Je, ‘Kubeti’ Ni Ishara ya Vijana Kukosa Ubunifu?

Habari rafiki,

Karibu tena katika makala nyingine inayolenga kukupatia maarifa ya ujasiriamali, ubunifu na stadi za maisha.

Makala ya leo itaongelea tabia ambayo imezoeleka hivi sasa, hasa kwa vijana, ingawa kuna wazee kadhaa pia wanashiriki. Hii ni tabia ya kusaka pesa kwa njia ya kubahatisha, maarufu kama kubeti.

Kubeti kunapoteza muda na nguvukazi kubwa ikishinda kutwa nzima kwenye vibanda hivi

Hivi sasa, ukikutana na vijana wa Kitanzania watatu au zaidi wakiongea, hasa wapenzi wa soka, si ajabu ukasikia lugha ya, “eeh bwana eeh, jana nimetandika mkeka ukachanika.” Yaani ameweka dau fulani katika kamari ya kubashiri ushindi wa timu fulani lakini ameliwa.

Wapo wanaodai kuwa kubeti ni njia ya kutafuta mtaji wa biashara, kama mchangiaji mmoja wa Jamii Forum alivyoandika kuwa, “kuna jamaa yangu ana kibanda cha chips Morogoro, na aliniambia kuwa mtaji wa kuanzisha biashara hiyo, shilingi laki tatu, ulitokana na kubeti.”

Jinsi siku zinavyokwenda kumekuwa na ongezeko la vijana wanaopenda kushiriki michezo ya kubahatisha, na kuna ongezeko pia la matangazo ya kuhamasisha watu kushiriki bahati nasibu hizi ili kutajirika haraka.

Pamoja na kwamba tabia hii kwa vijana wengi inaweza kuonekana kama fursa ya kujipatia mtaji au utajiri wa haraka, lakini inapaswa kuhojiwa.

Kubeti ni kamari, yaani ni kucheza bahati nasibu, ambayo ina kupata na kukosa. Kwa hiyo vijana wanaojihusisha na zoezi hili wanahangaikia maisha ya bahati nasibu, na ukweli ni wachache wanaofanikiwa.

Sasa tujiulize, je ndio kusema vijana wetu wamefilisika kimawazo kwa kiwango hicho kwamba wamekosa mbinu za ki-bunifu za kuwapatia kipato hadi wapoteze pesa zao, hata kama ni ndogo; na muda wao mwingi kwa kucheza kamari kutwa?

Hii inaonesha kuwa kama Taifa, nchi yetu imeshindwa kuwapatia vijana wetu maarifa ya ujasiriamali na ubunifu, na hivyo wamekosa mbinu za kujipatia ajira kupitia uthubutu, ujasiri na ubunifu – kwa kutumia rasilimali nyingi zinazotuzunguka.

Kwa kukosa maarifa haya, vijana wameamua kutumia muda wao mwingi kubahatisha kupata fedha za harakaharaka kupitia kubeti. Tatizo ni kwamba, kuna ukweli, wanaobahatika kupata ni wachache, lakini wanaoshiriki na kushinda mitandaoni wakibeti ni wengi – na hivyo nguvukazi inayopotea kila siku bila kuleta tija kwa Taifa ni kubwa.

Nguvukazi inayotumika katika mitandao ya kijamii, kubeti, ingetumika katika kilimo, ufugaji au biashara, Taifa na vijana hawa wangepiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

Ongezeko la matangazo ya kuhamasisha kubeti yameongeza ushiriki wa vijana

Hasara wanayopata vijana hawa ni pamoja na fedha wanayotoa, au dau, fedha ya kununua bando la internet, na muda wa kucheza. Hasara nyingine mbaya zaidi ni kudumaa kwa ubongo na kushuka kwa uwezo wa kufikiri na kudadisi – ili kuibua mawazo bunifu.

Hatua ya kuchukua kwa serikali na waelimishaji binafsi, kama jukwaa la Mbunifu Blog, ni kuzidi kutoa elimu ya ujasiriamali inayowalenga vijana hawa. Elimu hii itawawezesha kuona, kusikia na hata kunusa vitu vilivyomo ndani ya mazingira yetu, na kufanya udadisi.

Udadisi huu ndio utawawezesha vijana kutengeneza mawazo ya kibunifu ambayo yatazaa fursa za biashara au shughuli yoyote halali ya kuzalisha kipato – badala ya kushinda kwenye vibanda vya kamari kubahatisha.

Kijana, ukiwa na elimu ya ujasiriamali unapata uwezo wa kuitazama dunia au mazingira unayoishi kwa ‘jicho maalumu’ lenye uwezo wa kuviona vyanzo mbalimbali vya fursa. Lakini pia unajenga hamasa na uthubutu wa ‘kuinyakua’ fursa unayoiona na kuibadilisha kuwa kitu halisi kivitendo.

Soma pia: Jinsi Wasanii Wanavyofanya Ubunifu – Somo Kwa Wajasiriamali

Kwa hiyo, kijana unahimizwa kujifunza ujasiriamali na kuacha kufikiria kutajirika kwa njia za mkato kama kubeti. Elimu hii itakupanua akili na kukupatia uwanja mpana na uwezo wa kuziona fursa, na kuzitumia ili kujinasua na umaskini. Hivyo jiunge na Mbunifu Blog upate maarifa haya.

Makala hii imeandikwa na Bw. Laurent Fungavyema, mtaalamu wa fani ya biashara na mjasirimali kivitendo.

Anapatikana kwa simu: 0718219530; e-mail: nzyy2001@gmail.com