
Rafiki,
Kuna watu wanaingia katika ujasirimali, wanaanzisha biashara wanayoipenda, inakuwa kubwa, na inawapatia mafanikio kiuchumi, kwa kuwa tokea mwanzo hawaoni sababu ya kumtumikia mtu mwingine ili awapangie jinsi ya kuendesha maisha yao.
Watu hawa husukumwa kuanzisha biashara zao binafsi wakiongozwa na hamasa ya kutafuta uhuru binafsi kiuchumi.
Wapo watu wengine ambao huvutiwa na mafanikio waliyoyapata Wajasiriamali hawa, na hupata hamu ya kuingia katika biashara wakiwa na fikra kuwa, kumbe ukishaanza biashara, baada ya muda mfupi utafanana na waliofanikiwa.
Mara nyingi watu hawa hupata simulizi kutoka kwa waliofanikiwa, ya kwamba ulipata wazo, anza….na ukishaanza tia juhudi na maarifa…na ukiweza kufanya haya utafanikiwa.
Hadithi hizi mara nyingi hugusia maeneo chanya zaidi, yanayomwacha msimuliwaji akiwa na hisia kuwa kumbe ukishaanza na kutia juhudi basi utafanikiwa kama waliotangulia.
Hata hivyo, wakati ni muhimu kusikia upande chanya wa ujasiriamali, ili upate hamasa ya kuanza, unapaswa pia kujua kuwa kuna upande hasi. Kwa bahati mbaya upande huu huwa hauongelewi sana na Wajasiriamali waliokwisha fanikiwa.
Huu ni upande uliogubikwa na changamoto za milima, mabonde, miiba, visiki na mahangaiko mengine, ikiwa ni pamoja na kufeli.
Ukifuatilia simulizi nyingi kuhusu mafanikio katika biashara utakutana na maelezo mengi mazuri, ya kutia moyo na hamasa. Hili ni jambo zuri kwa kuwa haifai kumpa mtu anayetaka kuingia katika biashara simulizi ambazo zitamkatisha tamaaa na kumfanya aogope, na hivyo asianze.
Naomba sasa leo nikupatie simulizi kidogo kutoka upande wa pili wa sarafu. Huu ni ule upande usiopenda kuongelewa sana lakini ni wa muhimu. Makala hii itakupatia mambo saba yanayowapata Wajasiriamali, kama ifuatavyo:
Moja, msongo wa mawazo. Unapoingia katika biashara kwa umakini hasa, unawekeza rasilimali zote muhimu katika kitu unachofanya; muda, fedha, nguvu na kadhalika. Wapo wanaokopa fedha nyingi na kupiga kazi kisawasawa, bila uzembe, lakini wanafeli vibaya!
Likitokea hili, utamwona mtu kama amechanganyikiwa, kapata uchizi hivi! Msongo mkubwa wa mawazo unamwandama asijue nini afanye ili mambo yarudi katika mkondo wa mafanikio. Mtu akifikia hatua hii ni muhimu akapata washauri wa biashara, ambao humsaidia kutafuta sababu za kufeli, na njia za kurudisha mambo sawa.
Mbili, mafanikio huja taratibu na kwa taabu. Waliofanikiwa, wengi hawakupitia mteremko. Kuna watu wakiwaona waliofanikiwa wanadhani mafanikio hayo yamepatikana mara moja tu, kufumba na kufumbua. Haiko hivyo.
Kukuza biashara hadi kuifanya iweze kutoa manufaa yanayoonekana ni jambo linalohitaji muda wa kutosha wa uwekezaji wa nguvu, juhudi, maarifa na uvumilivu. Utaanza biashara, utakua kiasi fulani, utaanguka, utainuka kwa taabu na utaanza kukua tena hadi kufikia mafanikio.
Tatu, hupata misukosuko ya madeni. Ili kuingiza mtaji katika biashara na kuifanya isimame vizuri Wajasiriamali hulazimika kukopa. Mikopo hupatikana katika mabenki na taasisi za fedha. Mikopo hii huja na masharti kadhaa ikiwa ni pamoja na riba.
Mzunguko wa biashara huathiri sana uwezo wa mfanyabiashara kulipa mkopo. Hali hii ikitokea na gharama za uendeshaji biashara zikawa kubwa, uwezo wa kulipa madeni hupungua na jambo hili hugeuka kuwa mzigo na kero kubwa ambayo watu wasiohusika hawawezi kuibaini.
Nne, hukumbana na changamoto za kodi na tozo. Kodi na tozo za serikali ni wajibu zilipwe bila kukosa. Malipo haya hutoka katika mapato ya biashara husika. Sasa inapotokea mzunguko wa biashara ukawa mdogo na gharama za uendeshaji zikawa kubwa; au biashara ikikumbwa na majanga kama bidhaa kuharibika, suala la kodi na tozo huwa lipo palepale. Jambo hili husababisha maumivu makubwa kwa Mjasiriamali.
Tano, muda wa kufurahia maisha hupungua. Kimaumbile, watu hupenda kufurahia maisha. Hupenda ‘kujirusha’! Hupenda wakutane na marafiki zao waongee, wale na kunywa pamoja huku wakicheza muziki n.k. Yote haya ni mema.
Hata hivyo, ili upate kufanikiwa kibiashara unapaswa uwekeze muda wa kutosha. Ukijikita kikamilifu katika kazi mara nyingi unakosa muda wa kufurahia maisha, au kujirusha. Utalazimika kuamka mapema na kuchelewa kulala, lakini hata muda wa kupumzika mchana au siku za mwisho wa juma huwa mdogo.
Hili huwasononesha wengi ambao hulazimika kuvumila wakiwa na imani kuwa baada ya mambo kukaa vizuri muda wa kujirusha utafika.
Sita, afya zao huzorota. Ukiwa umebanwa sana na kazi utajikuta muda mwingi unakimbizana na majukumu yaliyopangwa au yanayotokea ghafla ili kutimiza mipango iliyopo. Kwa kufanya haya, wengi hukosa muda wa kupumzika, kwani hulala masaa machache na kusafiri sana.
Mara nyingi pia hula chakula kisichopangiliwa au kupikwa vizuri na hawali kwa muda unaotakiwa. Mazingira haya huzorotesha sana afya zao na kusababisha madhara ya mwili endapo tahadhali haikuchukuliwa.
Saba, mahusiano na jamii huzorota. Ili wafanikishe malengo yao Wafanyabiashara kutwa nzima hukimbizana na fursa au jinsi ya kutatua changamoto.
Fursa au changamoto ikitokea Mjasiriamali husahau kuwa kuna watu wanamhitaji yeye pia; watoto, mke, ndugu, rafiki n.k, wapo na wangependa kupata ushauri, msaada n.k. Inapotokea mtu huyu muda wote unatumika kusaka pesa ni wazi atakosa muda wa kufuatilia mambo ya kijamii na kifamilia, na hili ni jambo linalomuumiza yeye na jamii pia.
Kwa hiyo basi msomaji wangu, usione mtu kafanikiwa ukawa na mtazamo mmoja. Ni vizuri kufuatilia nyuma ya pazia kujua yale mengine ambayo mara nyingi huwa hayazungumzwi. Ni muhimu kuyajua haya ili kujiandaa kisaikolojia au kuweka mikakati maalum ya kupunguza athari zake.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.
Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com








