Watu Wengi Hawana Stadi Muhimu Za Maisha (1)

Kutafakari ni njia mojawapo muhimu ya kuijengea uwezo akili

Habari rafiki,

Ukifanya uchunguzi leo, utagundua kuna watu wazima wengi walioelimika vizuri ingawa wapo pia wasio na elimu ya kutosha. Wapo wengi wenye elimu ya Chuo Kikuu ingawa wapo wasio na elimu hii lakini wana ujuzi mkubwa katika fani zao, kwa mfano mafundi, wasanii na hata wanamichezo.

Pamoja na elimu na ujuzi walionao watu hawa ukweli ni kwamba wengi wao bado wana upungufu. Wengi wanapungukiwa stadi muhimu za maisha, na upungufu huu una madhara makubwa katika maisha yao na ya jamii.

Kwa mfano siyo jambo la ajabu leo kumwona mtu mzima anahangaika kupata jawabu la hesabu ndogo tu ambayo ungetarajia aifanye kwa kichwa. Hesabu kama 42 gawanya kwa 7 kimsingi ni hesabu ya kichwa, lakini utamsikia mtu akiomba simu au kikokotoo ili apate jawabu.

Maarifa ya kumudu kufanya hesabu hii ni yale yanayopatikana katika ngazi ya shule ya msingi. Sasa tujiulize je, tatizo ni mfumo wetu wa elimu hauwapi wahitimu maarifa ya kutosha….au tuilaumu teknolojia… au tujilaumu sisi wenyewe kwa kupuuzia vitu muhimu kama hivi?

Kiukweli kuna mambo ambayo mwalimu au mfumo wa elimu unaweza kulaumiwa. Hata hivyo kimsingi jukumu kubwa la mwalimu ni kumpatia mwanafunzi maarifa ya msingi, na mbinu za kujifunza…baada ya hapo linabaki jukumu la mtu binafsi nje ya darasa kusaka maarifa ili kupambana na mazingira yake.

Mtu anapokosa stadi muhimu za maisha hujikuta amejiweka katika wakati mgumu ikiwa ni pamoja na kuzikosa fursa za mafanikio, kuingia matatani au kujidhalilisha mbele ya jamii.

Kwa muktadha huu inasisitizwa kuwa watu wajifunze stadi za maisha ili waboreshe maisha, wapambane vizuri na changamoto na wayamudu vizuri mazingira yao.

Zifuatazo ni stadi za maisha ambazo watu wengi hawana na wanapungukiwa mambo mengi kwa kutokuwa nazo, hivyo wanahimizwa kujifunza.

Leo nitaanza na stadi moja ambayo ni uwezo wa kutumia akili ya kuzaliwa – halafu katika makala zijazo nitajadili stadi nyingine. Akili ya kuzaliwa hujionesha kupitia maneno au matendo ya mtu. Haya ni maarifa ambao mara nyingi watu hawafundishwi.

Ili mtu aonekane anatumia vyema akili yake ya kuzaliwa inampasa mtu huyu kujijengea umakini wa kutosha kwa kila anachofanya ili kilete matokeo chanya au kisilete madhara kwake na kwa wengine.

Kwa mfano upo jikoni unakaanga vipande vya nyama kwenye kikaangio, juu ya jiko. Akili ya kawaida inapaswa kukuongoza kuwa unapotaka kutoka jikoni ama uipue mboga au upunguze au uzime moto, la sivyo unaweza kuunguza kila kitu ikawa balaa.

Vilevile hatutarajii mtu makini akatize barabara kubwa, yenye wingi wa magari, huku anaandika au kusoma meseji kwa simu yake. Ukosefu wa umakini unanikumbusha maafa ya kutisha yaliyotokea Arusha siku za nyuma.

Mama mmoja alipaki gari lake juani, pembeni kidogo mwa duka kubwa la bidhaa za matumizi ya nyumbani, Supermarket. Alikuwa na watoto wadogo watatu ndani ya gari. Kabla ya kushuka alipandisha vioo vyote vya gari na kufunga milango kwa loki akiwaacha watoto wale ndani ya gari.

Aliingia dukani na kuanza manunuzi ambayo yalimchukua muda mrefu. Alipotoka nje alikuta umati wa watu wamezingira gari lake wakitaka kulivunja ili wawaokoe watoto waliokuwa wakihangaika kwa joto na kukosa hewa. Alipofungua milango alikuta tayari watoto wako hoi na baadaye walifariki.

Hatua ya kuchukua: Akili ya kuzaliwa ni uwezo wa kujiongeza na kufikiri kwa haraka, kwa kina na umakini mkubwa kila unachotaka kufanya au kusema ili kilete matokeo mazuri au kisikutie katika matatizo.

Kwa mtazamo huo, mtu mzima hahitaji kukumbushwa kuacha kuongea na simu wakati anaendesha gari kwani balaa lolote linaweza kumtokea bila kutarajia. Yupo mtaalam mmoja wa falsafa aliwahi kusema, “akili ya kuzaliwa ni bora kuliko akili ya darasani.”

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Jinsi Ya Kutengeneza Ajira Kupitia Ubunifu

Vijana wakipewa mazingira stahiki wana uwezo wa kufanya maajabu katika ubunifu

Habari rafiki,

Wakati Tanzania ikijielekeza kwenye uchumi wa viwanda, vijana wakitumiwa vizuri wana uwezo wa kuipeleka nchi pazuri.

Ukweli uliopo ni kwamba vijana wengi wanaomaliza shule au vyuo hawapati ajira, kwa kuwa hazipo za kutosha, hivyo wengi wanabaki mtaani wamenasa. Ili kuwanasua, mkakati maalum unatakiwa kuwepo..

Lengo kuu la makala hii ni kuwafumbua macho vijana wenye mawazo au hamu ya kufanya mambo makubwa kupitia ubunifu, waione njia.

Ki-ukweli wapo vijana wenye vipaji au mawazo bunifu lakini hawajui pa kuanzia ili kukuza bunifu zao ziwasaidie. Hivyo uwezo wao unabaki vichwani mwao tu. Makala hii itawapatia njia rahisi ya kupita.

Akizungumza katika Wiki  ya Ubunifu, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk. H. Msinda anasema vijana wabunifu wanatakiwa kushikwa mkono, na hii ni kazi mojawapo ya Costech.

Kulifanya hili ki-vitendo Dk. Msinda anasema Costech kila mwaka inazalisha vijana wengi wenye ubunifu kupitia Tehama, hivyo wanajengewa uwezo wa kuchangia katika uchumi wa viwanda kwa kutumia teknolojia.

Anasema vijana nchini Tanzania wanaelewa vyema changamoto zinazowakabili watu katika jamii zao; hivyo wanapaswa kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto hizi, ndio maana wanatakiwa kulelewa kuwa wabunifu.

“Vijana wabunifu wakipata fursa ya kubadilishana uzoefu na wenzao katika sekta za afya, elimu, maji, usafi wa mazingira n.k., kwa kuangalia changamoto zinazozikabili sekta hizo, wanaweza kuzipatia ufumbuzi,” anasema.

Kwa kuliona hili, Costech imekuwa mstari wa mbele katika kuwatambua na kuwakusanya vijana wenye mawazo bunifu na kuwaandalia mafunzo ili kuwajengea uwezo na kuwanufaisha kiuchumi.

Kwa upande wa Tehama, Costech kupitia atamizi (incubators) kama BUNI na DTBi, imeweza kuwasaidia vijana wabunifu kufanya bunifu zao kutoka kwenye hatua ya wazo hadi kwenye hatua ya bidhaa halisi.

Kupitia Costech wapo vijana ambao wameweza kufanya bunifu zao kuwa zenye manufaa kwa jamii na kwao binafsi, kwa kuwapatia ajira zenye kipato.

Kwa  mujibu wa Dk. Amos Nungu, Kaimu Mkurugenzi wa Costech, jukumu kubwa la Costech ni kuratibu na kuendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu nchini Tanzania.

Kwa upande wa teknolojia na ubunifu, walengwa wake wakuu ni vijana wenye mawazo bunifu ambao huchukua matokeo ya sayansi na kuyaingiza katika ubunifu.

Lulu Amir ni mmoja wa vijana walionufaika kupitia fursa ya Costech. Lulu anasema, “Costech kupitia atamizi ya BUNI na DTBi, wanatoa msaada wa mafunzo na ushauri (mentorship).”

Kwa mujibu wa Lulu, wakikupokea wanasikiliza wazo lako na kutoa ushauri. Wanakusaidia kuliboresha wazo lako ili lieleweke bayana. Wanabainisha pia kama wazo linahusu bidhaa au huduma, na kama linaweza kuzalisha fedha.

Wanachunguza kuanzia changamoto uliyoiona katika jamii hadi utatuzi wake. Wazo likionekana linatekelezeka mbunifu anaingizwa kwenye atamizi ambako anakaa kwa miaka mitatu kuliendeleza.

Akiwa ndani ya atamizi kijana mbunifu anasaidiwa kulifanya wazo lake liwe halisi kiteknolojia. Bidhaa ikiwa tayari anafundishwa mbinu za kibiashara pamoja na namna bidhaa yake itakavyoingia sokoni.

Mfano hai wa ubunifu uliosimamiwa na Costech ni utengenezaji wa mbolea ya asili (organic fertilizer) uliofanywa na vijana wabunifu ambao hatimaye walifungua kampuni ya Guavay.

Akihojiwa katika kipindi kimoja cha Tv, Latifa Mafumbi ambaye ni mtafiti katika kampuni hii anasema wanafanya uzalishaji wa mbolea ya asili kutokana na takataka za majumbani na viwandani.

Kupitia atamizi, kampuni imeweza kutumia Tehama kubuni formula ya kutengeneza mbolea asilia ambayo inatumia sehemu kubwa ya takataka zilizooza na malighafi nyingine za mabaki ya mazao na mimea.

Je, wazo la kuzalisha mbolea asilia walilipataje? “Tuliona kiwango kikubwa cha takataka kinachozalishwa sehemu nyingi hapa Dar-es-salaam, na kugundua jinsi madampo yanavyozidiwa na wingi huu wa takataka.” Anasema Latifa.

“Tuliona jinsi takataka hizi zinavyosababisha jiji kuwa chafu na hivyo kuwa chanzo cha magonjwa hasa kwa watoto wanaocheza katika maeneo hayo. Kwa hiyo tuliugeuza uchafu huu kuwa fursa.”

“Upande wa pili wa wazo letu tuliangalia kilimo na changamoto zinazowakabili wakulima. Ardhi kubwa katika Tanzania imechoka kutokana na matumizi mabaya, hivyo haina rutuba ya kutosha.”

Hivyo Latifa na wenzake waliona watumie changamoto hizi mbili zinazoikabili jamii kama fursa ili waje na ubunifu utakaozitatua wakati huohuo wakijitengenezea fedha.

Wakiwa na wazo lao tayari, Costech wakishirikiana na DTBi walitangaza shindano kutafuta watu wanaoweza kutengeneza program za Tehama ili kusaidia kutatua matatizo ya jamii.

“Tulishiriki, tukaweza kuchaguliwa na kisha tukawekwa chini ya usimamizi wa DTBi hadi tukafanikisha ubunifu wetu uliotupatia bidhaa yenye tija kwa jamii na kipato kwetu.” Alisema Latifa.

Kwa hiyo, makala hii inakusudia kuwaamsha vijana kwanza waanze kuwaza kiubunifu kwa kuiga mfano hapo juu.

Pili vijana wachangamkie fursa zinazotolewa na taasisi mbalimbali, kama Costech, ili wapate fursa ya kushikwa mkono katika kugeuza mawazo yao kuwa bidhaa au huduma kwa jamii…na kipato kwa wao wenyewe.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Wabunifu Waliofanikiwa Ni Wale Wenye Maarifa Haya

Kudadisi na kuuliza maswali ni njia muhimu sana ya kupata maarifa ya kufanya ubunifu

Habari,

Imani kubwa waliyonayo watu kuhusu ubunifu ni kwamba ubunifu ni kipaji anachozaliwa nacho mtu. Labda kuna ukweli fulani katika hili. Hata hivyo, kiuhalisia ubunifu ni fani ambayo kila mtu anaweza kufundishwa.

Ukimchunguza mtoto wakati akicheza peke yake au na wenzake, utagundua watoto wana vipaji vikubwa. Hii inatupatia picha kuwa watu wengi wanazaliwa wakiwa na uwezo wa ubunifu.

Tatizo linajitokeza katika umri mkubwa ambapo uwezo wa watu kufanya ubunifu unapungua. Mtaalam mmoja anaielezea hali hii kama tabia ya kukosa ubunifu ambayo watu hujifunza pia.

Mtaalam huyu anasema watu hujifunza tabia ya kukosa ubunifu kutoka kwa wazazi, walezi au walimu mashuleni, jinsi wanavyoendelea kukua.

Tabia ya wazazi au walimu kutoa maelekezo na kuwapangia watoto au vijana nini cha kufanya hutoa mafunzo, ambayo huua ubunifu.

Kuna misuli ndani ya ubongo inaitwa ‘misuli ya ubunifu’, ambayo inatakiwa ijengwe iweze kuwa imara na yenye afya ili mtu awe na uwezo mkubwa wa ubunifu.

Misuli ya ubunifu isipotumika ipasavyo hasa katika umri mdogo inajenga ugoigoi na uzembe. Yaani inabweteka isiweze kufanya kazi yake.

Kwa mfano, kama mtoto anaelekezwa kila kitu, au kila anachotaka kufanya anakatazwa, kutishwa au kufokewa, anajenga woga na kufanya misuli ya ubunifu kusinyaa.

Ubunifu ni matokeo ya kuufikirisha ubongo ili kupata njia mpya na nzuri zaidi za kuleta mabadiliko, kutatua changamoto au kuondoa tatizo lililojitokeza katika biashara, kazi au jamii.

Sasa, ili kujenga uwezo mkubwa wa ubunifu kuna maarifa ambayo wabunifu wengi wakubwa wanayo. Ni muhimu kila mtu anayetamani kuwa mbunifu ajifunze kuwa na maarifa haya ili yamsaidie.

Moja, maarifa ya kuunganisha vitu. Maarifa haya humpa mtu uwezo wa kuunganisha mawazo, vitu au mambo yasiyofanana au kuhusiana, kutoka katika fani, eneo au watu tofauti, ili kupata kitu kipya chenye thamani.

Watu wengi tunaowahusudu kwa ubunifu wao ni wale wenye uwezo wa kuunganisha mawazo yao na ya wengine ili kuunda vitu vipya.

Mbili, maaarifa ya kuuliza maswali. Huu ni uwezo au mazoea ya kuuliza maswali magumu ambayo yanafikirisha na kuvunja kuta za mazoea.

Moja kati ya mambo muhimu mfanyabiashara unatakiwa kufanya ni kuuliza maswali. Suala sio wingi wa maswali – bali ubora wake, yaani maswali yenye tija.

Kwa mfano kuhoji, “kwa nini jambo fulani linafanyika kwa mtindo huu?”, au “kwa nini jambo hili lisingefanyika kwa mtindo huu?”… ni njia bora ya kujenga misuli ya ubunifu ndani ya ubongo. Ni maswali fikirishi.

Tatu, uwezo wa kutazama kuidadisi. Huu ni uwezo wa kudadisi kila unachokiona. Ni uwezo wa kuhoji tabia za watu, mifumo au michakato ili kugundua ubora au udhaifu wake.

Udadisi ni uwezo wa kuchunguza ili kuona nini kinatokea, changamoto zilizopo, namna mambo yanavyofanyika na mahusiano yaliyopo baina ya vitu au watu, kwa mitazamo mbalimbali.

Nne, uwezo wa kufanya majaribio. Huu ni uthubutu wa kufanya majaribio ili kuona uwezekano wa kufanyika kwa vitu vipya vyenye ubora na thamani zaidi.

Kuwa mahiri katika ubunifu kunatokana na uwezo wa kukubali kujaribu vitu bila kujali uwezekano wa kufeli. Kampuni ya Amazon imepiga hatua kiubunifu kwa kuwa wafanyakazi wake wanahimizwa kuvunja mazoea kwa kujaribu kila kitu.

Tano, uwezo wa kujenga mtandao. Kuwa na mahusiano na watu muhimu wenye fikra, fani, ujuzi na uzoefu mbalimbali kunasaidia kujenga mitazamo tofauti au namna mpya ya kuyatazama mambo.

Ni muhimu sana kila mfanyabiashara au mjasiriamali ajenge tabia ya ubunifu kwa sababu bila hivyo itakuwa vigumu sana kukabiliana na ushindani uliopo na ujao.

Maarifa haya yanakupatia mbinu za kujenga na kuimarisha misuli ya ubunifu ndani ya ubongo 

Ukiyatia maarifa haya katika vitendo, kila siku, utazidi kujijengea uwezo wa ubunifu utakaokuwezesha kufanya mambo ki-utofauti na kuiongezea thamani biashara yako.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Ukizingatia Vitu Hivi Vinne (4) Biashara Yako Itapaa!

Furaha ya huyu dada haitokani tu na vitu alivyovaa, bali thamani aliyojiongezea

Habari

Kwa wale waliokwisha thubutu na tayari wamo katika biashara watakubaliana na mimi kuwa kuendesha biashara siyo kazi rahisi. Kuna changamoto nyingi ambazo unapaswa kukabiliana nazo.

Kutokana na changamoto hizi zipo biashara zinazofanikiwa na zipo zinazofeli. Kuna takwimu zinaonesha kuwa kati ya biashara tatu zinazoanzishwa, biashara moja hufa ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Tunaambiwa pia kuwa hata biashara zenye majina makubwa duniani, muda wake wa kuishi umepungua kutoka miaka 75 hadi miaka 15 tu! Kwa hiyo biashara zote zinakabiliwa na changamoto.

Hata hivyo zipo biashara kadhaa ambazo zina mwenendo ulio tofauti. Kampuni ya P&G ya Marekani, inayotengeneza na kuuza vifaa vya matumizi ya nyumbani, ni mfano mmoja.

Kampuni hii ilianzishwa mwaka 1837 na ipo hadi sasa, pamoja na misukosuko na mabadiliko mengi ya kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia yanayotokea duniani.

Sasa, kwa nini biashara fulani zinayumba hadi kufa wakati zingine, kama P&G zinazidi kuchanja mbuga? Iko sababu moja ya msingi kabisa!

Ili biashara ijiweke katika nafasi nzuri ya mafanikio haina budi kuja na majawabu kwa maswali muhimu yanayohusu thamani ya bidhaa na huduma inayotolewa.

Hii inahusisha jinsi thamani inavyotengenezwa, jinsi inavyotolewa, jinsi Kampuni inavyogeuza thamani kuwa fedha, na jinsi thamani inavyoboreshwa. Naomba nitoe ufafanuzi kama ifuatavyo:

Moja, jinsi thamani inavyotengenezwa. Profesa Clayton Christensen, wa Chuo Kikuu cha Havard, amenukuliwa akisema kuwa makampuni yanaundwa ili kuzalisha thamani.

Kwa mujibu wa Profesa huyo, kila biashara inayoanzishwa inapaswa ilenge katika kutatua matatizo au changamoto zinazowasumbua watu, na kuzipatia majawabu.

Watu wanahitaji majawabu ya changamoto zao bila kujali ni bidhaa gani imehusika katika kutoa utatuzi au majawabu hayo. Watu wanahitaji kuona thamani iliyotolewa na bidhaa au huduma husika na si vinginevyo.

Steve Jobs ni mwanzilishi wa Kampuni ya Apple. Mara zote Steve alikuwa akiguswa na changamoto za watu na kuwaza jinsi ya kuziondoa. Aliporudi Apple kwa mara ya pili Steve hakuridhishwa na ubora wa kifaa cha muziki, MP3 Player, aliyoikuta…akapania kuiongezea thamani.

Steve aliishughulisha akili yake na baada ya muda alifanikiwa kutengeneza iPod, kifaa kilichokuwa na muundo na uwezo mzuri zaidi wa kuhifadhi, kucheza na kusafirisha muziki kwenda katika vyombo vingine.

Pili, jinsi thamani inavyotolewa. Unaweza kuwa mzuri sana katika kutengeneza thamani lakini ukashindwa kuifikisha kwa walengwa kwa ubora na ufanisi uliotarajiwa.

Kampuni ya kutafuta taarifa mtandaoni, Google, hawakuridhika tu na ubunifu huu, bali walienda mbele zaidi kuhakikisha wana mitambo (Search Engines) ya uhakika kuwawezesha wateja kupata taarifa kwa uwingi na kasi ya kiwango cha juu. Hii inaitwa ‘kujiongeza’.

Tatu, jinsi ya kuigeuza thamani kuwa fedha. Ni jambo la maana sana kuwa na Kampuni ya kutengeneza na kutoa thamani kwa ubora. Hata hivyo, kama thamani hiyo haiingizi fedha inakuwa haina tija kwa mtoaji.

Mtaalamu mmoja wa biashara anadai kuwa kuna kitu ambacho wamiliki wa biashara kama Hoteli au Pub wanashindwa kukiona. Kwa kiasi kikubwa, faida yao hutokana na vinywaji na vitafunwa tu.

Anadai, kiuhalisia kuna thamani kubwa inayotolewa ambayo haipangiwi bei kwa mfano muziki unaopigwa mubashara, vibanda maalum vilivyopambwa kwa miti na maua yenye harufu nzuri, na wahudumu maalumu kwa wateja maalum.

Kwa hiyo kila biashara inapaswa kupima thamani wanayoitoa kwa wateja wao ili kuona jinsi gani inavyoweza kuinufaisha biashara hiyo kifedha bila kuathiri uwezo wake wa kushindana katika soko.

Nne, jinsi thamani inavyoboreshwa. Usipokuwa makini usishangae ukiona thamani uliyoitengeneza inapotea haraka. Kumbuka dunia ya leo ina ushindani mkubwa, na kila biashara inajitahidi kufanya ubunifu.

Ukweli ni kwamba modeli za biashara leo hazidumu sana. Ukibweteka tu ukasahau kutafiti ili kuboresha, au kudadisi, utakuta tayari umeshapitwa na wakati.

Wataingia washindani wenye teknolojia mpya na njia za kisasa zaidi za kuzalisha, kusambaza na kutangaza bidhaa au huduma…wewe utabaki kushangaa tu!

Hatua ya kuchukua. Ukiwa mmiliki wa biashara, unapaswa kujifunza kila siku ili uweze kutengeneza, kuitoa kwa ubora, kuibadilisha kuwa fedha na kuiboresha thamani ili uweze kubaki salama katika soko. Na ubunifu ndio jawabu la swali hili.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Jinsi Ya Kuanzisha Na Kukuza Mahusiano Ya kibiashara

Usifikiri mamba ana mpango wa kummeza huyu ndege, la hasha! Hapa kuna msaada mamba anapewa

Habari rafiki,

Mara nyingi neno mahusiano linapotajwa watu wengi hupeleka fikra zao katika mahusiano ya kimapenzi. Ukweli mahusiano ni zaidi ya hapo, kwani kuna mahusiano ya kibiashara pia.

Mahusiano ni suala la lisaikolojia linalohusisha fikra, hisia na akili ili kujenga ukaribu na mshikamano baina ya watu au taasisi. Kwa hiyo mahusiano ni suala linalohusisha mtu na mtu, mtu na taasisi au taasisi na taasisi.

Mahusiano baina ya watu au taasisi huzaa kitu kinachojenga daraja baina ya watu au taasisi hizi ili ziweze kufanya mambo kwa kutegemeana au kusaidiana.

Kuna mambo ya msingi ya kufanya ili kufanikiwa katika kujenga mahusiano bora ya kibiashara.

Kwanza, kama wewe, unapaswa kujifanyia tathmini binafsi. Ili uweze kujenga mahusiano na watu wengine inabidi ujifahamu vizuri kwanza. Jiulize, “je mimi nina tabia au uwezo wa kuhusiana vyema na watu?”

Pili, elewa unataka kujenga mahusiano hayo kwa lengo gani, na kwa hiyo unapaswa kujielekeza katika lengo hilo. Elewa unachotaka kufanikisha, kwa mfano kuongeza mauzo ya bidhaa zako.

Tatu, ukifanikiwa kujenga mahusiano unapaswa kuyalinda kwa nguvu zako zote ili yadumu na yakuletee faida kibiashara.

Mahusiano ya kibiashara yanahusisha wadau wengi hivyo unahitaji kujenga na kuendeleza mahusiano mema na wadau hao kwa manufaa ya biashara yako. Wadau hao ni wafuatao:

Moja, wafanyakazi. Lazima ujenge na kudumisha mahusiano na watu hawa. Elewa kuwa wafanyakazi ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya biashara. Usimdharau au kumpuuza mfanyakazi.

Jitahidi kuwasikiliza wafanyakazi wako, kuelewa shida zao, na kuyafanyia kazi mawazo au maoni yao. Ukiweza jitahidi kuwafahamu kwa majina yao. Wasalimie na ongea nao ki-urafiki, na ikibidi wafanyie utani kidogo ukikutana nao.

Watie wafanyakazi hamasa ya kufanya kazi. Kumbuka kuwa ukijenga mahusiano bora na watu hawa hakika biashara yako itafanikiwa.

Pili, wateja. Kujenga mahusiano na wateja ni mbinu nzuri inayolenga kujenga kundi la wateja waaminifu. Kuna njia nyingi za kujenga mahusiano na wateja.

Jenga tabia ya kuwakaribisha vizuri wateja kila wakija katika biashara yako. Ongea nao kirafiki na sikiliza shida zao. Wapatie wateja bidhaa na huduma iliyo bora. Waoneshe wateja kuwa unawajali na kuwathamini.

Wafanye wateja waikumbuke biashara yako kila siku kwa kuwapatia kadi yako ya biashara, na usisite kutoa zawadi, hata ndogo, kwa wateja wako watiifu, kama vile kofia, T-shirt, lesso au punguzo la bei inapobidi.

Tatu, mabenki. Ukiwa mfanyabiashara utalazimika kuhusiana na taasisi za fedha, mfano mabenki. Hata kabla ya kuanza biashara unaweza kuanzisha mahusiano haya.

Unaweza kuanza kwa kufungua akaunti na kuweka akiba kidogokidogo humo. Uhusiano huu utakupa urahisi wa kupata taarifa, mfano jinsi ya kupata mkopo, utakapoanza biashara. Ukiwa mteja wao mzuri watakuamini.

Nne, mamlaka ya mapato. Hawa nao ni wadau muhimu katika biashara ambao unapaswa kujenga mahusiano nao, kwani mapato ya serikali hulipwa kupitia kwao.

Utawahitaji hawa katika uendeshaji wa biashara yako kwa kuwa wao hutoa namba ya utambulisho  wa mlipa kodi na cheti cha utambulisho kwa mamlaka za utoaji leseni ya biashara.

Tano, mamlaka za leseni. Kutegemeana na biashara unayotaka kufanya, unahitajika kupata leseni ya biashara, ambayo utaipata kupitia mamlaka husika.

Ukijenga mahusiano mazuri na wadau hawa itakuwa rahisi kupata taarifa zote muhimu kuhusu masharti au miongozo ya uendeshaji wa biashara yako.

Sita, ofisi ya mipango miji. Ukijenga mahusiano na ofisi hii utafahamu mapema endapo biashara unayotaka kufanya inaruhusiwa au hairuhusiwi katika eneo unalotaka kuiweka, au utapewa masharti ya kufuata mapema.

Saba, majirani zako. Hawa ni wadau muhimu sana kwa kuwa ndio wateja tarajiwa wa mwanzo kabisa. Majirani ndio unatarajia ukipata tatizo lolote waanze kutoa msaada, na utapata taarifa nyingi kupitia majirani unaohusiana nao vizuri.

Wapo wadau wengi, lakini kwa leo hawa wanatosha. Kilicho muhimu ni kujitahidi kujenga mahusiano bora na kila mdau muhimu na utaona biashara yako inakua na kufanikiwa.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Hivi Ndivyo SIDO Inavyosaidia Kukuza Ubunifu Kwa Vijana

Vijana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya ubunifu

Habari rafiki,

Nadhani utakubaliana na mimi kuwa kuna idadi kubwa tu ya vijana wenye vipaji vikubwa katika ubunifu.

Vipaji hujidhihirisha kupitia uwezo asilia wa kufikiri, kubuni, kusanifu na kufanya uvumbuzi wa vitu.

Vijana hawa wakitambuliwa na kuwezeshwa, nchi yetu itapiga hatua kubwa kimaendeleo, na vijana hawa watajipatia ajira.

Ubunifu ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya sayansi na teknolojia na kwa sababu hiyo kuna umuhimu mkubwa kwa serikali kuweka mkono wake katika jambo hili.

Kwa muda mrefu, Serikali ya Tanzania, kupitia taasisi zake, imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuwasaidia wagunduzi na wabunifu hasa katika nyanja za sayansi na teknolojia.

Moja kati ya taasisi zilizo mstari wa mbele katika kukuza ubunifu ni SIDO, ambayo ni taasisi inayosimamia na kuendesha viwanda vidogo vidogo Tanzania.

Siyo siri kwamba mataifa mengi yaliyoendelea yamefanikiwa baada ya kutia nguvu katika kukuza ubunifu.

Kwa kubaini ukweli huu, SIDO imeandaa utaratibu mzuri wa kusaidia zoezi la ukuzaji wa ubunifu kwa vijana.

Kupitia SIDO, vijana wenye mawazo bunifu wanapata jukwaa ambalo huwasaidia kufanyia majaribio na hatimaye kuibua na kuendeleza ubunifu wao.

Kinachofanywa na SIDO ni kuwakaribisha vijana wenye mawazo bunifu machanga, au mawazo yaliyofikia hatua fulani ya juu, au prototype, na husaidia kuyapa atamizi (incubation). 

SIDO wanajinasibu kutoa fursa zifuatazo, ili kukuza ubunifu kwa vijana:

Moja, kupokea na kulea wazo bunifu kwa kuwapatia wabunifu eneo maalum (incubation space) ambalo hutumika kulea mawazo bunifu ili kupata bidhaa tarajiwa. Kwa mujibu wa SIDO, mbunifu halipii eneo hili kwa miaka mitatu.

Mbili, Kuwaunganisha wabunifu na taasisi nyingine zinazohusika kulea ubunifu, kama Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania, COSTECH.

Kwa kuwa mchakato wa ubunifu unahusisha gharama nyingi, kuna taasisi za fedha ndani na nje ya nchi ambazo huwa tayari kuwasaidia kifedha wabunifu wenye mawazo ya maana, mfano mmoja ni benki ya CRDB.

Ikipatikana taasisi iliyo tayari kutoa msaada wa fedha, SIDO huwahimiza vijana wabunifu waombe fedha hizo. Sasa, ili aweze kufikiriwa kupewa hizo fedha, inampasa mbunifu kutengeneza andiko, au proporsal.

Kwa kuwa wataalamu wa uandishi wa proporsal wanapatikana COSTECH, hivyo SIDO huingia tena hapa, kuwaunganisha wabunifu na COSTECH ili wawasaidie kuandika proporsal. Proporsal ikikubaliwa, taasisi husika hutoa fedha kwa wabunifu.

Tatu, SIDO hufanya kazi pia ya kuwaunganisha wabunifu na vyuo vya elimu ya juu kama UDSM, Mzumbe au DIT, kuwasaidia wabunifu ki-utaalamu na ki-teknolojia ili bidhaa inayobuniwa ilete matokeo mazuri katika soko.

Ili mbunifu apate nafasi SIDO, kuendeleza wazo lake, wazo hilo linatakiwa liwe katika maeneo maalum ya vipaumbele.

Maeneo yanayopewa kipaumbele zaidi ni yale yanayohusika na kuongeza thamani ya mazao. Kila mtu anafahamu kuwa kuna miezi fulani baadhi ya mazao, kama matunda, huwa yanazagaa mitaani kwa kukosa soko.

Sasa, njia pekee ya kuongeza muda wa matumizi ya mazao haya ni  kuyaongezea thamani kwa kuyasindika, ambapo wanatakiwa wabunifu kuja na technolojia ya kufanikisha hili.

Kwa mfano, achali ya embe au mango pickle ni zao la maembe yaliyoongezewa thamani  kwa rosti ya viungo,  kisha  kuhifadhiwa ndani ya vinegar au siki. Ukiikuta achalihii super market, ina thamani kubwa, kuliko vipande vya maembe pekee.

Eneo jingine la kipaumbele ni ubunifu unaolenga kuboresha namna watu wanavyoishi na kuzikabili changamoto za kijamii na kiuchumi.

Kwa mfano yupo mbunifu mmoja aliyeguswa na changamoto wanazopitia watu katika suala la ununuzi wa bidhaa, ambapo inabidi mtu aondoke nyumbani au ofisini aifuate bidhaa mbali, hivyo kupoteza muda wa uzalishaji mali.

Ili kutatua changamoto hii alitengeneza jukwaa, au e-commerce platform, ambayo anaitumia kutangaza bidhaa zake. Mteja akihitaji bidhaa hutoa oda kwa mtandao au kwa simu ambapo huletewa bidhaa hiyo hadi mlangoni kwake.

Ushauri kwa vijana ni kwamba wanatakiwa wachangamkie fursa hizi. Kijana unapaswa kujifunza kufikiri ki mkakati. Unapaswa kujenga uwezo wa kuyasoma mazingira yako ili kuziona changamoto na kuja na mawazo ya utatuzi

Ukishapata wazo, wasiliana na SIDO ambao wanakuhoji na kukusikiliza kwa umakini ili kuona ubora wa wazo lako na jinsi litakavyoleta tija kwako na kwa jamii nzima.

Wakiridhika na wazo lako hatua inayofuata ni kukusajiri na kukupatia hilo jukwaa ambalo utalitumia kuatamia wazo lako hadi upate bidhaa uliyokusudia ambayo watakusaidia pia namna ya kuiingiza sokoni ili uanze kunufaika kiuchumi.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Huu Ni Mfano Wa Kuigwa Kuhusu Dhana Ya Kujiajiri

Kilimo cha bustani kwa teknolojia ya green-house ni njia mojawapo ya kujitengenezea ajira binafsi

Habari rafiki,

Hivi karibuni, nikiwa nasoma gazeti moja la kila siku nilikutana na kichwa cha habari, “tatizo la ukosefu wa ajira lamtisha Rais mstaafu, Mkapa.”

Habari hiyo ilielezea hofu aliyoionesha Rais mstaaafu huyo kuhusu tatizo hilo, hasa kwa vijana, ambao wengi wanaonekana wakizagaa mitaani bila kuwa na shughuli maalum.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, tatizo la ajira linajidhihirisha wazi pale ambapo mwaka 2017 watu 56,000 walijitokeza kuwania nafasi 400 za ajira zilizotangazwa TRA.

Kwa takwimu hizi utakubaliana na mimi kwamba kuna umuhimu  wa kuliangalia suala la ajira kwa jicho maalum. Kuna haja ya kuwepo na jitihada za makusudi za kuwajengea vijana wetu uwezo binafsi wa kujitengenezea ajira.

Hili linaweza kufanyika kwa kuwapatia vijana maarifa ya ujasiliamali na ubunifu ili waweze kuzisaka fursa zilizomo katika mazingira yao na kuzikamata.

Bi Muse Marwa, msomi wa Chuo Kikuu na mkazi wa Dar-es-Salaam, anatupatia maarifa na uzoefu muhimu katika hili. Vijana wakiiga mbinu alizotumia kujitengenezea ajira na kipato hakika tatizo la ajira litapungua.

Tukiongelea dhana ya ubunifu tunaongea kuhusu matokeo ya kuufikirisha ubongo ili kupata njia mpya na nzuri zaidi za kuleta mabadiliko, kutatua changamoto au kuondoa tatizo lililojitokeza katika  jamii.

Akisimulia jinsi alivyojipatia ajira binafsi, Bi Muse anasema kuwa baada ya kumaliza Chuo Kikuu mwaka 2011, akiwa amesomea fani ya usimamizi wa mazingira, hakuweza kupata ajira, wala hakuona dalili za ajira.

Akiwa amejishikiza katika kazi ya ualimu, alianza kufikiri kwa kina jinsi ya kujipatia ajira binafsi, ambayo itaendana pia na fani aliyosomea.

“Kabla ya kuanza biashara ya welding, nilianza kwa ku-google. Nilikuwa naingia google kutafuta mawazo ya biashara…yaani biashara gani naweza kuifanya kwa mtaji mdogo. Nimehangaika sana kila siku.” Anasema Bi Muse.

“Kila wazo nikilipata nilikuwa najiuliza je wazo hili linaweza kufanyika katika mazingira yangu, kwa mtaji mdogo?”

Akiwa anaendelea kufanya utafiti, ndipo wazo la kufanya kazi kama ya baba yake lilipomjia. Baba yake alikuwa anatengeneza grili za milango na madirisha ya nyumba kwa vyuma, kwa kuchomela, au welding.

Aliamua kufanya kazi hii, lakini yeye aliifanyia mabadiliko kidogo, kuonesha ubunifu wake. Badala ya kutengeneza grili za madirisha na milango, yeye alitengeneza fenicha za nyumbani na ofisini.

Anadai, “mafundi wengi hutengeneza fenicha kwa kutumia mbao, lakini mimi nilihitaji kulinda mazingira pia, kupunguza ukataji miti, kama nilivyosoma chuoni, hivyo nilichagua matumizi ya chuma badala ya mbao.” Huu nao ni mfano wa ubunifu.

Alianza biashara hii bila mtaji na anasisitiza kuwa siyo kila biashara inataka mtaji. Anasema alianza biashara hii kama dalali, na kwamba huu ni aina ya ubunifu unaotakiwa kuigwa na vijana…kuanza na ulicho nacho!

Ubunifu mwingine aliojinasibu nao ni matumizi ya mitandao ya kijamii katika kufanya biashara. Anasema vijana wengi wanatumia mitandao ya kijamii kuandika umbea au udaku. “Mimi nilitumia Instagram yangu kupost mitindo ya fenicha niliyoona inawafaa wateja wangu.”

Anasema, “nachukua dizaini nzuri za makochi, vitanda au stendi za maua, naposti kuwavutia wateja wangu, na bei yake naweka. Wakivutiwa wanatoa oda. Hapo ndipo na mimi nilikuwa najiongeza kwa mbinu za udalali.”

“Nikipata oda naipeleka kwa mafundi, nawashawishi, ili wanitengenezee kwa bei ya chini kidogo. Nikiuza oda hiyo kwa bei ya juu, tofauti yake ndio faida yangu, ambayo naiweka akiba, na baada ya muda nilipata mtaji wangu na kufungua rasmi biashara yangu.”

Kuonesha ubunifu wake zaidi, Bi Muse anasema kwamba kwa kuwa anapenda sana maua nyumbani kwake, kama mapambo, aliona ajiongeze kwa kuchanganya bidhaa zake mbili. Alianza kutengeneza stendi za maua na kuotesha maua humo, kisha kuviuza vitu hivi pamoja.

Kwa muunganiko huu alijiongezea sana kipato hasa kutoka kwa wanawake wapendao mapambo majumbani mwao.

Ushauri anaotoa Bi Muse ni kwamba kijana usibweteke. Usisubiri ajira ikufuate miguuni. Jifunze kuitafuta ajira, hasa ajira binafsi.

Anahimiza kuwa sio kila ajira itakuja moja kwa moja. Ajira nyingine huja kwa njia ya mzunguko ndipo baadaye upate unachotaka. Hivyo ukipata wazo lako zuri anza mara moja kisha tia nia, tia jitihada, tia ubunifu na usikate tamaa, utafanikiwa.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Fursa Za Mafanikio Unazo Hapo Hapo Ulipo

Usidhani fursa za mafanikio kila wakati ziko mbali, hapana, wakati mwingi zipo hapo hapo ulipo

Habari rafiki,

Leo nakuletea simulizi ya zamani iliyonivutia, nikaona ni vyema nikushirikishe pia. Ni simulizi yenye kuhamasisha na kutoa mafunzo kwa wabunifu na wajasiriamali wenye hamu ya mafanikio.

Ni simulizi yenye maudhui  murua yenye lengo la kukufumbua macho ili uwe na uwezo wa kuziona fursa ambazo zimekuzunguka au umezikalia, ambazo kwa bahati mbaya au kwa uzembe tu umeshindwa kuziona au kuzikamata!

Simulizi hii inamhusu mkulima mmoja aitwaye Al Hafed, aliyeishi jimbo moja maarufu nchini India. Huyu alikuwa tajiri aliyemiliki mashamba makubwa, na kwa sababu hii alionekana kuridhika na maisha yake.

Kumbe matajiri huwa hawaridhiki bwana! Siku moja alipata taarifa kuwa kuna wakulima kama yeye mahali fulani amejipatia mamilioni ya pesa kwa kuuza madini yenye thamani yaitwayo almasi.

Taarifa hii ilimpa msisimko mkubwa na hamu ya kuupata utajiri mkubwa zaidi  kupitia madini ya almasi. Hata hivyo Al Hafed hakuwa na ufahamu wowote kuhusu madini haya.

Bila kuchelewa, alimtafuta mnunuzi wa shamba lake na alipompata aliliuza na kufunga safari kutafuta sehemu ilipo hiyo almasi. Akitumia akiba yake ya pesa alizunguka kila mahala bila mafanikio, hadi akiba yake ikamalizika.

Huku nyuma mnunuzi wa shamba lake aitwaye Hafidh, siku moja aliwachukua ngamia wake hadi kwenye kijito kimoja ndani ya shamba lake ili wakanywe maji.

Wakiwa wanakunywa maji ghafla Hafidh alipigwa machoni na mwanga usio wa kawaida, wenye mchanganyiko wa rangi ya bluu na nyekundu, kutoka katika kitu kilichokuwa kimelala chini ya sakafu ndani ya kijito kile.

Ulikuwa ni mwanga mng’aavu ulioakisiwa juu ya jiwe moja kubwa ndani ya kijito kile. Alivutiwa na jiwe lile, akainama akaliokota na kwenda nalo nyumbani kwake ambapo alilihifadhi jikoni.

Baada ya siku kadhaa alilichunguza lile jiwe, ndipo alipogundua kuwa lilikuwa sio jiwe la kawaida. Alipofuatilia zaidi akagundua kuwa jiwe lile kumbe lilikuwa almasi! Hafidh alipata furaha isiyo kifani baada ya kugundua anaishi juu ya utajiri mkubwa.

Habari hii ilimfikia Al Hafed ambaye hakuamini alichoambiwa. Walipokutana alimwambia Hafidh, “kijito kile kina mawe mengi ya aina hiyo, kwa hiyo basi shamba zima limejaa almasi…na kwa maana hiyo wewe sasa ni tajiri mkubwa.”

Kwa hiyo, shamba ambalo Al Hafed aliliuza ili aende mbali kutafuta almasi, aiuze na kupata utajiri mkubwa, limegeuka kuwa chanzo kikubwa kwa almasi zenye thamani kubwa.

Al Hafed aligundua kuwa kumbe alimiliki eneo kubwa lenye almasi nyingi…lakini bila kujua aliamua kuliuza kwa gharama ndogo kabisa ili aende akatafute almasi sehemu nyingine.

Kuna somo muhimu katika simulizi hii. Binaadamu tuna tabia ya kupuuza vitu vyetu kwa hisia tu, kuwa havina thamani. Tunapenda kudhani kuwa vitu vya mbali ndivyo vyenye ubora na thamani zaidi.

Msomaji wangu, unapaswa kujifunza kuwa huhitaji kuzitafuta fursa, utajiri au mafanikio mbali na pale ulipo.

Zipo fursa nyingi unazoweza kuzibadilisha kuwa mali au utajiri zinazopatikana hapo hapo ulipo…kwenye jamii yako, kwenye familia yako, au kwenye kazi yako, na kadhalika.

Kuna msemo maarufu wa kiingereza usemao , “majani bora ni yale yaliyoko upande wa pili wa fensi”. Kwa hiyo watu wamejenga fikra kuwa mafanikio yao yatapatikana upande mwingine, mji mwingine au kwenye kazi nyingine.

Kwa bahati mbaya unapoamua kuyatafuta majani bora upande wa pili wa fensi ndipo unapogundua kuwa kumbe wala majani yenyewe siyo laini na matamu kama ulivyofikiria, na hapo ndipo unapoanza kuyakumbuka majani uliyoyaacha kwanza.

Mkulima Al Hafed aliishi miaka mingi juu ya almasi. Tatizo lake kubwa ni kwamba hakuwa na maarifa wala udadisi kuweza kubaini utajiri aliokuwa ameukalia.

Vipo vitu au fursa hapo hapo ulipo lakini zimefunikwa na vumbi, udongo au takataka fulani kukufanya usiweze kuona kilichomo ndani yake. Kwa hiyo ukikosa umakini na udadisi fursa hizi hupotea.

Unasisitizwa hapa ujifunze kujifunza. Jifunze kutafuta maarifa kwa kudadisi mambo mbalimbali ili uweze kuziona fursa zilizokuzunguka au kujificha hapo hapo ulipo ili uzikamate badala ya kudhani majani bora yanapatikana upande wa pili wa fensi.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com

Tunawezaje Kuwasaidia Vijana Wetu Kuwa Wabunifu?

Ili kufanya ubunifu kijana hutakiwa kuishughulisha sana akili yake

Habari rafiki,

Nadhani utakubaliana na mimi kuwa kuna idadi kubwa tu ya watoto na vijana majumbani mwetu wana vipaji vikubwa lakini kwa bahati mbaya wazazi wao hawajui au hawawapi msaada stahiki.

Vipaji hujidhihirisha kupitia uwezo asilia wa kufikiri, kubuni, kusanifu na kufanya uvumbuzi wa vitu.

Kipaji kikigundulika na kutumika ipasavyo kinaleta tija, lakini kisipogundulika kinamnyima mhusika au jamii fursa za kiuchumi na kijamii.

Moja kati ya vipaji muhimu walivyonavyo vijana wetu ni uwezo wa kufanya ubunifu.

Tanzania imejaliwa kuwa na vijana wengi wenye ubunifu, ambao wakitambuliwa na wakawezeshwa, nchi yetu itapiga hatua kubwa kimaendeleo; lakini pia vijana hawa watajipatia maendeleo binafsi.

Ubunifu ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya sayansi na teknolojia na ndio maana masomo haya yanatiliwa mkazo mkubwa hivi sasa.

Wanafunzi wakiyatumia vizuri maarifa yanayopatikana katika masomo ya sayansi na teknolojia, halafu wakachanganya na vipaji walivyozaliwa navyo, uwezo wao wa ubunifu unakua wa hali ya juu.

Wakati fulani ubunifu hauna uhusiano sana na elimu ya darasani, kwani wapo vijana waliofanya ubunifu mkubwa wakiwa na elimu ndogo kabisa, ya msingi.

Ubunifu uliofanywa na vijana hawa ni kielelezo kuwa kama elimu yetu itatilia mkazo vitendo, kuliko nadharia pekee, vijana wetu watafanya mambo makubwa.

Kwa hiyo ni jukumu la wazazi, walezi na walimu kuwasaidia vijana wetu kuyapa uhai mawazo yao ili yaweze kuwa bayana.

Tuwasaidie vijana kutengeneza na kupata picha halisi ya kitu wanachokiwaza ili kukipa umbo au uhalisia.

Hii ni hatua muhimu kwani husaidia kumpa msukumo kijana ili asiweze kukata tamaa, kuona giza, au kurudi nyuma. Tumsaidie kuona kuwa wazo lake lina umuhimu na linaweza kuwa kitu halisia.

Naomba nikushirikishe mfano mmoja wa kijana aliyefanikisha ubunifu mkubwa kwa uwezo wake binafsi uliochochewa na jitihada za ‘wazazi’ wake.

Kijana Simforia Kasokola alibahatika kupata ajira katika shamba la miti Kiwira, Mbeya, ingawa hakuwa na elimu kubwa ya darasani.

Baada ya muda kidogo aligundua kuwa ofisi aliyofanyia kazi ilikuwa inaingia gharama kubwa kununua dizeli kuendeshea jenereta ya kuzalisha umeme kwa matumizi ya ofisi.

Simforia aliguswa na changamoto hii, na kuanza kuishughulisha milango yake ya fahamu, hasa macho, na akili.

Akiwa anatafakari, macho yake yakakutana na mto Kiwira, uliopita karibu kabisa na shamba lao. Mto huu hutiririsha maji mwaka mzima.

Picha ya pili iliyoingia katika ubongo wake ni jinsi dainamo ya baiskeli inavyofanya kazi ya kuzalisha umeme kwa matumizi ya baiskeli, usiku.

Picha hizi mbili zilimpatia wazo kichwani. Na ndipo alipotamka, ‘naweza kutengeneza umeme hapa’.

Alijisemea, ‘haya maji yatachukua nafasi ya gurudumu la baiskeli, kwa hiyo ninachotakiwa kufanya hapa ni kutengeneza mtambo unaofanana na dainamo’.

Kwa kuwa Simforia alikuwa mtundu aliweza kubuni mtambo hafifu wa kienyeji uliowezesha kuzalisha umeme wa voti 150, ukisukumwa na maji ya mto Kiwira, aliyoyatega kwa utaalamu mkubwa.

Viongozi (wazazi) wake waliuona uwezo wa Simforia, na kuguswa nao. Waligundua Simforia ana kipaji cha ubunifu lakini waligundua pia kuwa hakuwa na elimu ya fani ya umeme.

Walichokifanya viongozi wake ni kumsaidia kujiunga na Chuo Cha Ufundi VETA kusomea elimu ya umeme ili kukuza kipaji chake.

Elimu hii, ingawa haikugusia moja kwa moja ujuzi wa mitambo ya kuzalisha umeme, lakini ilimpa mwanga mkubwa uliomfanya aweze kuboresha wazo lake.

Kwa kutumia elimu hii na uwezo mkubwa wa fikra zake aliweza kusuka mtambo mkubwa wa kuzalisha umeme kwa kuiga teknolojia inayotumika katika dainamo ya baiskeli.

Simforia aliendelea ‘kuunganisha doti’, kichwani mwake, hadi akaweza kuzalisha umeme uliofikia voti 180, na kutatua tatizo la umeme lililokuwepo.

Hatua ya kuchukua: ili kumsaidia kijana kuwa mbunifu, mzazi una jukumu la kumsaidia mwanao kukinoa na kukiendeleza kipaji chake kwa kumwonesha njia sahihi za kupita, na kumtia moyo.

Kumbuka piakipaji peke yake bila maarifa ni kazi bure. Bila elimu ya kutosha katika fani aliyojaliwa, kijana anakosa umahiri, uwezo wa kujiamini na uendelevu, hivyo msaidie kijana wako kupata elimu stahiki .

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530

Haya Ndiyo Makosa Wahudumu Huwafanyia Wateja Wao

Wateja Hujisikia Vibaya Wakicheleweshewa Huduma

Habari rafiki,

Zipo tabia au makosa yanayofanywa na wamiliki wa biashara au watoa huduma wao ambayo humfanya mteja ajisikie vibaya.

Huduma bora kwa mteja si jambo la kupuuziwa hata kidogo kwa mfanyabishara anayejitambua kwa kuwa bila mteja hakuna biashara itakayopata mashiko.

Kwa hiyo kila mfanyabiashara anapaswa kuyajua makosa ambayo akiyafanya yatamgharimu kwa kumfukuzia wateja wake.

Yafuatayo ni makosa ambayo wafanyabiashara wanapaswa kuyaepuka:

Moja, Kushindwa kujenga mahusiano na mteja. Wateja walio wengi hupenda kufanya biashara na mtu anayewajali, mcheshi na ajengaye mahusiano.

Wateja hufarijika sana wanapoingia katika biashara na kukaribishwa vizuri kwa maneno ya kirafiki. Kwa mfano, “Karibu sana baba yangu, pole na safari, naomba nikusikilize.”

Au kama umemkosea atafurahi akisikia, “oooh, pole sana kaka yangu, nimeelewa tatizo lako, naomba unisamehe. Naomba ufanye subira kidogo nilifanyie kazi suala lako.”

Ukishindwa kumfanyia mteja wako ukarimu kwa kuongea naye kirafiki ujuwe upo katika hatari ya kumpoteza.

Mbili, spidi ndogo ya kutoa huduma. Katika dunia ya leo mbayo watu wengi wanathamini muda, na wanajitahidi kufanya mambo yao kwa uharaka ili watimize malengo yao, ukitoa huduma kizembe unafanya makosa makubwa.

Wateja wanapokuja kaunta au wale wanaonunua kupitia mitandaoni kama tweeter, intagram, barua pepe au simu – hupenda huduma ya haraka.

Kwa mfano, kama mteja anahitaji taarifa fulani, basi hufurahi akijibiwa kwa haraka. Mtoa huduma akiwa mtu wa kujivuta katika kutoa huduma basi anafanya kosa ambalo lina madhara kwa biashara yake.

Tatu, mtoa huduma kuongea sana badala ya kusikiliza. Hili nalo ni kosa, tena kubwa! Utajuaje mahitaji ya mteja wako kama hujamwelewa? Na utamwelewa vipi iwapo humsikilizi?

Inashauriwa tujenge tabia ya kusikiliza kwa asilimia 80 halafu tuongee kwa asilimia 20 tu ya muda wa kuwa na mteja. Tusipofanya hivi tunakosea.

Nne, mtoa huduma kuongea kwa ukali. Wapo wahudumu wa aina hii ambao hawajui lugha au sauti sahihi ya kuongea na mteja wake. Hawa wanahitaji mafunzo!

Sauti kali, ya juu na yenye dharau haifai kwa mteja. Mara nyingi mteja hawezi  kuvumilia mtoa huduma mkali, mkaidi na mkorofi. Akiona hali hii hatakaa, bali atajiondokea na hutampata tena.

Tano, kujihami badala ya kukubali udhaifu. Kuna wakati mteja hugundua udhaifu wa huduma inayotolewa katika biashara fulani. Wapo wateja ambao huamua kushauri au kukosoa huduma isiyofaa.

Sasa tatizo linakuja pale mtoa huduma, badala ya kujichunguza ili auone udhaifu wake, yeye hukasirika na pengine kuanza kujibizana na mteja. Ukifanya kosa hili ujuwe tayari unamkosa mteja huyu na wengine pia.

Katika hili mtoa huduma unashauriwa kujiwekea utaratibu wa kujihakiki kila mara ili kugundua udhaifu wako na kujirekebisha mapema kabla ya mteja kugundua chochote.

Sita, mtoa huduma hapatikani ki-urahisi. Unapofanya biashara na watu unalenga kutatua matatizo yao. Ukishaiweka bidhaa yako sokoni unakaribisha maswali, malalamiko, au maoni kuhusu biashara au bidhaa yako.

Kitu cha hovyo kabisa kinachofanywa na baadhi ya wafanyabiashara ni kutokupatikana. Mteja ana shida anataka umsaidie kuitatua…hupatikani kwa simu, e-mail wala ana kwa ana. Jambo hili huwaudhi sana wateja.

Saba, kumhudumia mteja kiulaghai. Wakati fulani mteja anarudi dukani au anapiga simu kuilalamikia bidhaa ambayo haikufanya kazi alivyotarajia.

Pengine mteja anataka maelezo au ufafanuzi tu ili aelewe…wala hana haja ya kuirudisha bidhaa hiyo, anataka tu mtoa huduma afahamu tatizo na kufanya marekebisho.

Cha ajabu mtoa huduma badala ya kusikiliza vizuri ili aeleweshwe na kuchukua hatua, yeye ndio kwanza anaanza kubishana na mteja na kutoa majibu ya ujanjaujanja au ya uongo. Huu ni udhaifu mkubwa.

Hatua ya kuchukua: haya ni baadhi ya makosa au tabia mbaya ambazo wateja hawazipendi. Kwa hiyo, kama unataka kupiga hatua katika mazingira ya ushindani wa biashara jiepushe na makosa haya.

Ni vizuri kukumbuka kuwa ni rahisi kumpata mteja mpya lakini ukisha muudhi atakukimbia, na atapeleka sifa hiyo mbaya kwa rafiki zake ambao utawakosa pia.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com