Fanya Hivi Kumjengea Mtoto Uwezo Wa Kufikiri (1)

Kufikiri kunajenga namna ya kuyatazama mambo kwa jicho lenye udadisi.

Habari rafiki,

Kwa mujibu wa Mwandishi nguli, Freddy Macha, yupo Profesa mmoja Mzambia, aliongea katika kongamano moja, akisema: “Waafrika hatufundishwi kufikiri. Tunafundishwa kukariri tu!” Kwa mfano, anasema utakuta usiku kucha mtoto anakariri idadi ya meno ya mbwa au sayari zilizopo angani, akijiandaa kujibu mtihani wa sayansi kesho yake.

Elimu hii, anasema, ina lengo la kutengeneza ‘wasomi’ kwa kazi za kutumwa, na sio kujenga uwezo wa kijana kuwa mchunguzi, mdadisi, mgunduzi au mbunifu. Yaani haimpi kijana uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo.

Kwa kuzingatia hili, mtaalamu wa masuala ya elimu, Brian Oshiro, anasema tukitaka vijana wetu waweze kuhimili vishindo vya dunia hii ya ushindani tunapaswa kuwafundisha kufikiri. Anasema ili tuwafanye wawe wajanja, ambao watakuwa tayari kupokea taarifa, kujenga maarifa, kukamata fursa na kutatua haraka changamoto, ni lazima tuwafundishe kufikiri.

Kufikiri ni shughuli inayofanyika ndani ya ubongo, na kinachozalishwa huitwa fikra. Fikra ni mtazamo anaokuwanao mtu juu ya jambo fulani – ndio maana utasikia mtu anasemwa ana fikra chanya au hasi kuhusu jambo fulani. Kijana akijengewa uwezo wa kufikiri anapewa uwezo wa kuyatazama mambo kwa jicho maalum, lenye udadisi.

Fikra ni kitu kinachotengenezwa ndani ya ubongo au akili ya mtu katika hali isiyoonekana. Kuna vitu (vyanzo vya fikra) ambavyo vikiingizwa ndani ya akili ya binaadamu vinatengeneza fikra zake. Vyanzo vya fikra ni vitu vinavyopatikana katika mazingira au maeneo ambayo kijana anaishi au anapendelea kuwepo.

Kisayansi, kompyuta au simu huonesha video au kucheza muziki uliowekwa humo kabla. Kompyuta inafanya kazi kulingana na program iliyoingizwa. Kioo cha compyuta kina kazi ya kutoa taswira ya kitu kilichoingizwa humo. Ukiweka picha ya utupu, kioo kitaonesha picha hiyo. Ndivyo alivyo binaadamu. Akiwekwa katika mazingira hasi, ataingiza vitu hasi katika akili yake, na baadae ataonesha vitu hivyo kwa jamii.

Aina ya vitu, na namna kijana anavyoingiza vitu hivyo ndani yake, ndivyo uwezo wake wa kufikiri unavyojengwa. Kuna msemo usemao, “limjaalo mtu ndilo limtokalo”. Wapo vijana walioathirika na mazingira au aina ya malezi waliyopewa, wakawa na fikra zisizojenga. Kumbuka binaadamu tunaishi katika jamii yenye watu wa aina tofauti. Hivyo, kupitia maongezi au vitu anavyoviona, mtoto au kijana hujenga msingi mzuri au mbaya wa kufikiri.

Hii ndio sababu wazalishaji wa filamu wana utaratibu wa kuzipanga filamu zao kulingana na maudhui yaliyomo, na umri unaoendana na maudhui hayo. Kwa mfano filamu ya X hairuhusiwi kutazamwa na mtoto chini ya miaka 18. Lengo ni kuzuia vitu ambavyo vikiingia akilini mwake vitamwathiri na kumjengea namna fulani ya kuyatazama mambo, na mwisho vitajenga msingi wa matendo yake.

Kwa maana hiyo ni muhimu vijana wajengewe uwezo wa namna ya kupokea, kufikiri na kuchambua mambo. Wajue mambo yepi yachukuliwe (kupitia kuangaliwa au kusikilizwa) na yepi yaachwe. Wajue yepi ni sahihi na yepi si sahihi, na kwa nini.

Fikra au mtazamo hutengenezwa ndani ya mtoto au kijana toka akiwa katika umri mdogo, nyumbani na shuleni. Tukijikumbusha mtazamo wa Profesa Mzambia hapo juu, kuhusu elimu yetu Waafrika, kuna mazuri yaliyomo katika elimu yetu, ingawa yapo ya kurekebisha.  Kwa mfano kuna aina ya maswali wanayopewa watoto katika mitihani ambayo siyo fikirishi.

Na kwa bahati mbaya maswali haya ndio hupendwa zaidi na watoto. Kwa mfano, swali kama, “taja sababu zinazoleta mabadiliko ya hali ya hewa” sio fikirishi. Mtoto yeyote mwenye uwezo wa kukariri anaweza kulijibu, hivyo halimjengei uwezo wa kufikiri. Ukitaka kumjenga kifikra mtoto usiishie hapo, muulize, “kwa kila sababu uliyotaja eleza kwa vipi sababu hiyo inaathiri mabadiliko hayo”. Swali hili linamtaka mtoto atumie akili zaidi kwa kufanya tafakuri.

Kama nilivyosema, uwezo wa kufikiri kwa mtoto au kijana unapaswa kujengwa kuanzia nyumbani na baadaye shuleni.

Tukianza na nyumbani, mzazi unapaswa uwe makini katika malezi na makuzi ya mtoto wako. Jifunze kumjengea mtoto mazingira ambayo yatamjenga na hayataua uwezo wake wa kufikiri, kuchambua na kuhoji vitu. Ukiweza kumfanya mtoto awe na ujasiri wa kufikiri nje ya mazoea, badala ya kukariri, utamfanya mtoto ajiamini na kuyaamini mawazo yake; na kuna njia kadhaa ambazo mzazi akizitumia zinaweza kumjengea mtoto au kijana uwezo mkubwa wa kufikiri.

Kwa upande wa shule, kuna njia (approach) ambazo zikitumika ipasavyo kila mtoto au kijana atajengeka na kupata uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo. Akijenga tabia ya kuhoji mambo anajenga uwezo wa uthubutu na ubunifu unaomfanya amudu kuzielekeza fikra zake katika kufanyika kwa vitu halisi.

Msomaji wangu, hii ni sehemu ya kwanza ya makala hii. Katika makala ijayo nitakuletea sehemu ya pili, ambapo nitaingia ndani zaidi kufafanua wajibu wa mzazi, na njia ambazo mzazi anapaswa kuzitumia ili kumjenga mtoto au kijana wake ili awe na uwezo mkubwa wa kufikiri.

Katika sehemu hiyo ya pili nitajadili pia wajibu wa shule, hasa mwalimu, na njia wanazopaswa kutumia ili kumsaidia mtoto au kijana kujenga na kukuza uwezo wake wa kufikiri.

Mtoto akijengeka kifikra, akaweza kufikiri kwa mtazamo chanya, anafanywa kuwa na uwezo wa uchunguzi, udadisi, ugunduzi na ubunifu; na uwezo huu unamsaidia kuziona fursa mbalimbali za kimaendeleo zinazoweza kumkomboa kiuchumi na kijamii, lakini pia anapata uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; mobile: 0718219530…

Fanya Haya Unapojiandaa Kustaafu

Kustaafu ni moja ya tunu muhimu katika maisha baada ya ajira

Habari rafiki,

Leo naomba tujadili kitu kiitwacho Kustaafu. Je, nini maana ya kustaaafu? Kwa bahati mbaya neno hili mara nyingi huongelewa na watu walio katika ajira za Serikalini, Mashirika na Makampuni mbalimbali ya Umma na Binafsi. Hutalisikia sana kwa watu waliojiajiri katika Biashara, Kilimo au Ujasiriamali mwingine, na hii ni ajabu kidogo.

Hata hivyo, kuna watu wanaelezea Kustaafu kama kuondoka katika kazi au ajira rasmi baada ya kufikisha umri fulani maalum. Huu ni umri ambao imekubalika kuwa uwezo wa Mtumishi, ki-nguvu na ki-akili, utakuwa umepungua, na inafaa akapumzike. Kwa Tanzania umri wa wengi, wa kustaafu, ni miaka 60 kwa sasa, ingawa zamani ulikuwa miaka 55.

Umri huu hauwekwi tu, hapana.  Kuna vigezo vinatumika na pengine utafiti unafanyika, kutafuta umri muafaka wa kustaafu, ambapo mchango wa Mfanyakazi husika katika kazi huonekana kupungua, hivyo hutakiwa aondoke ili akajishughulishe zaidi na shughuli binafsi ambazo haziumizi sana akili na mwili, akiwa anamalizia miaka yake ya kuishi hapa duniani.

Watu wote walioajiriwa wanajua iko siku watahitajika kustaafu, yaani kuondoka katika kazi waliyoifanya zaidi ya nusu ya maisha yao yote. Katika kipindi cha utumishi mara nyingi Mfanyakazi huwekeza karibu kila kitu kwa Mwajiri: nguvu, akili, muda, ujuzi na maarifa aliyonayo.

Mwajiri pia huhakikisha katika kipindi cha utumishi wa Mfanyakazi huyu amepata manufaa ya juu kutoka kwa Mwajiriwa, ili taasisi au biashara yake ipige hatua, itengeneze faida, na iendelee kuwepo.

Sasa unapokaribia muda wa kustaafu, mara nyingi Waajiriwa huingiwa na hofu, kwa kuwa wanajua wanaenda kuingia katika maisha mapya wasiyoyazoea wala kuyajua vizuri. Walizoea kuwajibika kwa mujibu wa matakwa na miongozo ya mwajiri, sasa hawajui hali itakuwaje baada ya hapo.

Wengi wanajua wana maarifa, ujuzi na uzoefu katika fani zao (ujenzi, udaktari, ualimu, ufundi, uhasibu n.k) lakini wanakuwa hawajui kwa uhakika ni maarifa gani yanahitajika ili kuwawezesha kuingia katika maisha ya kustaafu kwa mguu mzuri, na kuyatendea haki.

Kwa sababu hii, ndio maana baadhi ya Waajiri huwaandaa wastaafu wao kwa kuwapatia mafunzo maalum yenye lengo la kuwapatia maarifa na stadi muhimu za maisha ya kustaafu. Wanaokosa fursa hii huyumba sana baada ya kustaafu, na wengi wao huishia kuchanganyikiwa na kuishi maisha duni uzeeni.

Kama ilivyo katika maisha katika Ajira, kustaafu kwa furaha hupatikana kwa mtu ambaye ameandaliwa na kuwekwa tayari kuzijua na kuwa tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha nje ya Ajira. Sio rahisi kuzijua changamoto zote au namna ya kukabiliana nazo, hata hivyo ni muhimu kujiandaa kabla ya kuianza safari yoyote.

Kumbuka kuna suala la mazoea katika maisha ya Ajira. Mtu amezoea kufanya kazi kwa maelekezo na utaratibu aliowekewa na Mwajiri. Muda wa kazi, kazi inavyofanywa, malipo, likizo n.k, vyote huamriwa na Mwajiri. Sasa muda wa kustaafu ukifika Mstaafu anatakiwa aanzishe maisha yake, na kila kitu kiwe chini ya mipango na usimamizi wake. Jambo hili linahitaji maarifa mapya, mbali ya yale ya kazini.

Zifuatazo ni stadi au maarifa muhimu ya maisha ya kustaafu, na nitazijadili hapa:

Kwanza, jiandae kisaikolojia. Kustaafu ni kipindi tofauti sana ambapo Mstaafu anakutana na mtindo mpya wa maisha tofauti na mazoea. Kuna mazoea kama kwenda kazini kwa muda wa Mwajiri, kulipwa mshahara, kupewa nyumba au gari la ofisi, kutoa amri jambo lifanyike, kwenda likizo ya malipo, kutibiwa na ofisi n.k. Ukijua haya hutayapata baada ya kustaafu, unapaswa kujiandaa kisaikolojia ili siku yakiondoka usibabaike.

Pili, jiandae kustaafu. Kila mwajiriwa anajua atastaafu lini, kwa kuwa umri wa kustaafu unajulikana. Kwa sababu hiyo kila mstaafu anapaswa kujiandaa, ikiwezekana miaka mitano kabla.

Unapostaafu unatakiwa kujua utaenda kuishi wapi. Ni vizuri kuandaa mapema makazi, mahala na nyumba ambamo utaishi ukishastaafu. Ujue utafanya shughuli gani binafsi ya kukupatia kipato, mbali na malipo ya uzeeni, ambayo huwa hayatoshi. Kama bado una wategemezi jiandae namna utakavyolibeba jukumu hili katika kipindi hicho.

Tatu, usiondoke na maarifa au taarifa zote. Unapostaafu unawaacha watu nyuma yako wakifanya  majukumu yako, ili kazi iendelee kama ulipokuwepo. Kwa hiyo, usiondoke ukaacha mazingira mabaya kazini. Acha kitu utakachokumbukwa nacho.

Waachie waliobaki maarifa na taarifa muhimu. Usiondoke na vitu hivyo kichwani, au usiwe mchoyo, watu wanahitaji ujuzi na uzoefu wako. Watu wakikwama kitu wakahitaji msaada wako, wapatie. Hii ni hazina ambayo  italifanya jina lako liendelee kutajwa na kupewa heshima, na itakuletea  amani ya roho katika maisha yako ya kustaafu na kukujengea marafiki.

Nne, jenga matumaini. Wapo watu wanapokaribia kustaafu wanapata hofu. Mara nyingi wanaogopa vitu wasivyovijua. Wanajiuliza maisha nje ya ajira yatakuwaje, watakuwa wanafanya nini, au wataishije. Wanawaza jinsi watakavyopokelewa na wengine huko uraiani. Sasa kinachotakiwa hapa ni kujiamini na kujipa matumaini kwamba kila kitu kitakuwa sawa. Ukiliweza hili utayaanza maisha bila presha.

Tano, tafuta chanzo kipya cha kipato. Ukiwa Mfanyakazi chanzo chako cha mapato ni mshahara kutoka kwa Mwajiri wako. Unapostaafu chanzo hiki kinaondoka. Kimsingi, inatakiwa ukistaafu tu ulipwe mafao yako ya kustaafu. Hili halijakaa vizuri, wengi huchelewa sana kupata mafao yao. Hata hivyo ni muhimu kuwa na wazo au fursa tayari, itakayochukua nafasi ya Ajira, ili itumike kukuingizia kipato kipya.

Hapa ndipo umuhimu wa kujenga uzoefu wa kufanya biashara kabla ya kustaafu unapoonekana. Uzoefu kidogo wa Ujasiriamali ukiwa ndani ya ajira una maana, kwa kuwa unakupa uwezo wa kujenga fikra na kuziona fursa. Kama inawezekana ni vizuri kufikiria fursa zinazoendana na fani uliyomo. Kama wewe ni Mhandisi basi fikiria nini utaanzisha kitakachotumia ujuzi ulionao.

Sita, jichanganye na watu. Unapokaribia kustaafu unatakiwa kujichanganya zaidi na watu wengine (networking). Mzee Reginald Mengi alihimiza sana tabia ya unyenyekevu na kujenga ukaribu kwa watu wote, na kusikiliza maoni yao. Tabia hii humfanya mtu aweze kuwa na mahusiano mazuri na watu wa aina na rika zote, na hii humsaidia sana mtu kuzisikia na kiziona fursa mbalimbali.

Saba, ondoa matumizi yasiyo ya lazima. Mara nyingi watu wakiwa katika ajira hujisahau sana, na hivyo hujitanua na kujitutumua sana katika matumizi. Katika ajira kuna wakati pesa inakuja kwa jinsi isiyotarajiwa; mfano posho za semina, vikao na safari, au ofa kutoka kwa wateja.

Mazingira haya huwapumbaza wengi na kuwafanya wawe na matumizi makubwa kuliko kipato chao halisi (mshahara). Lakini fursa hizi hukoma baada tu ya kupewa barua ya kustaafu. Kama hujajitayarisha ni wazi kuwa utataka matumizi haya yaendelee nje ya ajira, na hii ni hatari. Kwa hiyo unapofikisha umri wa kustaafu utapaswa kurekebisha matumizi kwa kuyaondoa yale yote yasiyo ya lazima, yanayopenda kuitwa matanuzi.

Nane, jifunze maarifa na nidhamu ya usimamizi wa fedha. Baada ya kustaafu watumishi hupewa mafao yao ya kustaafu. Kwa namna fulani huu ni mtaji. Hata hivyo wafanyakazi wengi huwa hawana nidhamu ya fedha. Ndio maana wengi wakipata fedha hizi huishia kujitanua, kwa kuwa hawajui hata mbinu za uwekezaji.

Ili ujijengee kipato endelevu baada ya kustaafu kwa kutumia mtaji huu, yakupasa ujifunze nidhamu ya fedha mapema. Maarifa haya, pamoja na mbinu za Ujasiriamali, yatakupa uwezo wa kuanzisha shughuli ya uwekezaji. Kipato kitakachotokana na uwekezaji katika fursa ulizoziona, ndicho kitakachochukua nafasi ya malipo ya Mwajiri wako, baada ya kustaafu.

Ukiweza kufanya haya machache, na mengine, utafaidi na kunufaika kabisa na maisha ya kustaafu, ambapo tofauti na wengine, utaona kuwa kustaafu ni tunu na jambo la kufurahia badala ya kuogopwa, hivyo anza sasa kufanya haya, utanufaika!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com

Fursa Zina Tabia Ya Kuwaruka Watu Waoga

Ukiondoa hofu jitihada zako zitakulipa

Habari rafiki,

Karibu tena katika mfululizo wa makala zangu zenye lengo la kuelimishana kuhusu masuala ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Katika makala hii nimesisitiza umuhimu wa kuanza…mara tu unapoiona fursa…kwani wengi hukwama hapa, kwa kuanza kusitasita! Nimejikuta narudi kuipitia makala hii ili niunganishe maudhui yake na kitu nilichojifunza hivi karibuni, kinachoonesha wazi kuwa vijana wengi wana mtazamo hasi kuhusu suala la kuchangamkia fursa.

Nimejifunza na kubaini kuwa fursa ikijitokeza, badala ya kuichangamkia, vijana wengi huanza kusitasita, huingiwa na hofu, hujirudisha nyuma na kuipuuzia. Huu ni mtazamo hasi…na ni hatari sana! Hii ni sababu mojawapo kubwa kwa nini vijana wengi huishia kulalamika tu. Nitajadili hapa.

Mwandishi Mika Ayo anaielezea fursa kama mtazamo unaobainisha manufaa ya sasa au baadaye, ambao mtu anaupata baada ya kusikia, kuona au kufikiri jambo au kitu kinachoonesha uwezekano wa jambo au kitu hicho kuleta manufaa hayo kwake au kwa jamii.

Anasema hakuna mahala kokote duniani, ambako hakuna fursa. Ukimsikia mtu anasema sehemu fulani hakuna fursa za kiuchumi au biashara basi ujue mtu huyo hajawa makini. Hawezi kufumbua macho…ili azione hizo fursa, kwani zingine hujileta zenyewe hadi mikononi mwetu, tunashindwa wenyewe kuzikamata!

Kwa kuzingatia mtazamo wa Ayo, naomba sasa tujadili uwezo wa vijana wetu kuziona, kuzikubali na kuzichangamkia fursa zinazojitokeza. Mjadala huu unabebwa na maoni ya Wachangiaji katika mjadala mmoja uliojitokeza katika Mtandao mmoja wa kijamii. Mjadala huu ulinivutia nikaona inafaa maudhui yake yawafikie wengi ili kwa pamoja tujifunze.

Ilianza hivi: Mfanyabiashara mmoja, Tajiri, hapa Tanzania, alifikisha wafuasi (followers) milioni moja katika Mtandao huo, akafurahi sana. Kuonesha furaha yake alitoa ahadi kutoa shilingi milioni moja au zaidi, kwa watu kumi, ambao wangempelekea mawazo bora ya biashara wanayoweza kuyaendeleza wenyewe, wakipatiwa kiasi hicho cha pesa.

Ni wazi kila mtu ameshasikia malalamiko ya vijana kuhusu ajira, hata kufikia hatua ya kuisema vibaya serikali kuhusu suala la mitaji. Utasikia,… “wanasema tujiajiri…sasa sisi tunapata wapi hiyo pesa (mtaji)…hii serikali hovyo kabisa, haitujali!” Sasa, baada ya ujumbe na ahadi ya Tajiri huyu, ndipo nilipoielewa vizuri mitazamo ya vijana wetu kuhusu suala la fursa. Utashangaa!

Mmoja aliandika, “….sisi Watanzania tumelogwa aisee! Hivi unawezaje kuuza wazo lako la biashara kwa shilingi milioni moja? Hivi unajua wazo lako ni mtaji kwa kiasi gani? Hivi unajua wazo lako unaweza kuliandikia ‘proporsal’ na ukaenda benki ukapewa mkopo? Huyu jamaa sio mtu mzuri, hana nia ya kusaidia, ana lake jambo…” Wengi waliunga mkono hoja hii.

Mwingine aliandika, “…wasomi wa Kitanzania msikubali kufanywa fursa za watu wengine. Usikubali kutoa wazo lako kwa mtu mwingine, ukifanya hivyo usije kushangaa kuona wazo lako limetumiwa na mtu huyo kwa kuanzisha biashara yenye brand yake. Huwezi kushindana na Tajiri wewe, utamnufaisha yeye, na wewe utaendelea kubaki maskini…” Huyu pia aliungwa mkono na watu wengi wenye mtazamo kama wake.

Kwa upande mwingine kuna mtu aliandika, “….inahitaji akili kidogo sana kubaini kuwa hii ni zawadi ya Tajiri huyu kwa vijana wenye maono. Wanaobeza fursa hii hawajui wasemalo.”

“Kama lengo la tajiri huyu lingekuwa kupata mawazo ya ziada ya biashara, angewapa jukumu hili watu wake wa idara ya Utafiti na Ubunifu. Siamini kuwa timu yake imeshindwa kazi ya ubunifu hadi itafute mawazo mapya kwa watu wa mitandaoni. Kama una wazo zuri lipeleke lipimwe ili upate mtaji ufanye biashara…”

Mchangiaji mwingine aliandika. “…hata hivyo hakuna jipya chini ya jua. Kila unachowaza leo usifikiri uko peke yako – kuna watu wengine walishakuwa na wazo hilo, na pengine wanalifanyia kazi mahala hapo hapo au pengine, acha watu wajaribu bahati zao. Bora ulitoe, huenda wazo lako litaonekana lina tija, ukapata mtaji…”

Mwingine aliandika, “…kwanza issue kubwa sio wazo, issue ni kulitia wazo hilo katika vitendo. Mtu anaweza kuiba wazo lako akashindwa kulifanya vile ulivyofikiria wewe, hivyo lisiwe na maana kwake. Na kama tatizo ni mtaji utakaa na wazo hilo kichwani hadi lini, bora ulitoe…na kama litachukuliwa na kutumiwa basi isiwe taabu, utapata wazo jingine.

Mchangiaji mwingine aliandika, “…watu wanaogopa bure tu! Hata kama Tajiri huyo atachukua wazo lako, akalifanyia kazi Dar –es-salaam, na wewe mtoa wazo uko Mbeya, utashindwa vipi kulitia wazo lako katika vitendo huko Mbeya?” “

“Na kama ni wazo zuri hivyo, mbona sasa hujalifanyia kazi, unangoja nini? Kama kajitolea kutoa hiyo offer, sidhani kama Tajiri huyu ana nia mbaya, na usichokijua ni kwamba usipolitoa wazo lako nje ili litiwe katika vitendo halina maana yoyote kwako.”

Yupo aliyeandika, “…hata hivyo, benki gani inatoa hela kupitia mpango wa biashara (business plan) ? Mabenki yote hutoa mikopo kwa biashara ambazo tayari zimesimama na ziko katika hatua ya kukua, bila hivyo, kwa wazo peke yake, hupati mkopo ng’o! Mbali na biashara kuwa endelevu usipokuwa na dhamana ya mali (asset) usitarajie kukopeshwa…”

Sasa, ukifuatilia maoni ya wachangiaji hawa utaona yamegawanyika kimtazamo katika makundi mawili. Yapo maoni ya watu wenye mtazamo chanya na wale wenye mtazamo hasi.

Wenye mtazamo hasi wamejawa na woga na ubinafsi. Hawa wanaamini katika kuibiwa mawazo yao na kumfaidisha Tajiri huyo. Ukichunguza, hawa hawana ujasiri na uthubutu, na hivyo hawana sifa ya Ujasiriamali. Sifa moja muhimu ya Mjasiriamali ni kujaribu kufanya kitu ambacho wengi wanasita kufanya (risk), akijua kuwa kuna uwezekano wa kufeli.

Wenye mtazamo chanya ni wale wenye ujasiri na uthubutu. Hawa sio waoga na wanaamini kuwa Tajiri huyu hana nia mbaya, kwani kwa utajiri wake hashindwi kupata mawazo mapya kwa njia nyingine hadi aangukie kwa watu, hasa vijana maskini. Wanaamini pia kuwa kukaa na wazo zuri kichwani haina maana kama wazo hilo halitawekwa wazi ili lifanywe ki-vitendo.

Kwa hiyo, kwa kumalizia, napenda kusisitiza kuwa ni vizuri watu wakajenga utaratibu wa kuwaza chanya na kuondoa woga au ubinafsi. Kuna fursa nyingi hujitokeza kila siku katika maeneo yetu. Wenye mawazo hasi wanaziogopa na kuzipuuza, lakini wenye mawazo chanya huzichangamkia na mara nyingi hufanikiwa na kuboresha maisha yao. Tuache hofu isiyo na maana – la sivyo tutazidi kuzama katika umaskini.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com

Ubunifu – Somo Kutoka Kwa Wasanii Wa Muziki

Muziki ni zaidi ya uwezo wa kuimba…wanamuziki makini hujiongeza kwa kujifunza kupiga vyombo

Habari rafiki,

Kwa muktadha wa ubunifu na ujasiriamali, leo nataka kujadili nafasi ya Wanamuziki wa Tanzania, wale wa zamani, na hawa wa Kizazi Kipya, kuona jinsi na kwa kiasi gani wanafanya ubunifu, na jinsi wanavyoutumia ubunifu kama daraja la mafanikio yao ki-muziki na ki-maisha.

Nimeandika huko nyuma kwamba ubunifu ni matokeo ya kuufikirisha ubongo ili kuibua fursa, au kupata kitu kipya au njia mpya na nzuri zaidi ya kuleta mabadiliko, au kutatua changamoto au tatizo linaloikabili jamii, kazi au biashara. Ubunifu ni pamoja na uwezo wa mtu ‘kujiongeza’ ili kuja na kitu cha ziada kinachoongeza tija zaidi.

Hapa tunaongelea Muziki kama shughuli ya ki-jasiriamali inayotumiwa na Wasanii katika kujiingizia kipato na kuendeshea maisha yao. Sasa, kama Ujasiriamali mwingine, ili Muziki uwe na ubora, uguse hisia za watu na uzalishe kipato, ni lazima ufanywe ki-ubunifu. Ubunifu ukikosekana Muziki unakuwa wa kawaida, usioweza kukonga nyoyo za watu.

Baada ya kufuatilia, kupitia Waandishi, Watangazaji na Wapenzi wa Muziki wa Tanzania, pamoja na kusoma maoni ya Wanamuziki wa ‘Kizazi Kipya’ na ‘Kizazi cha Zamani’, nimegundua, kwa maoni yangu, kuwa suala la ubunifu katika Muziki kwa sasa liko chini sana. Nitafafanua.

Asha Baraka ni mdau mkubwa wa Muziki nchini Tanzania. Akiulizwa na Redio moja sababu za kuporomoka kwa Muziki wa Dansi hivi sasa, anasema, “…ni ukosefu wa ubunifu tu… yaani Wanamuziki wameng’ang’ania kuiga na kurudiarudia mtindo na vionjo vilivyomo kwenye nyimbo zilizovuma zamani, wakishindwa kufikiri na kuja na vionjo vipya vinavyoendana na kizazi cha sasa.”

Mwanamuziki mkongwe Abuu Omary, akimzungumzia Mwanamuziki mwingine maarufu wa zamani, Wilson Peter Kinyonga, wa Bendi ya Simba wa Nyika, kama kielelezo cha ubunifu na kipaji katika Muziki, anasema, “…alikuwa anatumia uwezo mkubwa wa kufikiri na kubuni, ndio maana alitunga nyimbo nyingi zenye vionjo na maudhui ya kuvutia.” 

“Yeye, akijilaza anakuwa kama anaota hivi…akiamka anaanza kuandika utunzi, na bila kuchelewa anatukusanya na kutushirikisha, tunajadili, tunabishana, tunaongeza vionjo, mwisho tunaibuka na muziki safi kabisa, na hii ndio siri ya ubunifu.” Anasema Omary.

Kama Asha Baraka, Mwanamuziki Abuu Omary naye anakosoa tabia ya kuigaiga. Anasema Wanamuziki wetu, hasa wa Kizazi Kipya wanapenda sana kuiga, hasa vitu vya nje. “Vijana wanaiga sana; kuimba, kuvaa, kucheza, na hata maeneo ya kuchezea video zao…wanaiga kila kitu. Hii inasababisha muziki wetu kukosa vionjo vyetu vya Kitanzania, na hii si sawa!”

Omary anasema, “…wanamuziki wetu wanarekodi video zao Afrika ya Kusini au nchi nyingine kama hizo. Kwa nini wanafikiri maghorofa au ma-fly-over ndio kivutio cha muziki? Huku ni kukosa ubunifu, kwani kuna vionjo vingi hapa Tanzania, kwa mfano Mbuga za Wanyama, Mlima Kilimanjaro, Misitu, Maziwa, Mito n.k.”

Anasema kwamba maeneo haya yana mvuto kwa wote, Watanzania na Wageni pia. Kwa kurekodia Muziki hapo, ingesaidia kuufanyia promosheni Muziki wetu Kimataifa, ku-promote rasilimali zetu nje ya nchi, kuisaidia nchi yetu kujitangaza Kimataifa na kutoa mchango katika kukuza Utalii.

Kwa mujibu wa Mtaalamu mmoja wa fani ya muziki, baadhi ya vijana wanaojinasibu kuwa ni Wanamuziki, ki-ukweli sio Wanamuziki, ni waimbaji tu! Wengi wanaweza kuimba tu, wakiwa hawana uwezo wa kutunga mashairi wala kutengeneza melodia (beat). Anasema kuna matatizo sana kwenye ubunifu.

Anatoa mfano wa Mwanamuzikimmoja aliyekuwa ndani ya Tano Bora za Bongo Star Search (BSS) miaka kadhaa nyuma. Anasema, huyu aliweza kutoa ‘ngoma’ moja tu, kali, kisha akapotea! Anasema kuwa chanzo cha hali hii ni ukosefu wa ubunifu.

Anasema utakuta Wanamuziki wa aina hii ni wale ambao wanaweza kuimba lakini hawana uwezo mwingine zaidi. Wengi wao wanaandikiwa mashairi (lyrics), wanayafanyia mazoezi kisha wanaingia studio, wanarekodi. Kipaji chao hawa ni kuimba tu, ndio maana wakifanikiwa kutoa ngoma moja kali – wanapotea, maana hawana uwezo wa kufikiri na kubuni, kama wao!

Mwandishi mmoja anasema wapo pia Wanamuziki ambao wana uwezo mkubwa wa kutunga mashairi (mistari). Ubunifu wao uko katika uandishi wa mashairi tu, na sio kutengeneza ‘beat’ au melodia. Na wale wanaojitahidi kutengeneza melodia, wengi wao hawana uwezo wa kubuni melodia zao – wengi huiga melodia za muziki wa nje, mfano Nigeria. Anasema ingawa kuiga sio vibaya, lakini lazima ubunifu wako uonekane juu ya hicho unachojaribu kuiga.

Mwanamuziki John Kitime anaandika, “…zamani, muziki, ilikuwa lazima ujue kuunda melodia ya wimbo wako. Yaani ukishatunga mashairi yako unabuni na melodia. Kisha, tungo yako na melodia (ukiipiga kwa mdomo), inaletwa mbele ya wenzio, inasikilizwa, inafanyiwa mchakato, inapangiwa sauti na vyombo. Mwisho inafanyiwa mazoezi na kuanza kupigwa hadharani, kui-test. Kulingana na hisia za walaji, inafanyiwa marekebisho na ikionekana ‘inalipa’, inarekodiwa.”

Kitime anasema aina hii ya mchakato wa kutengeneza muziki ulijali sana ubunifu na umakini. Ulizingatia sana nia ya kugusa vionjo vya wapenzi. Muda wa kutosha ulitumika kupata kitu bora – na hii ndio sababu nyimbo hizo zilimudu kukaa sokoni kwa muda mrefu bila kuchuja.

Mwanamuziki Ben pol, alipoulizwa kwa nini Muziki wa sasa unakaa muda mfupi sana kwenye nyoyo za watu, wakati kuna miziki ya zamani inavuma hadi leo, alijibu, “hivi sasa wasanii wanatumia muda mfupi sana kwenye kutengeneza ‘muziki wenyewe’ (audio). Muda mwingi wanauweka mwenye utengenezaji wa video (photo shoot).”

Anasema muda ukiwa mfupi sana kwenye utengenezaji wa audio, muda unapungua katika kufikiri, kujenga mawazo, kubuni hadithi, kuchambua ujumbe na kuainisha vionjo vinavyoweza kugusa hisia za watu. Anasema, “…mimi Ben Pol, nawekeza sana katika kufikiri, nikihimiza ubunifu wa pamoja. Kama kikundi, tunachangia mawazo, tunabishana, tunajadili na mwisho tunapata audio kali.”

Ben pol anasema hata wanaporudia kurekodi nyimbo za zamani (Remix) wanapata muda wa kufikiri. “..Tunachangia mawazo ili kuingiza vionjo vya kisasa katika nyimbo za zamani. Tunaingiza misemo ya kisasa. Juu ya hilo, tunatumia vyombo vya kisasa, vyenye ubora wa juu. Kwa kufanya hivi ‘tunawakuna’ wazee wa zamani, na kugusa hisia za vijana wa sasa. Mfano ni Wimbo wa ‘Nipate Lau Nafasi’, wa Kilwa Jazz, tulioufanyia remix.”

Soma pia: Je, Twaweza Kujifunza Ubunifu Kupitia Wasanii Wa Filamu?

Mwanasiasa January Makamba aliwahi kusema kwamba Muziki wa Kizazi kipya hauna maisha, ni bubble gum. Yaani muziki unatoka, unavuma sana muda mfupi tu kisha unapotea. Alitaja ubunifu mdogo kama chanzo cha hali hii. Aliwahimiza wanamuziki, pamoja na mambo mengine, wajifunze matumizi ya vyombo (ala za muziki), na wasipende kufanya ‘play back’ ili kuongeza thamani ya kazi zao.

Kwa kumalizia, ni kwa kupitia ubunifu, kama nilivyojadili hapo juu, ambapo utaongeza ubora na thamani ya bidhaa, sanaa au huduma yoyote unaoitoa. Na ongezeko hilo la thamani ndilo litakalokuhakikishia ongezeko la mapato na mafanikio makubwa katika shughuli au biashara yako.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Huu Ndio Mchango Wa Unyenyekevu Katika Biashara

Kumbe hata vyombo vya Dola hujishusha kwa Wananchi…wakigundua wameenda nje ya mstari

Habari rafiki,

Kwa mujibu wa Biblia, Yesu Kristu alikuwa na uwezo, akili, hekima na ujuzi usio na kifani. Pamoja na sifa zote hizi, Yesu hakuwahi kujivunia mambo hayo. Pamoja na hadhi yake ya u-Mungu, aliishi maisha ya unyenyekevu, upole na kujali wengine.

Mbali na kuishi maisha ya unyenyekevu, Yesu Kristu aliwahimiza watu wengine waishi hivyo pia, aliposema, “…yeyote atakayejinyenyekeza…kama mtoto huyu (aliyekuwa kando yake)…ndiye atakuwa mkuu zaidi katika Ufalme wa Mbinguni.” [Mat. 18:2-4]. Kwa hiyo, kumbe unyenyekevu huzaa hadhi ya UKUU.

Hata hivyo, Dunia imejaa watu wa aina nyingi; wenye majivuno na kiburi, na wanyenyekevu pia. Rick Warren anauelezea unyenyekevu kama ile hali ya mtu kuacha kujifikiria yeye peke yake. Yaani kunyenyekea ni ile hali ya kujishusha mbele ya wengine kwa kujifanya mdogo.

Watu wenye majivuno huishi kwa kujitutumua, na mara nyingi hupenda kuwanyanyasa wengine. Hawa ni watu wanaojiona bora, na wa maana kuliko wengine, na hupenda kunyenyekewa hata pale wasipostahili. Wapo wanaojivuna kwa sababu ya mali, cheo, sura au rangi ya ngozi zao. Hawa huwaona wengine si kitu kwao, na hivyo hujenga kiburi.

Watu wenye unyenyekevu ni wapole na hutanguliza upendo na heshima kila wanapokutana na wengine. Kwa tabia yao hii, wanyenyekevu huonwa kama watu dhaifu na wasiojiamini. Hii inatokana na tabia yao ya kupenda kufurahia, na hata kusifia, ubora wa wengine. Hawa hujishusha na hawana roho mbaya wala wivu.

Ingawa Yesu Kristu anaelezewa kama kielelezo cha unyenyekevu, yeye hakuwahi kuwa dhaifu, asiyejiamini, mwoga wala mwenye kujipendekeza. Kwa tabia hii, aliheshimika, alisikilizwa na aliwavutia wengi. Kwa hiyo, kumbe ukiwa mnyenyekevu unajenga upendo, heshima na mvuto kwa watu.

Sasa tuje kwenye biashara. Tunajua kuwa biashara ni watu. Biashara ni wateja. Pasipo wateja hakuna biashara. Lakini pia, ili biashara ifanyike kwa ufanisi, kuna wadau wengi wanahusika. Wadau hawa ni pamoja na wateja, wafanyakazi, wagavi (suppliers) na idara au taasisi za umma zinazosimamia biashara.

Mara nyingi mtu anapoanza biashara huwa mpole, na hujishusha kidogo. Wengi hufanya hivi siku za awali tu, kwa sababu ya ugeni wao katika biashara. Biashara ikianza kuchanganya, na mapato kuonekana wazi, furaha na majivuno fulani huingia.

Wakati hakuna ubaya kufurahia mafanikio, kinachogomba ni kwamba usipokuwa makini, furaha ikizidi hujenga kujiamini kupita kiasi na mwisho hujenga majivuno. Majivuno hujenga kiburi kinachokufanya uanze kuwaangalia watu wengine kama wadogo na wasio na maana. Na hapa ndipo mambo huanza kuharibika.

Bila kujali umepata mafanikio au una nguvu kiasi gani katika biashara yako hakuna mtu anayependa kufanya kazi na mtu mwenye majivuno au kiburi, au anayejiona ‘matawi ya juu’, na mwenye kujua kila kitu (mjuaji).

Wakati unahitaji kuwa shupavu na mwenye kujiamini, ili uweze kushawishi biashara yako ifanye vizuri sokoni, na kukuingizia faida zaidi…unyenyekevu ndio sifa inayosaidia kukuzuia usifurahi na kujiamini kupita kiasi, hadi ukajenga kiburi na majivuno.

Ukijitutumua, ukajifanya ‘matawi ya juu’…watu unaofanya nao kazi; wateja, wafanyakazi, wagavi wa bidhaa na wadau wengine wataanza kujenga hisia kuwa hawawezi kukubaliwa, au kuonwa wa maana, na mtu kama wewe, hivyo watakuepuka.

Elewa kuwa wadau wote wa biashara yako wana mchango katika ukuaji wa biashara hiyo. Ukishindwa kutengeneza mahusiano mazuri nao, biashara yako itadorora. Utaweza kujenga mahusiano yenye tija na wadau wako pale tu utakapoonesha unyenyekevu kwao na kuwaonesha kuwa unawajali, kuwaheshimu na kuwaelewa.

Naomba sasa niwajadili baadhi ya wadau wa biashara ambao wanahitaji unyenyekevu wako ili uishi nao vizuri, na ufaidike nao ki-biashara.

Kwanza, wateja. Kupitia internet, wateja sasa hivi wanaelewa bidhaa mbalimbali mapema sana. Wanapokuja kwako usidhani hawajui, ukaanza kujiona wewe ndio mtaalamu zaidi. Hapana. Wasimamizi wa mauzo, wale wajanja…huitumia hali hii kwa faida. Wao huwa wapole na wanyenyekevu!

Wakiona mteja anaeleza jinsi anavyoielewa bidhaa fulani, wao humsikiliza kwa umakini, na kumtupia maswali ya udadisi, ili afunguke zaidi. Hawamkatizi mteja kumweleza wanachokijua wao, hapana, humsikiliza! Kwa kufanya hivi hugundua kwa kina mahitaji yake, na mwisho humpatia kitu hasa mteja anachotaka, na kumwondoa akiwa mwenye furaha.

Pili, wafanyakazi. Mfanyabiashara, kama una wasaidizi, una wajibu wa kuhakikisha wana furaha. Huwezi kuwafanya wawe hivi kama huna unyenyekevu. Hakuna mtu atakayejisikia raha kufanya kazi na bosi jeuri, mwenye kiburi na majivuno. Ukiona wanaendelea kukaa kwako katika mazingira hayo, ya kuwanyanyasa, ujue kuna kitu! Kitafute!

Ukiwa mnyenyekevu wasaidizi wako watapenda kuwa karibu na wewe, kujieleza, kutoa ufafanuzi wa mazuri na mabaya wanayokutana nayo kazini na jinsi ya kuyatatua. Kama kuna mapungufu ya ki-uongozi, mifumo au urasimu usio na tija, watasema. Ukiwasikiliza, ukayafanyia kazi, wewe ni mshindi, na biashara yako itazidi kufanikiwa.

Kwa kumalizia, wafanyabiashara wanyeyekevu hawashindwi kujishusha na kukubali ukweli wa mambo. Wapo tayari kuwaambia wasaidizi wao, wateja au wagavi kuwa wamekosea au hawajui baadhi ya vitu, ili wasaidiwe maarifa. Hawana majivuno wala kibri, na kwa kufanya hivi kuthaminiwa… na biashara zao hupiga hatua kubwa.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com

Hivi, Kwa Nini Maskini Hufanya Mambo Haya? (2)

Kufeli kuna maumivu yake…lakini hupaswi kuogopa… kufeli ni sehemu ya safari ya mafanikio

Habari rafiki,

Hii ni sehemu ya pili ya makala hii inayojadili suala zima la umaskini na dhana ya umaskini wa mtu binafsi. Katika makala iliyopita nimejadili maana ya umaskini na utajiri kwa ujumla, na hatimaye nikaonesha kuwa umaskini au utajiri ni dhana linganifu.

Nikasema kama wewe unajiona unaangukia katika kundi la watu maskini basi jitahidi kusoma makala hiyo, kwani itakusaidia kuanza kuiangalia hali yako ya sasa kwa udadisi, na utajiepusha kufanya yasiyofaa, yanayofanywa sana na maskini, na kuwafanya wazidi kudidimia katika umaskini.

Katika makala iliyopita nimejadili mambo matano yasiyofaa, yanayotakiwa kuachwa. Leo naomba niongeze mengine matano yafuatayo:

Kwanza, maskini hufa na vipaji vyao. Ki-ukweli, ni vigumu kudhibiti (ku-control) kuzaliwa kwako, yaani kama unazaliwa katika utajiri au umaskini. Unajikuta tu uko duniani. Kila mtu huwa na fikra au ndoto fulani, lakini tofauti na matajiri, maskini huzikalia ndoto au vipaji vyao, hawavitii katika matendo.

Ukiwa na wazo zuri ukashindwa kuligeuza ili likuletee manufaa, wazo hilo halina maana. Kama huwezi ku-control kuzaliwa…unaweza ku-control matendo yako, namna unavyotumia muda wako, maarifa, vipaji na nguvu zako.

Kama unafanya bidii kutia katika vitendo ndoto, kipaji, au vitu unavyovipenda… ni suala la muda tu, mafanikio utayaona. Kama una wazo lako, lifanyie kazi, angalia jinsi linavyoleta manufaa, liboreshe, kisha tia bidii, muda, na maarifa yako…matunda utayaona.

Pili, maskini husubiri neema ishuke, iwakomboe. Wapo watu ambao ukiwachunguza utaona wana hamu sana ya mafanikio, lakini hawajui njia ya kupita. Hawa ni watu ambao wanatafuta mafanikio kupitia ‘nguvu maalum’. Wanangojea serikali, wafadhili au Mungu ashuke awaletee mabadiliko.

Hawa ni watu wasiojishughulisha, wakiamini wapo ‘watu’ wengine, mahala fulani, watakaoleta neema. Watu wa aina hii wanapohitaji mafanikio, kazi yao kubwa ni kufunga na kuomba, usiku na mchana, kila siku. Huwaoni wakifanya chochote, wao wanamtegemea Mungu – wakisema, “mpaji ni Mungu”.

Mwandishi mmoja anaandika, “kila mtu ni Meneja wa mafanikio yake. Usitarajie miujiza, kwamba yupo mtu mwingine anayefikiria maisha yako. Maisha yako yanakuhusu wewe mwenyewe. Ni wale tu wanaojibidisha, wasiokata tamaa, na wanaong’ang’ania – ndio hufanikiwa. Usisubiri neema – chukua hatua!”

Tatu, maskini hupenda kuchagua marafiki wasiostahili. Katika maisha unahitaji watu wa kukutia moyo. Wapo watu ambao wako bize wakifikiria kusonga mbele, watu wenye fikra na maono, wanaowaza kufanya vitu vya ajabu, wanaofikiria ‘kupaa juu’ ili wazikamate mbingu.

Maskini wengi hawana maono, na wakiwa nayo hawayafanyii kazi au hawajui wayafungashe vipi ili yawaletee manufaa. Ndio maana inasisitizwa maskini achague rafiki tajiri, mwenye maono na mafanikio.

Mafanikio na mipango yao (matajiri), na jinsi wanavyoyasukuma mambo yao, vitakupatia darasa kubwa, vitakupa hamasa na msukumo, na kukubadilisha uelekeo kifikra na kimatendo – na hii ndio siri ya mafanikio yako. Jifunze mafanikio kupitia kwa waliofanikiwa – anza sasa!

Nne, maskini wanaishi kwa kutegemea bahati. Kuna watu wakijilaza kitandani hujiwa na mawazo ya utajiri, kama ndoto hivi. Wanajisemea, kwa mfano, “laiti ningekuwa tajiri nisingeishi hivi, ningeishi katika ghorofa zuri kabisa.” Huyu mtu, kama hachukui hatua, ataishia kuota tu! Kusubiri bahati itokee ili upate unachotamani ni ujinga.

Wale wanaotaja sana bahati katika shughuli zao ni wale waliojikita zaidi katika imani ya ‘nguvu’ maalum iliyopo kwa ajili ya kuwapigania. Ni wale wanaosali sana bila kufanya chochote, wakimsubiri Mungu atende miujiza. Mafanikio ni kujituma, ni kuwekeza, ni kutia bidii na maarifa. Ukisubiri bahati – utasubiri sana!

Tano, maskini ni waoga wa kufeli. Hii mara nyingi hutokea wakati mtu hata hajaanza kufanya kitu, anaanza kujishtukia. Mawazo ya kufeli huzunguka vichwani mwa watu waoga ambao hujiuliza, “hivi itakuwaje nikifeli, au jambo hili litawezekana kweli?”

Hawa ni watu ambao wamejijengea mawazo hasi vichwani mwao, na hii si sawa. Tunashauriwa kuwa na mtazamo chanya. Yaani tujenge tabia ya kujipa moyo kwa kusema, “ nina hakika nitafaniwa kulifanya jambo hili, kwani uwezo na nia ninayo.”

Tunaambiwa kuwa matajiri wengi wamefanikiwa kwa kuwa na mawazo chanya, hivyo unatakiwa kubadilika, badilika sasa. Acha tabia za kimaskini kwani zitazidi kukudidimiza katika umaskini.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Hivi, Kwa Nini Maskini Hufanya Mambo Haya? (1)

Wapo matajiri ambao wanadai umaskini unatokana na uvivu, je kuna ukweli katika hili?

Habari rafiki,

Kuna dhana mbili muhimu duniani, zinazoongelewa sana; Utajiri na Umaskini. Kwa maana hiyo duniani kuna watu maskini na matajiri. Kuna nchi tajiri na maskini, na kuna familia tajiri na maskini. Vile vile, kuna tabia za kitajiri na tabia za kimaskini.

Tujiulize sasa; umaskini ni nini, na utajiri ni nini? Kuna mitazamo mingi katika kuuelezea umaskini. Umaskini ni ile hali ya mtu kukosa pesa au mali kwa ajili ya kumudu uendeshaji wa maisha yake.

Katika dunia ya sasa watu hununua mahitaji yao kwa kutumia pesa, hivyo wakikosa njia ya kujipatia pesa, wanashindwa kununua vitu hivyo. Kwa mfano mtu akikosa mtaji (pesa) wa kufanyia shughuli (biashara) ya kumwingizia kipato, huyu huhesabiwa kama maskini.

Maana nyingine ya umaskini ni ile hali ya kukosa uwezo wa kutatua matatizo au kumudu mahitaji ya msingi ya binaadamu kama vile chakula, maji salama, tiba, elimu, makazi, mavazi, usafiri na kadhalika, kwa kukosa uwezo wa kuvinunua.

Sasa, kama umaskini ndio huo, basi tuseme kinyume chake ndio utajiri. Kwa hiyo, tajiri ni mtu mwenye uwezo wa pesa na mali kuweza kuyamudu mahitaji  yake ya kibinaadamu na pia uwezo wa kubakiwa na pesa (mtaji) kwa ajili ya kuendelea kutengeneza pesa zaidi.

Hata hivyo yafaa tujiulize kwa kina; hivi tajiri ni mtu gani hasa? Je, ni yule mwenye mabilioni ya shilingi katika akaunti yake? Ni yule mwenye mamilioni au malaki? Ni yule mwenye mashamba au viwanda vikubwa? Au ni yule mwenye nyumba nzuri ya kuishi, gari la kifahari, au anayemiliki ndege ya kutembelea?

Ukichunguza kwa kina, utaona kuwa utajiri au umaskini ni dhana ‘linganifu’. Ukweli, hakuna tafsiri kamili ya utajiri au umaskini, kwa kuwa kuna tafsiri tofauti kulingana na nchi, mtu au mazingira husika. Wapo watu wanajiona matajiri kwao, lakini wakifika mahala pengine wanajiona hawana kitu.

Utajiri au umaskini linganifu ni hali ya nchi, mtu au taasisi kuwa na rasilimali (ikiwa ni pamoja na pesa), au kipato cha chini au juu ukilinganisha na nchi, watu au taasisi nyingine au hali ya wastani inayofahamika. Yaani unapimiwa umaskini au utajiri wako kwa kuwaangalia watu wengine.

Sasa, kwa kuzingatia maelezo haya, naomba ujiulize… hivi wewe ni tajiri au maskini? Ukihisi kuwa wewe unaangukia katika kundi la umaskini, makala hii inakuhusu, kwa kuwa itakupatia njia za kuondoka hapo ulipo, katika jitihada za kuusogelea utajiri.

Lengo la makala hii ni kuelezea mambo ambavyo watu maskini wanafanya ambayo huchochea kudidimia kwao katika umaskini zaidi. Makala hii itakusaidia kuanza kuiangalia hali yako ya sasa kwa udadisi. Itakufanya uanze kujiuliza, unafanya nini sasa, kwa utaratibu gani, ili kujiweka mahala bora.

Najua sio kila mtu ana uwezo wa kujibadilisha tabia, ndio maana tunatoa mafunzo haya, ili tusaidiane. Ukisoma makala hii, ukaielewa, utajiepusha kufanya yasiyofaa, na hivyo utakuwa umejiweka katika mazingira mazuri ya kufanikisha ndoto na malengo yako. Yafuatayo ni mambo ya ovyo yanayofanywa na maskini, yanayotakiwa kuachwa:

Kwanza, maskini wengi hawapendi kutafuta maarifa. Ili upige hatua kimaisha hakikisha hukai bila kujifunza. Mafanikio huenda kwa watu wanaopenda kujifunza. Kuna njia nyingi za kutafuta maarifa kama; kusoma vitabu na magazeti, kusikiliza redio na TV, kutembelea maonesho mbalimbali, au kutazama kimkakati jinsi watu wanavyofanya mambo, na kadhalika.

Pili, maskini wengi hawaheshimu muda. Hebu Kila mtu ajipime kwenye hili. Je  huwa unaamka saa ngapi, na kulala saa ngapi? Inaelezwa kuwa watu waliokwisha fanikiwa kimaisha ndio hao hao huamka mapema zaidi, na kwamba maskini wanapenda sana usingizi! Falsafa ya kuamka mapema inalenga kuongeza masaa ya kufanya kazi.

Usipokuwa na masaa mengi ya kufanya kazi huwezi kutimiza malengo yako kwa wakati. Matajiri kama Elon Musk na Warren Buffett wanasifika kwa kupangilia muda wao. Wanajua saa ya kuamka, saa ya kufanya kila jambo, na saa ya kulala, kila siku. Kinyume chake ni kwamba watu maskini hawajishughulishi na muda. Na hili huzidi kuwadidimiza zaidi.

Tatu, maskini hupoteza muda mwingi katika TV. Kuna mambo mengi ya maana katika TV, sikatai! Kuna vipindi vya TV vinavyotaarifu na kuelimisha kuhusu kilimo, biashara, uchumi n.k. Lakini pia kuna vipindi vingi vya TV vinatupotezea muda tu. Hivi, kujua kuwa Msanii maarufu XYZ ana uhusiano wa ki-mapenzi na msichana ABC, inakuongezea nini katika maisha yako?

Vipindi kama hivi, au mtiririko wa tamthiliya za mapenzi au vita, vinakuongezea tija gani? Vipindi hivi ni vingi sana katika TV zetu, na utakuta mtu kazi yake ni kuhama kutoka stesheni moja kwenda nyingine, kutwa nzima, akitafuta udaku, miziki mipya, au sinema. Kama huangalii TV kwa lengo la kuongeza kitu katika maisha yako, umaskini utakuganda.

Nne, watu maskini hushabikia sana michezo. Michezo ni furaha, ni burudani, wala sikatai! Hata matajiri wakubwa hushabikia timu zao fulani, na huenda kutazama zikicheza. Kinachogomba hapa ni uraibu! Kuna watu ambao, pamoja na umaskini wao, akili zao zote ziko katika ushabiki.

Uraibu huu katika michezo, hasa soka, ni wa hatari. Utakuta mtu ana familia na majukumu mengi ya kufanya, lakini yuko tayari kuacha kazi yake, siku nzima au zaidi, ili ashinde uwanjani kutazama timu yake, au kubishana. Na ikitokea timu yake ikashindwa, hukosa raha, kiasi cha kushindwa kufanya kazi zake, na hii huathiri sana uchumi wake.

Tano, maskini hupenda kutupa lawama kwa wengine. Hawa ni watu ambao hawakubali kuwajibika kwa mapungufu au uzembe wao. Wakishindwa kufanikiwa, wao hutupa lawama kwa wengine kama sababu ya kufeli kwao.

Wataalam wanasema kuwa vipo vitu vilivyo nje ya uwezo wetu katika maisha. Lakini, asilimia tisini ya mafanikio yako inatokana na juhudi na maarifa yako mwenyewe. Inategemea unapanga kufanya nini, na unachukua hatua gani kutimiza malengo yako.

Unataka mafanikio? Basi fanya mambo! Fanya kazi, na tia bidii. Ukifanya mambo ukafeli, usirushe lawama kwa wengine. Watu wakifeli, wamezoea kuilaumu serikali, wazazi, ndugu, washindani, taasisi za fedha n.k. Hii si sawa. Wa kujilaumu ni wewe mwenyewe. Mafanikio yako…yako mabegani mwako.

Matajiri, kama Aliko Dangote, Mnaijeria; wakifeli kufanya kitu, huanza kuchunguza na kujiuliza nini kimetokea, kimetokeaje, kimesababishwa na nini, na nini kifanyike ili kurudisha hali katika mkondo uliokusudiwa. Baada ya hapo matendo hufuata, haraka. Haya ndiyo mambo tunavyopaswa kuyaiga ili kupiga hatua.

Naomba niishie hapa kwa leo. Jiunge nami katika sehemu ya pili ya makala hii itakayojadili mambo mengine zaidi yanayofanywa na maskini, yanayopashwa kuachwa.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Maombi Yasipoambatana Na Matendo Hukosa Mashiko!

Yatupasa kusali kwa imani, huku tukimwomba Mungu abariki kazi za mikono yetu

Habari rafiki,

Leo nina simulizi kutoka kwa rafiki yangu mmoja ambayo ilinivutia nikaona nikushirikishe pia, kwani ina tija katika Ujasiriamali. Anasema, “siku moja nilikwenda katika mgahawa mmoja katika mji fulani. Pamoja na chakula kulikuwa na huduma ya ‘internet’ au ‘WIFI’, iliyotolewa kwa wateja.”

Anasema, “…niliagiza chakula nikala. Baada ya kunawa nilitoa kompyuta yangu ndogo nikaiwasha ili nimalizie kuandika kazi yangu niliyokuwa nimeianza nikiwa kazini kwangu. Nilimwita Mhudumu na kumwomba anitajie ‘neno la siri’ (password) ili niunganishwe na internet yao. Alinijibu, ‘KULA KWANZA’.

“Nilimwambia Mhudumu, tayari nimeshakula, ninahitaji ‘neno la siri’ ili nifanye kazi yangu ndogo katika kompyuta. Mhudumu alinitazama, kisha akaniambia tena, KULA KWANZA! Nilikasirika, lakini ili nisionekane mkorofi nikaagiza kahawa. Mara hii nikaamua kumuuliza Meneja wao, naye akanijibu KULA KWANZA, nikakasirika zaidi!”

“Nikiwa nimekasirika nilichukua kompyuta yangu nikitaka kuondoka zangu, ndipo ghafla macho yangu yakagongana na kibao kilichoandikwa: Kutumia WIFI yetu, ingiza password ‘KULA KWANZA’’. Kijasho kilinitoka kwa aibu na fedheha niliyopata.” Alimaliza simulizi yake.

Simulizi hii ina kitu cha kujifunza, hasa kwa Wajasiriamali, kuhusu maombi, na hasa maombi kwa Mwenyezi Mungu. Ni lazima tufanye maombi kila siku ili Mungu atushushie neema zake, tupate mafanikio kiroho, kimwili na kimaisha.

Hata hivyo, mfano huo hapo juu unatuonesha kuwa kuna wakati tunamwomba Mungu…halafu tunaanza kusubiri majibu wakati tumefumba macho na masikio tusiweze kuona au kubaini kuwa kumbe tayari Mungu keshatupatia majibu.

Kuna wakati Mungu anatuonesha mlango wa kupitia, lakini kwa kuwa tumefumba macho… hatuoni, bali tunaendelea kuomba tena na tena atuoneshe mlango ulipo. Hapa ndipo ‘tunapochemka!’.

Mwandishi Mark Ballenger anaandika, “imani potofu waliyonayo watu wengi kuhusu sala na imani ni kwamba kama una imani, na unasali sana, basi wewe tulia tu au lala kabisa, kwa kuwa una Mungu, na Mungu yupo ili kujibu maombi yako. Ni kana kwamba kukaa bure ndiyo ishara ya imani.”

Anasema, “ukweli ni kwamba Mungu anapokujalia imani ya kuongea naye, yaani kuomba ili akutimizie mahitaji yako, ni Mungu huyohuyo ambaye tayari ameshakupatia akili na nguvu ili uvitumie vipaji hivi kuibadilisha imani yako kuwa matendo.”

Maana ya maneno haya ni kwamba mtu aliye katika mazingira ya kufanya mambo yatokee ki-uhalisia, baada ya Mungu kuweka mkono wake, ni wewe mwenyewe. Kitendo cha kukaa tu, eti unasubiri ‘mtu fulani’ aje akufanyie kazi, ili uliyoyaomba yatokee, ni kukosa busara, na ni kuomkosea Mungu pia!

Baba mmoja, Mkristu, anasema, “…sisi, kama Wakristu, tunafundishwa kusali na kuomba ili tupate neema za Mungu na tutatuliwe matatizo yetu. Hata hivyo, pamoja na kwamba Mungu wetu ni wa maajabu, ukweli ni kwamba maombi yote, sala zote, zinapaswa kukamilishwa na matendo.”

Sala zinataka matendo upande wetu, lakini wengi wanaosali husahau au hupuuza kukamilisha sala zao kwa matendo. Wanaomba sana wapate nafuu ya maisha, wapone magonjwa, na wafanikiwe katika biashara au kazi zao. Wakishamaliza kusali wanajilaza wakisubiri Mungu aingie kazini, ili yeye ndiye afanye matendo! Hii si sawa!

Kwa mfano, kama unatamani kuwa Mjasiriamali mwenye mafanikio, unachopaswa kufanya ni kumtanguliza Mungu, kumwomba kwa bidii, ukimweleza azma yako ya kupata mafanikio. Mungu ana namna zake za kutoa majibu. Atakujibu kwa kukufunulia vitu; uone, usikie au usome vitu ambavyo ukivifuatilia kwa matendo na bidii, azma yako itatimia. Ukivipuuza utakwama.

Mwandishi mmoja ameandika kuhusu namna Wakristu wanavyotumia ‘Maandiko’ kutatua matatizo katika jamii. Anaanza kwa kuuliza, “je umeshawahi kumwona Mbuni akizika kichwa chake mchangani?”

Anasema, kwa kutumia mfano wa Mbuni, wapo Wakristu wanaoyatumia Maandiko kukwepa wajibu wao. Wanafukia kichwa mchangani! Hawa, wanapokuwa na matatizo au matamanio, haraka hukimbilia katika Maandiko, na maombi, wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo peke yake, matatizo yataondoka. Mara nyingi haiwi hivyo!

Anatoa mfano, “katika familia moja ya Wakristu kulikuwa na mgonjwa wa Kansa. Hakuwahi kupelekwa hospitali, kilichokuwa kinafanyika ni maombi tu. Baada ya muda fulani mgonjwa akafariki. Kilichoendelea huku nyuma ni hisia, kuwa Waombaji au Mgonjwa ndiye hakuwa na imani ya kutosha.

Kwa muktadha huu, anahimiza tutumie Maandiko kama chombo cha kutoa ufumbuzi wa matatizo au matamanio. Tumwombe Mungu kwa imani, lakini juu ya imani hii tuweke matendo ili yawe sehemu ya utatuzi, kwani ahadi nyingi za Mungu zinataka MATENDO pia.

Kuna wakati matendo hayo, yanayotakiwa kukamilisha majibu ya Mungu, huwa mepesi tu, na mambo yananyooka. Lakini wakati mwingine matendo hayo huwa magumu, ya muda mrefu, na yenye gharama kubwa. Ukibweteka, ukakosa bidii na uvumilivu, hakuna kitakachotokea. Hapa ndipo watu huanza kutia shaka ya uwepo wa Mungu, na kuanza kutafuta ‘mbadala’.

Kwa kumalizia, kuna msemo unaosema: Usikazane kumwomba Mungu ili akuonesha njia ya kupita, wakati wewe mwenyewe hauko tayari kuinua miguu yako ili uianze safari’. Yatupasa kusali sana – lakini tusisahau kutia matendo juu ya sala zetu kwa kuwa mara nyingi Mungu huwa tayari keshatupatia MAJIBU.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Je, Mafanikio Ni Matokeo Ya Bidii Au Bahati?

Mche huu ukitunzwa kwa bidii na maarifa hunawiri na kukua vyema

Habari rafiki,

Tunapozaliwa huwa hatujui endapo tunazaliwa katika familia tajiri au maskini. Hatujui kama tunazaliwa watoto wa kiume au wa kike, wala hatujui kama tunazaliwa walemavu wa viungo au akili…au tunazaliwa tukiwa wakamilifu. Hatujui pia kama tunazaliwa katika nchi yenye amani au nchi yenye vita, machafuko au majanga ya asili. Tunazaliwa tu!

Bila kujali walivyozaliwa na mazingira waliojikuta wamo, wapo watu katika mazingira hayo hayo wanaofanikiwa kimaisha na wanaofeli na kuishia kuishi maisha duni maisha yao yote. Sasa tujiulize, kuna kitu gani nyuma ya hali hii?

Marehemu Reginald Mengi ni mfano wa watu waliozaliwa katika umaskini lakini wakaja kuishi katika utajiri mkubwa. Katika kitabu chake cha I can, I must, I will, Mzee Mengi anaandika, “…nimezaliwa katika umaskini wa kutupwa. Familia yetu iliishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng’ombe, mbuzi na kuku…”

Katika maisha ya mafanikio kuna vitu viwili ambavyo hujadiliwa sana. Vitu hivi ni bahati na bidii. Inasemekana kuwa kuna watu wanafanikiwa kwa bahati na wengine wanapambana (bidii), ili kufanikiwa. Hebu na sisi tujadili hapa!

Tuchukue mfano mmoja. Unasafiri masaa mengi porini bila chakula na unajikuta una njaa kali. Ghafla unafika chini ya mwembe wenye maembe yaliyokomaa, yakining’inia. Ukiamua kufanya kitu…kuyapiga au kutingisha mti, ni wazi maembe yatadondoka, na utatuliza njaa yako.

Ukiamua kukaa chini ya mwembe, bila kufanya kitu, ukitarajia muujiza utokee, hilo linaweza lisitokee, na ni wazi utashinda na njaa. Hata hivyo, inawezekana ukajilaza tu chini ya mwembe, halafu ghafla ukaja upepo ukadondosha maembe, ukaokota ukala, na usione umuhimu wa bidii. Hii huitwa bahati!

Huu ni mfano wa matokeo ya kutegemea bidii au bahati katika maisha. Kilicho wazi hapa ni kwamba binaadamu hatuna uwezo wa kudhiti bahati. Mwandishi mmoja anasema tunachoweza kudhibiti ni ile nguvu, bidii na maarifa tunayoyatia katika kufanya jambo lifanikiwe.

Mara nyingi tunapowaona watu waliofanikiwa kama Bill Gates na Reginald Mengi tunaishia kusema aah hawa wana bahati bwana, au wamezaliwa katika familia tajiri. Hapana, tuna kitu cha kujifunza kutoka kwao.

Mwandishi huyo anasema, “hata hicho kinachoitwa bahati…mara nyingi huwa upande wa watu waliopania hasa kushinda…watu wanaojituma na kupambana! Hawa ni watu wanaojiuliza…hivi mimi nataka nini hasa katika maisha yangu…na nifanye nini ili nifanikiwe?” Anasema majibu ya maswali haya ndio hujenga msingi wa matendo na msukumo wa ndani.

Reginald Mengi na Bill Gates wamefanana katika mambo mawili hivi. Wote ni matajiri… na wote wametoka familia duni. Lakini je utajiri wao umetokana na nini? Ki-uhalisia watu hawa wamesotea utajiri wao. Wamepitia vikwazo vingi, wamejituma, wamekesha n.k.

Bill Gates anasema, “…sikutoka katika familia yenye uwezo mkubwa…hata hivyo kilichoniinua ni uwezo wangu mkubwa wa kuutumia ubongo, masikio na macho yangu kuona fursa. Nilipouona mlango niliurukia haraka, nikakutana na watu, nikajifunza, nikafanya bidii n.k.”

Mwanasaikolojia mmoja anasema, “wapo watu wanaishi na umaskini mkubwa. Hawa, sio kwamba hawana bahati, hapana; tatizo ni kwamba wamekosa uwezo wa kujaribu au kuthubutu, kama wa Mzee Mengi.” Mengi mwenyewe anakiri kuwa pamoja na kuzaliwa familia maskini, kila siku walipambana na umaskini, bila kuchoka!

Kuhusu bidii na bahati, Mjasiriamali Sam Parr, anayemiliki Hustle Con anasema, “ kila nilivyojituma kufanya mambo ndivyo nilivyopata bahati zaidi. Jinsi nilivyoushughulisha ubongo ndivyo nilivyoziona fursa zaidi. Jinsi nilivyolala muda mfupi ndivyo nilivyotimiza malengo. Jinsi nilivyoweka akiba ndivyo nilivyoongeza mtaji. Jinsi nilivyojifunza ndivyo nilivyofahamu mengi.”

Bila kujali mazingira mtu aliyomo, kinachomtofautisha mmoja na mwingine ni jinsi anavyomudu kuzitumia fursa zinazojitokeza, kwa jinsi na kwa wakati zinapojitokeza.

Mwandishi mmoja anasema Bahati na Bidii ni watoto mapacha. Lakini Bidii ni mkubwa…kazaliwa mapema zaidi ya Bahati. Bahati ni mdogo wa Bidii, na mara zote hujiweka mgongoni mwa Bidii.

Anasema, “Bidii mara zote hushinda bila kujali mazingira. Kama unajituma, unatoka jasho kwa kile unachokipenda, ni wazi utafanikiwa, na kwa upande mwingine watu watakuona una bahati…ingawa wewe ndani yako utakuwa unaiona bidii yako kama sababu.”

“Na kama itatokea bahati haiko upande wako, wewe unayejituma, basi kuna nguvu ya asili ambayo huja kufidia hili. Hii nguvu hukaa upande wako, ikakupa hamasa ya kutokata tamaa, kutia bidii na maarifa zaidi, kuamka mapema na kulala saa mbaya, ili kupambana na ‘balaa’ la kukosa bahati.” Matokeo ya hamasa hii ni mafanikio.

Yuko Mwandishi kaandika, “wapo watu ambao wala hawafanyi jitihada kubwa. Hawana mipango ya maana wala maarifa ya kutosha, lakini kila wanachoanzisha kinafanikiwa tu.” Anasema hawa ni watu wenye bahati ya kipekee, isiyotokana na mapambano!

Hata hivyo anasema bahati ya aina hii ina walakini. Inatokana na kitu kiitwacho ‘ngekewa’. Ni mazingira yasiyotabirika. Mazingira ya aina hii yana hatari mbele yake. Bahati ya aina hii inaweza kupotea saa yoyote bila kutarajiwa. Lakini mafanikio yanayotokana na bidii, hudumu, na hata balaa likitokea sababu yake hufahamika, na hufanyiwa kazi.

Wale wanaotaja sana bahati katika shughuli zao ni wale waliojikita zaidi katika imani ya ‘nguvu’ maalum iliyopo kwa ajili ya kuwapigania katika mipango yao. Wapo waliozama sana katika imani hii ambao muda wao mwingi huutumia kuongea na ‘nguvu’ hii maalum, bila kazi, kiasi cha kuishi katika umaskini mkubwa wa kipato.

Mwandishi mmoja anasema kimsingi unaweza kufanikiwa kwa bahati, wakati fulani, kama mfano wa maembe hapo juu, lakini kiujumla chachu ya mafanikio muda wote ni bidii. Kama unataka kufeli basi wewe endelea kuamini katika bahati.

Hata hivyo kuna wakati mtu anafanya bidii sana, na bado anafeli. Ikitokea hivi tulia…hii ni kwa muda tu! Cha kufanya; tia bidii, jifunze zaidi, wasiliana na watu, fumbua macho, masikio na ubongo zaidi, halafu muombe Mungu…hakika utafanikiwa!

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Kwa Hili – Suala La Ubunifu Katika Biashara Haliepukiki

Biashara sio uchawi, ni suala la ubunifu tu!

Rafiki

Kama ilivyo kawaida siku hizi, mambo na taarifa nyingi zinapatikana katika mitandao ya kijamii. Nikiwa napitapita ndani ya mtandao mmoja nilikutana na bandiko lililowekwa na Mfanyabiashara mmoja maarufu nchini Tanzania.

Kwa muktadha wa makala hii naomba nimuite Jocker. Bwana Jocker aliandika: “Hili ni Pepo, pale mwenzako anapoanzisha biashara, badala ya kumuunga mkono, wewe unaenda kufungua biashara ile ile, mahala palepale na unaanza kugombea wateja wale wale.”

Mfanyabiashara huyu, kabla ya kuingia katika biashara anayofanya sasa, ya kulima mpunga na kuuza mchele, alikuwa Msanii maarufu wa sanaa za vichekesho.

Mimi binafsi, niliposoma bandiko lake nilifadhaika kidogo, kwa kuwa, kwa jinsi ninavyomfahamu na kuufahamu ujasiri, uthubutu na uchakarikaji wake, sikutarajia kusikia akitoa kauli ya aina hiyo, yaani kulalamikia ‘kuingiliwa katika anga zake’.

Nilipoendelea kusoma nilikutana na maoni kadhaa ya wasomaji wengine ambao walikuwa na mshangao kama mimi. Wapo waliomkosoa , wengine walimshambulia kwa ukali, na wengine walimpa ushauri wa nini cha kufanya.

Naijua kidogo historia ya Bwana Jocker, ambae mafanikio yake, kwa kiasi kikubwa yamebebwa na uwezo wake katika usanii, akiwa katika kundi moja maarufu la sanaa za maigizo wakati huo.

Wakati kundi hili linaanzishwa kulikuwa na makundi mengine yaliyokuwa yanatoa burudani hii kupitia Redio na TV. Hata hivyo kundi hili, haraka sana, lilipata umaarufu ambao kwa kiasi kikubwa ulitokana na uwezo mkubwa wa ubunifu wa Wasanii hao.

Kutokana na ubunifu wao, na uwezo wao mkubwa wa kuchekesha, nakumbuka jinsi walivyokuwa na mashabiki wengi. Wengi hawakupenda kupitwa na kipindi chao kilichorushwa kila Alhamisi. Watu walikuwa wanatoka ofisini mapema, na wanafunzi vyuoni walikacha vipindi kwenda kuwatazama wao. Kifupi walipendwa kutokana na ‘bidhaa bora waliyowapatia walaji’.

Akionesha kufadhaishwa na maoni ya Bwana Jocker, mchangiaji mmoja aliandika, “usilalamike kaka, kumbuka wakati mnaanzisha kundi lenu la maigizo, kulikuwa na makundi mengine ya burudani hiyo. Hata hivyo wadau waliwachagua nyie, kwa kuwa mlikuwa bidhaa bora.”

“Kumbuka pia ulipoingia kwenye kilimo cha mpunga umewakuta watu wanafanya kazi hiyo…wanalima mpunga, wanauza mchele sokoni. Bila kujali hilo na wewe ukaingiza bidhaa yako katika soko hio hilo. Uliowakuta hawajawahi kukuona wewe ni Pepo. Sasa unawachukia wakulima wapya kwa nini?”

Mchangiaji mwengine aliandika, “ingekuwa ni hivyo basi, ungekuta sokoni Kariakoo kuna duka moja tu la nguo, au Dar es Salaam kungekuwa na daladala za mmiliki mmoja tu, na kungekuwa na mtandao wa simu mmoja tu Tanzania. Naomba uelewe kuwa ushindani ni jambo muhimu sana maana linasaidia kupunguza bei na kuongeza ubora wa bidhaa na huduma.”

Yupo mchangiaji aliyeandika, “ tunaishi katika dunia ya utandawazi na kinachohitajika ni ubunifu na mipango madhubuti ya kukuza biashara… maana dunia ya sasa ni ya ushindani…na katika ushindani watakaopenya ni wale walio bora katikati ya ushindani uliopo.”

Mwingine aliandika, “ushindani kwenye biashara ndio chachu ya kuleta maboresho katika bidhaa na huduma zako. Unapaswa kufanya vitu vitakavyokutofautisha na washindani wenzio. Jitahidi kujinasua kutoka kwenye ‘ukanda wa faraja’ unaoishi ndani yake, na kujaribu njia mpya za kufanya mambo.”

Ukifuatilia hoja za wachangiaji hawa utagundua kuwa wote wanamkosoa Bwana Jocker kwa kuogopa ushindani uliopo katika biashara yake. Juu ya hili, wanamkosoa kwa kile wanachokiita ‘ukosefu wa ubunifu’.”

Nakubaliana na wachangiaji hawa mia kwa mia. Katika makala hii, niliyoandika siku za nyuma, nimesisitiza kuhusu changamoto za ushindani katika biashara, na kusisitiza pia umuhimu wa kujitofautisha, kama njia ya kupambana na ushindani katika soko.

Nimeandika huwezi kukwepa suala la ushindani katika biashara…kinachotakiwa ni kutafuta mbinu za kuifanya biashara yako vizuri ndani ya ushindani uliopo. Katika makala hiyo nimetoa mbinu kadhaa za kupambana na ushindani, jaribu kuipitia.

Ukiona mwenzio kafungua biashara kama yako, pembeni, huenda amekusoma na kugundua udhaifu wako, kwamba bidhaa au huduma zako ni duni au zina upungufu fulani …na yeye anakuja na mbinu za kuziba pengo hilo ili wateja wapate kitu kinachokosekana kwako. Ukiona hivi, jitafakari!

Hatua ya kuchukua: Ili uwe Mjasiriamali mzuri usiogope ushindani katika biashara maana hauepukiki. Kinachotakiwa ni kujitahidi kujenga fikra bunifu, kila siku, ili kuja na bidhaa au huduma bora zaidi. Usipende kufanya biashara kwa mazoea; yaani kufanya mambo yaleyale kwa utaratibu uleule, kila siku. Hapana. Fungua ubongo, macho, masikio n.k, ujifunze, na hii itakusaidia kujitofautiasha na wengine, na kuushinda ushindani.

Makala hii imeandikwa na Bw.. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo. Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com