ya msingi hawaivi. Kile ulichokuwa unavutiwa nacho kikiondoka, mapenzi nayo huondoka, na hapo ndipo mivutano na migogoro huanza kumea.
Yakitokea haya, mahusiano ya ndoa huanza kumomonyoka na mapenzi hugeuka kuwa ugomvi na mitafaruku isiyoisha. Katika mazingira haya, siyo rahisi mipango ya maana kufanywa. Nani hapa atakuwa na muda wa kujenga mawazo ili kuziona fursa za biashara? Mazingira haya hayawezi kujenga fikra za kuweka akiba wala kuwekeza, kwani matumizi ya ovyo, au ya kukomoana – hutamalaki!
Ukifuatilia, utagundua kuwa wajasiriamali na wafanyakazi (walio na biashara) hulalamikia kushindwa kuendesha vyema biashara zao; kwa kukosa mtaji au msaidizi bora wa usimamizi; wakati mke au mume wake yupo, na pengine hana kazi. Sababu mojawapo ni hiyo hapo juu! Ukiwa na mwenza asiye na upendo wa dhati, weledi wala bidii; sio rahisi kufanikisha malengo yako!
Lakini pia, mahusiano mabaya ya wenza yana nafasi kubwa ya kuwagawa hata watoto; hivyo kuwanyima malezi bora. Watoto hugawanyika; wakawepo watoto baba na wa mama. ‘Mtoto wa mama’ atafuata zaidi maelekezo ya mama, kiasi cha kuweza kukubali hata kumwibia, kutumia pesa ovyo, au kuhujumu miradi ya baba; ili tu kumridhisha mama,..na kinyume chake!
Mwanasaikolojia Rossana Snee anasema mapenzi ya kweli, yanayoleta mahusiano ya kudumu, siyo ‘romantic love’. Ni mapenzi yanayotokana na ‘shared values’; yaani vile vitu vya msingi ambavyo kila mmoja anavikubali na kuviamini kwamba ndivyo vinatengeneza gundi kati yao. Hivi ni vitu vyenye mashiko; ambavyo unaviona kwa mwenzi wako…vinavyokufanya ujisike utakuwa salama na mwenye amani endelevu.
Kwa hiyo, iwapo uchaguzi wa mwenza utaufanya vizuri, kwa kuzingatia ‘shared values’, ndoa hii itajaa heshima, maelewano, na majadiliano; kuwezesha kupanga na kuweka mikakati ya maendeleo ya familia. Na kama ulishakosea kuchagua, ukathamini zaidi ‘fahari ya macho’ – ni vyema umshirikishe Mungu, ili aweke mkono wake; kwani bila maelewano ya kweli, maisha ya ndoa huwa ya mashaka makubwa.
Kwa mujibu wa wanasaikolojia, zifuatazo ni ‘shared values’ ambazo ndizo hasa hutengeneza kiunganishi cha uhakika kati ya mawili wapendanao, waliomua kuishi pamoja:
Kwanza, kuaminiana na kumcha Mungu. Kuaminiana ni jambo muhimu katika maisha ya ndoa. Tunaambiwa kuwa wanandoa wanaoaminiana hawajengi mawazo hasi, au kuchokonoa-chokonoa maneno au matendo ya wenza wao. Mara zote hutazama matendo na maneno ya wenza wao kwa mtazamo chanya wenye lengo la kuboresha mahusiano. Suala la imani ya dini lina maana sana pia. Ni vizuri wapenzi wakawa na imani moja; kwa kuwa tofauti ya imani mara nyingi huishia katika mitafaruku.
Pili, mawasiliano thabiti. Hili ni jambo la msingi sana kwa kuwa ndio hasa huanzisha mahusiano. Kama unatamani furaha endelevu katika mahusiano ya ndoa, basi unapaswa kuhakikisha panakuwepo mawasiano bora kati yenu; tokea mwanzo. Kutokuelewana katika jambo lolote kukitokea, majadiliano ni muhimu; ili kuweka mambo sawa. Mawasiliano thabiti yakiwepo huzaa fikra, mipango na mikakati ya maendeleo; na huondoa mitafaruku.
Tatu, uaminifu. Hiki ni kiunganishi muhimu sana katika mahusiano; kwa sababu bila uaminifu hata neno ‘nakupenda sana mpenzi wangu’ hukosa maana, au huonekana ni unafiki! Kama wewe na mwenza wako mmejijengea uaminifu wa kutosha, na kila mmoja anamwamini mwenzake; basi kiwango cha mshikamano huwa cha hali ya juu; na hulifanya penzi kuwa lenye uhakika, na furaha endelevu.
Nne, nidhamu binafsi. Huu ni uwezo wa kujipanga vizuri na kudhibiti tabia au matendo binafsi. Kwa mfano, unaweza kujizoeza kuamka saa 11 asubuhi, ukafanya mazoezi, ukasali, ukaoga… na kisha ukaanza shughuli zako za kazi mapema. Sasa hebu fikiria utajisikiaje ukiwa na mwenza; amka yake ni saa 2 asubuhi, asiyeweza kufanya usafi, hawezi kupika; akiwa na nja anataka akale mgahawani, asiyependa kujituma…utajisikiaje? Kwa vyovyote baada ya muda, hata akiwa mzuri kama malaika, utamchoka!
Tano, matumizi ya fedha. Katika hili jaribu kujiuliza je, wewe ukipata fedha unapenda kuzitumiaje? Kitu gani ni muhimu sana kwako katika matumizi ya fedha zako? Je, ni uwekezaji katika vitu au shughuli za maendeleo? Je, ni kujiendeleza ki-elimu? Je, ni kujijengea makazi bora? Sasa, hebu mtazame mwenza wako – akiwa na fedha anafanyia nini? Je, unamwona ana mtazamo kama wako, au mwelekeo wake uko zaidi katika matanuzi na ununuzi wa vitu vya anasa? Ukigundua hilo, tambua uwezekano wa mahusiano haya kukwama, huko mbele, ni mkubwa.
Sita, mtindo wa maisha. Moja kati ya gundi muhimu sana katika mahusiano ni staili ya maisha. Kila binaadamu ana hulka yake, na vitu anavyopendela kuwa navyo; au kuvifanya katika maisha yake. Wapo wanaopenda anasa na kujionesha, na wapo wasiotaka makuu. Wapo wanaopenda sifa, na wengine hufanya mambo yao kwa usiri. Wakati wewe unapenda kubana matumizi, kuweka akiba, na kuwekeza – unakuta mwenzio anawaza ‘shopping’ ghali, na kujirusha; karibu kila siku! Hali hii ikitokea, mshikamano huanza kulegea, na ndoa huwa katika hatihati.
Saba, hamu ya kujiendeleza kimaisha. Wapo watu wanawaza muda wote kufanya vitu ili kubadili maisha yao; yawe bora zaidi. Hawa hupenda kujifunza mfululizo, kupanga mipango na mikakati ya maendeleo…na kuweka ratiba za utekelezaji wa mipango hiyo. Sasa, mtu huyu akigundua mwenza wake hana kitu hiki kichwani mwake; yaani yeye mradi anakula, anavaa na kupata mahitaji ya kawaida – basi kwake inatosha; hapa uwezekano wa mahusiano haya kuwa ya furaha huko mbele, ni ndoto.
Nane, utayari wa kuwajibika ki-familia. Ikumbukwe; maisha ya ki-afrika yanabebwa na familia pana (extended family). Moja ya tabia za ki-afrika ni kusaidiana na kubebena, pale inapoonekana ndugu au watoto wa ndugu wanahitaji msaada. Sasa, kama mmoja anatamani kubeba jukumu hili, (la kusaidia, kutembelea au kujali ndugu) – lakini mwenzake haoni haja ya kufanya hivi; uhusiano huu, huko mbele, una nafasi ndogo ya kuwa na afya.
Kwa hiyo basi, ili kutengeneza mahusiano ya kudumu, endelevu na yenye furaha, yatakayoleta ndoa yenye amani, maelewano na maendeleo; ni jambo la maana sana kuchagua mwenza kwa kuangalia ‘shared values’, badala ya kunasa katika mtego wa ‘fahari ya macho’; ambayo huzaa penzi feki, la muda mfupi, na lenye mitafaruku isiyoisha!
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530









