
Habari rafiki,
Nimeeleza katika makala zangu zilizopita kuwa dunia ya kibiashara hivi sasa imetawaliwa na mazingira ya ushindani wa kiwango cha juu.
Kwa hiyo, ubunifu ndiyo njia pekee inayotumiwa na wajasiriamali wengi wanaojitambua ili kupambana na ushindani katika soko la bidhaa na huduma.
Ubunifu unaelezewa kama uundwaji wa bidhaa au modeli mpya; au uundwaji wa bidhaa au huduma fulani iliyoboreshwa.
Ubunifu unaelezewa pia kama bidhaa, huduma au modeli ya biashara iliyokuwepo lakini inaingizwa kwenye soko jipya kwa mara ya kwanza.
Makala hii inalenga kukupatia njia sita zinazoweza kuchochea akili yako na kukufanya uweze kujenga uwezo mkubwa wa kufanya ubunifu.
Moja, usongo au hamu ya kufanikiwa. Ukijenga nia au hamu ya kupata kitu, usongo huo huendelea kuisumbua akili yako. Jinsi unavyotia nia akili yako inafanya kazi ya ziada kuzalisha wazo bunifu au njia ya kutatua jambo.
Mbili, mfadhaiko. Unaposhindwa kupata kitu ulicholenga kukipata – unajisikia vibaya,, au unafadhaika.
Mfadhaiko unaotokea baada ya jitihada za kufanikisha kitu kukwama huuchochea ubongo ambao huanza kugonganisha mawazo kwa lengo la kupata njia mbadala ya kufanikiwa. Mgongano huu ndio huzaa ubunifu.
Tatu, udadisi. Kudadisi ni ile hali ya kusaka ukweli au kuufahamu undani wa jambo. Udadisi unapofanyika kichwani husababisha mishipa ya fahamu ya ubongo kujituma zaidi ili kuleta majawabu.
Kwa mfano unapojiuliza, “naona kuna tatizo hapa hivi chanzo ni nini? Hivi nani anahusika? Hivi utatuzi wake ni nini? Hivi nani anaweza kusaidia utatuzi?”
Udadisi ukifanyika kwa umakini matokeo yake ni upatikanaji wa wazo bunifu.
Nne, kujenga husuda. Unapohusudu kitu maana yake una mapenzi nacho. Sasa, unapopenda kitu au mtu, unajenga hamu ya kuboresha uhusiano kati yenu.
Angalia mambo unayomfanyia mtu umpendaye ndipo utagundua jinsi ubunifu unavyofanya kazi katika akili za watu.
Kwa mfano unapopanga kumpatia zawadi mpenzi wako – unaanza kuwaza, “hivi zawadi gani ataifurahia zaidi? Kama ni nguo, hivi rangi gani anaweza kuipenda zaidi…, aina ya kitambaa…, mshono je,…sijui niifungashe namna gani n.k?”
Jinsi unavyowaza haya ili utoke na kitu cha kumfurahisha mpenzi wako ndivyo akili yako inavyotanuka na kukupatia wazo bora zaidi, na hivyo kukufanya uzidi kujenga uwezo mkubwa wa ubunifu.
Tano, kujenga chuki. Kwa kawaida siyo jambo zuri mtu kuwa na tabia ya kuchukia watu. Tunahimizwa kupendana na kujaliana.
Mara nyingi unapomchukia mtu au kitu hupenda kitu au mtu huyo aangamie au apate wakati mgumu, na hii si sawa; hii ni ‘chuki hasi’! Tunapaswa kuwa na ‘chuki chanya’.
Ukiwa na chuki chanya unalenga kumchukia mtu au kitu kwa nia ya kukiboresha. Yaani unachukia, au unajisikia vibaya jinsi kitu au mtu alivyokaa kihasara-hasara.
Kwa mfano, unachukia jinsi nyumba ya wazazi wako ilivyochakaa au jinsi ndugu yako alivyo mlevi kupindukia. Unaona aibu! Unaanza kuufikirisha ubongo wako ili kutatua hali hiyo, hadi unafanikiwa. Hapa unajenga ubunifu.
Sita, kuweka malengo. Tunahimizwa kuishi kwa malengo. Unapokuwa na lengo au malengo yanayoisumbua akili yako, kila siku, unaujengea ubongo wako shauku ya kufanikiwa.
Ukiwa na malengo hauwezi kubweteka. Utajituma sana kufikiri na kuchanganua mambo ili ufanikiwe. Kwa jinsi unavyoufikirisha ubongo ndivyo unavyouchochea kufanya kazi zaidi – na hapa uwezo wa ubunifu unakomaa.
Hatua ya kuchukua: Makala hii imekupatia vitu sita vinavyoweza kuchochea akili yako na kukufanya uweze kujenga uwezo mkubwa wa kufanya ubunifu.
Unapaswa kuzitumia njia hizi na zingine za namna hii ili kuchochea uwezo wako katika kufikiri na kufanya ubunifu.
Hili likifanyika, kasi ya ubunifu itakuwa kubwa miongoni mwa wajasiriamali na maisha au biashara zetu zitapiga hatua zenye mafanikio makubwa.
Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.
Anapatikana kwa e-mail: nzyy2001@gmail.com; Simu 0718219530








